The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Parachichi Inavyokimbiza Kilimo cha Kahawa Mbozi

Wakulima wanasema kilimo cha kahawa hakina tija na kinahitaji gharama kubwa zaidi kukiendeleza ukilinganisha na parachichi.

subscribe to our newsletter!

Songwe. Wakulima katika wilaya ya Mbozi mkoani hapa wametaja masilahi duni, gharama kubwa na muda mwingi wanaoutumia kuandaa zao la kahawa kama sababu kuu za “kulipiga chini” zao hilo la biashara na kukumbatia kilimo cha parachichi, zao walilolipachika jina la “dhahabu ya kijani.”

Utafiti mdogo uliofanywa na The Chanzo umebaini kwamba zao la kahawa, ambalo kwa miaka mingi ndiyo limekuwa utambulisho wa wilaya ya Mbozi, liko hatarini kupotea wilayani humo baada ya wakulima wengi kugeukia zao la parachichi ambalo wakulima wameiambia The Chanzo linawanufaisha zaidi kuliko zao la kahawa.

The Chanzo imetembelea baadhi ya mashamba ambayo kwa miaka mingi yalikuwa yakilimwa kahawa na ilichokutana nacho kwenye mashamba hayo ni miche au miti ya maparachichi.

Kwenye mazungumzo ambayo The Chanzo imefanya na wakulima ambao wameacha kulima kahawa na kukumbatia zao hilo la parachichi, ilibainika kwamba mbali na hatua hiyo kuchochewa na masilahi ya kifedha maagizo ya viongozi wa Serikali pia yamechangia.

Wakulima wameeleza kuchoshwa na kauli kinzani za viongozi wa Serikali kwa wakulima hao ambao mwaka huu wanaweza kuwaambia walime zao hili, mwaka unaofuata wanaambiwa walime zao lingine.

Hali nzuri ya soko 

“Hali ya soko [la parachichi] iko vizuri,” anakiri  Anyingulile Msyani, mmoja kati ya wakulima walioacha kulima kahawa na kuanza kulima parachichi. “Kampuni inakuja kuchuma [parachichi] yenyewe. Kahawa unachuma mwenyewe, unaanza kuivundika halafu uioshe, uikaushe halafu ndiyo uchambue chambue halafu ndiyo uipeleke kwenye soko. Huduma ya kahawa ni ngumu, ni nzito, [na] ni kubwa ukilinganisha na parachichi.”

Utafiti wa The Chanzo umebaini kwamba bei ya parachichi kwa sasa sokoni ni kati ya Sh1,500 na Sh2,000 kwa kilo moja ambapo kilo moja huwa na parachichi nne, lakini kama parachichi ililimwa kwa kufuata taratibu za kitalaamu kilo moja huwa na parachichi tatu.

Lakini kwa upande wa kahawa, wakulima wamelalamika kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita bei ya zao hilo la biashara ziliwapa changamoto kubwa kwani bei ya kahawa ilifika mpaka Sh2,300 kwa kilo, kitu ambacho kimewavunja moyo wakulima wengi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Maparachichi Wilaya ya Mbozi (UWAMAMBO) Bernard Wazingwa alipoulizwa kuhusu Wilaya ya Mbozi kupoteza utambulisho na historia kupitia kilimo cha zao la kahawa alisema hakuna maana yoyote kama utaendelea kung’ang’ania historia wakati unateketea kiuchumi.

Huwezi kung’ang’ani historia

“Historia bila shibe haina maana,” anasema. “Basi kama ni historia ije kwa nini tulilima kahawa? Tulilima ili tujimudu kimaisha. Basi limekuja zao lingine ambalo linaipita kahawa. Kwa hiyo, hatuwezi kuishikilia kahawa kama sijui jina la ukoo au nini. Tulilima kahawa ili tupate pesa, sasa parachichi linatoa pesa zaidi kuliko kahawa.”

Pia, ameungana na Bwana Msyani kwa kukiri kuwa tija ya kilimo cha parachichi ipo juu kulinganisha na kilimo cha kahawa ambapo amesema kupitia zao jipya la parachichi unaweza kusomesha watoto hata kujenga bila shida.

“Kilimo cha parachichi kinatija zaidi kwa mkulima, kinaweza kikamlipa zaidi kuliko kilimo cha kahawa,” ameendelea kufafanua. “Kwa hiyo, kutokana na parachichi mtu anaweza akajimudu, anakajenga nyumba nzuri, akasomesha watoto na kwa gharama ndogo. Siyo kilimo cha thulubu kama ilivyo kahawa na mazao mengine.”

Daudi Lyela  ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maisha Daily, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya afya na kilimo mkoani hapa ambaye anabainisha kwamba mbali na bei ya kahawa kuwa ndogo pia wakulima wanalipwa kwa kuchelewa sana, na hata wanapozipata hizo fedha inakuwa hazikidhi mahitaji ya kugharamia maisha yao na zao hilo la kahawa.

“Tunaona kwamba wale wakulima ambao walikuwa ni wakongwe, wakulima tuseme ambao kwa sasa ni wazee ambao enzi hizo walinufaika na kahawa miaka ya 90 na 80, sasa hao ndiyo watu wa kwanza kukataa kahawa,” anasema Lyela wakati akizungumza na The Chanzo kwa njia ya simu.

Mtaalamu wa Kilimo na Umwagiliaji kutoka Wilaya ya Mbozi Aloyce Madaraka amekiri kuwepo kwa wakulima wanaoacha kulima kahawa na kulima parachichi, akihusanisha hali hiyo na tija inayotokana na zao hilo bali pia gharama nafuu za uzalishaji wake.

“Kwa mfano, kuna mtu anaweza akawa na miti yake ya maparachichi, labda heka moja, unakuta anaweka mbolea mara moja au wakati mwingine asiweke kabisa lakini bado akaendelea kuvuna na kupata kipato kukubwa kulinganisha na mkulima wa kahawa ambaye asipoweka mbolea kila mwaka basi uzalishaji wa unapungua,” anasema Madaraka.

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 responses

  1. Nami ni mkulima wa parachichi mbozi (vwawa -nyimbili) ekari tatu na nusu ambazo nimezipanda mwaka huu na mwakani nategemea kupanda nyingine

    1. Bwana Massawe naomba kujua mtaji wa kuanza kilimo cha parachichi kwa ekari inagharimu fedha kiasi gani,mm naishi Mbarali Ila nyumbani ni Mbozi Npo serious nataka kulima parachichi msimu ujao wa 2022/2023.naomba mchanganuo wa kila kinachohitajoka!

  2. Habari za leo. Mimi nimedhamiria kulima Parachichi Kisasa maeneo ya Madeke – Njombe na Mapanda – Mafinga. Ninaomba kumpata mtaalam wa kilimo hicho mwenye sifa za kitaalam.
    Asante

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts