The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wachumi: Tutegemee Bei za Bidhaa, Huduma Kushuka 2022

Wachumi hao wanabainisha juhudi zinazoendelea kuchukuliwa duniani za kupambana na janga la UVIKO-19, ikiwemo matumizi ya chanjo; kukamilika kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali; pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha kama zitaendelea kama msingi wa matumaini yao hayo.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wasomi na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi nchini wanaamini kwamba bei za bidhaa na huduma muhimu zitapungua kwa mwaka 2022, kitu ambacho wanaamini kitaleta afueni kubwa kwa wananchi ambao wanaendelea kukabiliana na athari za mfumuko wa bei, hali ambayo haijaikumba Tanzania tu bali dunia kwa ujumla.

Wasomi hao wameelezea matumaini yao hayo wakati wakiongea na The Chanzo kwa nyakati tofauti kuhusu hali ya mfumuko wa bei inayoikabili Tanzania, hali iliyopelekea kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu, ikiwemo vyakula, vifaa vya ujenzi na bidhaa na huduma nyenginezo.

Wakitaja sababu zinazowapelekea kuwa na matumaini hayo ya kupungua kwa mfumuko wa bei, wachumi hao wametaja juhudi zinazoendelea kuchukuliwa duniani za kupambana na janga la UVIKO-19, ikiwemo matumizi ya chanjo; kukamilika kwa ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali; pamoja na mvua zinazoendelea kunyesha kama zitaendelea.

“Hii hali haiwezi kuendelea,” anabainisha Profesa Humphrey Moshi, mchumi mashuhuri nchini Tanzania na Mwenyekiti wa bodi ya Tume ya Ushindani Tanzania (FCC).  “Tunaona mambo ya UVIKO-19 yameanza kupoteza nguvu kwa sababu ya haya mambo ya chanjo. Kwa hiyo, tunaona huu mwaka tayari kuna neema.”

Mtazamo wa mfumuko wa bei Tanzania, kwengineko

Mnamo Januari 10, 2022, Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) ilitangaza kwamba mfumuko wa bei wa mwaka ulioishia Disemba 2021 umeongezeka kidogo kutoka asilimia 4.1 mpaka asilimia 4.2, hali ambayo NBS iliihusisha na ongezeko la bei la bidhaa na huduma mbalimbali.

Bidhaa za vyakula ambazo NBS ilisema bei zake ziliongezeka kwa mwezi Disemba 2021 zikilinganishwa na bei za mwezi Disemba 2020 ni pamoja na mchele, unga wa mtama, nyama ya ng’ombe, nyama ya mbuzi, mayai, viazi pamoja na vinywaji baridi.

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei mwezi Desemba 2021 ni pamoja na vifaa vya ujenzi, gesi zinazotumika kwa matumizi mbalimbali majumbani na makazini, mafuta taa, dizeli na petroli.

Hali ya kuongezeka kwa mfumuko nchini ilianza kuonekana mwezi Juni 2021 ambapo mfumuko ulifikia 3.6 na uliendelea kuongezeka mpaka Disemba 2021 ambapo ulifikia 4.2 ukiwa ni mfumuko mkubwa zaidi katika kipindi cha miaka minne.

Hali hii ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei haikuripotiwa nchini Tanzania tu kwani hata nchi zingine za Afrika Mashariki zilishuhudia kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma muhimu nchini humo.

Nchini Uganda, kwa mfano, mfumuko wa bei uliongezeka kutoka asilimia 2.6 mpaka asilimia 2.9 huku Rwanda ikisajili mfumuko wa bei wa asilimia 1.9 kutoka asilimia 1.

Sababu za mfumuko wa bei zatajwa

Kwa upande wa Tanzania, sababu mbalimbali zimeelezwa ambazo zinaweza kuwa zimechangia hali hii ya kuendelea kupanda kwa bei za bidhaa na huduma muhimu. Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwenye hotuba yake ya salamu za Mwaka Mpya mnamo Disemba 31, 2021, alitaja janga la UVIKO-19 na kupanda kwa bei ya mafuta duniani kama sababu zilizochochea hali hiyo.

“Mlipuko wa UVIKO-19 ulipelekea viwanda vingi [duniani] kusimamisha uzalishaji na hivyo kusababisha uhaba na ongezeko kubwa la uhitaji wa bidhaa,” alisema Rais Samia aliyeshika hatamu za uongozi mnamo Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli.

“Kwa hapa nchini,” aliendelea kusema Rais Samia kwenye hotuba yake hiyo, “mfumuko huo wa bei ulichagizwa zaidi na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliotoa kiasi cha Shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu, maji safi na salama ambao ulisababisha upandaji wa bei za vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo na mabati.”

Kuna sababu nyengine pia. Profesa Moshi, kwa mfano, anaamini kwamba hali ya ukame iliyoikumba Tanzania kwa siku za hivi karibuni inaweza kuwa ni sababu nyengine inayohusika na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu, hususan vyakula.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, zaidi ya watu milioni mbili kutoka mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga wanakabiliwa na athari zitokanazo na ukame uliodumu kwa zaidi ya miezi minne mpaka sasa.

Taarifa hiyo ilitolewa siku chache tu baada ya vyombo vya habari nchini kuripoti kufa kwa mifugo zaidi ya 62,000.

“Tanzania imekumbwa na ukame,” Profesa Moshi anaieleza The Chanzo. “Na ukame huo ukafanya mazao kadhaa yakaadimika au yakawa machache, uzalishaji ukawa mdogo kwa hiyo nayo ikachangia huo mfumuko wa bei.”

Profesa Moshi pia anaamini kwamba hali hii ya kupanda kwa bei kunatokana na hatua ya baadhi ya wafanyabiashara ambao waliamua kupandisha bei za bidhaa zao licha ya kutoathirika na chochote katika soko lao, kwa sababu tu bidhaa nyingine zilipanda.

Dk Vincent Mughwai ni mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam anayehusisha hali ya mfumuko wa bei unaoendelea kwa sasa nchini na kile anachokiita “kuendelea kushuka kwa thamani ya pesa yetu dhidi ya dola na fedha nyingine za kigeni.”

Kwa mujibu wake, hali hii imepelekea bidhaa kuwa ghali kutokana na thamani ya pesa shilingi ya Tanzania kushuka.

Sababu za kuwa na matumaini

Lakini angalau sababu tatu zimetolewa na wachambuzi za kwa nini Watanzania wawe na matumaini kwamba hali haiwezi kuendelea hivi kwa mwaka 2022. Sababu ya kwanza ni hiyo inayobainishwa na Profesa Moshi ya vita inayoondelea dhidi ya janga la UVIKO-19, hususan kupitia chanjo, ambazo msomi huyo anaamini zitakuwa na athari chanya katika kuimarisha uchumi wa dunia.

“Endapo kama watu wengi nchini Tanzania na duniani kwa ujumla wakipata chanjo [dhidi ya UVIKO-19],” anasema Profesa Moshi. “[Basi] nguvu kazi ya uzalishaji wa bidhaa itakuwa salama, hivyo uzalishaji wa bidhaa utaongezeka katika masoko ya ndani na nje ya nchi.”

Profesa Moshi pia anategemea kukamilika kwa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo Tanzania inatekeleza kuchangia kushusha bei za bidhaa na huduma muhimu.

Miradi hii ni pamoja na mradi wa ufuaji umeme wa Nyerere, Rufiji; ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge; upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi, Mwanza; ujenzi wa Daraja la Tanzanite, Dar es Salaam; ujenzi wa Makao Makuu, Dodoma, unaohusisha ujenzi wa Ikulu ya Chamwino; upanuzi wa barabara za viwanja vya ndege; na barabara kadhaa zinazounganisha mikoa na wilaya za Tanzania.

The Chanzo ilimuuliza Dk Timothy Lyanga wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni kitu gani kitokee ili utabiri wa Profesha Moshi wa kushuka kwa bei za bidhaa na huduma utimie ambaye alibainisha kwamba ni kuomba mvua zinazoendelea kunyesha ziendelee.

“Kilimo chetu kinategemea mvua, hatujawa na kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika,” anasema Dk Lyanga. “Maana yake ni kuombea sasa hizi mvua zinazoendelea kunyesha taratibu ziendelee kuwepo ili kuhakikisha watu wameweza kulima mazao mbalimbali ya biashara na ya chakula. Hapo hapatakuwa na upandaji wa bidhaa mbalimbali.”

Dk Lyanga pia anashauri, ili kupambana vizuri na mfumuko wa bei, Tanzania inapaswa kuuza vitu vingi nchi za nje kuliko inavyonunua na kuingiza nchini, akisisitiza uwekezaji zaidi kwenye sekta za kilimo na viwanda.

“Ni lazima tuwe tunauza zaidi nje kuliko kuingiza,” anasisitiza msomi huyo wa uchumi. “Maana yake ni kwamba tunapokuwa tunauza nje tunapata fedha nyingi za kigeni ambazo zinakwenda sasa kuhakikisha hii mitikisiko haiwezi kutokea.”

Tayari mambo kadhaa yanaonyesha hali ya uuzwaji bidhaa na huduma nje inaendelea kuimarika. Kati ya Julai na Septemba 2021 mauzo nje ya nchi yaliimarika kufikia dola za kimarekani bilioni 2.7 hii ikiwa ni ongezeko ukilinganisha na dola bilioni 2.1 katika kipindi kama hicho 2020.

Sehemu kubwa ya ongezeko hili la mauzo nje likichangiwa na urejewaji wa biashara katika utalii ambapo mpaka mwishoni mwa Disemba 2021 hali ilionekana kuendelea kurejea kama awali.

Vilevile kuendelea kuimarika kwa soko la dhahabu duniani pamoja na kukua kwa uzalishaji nchini kunaendelea kuimarisha uuzwaji wa bidhaa nje. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita dhahabu  imeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato mengi yanayopatikana kwa uuzwaji wa bidhaa nje ya nchi.

Kwa mwaka 2020/2021 mauzo  ya dhahabu nje yaliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 3 sawa na takribani shilingi trilioni 7.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts