Mwanza. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa kituo cha afya katika kata ya Idetemya, tarafa ya Usagara, wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza sasa inategemewa kukamilika tarehe 28 Febrari, 2022. Mradi huo unaogharamiwa kwa fedha za tozo unatarajiwa kuwa na awamu mbili huku awamu ya kwanza ikielekea kukamilika.
Kulingana na taarifa ya TAMISEMI iliyotolewa tarehe 22 Augusti 2021, Usagara ni miongoni mwa tarafa tano kwenye mkoa wa Mwanza zilizopata mgao wa fedha hizo katika awamu ya kwanza. Tarafa nyingine ni pamoja na Ngula (Kwimba), Maisome (Buchosa), Katunguru (Sengerema) pamoja na Buhongwa (Nyamagana).
Akizungumza na The Chanzo Janauri 28, 2022, Paulo Francis Shori ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho, amesema mpaka sasa mradi umefikia zaidi ya asilimia 70.
“Mradi wenyewe ulikuwa umetazamiwa kukamilika mwezi wa kwanza, tarehe kumi tungekabidhi majengo hayo. Lakini hatukuweza kukamilisha. Hivyo tunatarajia sasa kukamilisha tarehe 28 ya mwezi wa pili.” Amesema Paulo na kuongeza kuwa upatikanaji duni wa vifaa vya ujenzi hasa saruji ni moja kati ya sababu zilizochelewesha mradi huo.
“Ilifikia wakati saruji haipo, tunapoagiza haifiki kwa wakati. Tulijaribu kuagiza kila sehemu lakini ilichelewa kufika kwa hiyo tumechelewa kukamilisha kwa sababu ya vifaa kama saruji.”
Shori ambaye pia ni Mwenyekiti wa kijiji cha Idetemya ametoa ufafanuzi wa matumizi ya fedha za awamu ya kwanza ambazo ni shilingi milioni 250 ambazo zimetumika kujenga jengo la Wagonjwa wa nje pamoja na Maabara huku wakitarajia kupokea fedha za awamu ya pili kukamilisha jengo la Upasuaji, Wodi pamoja na Chumba cha kuhifadia maiti.
Kituo hicho cha afya kikishakamilika kinatarajiwa kuwanufaisha wananchi wa tarafa ya Usagara ikiwa ni tarafa pekee ndani ya wilaya ya Misungwi ambayo haikuwa na kituo cha afya. Kabla ya ujenzi wa kituo hiki cha afya, tarafa ya Usagara ilikuwa na zahati moja ya Idetemya ambayo imejengwa kabla ya Uhuru ikihudumia watu zaidi ya 35,000.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Misungwi Kashinje Machibya Erasto, ameiambia The Chanzo kuwa tayari amekwisha iagiza kamati ya ujenzi waongeze kasi kwani hapo awali waliamua kuwekeza nguvu kwenye ujenzi wa madarasa kutokana na upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama saruji kupungua.
Machibya ambaye pia ni Diwani wa kata ya Usagara (CCM) ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kushiriki katika miradi ya maendeleo ikiwemo kituo hicho cha afya; “Sasa hatuna kikwazo kingine cha kuendelea kutuchelewesha, kwa hiyo tumetoa muda kwamba kufikia tarehe 28 mwezi wa pili, kituo cha afya hiki kwa haya majengo ya milioni 250 yawe yamekamilika.”
Wakizungumzia ujio wa mradi huo, baadhi ya wakazi wa kata ya Usagara wametoa shukurani zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa kituo cha afya. Kwani kwenye kata ya Usagara ndilo lilikuwa hitaji lao muhimu ukizingatia kata hiyo ndiyo yenye wakazi wengi ndani ya tarafa.
“Huduma nyingi tunapata katika hospitali ya wilaya [iliyopo katika mji wa Misungwi] kama huwezi kwenda huko basi utaenda Butimba [Nyamagana] ambako ni mbali. Kwa kuwa wanatujengea [kituo cha afya] hapa karibu itatusaidia.” Amesema Leticia James mkazi wa Usagara.
Jofrey Cosmas ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Mwanza, Tanzania. Anapatikana kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni cosmasjofrey54@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.