The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Ilipanga Kukusanya Shilingi Bilioni 228 Kupitia Tozo za Miamala ya Simu. Imeweza Kukusanya Shilingi Bilioni 64 Tu

Hii ni kwa kipindi cha Julai mpaka Septemba 2021 tu.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Serikali imeweza kukusanya Shilingi bilioni 64.4 tu, sawa na asilimia 28 ya lengo ililokuwa imejiwekea la kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 228.1 kama mapato kutoka kwenye tozo za miamala ya simu kati ya Julai na Septemba 2021.

Hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Utekelezaji wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ambayo  hata hivyo haielezi hali hiyo ya kutokufikia lengo ililojiwekea inaweza ikawa imesababishwa na nini. Ilitakiwa kupatikana walau bilioni 76 kila mwezi ili kufikia lengo la billioni 228 mwishoni mwa Septemba 2021.

Hata hivyo, tangu kuanzishwa kwake kufuatia marekebisho ya Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, Sura namba 306, tozo hizo zilizobandikwa jina la ‘Tozo ya Uzalendo’ haijawahi kuungwa mkono na wananchi waliowengi.

Na ukinzani huu haukupungua hata pale Serikali ilipoamua, kufuatia ukinzani mkubwa na mjadala mpana juu ya tozo hizo, kupunguza viwango vya tozo hiyo kwa asilimia 30.

Kufuatia uanzishwaji wa tozo hizo, wananchi wengi waligusia kufikiria kuacha kutumia simu kama njia ya kutuma na kupokelea pesa na badala yake watatumia njia za asili kama vile kuchukua daladala au bodaboda kufanikisha mchakato huo.

Wakati ni vigumu kuthibitisha moja kwa moja kwamba ni kweli watu wameamua kuchukua uamuzi huo, kwa sababu bado hakuna utafiti uliofanywa kwenye eneo hilo, taarifa kutoka kwenye makampuni ya simu zinaonesha kwamba kuna uwezekano kwamba hicho ndicho wananchi walichofanya.

Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania PLC, kwa mfano, ilibainisha hivi karibuni kwamba miamala iliyofanyika kupitia huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa kutumia simu ya mkononi ya kampuni hiyo M-Pesa imeshuka kwa asilimia 24.8.

Vodacom imebainisha hilo kwenye taarifa yake ya fedha ya robo ya mwisho wa mwaka 2021 ambapo inaonekana kwamba kampuni hiyo iliwezesha kufanyika kwa miamala yenye thamani ya Shilingi trilioni 14.2 katika robo ya mwisho ya mwaka 2021.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sababu inayoelezwa kuchochea anguko hilo la miamala ni tozo zinazotozwa kwa Watanzania pale wanapofanya miamala kwa kutumia simu za mkononi.

“Pamoja na punguzo la tozo, thamani na kiwango cha miamala bado ni kidogo kulinganisha na kipindi kabla ya tozo,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya Vodacom. “Ni kwa sababu ongezeko la tozo bado linachangia gharama kwa mtumiaji wa mwisho.”

Ni katika muktadha huu basi wadau mbalimbali wameendelea kuisihi Serikali kuangalia kwa jicho la pili suala hilo la tozo za miamala ya simu na kutafakari utekelezaji wake.

Moja kati ya wadau hawa ni Chama cha Watoa Huduma za Simu za Mkononi Tanzania (TAMNOA) ambacho kufuatia kikao kati yake na Mawaziri wa Fedha na Mawasiliano kilichofanyika Februari 2, 2022, waliishauri Serikali kuangalia vyanzo vipya  sehemu zenye vipato vikubwa na kutoa ahueni kwa wenye kipato kidogo.

Kikao hicho kililenga kupata maoni ya TAMNOA juu ya bajeti ya Serikali 2022/2023.

Moja ya vyanzo vilivyotajwa na TAMNOA ni makampuni makubwa ya dunia ambayo licha ya kuwa hayana ofisi nchini, huduma zao zinatumiwa na Watanzania na kuyaingizia makampuni hayo faida.

Hii, hata hivyo, haikuwa mara ya kwanza kwa TAMNOA kuisihi Serikali kufikiria upya uamuzi wake wa kung’ang’ani tozo hizi.

Mnamo Julai 19, 2021, kwa mfano, aliyekuwa Mwenyekiti wa TAMNOA na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Hisham Hendi alinukuliwa akisema kwamba mamilioni ya Watanzania, hususan wale walioko vijijini, wameacha kutumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu kwa sababu ya tozo hizo.

“Mapato yameshuka kwa kasi kwa sababu wateja wameacha kutumia huduma zetu kama walivyokuwa wamezoea kutumia zamani,” alisema Hendi. “Tunaamini Serikali italiona hili na kuchukua hatua stahiki kwa sababu hii tozo inaathiri biashara na inawaumiza watu.”

Hiyo ilikuwa ni Julai 2021 na Serikali inaonekana haikuliona kama Hendi alivyokuwa anategemea. Labda inaweza kuliona sasa.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *