Mnamo Novemba 6, 2017, kulitokea mkasa wa kusikitisha mkoani Kilimanjaro uliogusa hisia za watu wengi na kuvivuta vyombo vingi vya habari vya ndani na nje ya nchi kuufuatilia. Mkasa huu, ambao ulitokea katika Shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo mkoani hapo, ulianza kama fumbo la kesi ya mwanafunzi kupotea.
Siku ya tukio, katika maeneo ya shule, majira ya saa mbili usiku, walinzi wawili wa shule hiyo walikuwa wakiendelea na kazi katika maeneo tofauti. Mlinzi aliyefahamika kwa jina la Hamis Chacha, akiwa kwenye kibanda chake cha ulinzi, alisikia kishindo nje ya uzio, hali iliyo mlazimu kutoka kwenda kufatilia kilichosababisha kishindo kile.
Akiwa nje ya uzio wa shule, mlizi yule aliwasha tochi yake na kumulika vichakani ambapo alishuhudia watu wawili wakikimbilia vichakani mbali na uzio ule. Akiamini watu wale wanaokimbia ni wezi, mlinzi aliwakimbiza na kumuandama mmoja wao ambapo alipomkaribia alimkata mgongoni mtu yule kwa panga alilokuwa nalo.
Baada ya kukatwa na panga, mtu yule alikimbia kidogo na kuanguka chini, lakini Hamis Chacha akamkata tena kwa panga kichwani na mapajani. Haya yote yalifanyika gizani.
Mlinzi alipowasha tochi yake ili kumshuhudia aliyedhani ni mwizi, alishituka baada ya kuona mtu yule akiwa amevaa sare sawa na za wanafunzi wa shule aliyokuwa akifanyia kazi.
Mlinzi atoa taarifa ya tukio
Hamisi Chacha aliamua kuwapigia simu Mwalimu Labani Nabiswa, ambaye ndiye alikuwa akihusika na maswala ya nidhamu shuleni pale, pamoja na mmiliki wa shule aliyefahamika kwa jina la Edward Shayo, maarufu kwa jina la Kingsize.
Baada ya wote kuitikia wito na kufika eneo la tukio, mlinzi aliwaelezea mazingira yaliyozunguka tukio lile na Mwalimu Labani alipoulizwa kama anamtambua mtu yule aliyeshukiwa kuwa mhalifu ndani ya sare za shule, alikana kumtambua.
Mlinzi alishauri mtu yule asiyefahamika awahishwe hospitali kwani anaweza akawa bado yuko hai lakini Mkuu wa Shule, kwa kuhofia usumbufu ambao ungejitokeza, akashauri mtu yule atupwe kwenye Mto Ghona ulio umbali wa mita zaidi ya 300 kutoka ilipo shule ya Scolastica.
Mwalimu Labani, akishirikiana na mlinzi, wakatekeleza ushauri ule huku mwenye shule akiwaambia mambo mengine yote wamwachie yeye.
Walipomaliza kuutelekeza mwili ule mtoni, utatu usio mtakatifu ulitawanyika eneo la tukio, huku Mwalimu Labani na mlinzi wakiwa na shauku ya kuridhisha nafsi zao kama mtu yule sio mwanafunzi wa shule waliyokuwa wakifanyia kazi.
Kila mtu, kwa nyakati tofauti, alitekeleza jambo hili usiku uleule.
Aliyeanza kutekeleza hili ni Mwalimu Labani kwa kuitisha roll call ili kubaini kama kuna idadi kamili ya wanafunzi. Wanafunzi wote waliitikia majina yao, hivyo hakubaini upungufu wowote. (Naamini tunafahamu tabia ya wanafunzi kuitikiana majina ili kuwafichia makosa wenzao).
Usiku wa manane, mlinzi Chacha naye aliingia mabwenini ili kuhakikisha kama vitanda vyote wamelala watu. Alipofika kwenye moja ya kitanda cha double decker, alimkuta mwanafunzi mmoja tu aliyeitwa Raymond Mollel akiwa amelala kitanda cha chini huku cha juu kikiwa kitupu.
Chacha alipouliza ni kwa nini kitanda ni kitupu akajibiwa kuwa kilikuwa kinalaliwa na mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye ameshamaliza mitihani yake ya taifa na kuondoka. (Wanafunzi, kama tunavyojua, hawakosi majibu). Chacha akampigia simu Mwalimu Labani na kumjuza alichobaini.
Mwanafunzi mmoja hajulikani alipo
Mnamo Novemba 7, 2017, yaani siku iliyofata baada ya tukio, Mwalimu Labani akabaini kuwa kuna mwanafunzi wa kidato cha pili aitwaye Humphrey Makundi, hajafanya jaribio lake la somo la Fizikia. Baada ya kumtafuta mwanafunzi huyu bila mafanikio, Labani alimtaarifu mmiliki wa shule. Mwenye shule akamwambia Mwalimu Labani kuwa atawafahamisha wazazi wake na atalimaliza swala lile.
Mwenye shule akawasiliana na Inspekta Idd Juma ambaye alikuwa ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Himo. Haikujulikana walichowasiliana lakini mnamo Novemba 10, 2017, polisi wa Himo, wakiwa na mkuu wao wa kituo, walienda mto Ghona na kuuopoa mwili ule na kuupeleka Hospitali ya Mawenzi.
Mwili ule ulipokelewa na muuguzi aliyekuwa zamu aliyefahamika kwa jina la Anastazia January. Muuguzi alijulishwa na polisi kuwa mwili ule umeokotwa mtoni. Anastazia, bila kuufanyia uchunguzi mwili huo, alimwagiza mhudumu wa chumba cha kuifadhi maiti kuuifadhi.
Katika mazingira ya haraka isivyo kawaida mwili ule ulizikwa na manispaa siku ya Jumapili, Novemba 12, 2017, katika Makaburi ya Karanga kwa madai ya kutotambuliwa na ndugu zake japo Jumapili haikuwa siku ya kazi.
Ukweli unaanza kufunuka
Wakati harakati za kulifunika sakata hili zikiendelea, mzazi wa mwanafunzi Humphrey, aitwaye Jackson Makundi, alitaarifiwa juu ya kutoonekana shuleni kwa mwanae siku ile ile ilipobainika. Hivyo, Novemba 7, 2017, Mzee Makundi akawa mzito sana kuipokea na kuiamini taarifa ile hasa baada ya kuuona wasiwasi aliokuwanao mwenye shule.
Katika kufuatilia zaidi, Mzee Makundi alifahamishwa na baadhi ya wanafunzi kuwa Humphrey alikuwa ametoroka shule pamoja na wenzake wawili ili kwenda kununua chips na wakati wanarudi walikimbizwa na mlinzi, ambapo wenzake walifanikiwa kurudi shuleni lakini Humphrey hakuonekana tena tangu usiku hiyo.
Wanafunzi wakazidi kueleza kuwa walishatoa taarifa juu ya hilo katika Kituo cha Polisi Himo.
Taarifa hizi zikamfanya Mzee Makundi aende kituo cha Himo ambapo Mkuu wa Kituo alimjuza kuwa walipokea taarifa ile tangu Novemba 10, 2017. Inspekta Idd akaendelea kumjuza kuwa siku ile ile waliokota maiti ya mtu Mto Ghona.
Habari hizi zikamshtua Mzee Makundi na akaomba apate kuiona na kuitambua maiti hiyo. Hata hivyo, Mkuu wa Kituo akamjulisha kuwa maiti ile ilikuwa ni ya mtu mzima na imeshazikwa tangu Novemba 12, 2017, baada ya kushindwa kutambulika.
Mzee Makundi hakutaka kuliacha suala lile namna ile. Akaenda kuonana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro Khamis Issa ambaye aliamuru lifunguliwe jalada la uchunguzi.
Mnamo Novemba 17, 2017, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ikampa kibali Mzee Makundi cha kuufukua mwili ule kwa ajili ya uchunguzi. Baada ya mwili ule kufukuliwa, Mzee Makundi moja kwa moja aliutambua kuwa ni wa kijana wake kwa alama ya jino lililokuwa limekatika.
Uchunguzi wa kitaalamu wafanyika
Daktari aliyefanyia uchunguzi mwili ule aliweza kukadiria umri wa maiti ile kuwa ni kati ya miaka 14 hadi 17 kwa kuangalia idadi ya magego, kwani mtu aliye katika umri huu hawezi kuwa ameota magego yote mawili kwa kila taya.
Hii ilikuwa sahihi kwani marehemu Humphrey alikuwa na umri wa miaka 16 wakati mauti yanamkuta.
Pia, zilichukuliwa sampuli za mate na damu ya baba na mama wa Humphrey. Ikachukuliwa sampuli kutoka nyama ya tako, mfupa wa paja, kisigino, nywele za siri na nguo za marehemu ili kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupima vinasaba (DNA) ya sampuli zile.
Majibu yalibainisha maiti ile ni ya Humphrey Makundi.
Kwa upande wa simu, mawasiliano kati ya Mzee Shayo, mlinzi wa shule na Mwalimu Labani yalibainika ni kweli yalifanywa ndani ya muda wa usiku wa tukio. Kwenye miamala ilionekana Mzee Shayo alimtumia kiasi cha Sh500,000 Mkuu wa Kituo cha Himo.
Mwili wa Humphrey ulizikwa tena mnamo Disemba 2, 2017, baada ya ibada takatifu iliyoendeshwa na makasisi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Pastory Samweli na Elingaya Saria.
Viongozi mbalimbali walikuwepo ibadani wakiongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro hayati Anna Mgh’wira. Mwenyekiti wa taifa wa chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi James Mbatia pia alikuwepo.
Kesi ya jinai yafunguliwa
Mkasa huu ulizaa kesi ya jinai Na. 48 ya mwaka 2008 ambapo Hamis Chacha, Edward Shayo na Labani Nabiswa walishitakiwa kwa mauaji ya kukusudia ya Humphrey Makundi kinyume na Sura ya 196 kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Jinai.
Kesi hii ilipigwa danadana nyingi hali iliyomlazimu Mzee Makundi kumwandikia barua ya malalamiko Jaji Kiongozi kuwa anapoteza imani na Mahakama. Jaji Kiongozi akafanyia kazi malalamiko yale kwa kumteua Jaji Filmin Matogoro kutoka Mahakama ya Uhujumu Uchumi aende akasikilize kesi ile. Jaji Matogoro akaanza kuisikiliza kesi ile Aprili 2, 2019.
Upande wa mashtaka uliongozwa na wakili msomi wa Serikali Joseph Pande akisaidiwa na mawakili wasomi wa Serikali Abdallah Chaula, Omary Kibwana na Lucy Kyusa.
Upande wa mashtaka ulisimamisha mashaidi 34, pamoja na vielelezo halisi 15 ambavyo ni simu, kadi za simu, nguo za marehemu na panga. Vielelezo vya nyaraka vilikuwa ni 16 ambavyo ni ripoti ya daktari, ripoti za vinasaba na maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza.
Mashaidi wa Jamhuri walikuwa ni wazazi wa Humphrey, muuguzi wa hospitali ya Mawenzi aliyepokea mwili, mfanyakazi wa manispaa aliyezika na kuufukua mwili, mkemia wa Serikali na daktari aliyechunguza mwili.
Utetezi uliwakilishwa na mawakili wasomi David Shilatu, Elikinda Kipoko na Gwakisa Sambo.
Mshtakiwa ayakana maelezo
Wakati wa usikilizaji wa kesi mshtakiwa wa kwanza Hamis Chacha aliyakataa maelezo yake ya ungamo kuwa hayakuchukuliwa kwa hiyari yake bali baada ya mateso ikiwa kuchomwa na pasi, kuingizwa chupa njia ya haja kubwa nakadhalika.
Malalamiko haya yaliilazimu mahakama kuendesha shauri dogo ndani ya kubwa ili kuona kama inaweza kuyapokea maelezo yale. Baada ya kuendesha shauri dogo, jaji alitupilia mbali hoja ya utetezi na kupokea kielelezo cha ungamo.
Kwenye kesi kubwa Chacha alijitetea kuwa wakati anamkimbiza Humphrey alikuwa amelewa hivyo hakuwa katika hali ya kuweza kufanya maamuzi sahihi pia alikana kushiriki kutupa mwili wa Humphrey mtoni.
Hukumu ya kesi hii ilitolewa tarehe Juni 3, 2019, kwa Mheshimiwa Jaji Matogoro kumtia hatiani mshitakiwa wa kwanza Hamisi Chacha kwa mauaji ya kukusudia na kumuhukumu kifungo cha maisha.
Edward Shayo na Mwalimu Labani walikutwa na hatia ya kuficha taarifa za uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja.
Ilikuwa kidogo utokee ugomvi mkubwa nje ya Mahakama wakati wahukumiwa wanapelekwa gerezani pale Kingsize alipopaza sauti kwa baba wa Humphrey Makundi na kumwambia hana hatia na damu ya mwanae.
Fortunatus Buyobe ni mwandishi binasfi wa habari za uchunguzi jinai na siasa. Anapatikana kupitia ukurasa wake wa twitter @fbuyobe au kwa njia ya ujumbe mfupi kwa namba +255 788 916 060. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.