The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali Wilayani Mbozi Yadaiwa Kuhamisha Wananchi kwa Nguvu Kupanua Hifadhi ya Kimondo

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inalenga kuipanua hifadhi hiyo kwa ajili ya kutenga eneo maalum ambalo wanyama mbalimbali watawekwa na hivyo kukifanya Kimondo cha Mbozi kuwa eneo la utalii kwa mkoa wa Songwe.

subscribe to our newsletter!

Mbozi. Mgogoro mkubwa unaendelea kati ya wananchi wa kijiji cha Isela, wilayani Mbozi, mkoani hapa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kufuatia uamuzi wa mamlaka hiyo kutaka kuwahamisha wananchi wapatao 1,300 kutoka kwenye makazi yao ya asili kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Kimondo.

Hifadhi ya Kimondo, iliyopo katika kijiji cha Ndolezi, Kitongoji cha Isela, wilayani Mbozi, ipo chini ya NCAA ambayo inalenga kuipanua hifadhi hiyo kwa ajili ya kutenga eneo maalum ambalo wanyama mbalimbali watawekwa na hivyo kukifanya Kimondo cha Mbozi kuwa eneo la utalii kwa mkoa wa Songwe.

Juhudi za kutaka kuwahamisha wananchi hao wa Isela ambapo NCAA inataka kufanya upanuzi huo zimekuwa zikiendelea kwa takriban miaka mitatu sasa angalau tangu mwaka 2020 bila mafanikio yoyote kutokana na ukinzani mkubwa kutoka kwa wananchi ambao wamegoma kutoka kwenye eneo lao hilo.

Wakati zoezi hilo mwanzoni lilitarajiwa kuwa la hiari, na kwamba NCAA ilibainisha kwamba italipa fidia kwa wale watakao kuwa tayari kuhama, uchunguzi wa The Chanzo umebaini kwamba zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa nguvu kwa siku za hivi karibuni, huku Jeshi la Polisi likidaiwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika.

Wananchi wakimbilia maporini

Mnamo Februari 8, 2022, majira ya saa tisa za mchana, The chanzo ilifika eneo maarufu katika kitongoji cha Isela lijulikanalo kama Centre ambapo wananchi kutoka sehemu mbalimbali za kijiji huja kujitafutia huduma mbalimbali za kijamii na kukuta eneo hilo likiwa tupu na kugubikwa na ukimya mkubwa, huku maduka kadhaa yakionekana kuwa yamefungwa.

Eneo la centre ambalo kwa kawaida huwa ni eneo lenye shughuli mbalimbali likiwa katika hali ya ukimya wa kipekee

Mbali na kuwa eneo hilo halikuwa na mtu hata mmoja, pia The Chanzo ilishuhudia uharibifu wa maduka yaliyokuwepo hapo, huku mengine yakionekana kuwa yametolewa milango, na mengine ni madirisha ndiyo yaliyoharibiwa.

Atanas Andrea Cheyo ni mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Isela ambaye The Chanzo ilikutana naye kwa bahati wakati ikitembelea eneo la Centre ambaye aliweza kueleza chanzo cha hali hiyo akisema ni hatua ya Jeshi la Polisi kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wananchi waliokuwa wanagoma kuhamishwa, hali iliyosababisha wananchi kadhaa kukimbia makazi yao na kukimbilia msituni.

“Wananchi wanatakiwa watwae eneo lao kwenda kwenye Serikali na wao wananchi wameshakataa kufanya jambo hilo,” anasema Cheyo akiwa ameongozana na The Chanzo kwenda kuonana na baadhi ya wananchi walioko mafichoni.

Nyumba yake mwenyewe imepasuliwa vioo na mlango wakati wa taharuki iliyosababishwa na polisi. Akiongea kwa sauti ya huzuni, Cheyo anasema: “[Serikali] inadai italipa fidia, lakini haisemi shilingi ngapi. Haisemi ng’ombe watalipwa shilingi ngapi. Huo ndiyo msingi wa mvutano.”

Baadhi ya mali zilizoharibiwa katika zoezi hilo lililofanywa na Polisi

Tutazikwa hapa hapa

Baada ya kugoma kwa muda, wakidhani mwandishi wa makala haya ni askari, The Chanzo hatimaye iliweza kuongea na wananchi hao waliokuwa mafichoni. (Inaripotiwa kwamba, baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa wa polisi ambao wamekuwa wakija na kuwatisha na kuwanyanyasa wananchi wamekuwa wakivaa nguo za kiraia).

“Tumekuwa tukiishi hapa kwa takriban karne nzima sasa, ukihesabu na wazazi wetu walio makaburini,” Emmanuel Mwamwezi, ambaye ameshuhudia mlango wa nyumba yake ukivunjwa, ndoo zote za maji kutobolewa na magodoro kuloweshwa, anasema. “Hapa ni nyumbani kwetu. Tutazikwa hapa hapa. Hatuna mahali pengine pa kwenda.”

Charles Mwashambwa, mkazi mwingine wa kijiji cha Isela, ameihusisha hali ya ukosefu wa amani kijijini hapo na vitendo vya maofisa wa Jeshi la Polisi. Anafafanua: “Hapa [kijijini] hakuna amani. Usalama majumbani haupo. Kuna baadhi ya watu yaani wametoa vitu kabisa ndani. Ng’ombe wamezifungua, wametoka nazo. Wanaogopa kwa sababu maaskari hapa wanatutishia. Kila siku usiku ni lazima wafike.”

Moja ya mkazi wa Isela aliyeathirika katika zoezi hilo la Polisi

The Chanzo ilimuuliza Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Janeth Migomi kwa nini maafisa wa jeshi hilo wamekuwa wakivunja nyumba za watu huku wakiwa wamevalia kiraia. Wakati Migomi alikiri maafisa wake kwenda kijiji cha Isela wakiwa wamevalia nguo za kiraia, alikanusha tuhuma za askari wa Jeshi la Polisi kuvunja nyumba za wananchi.

“Hakuna hicho kitu, hakipo,” alisema Migomi kuhusu madai ya polisi kuvunja nyumba. “Na nikwambie tu ndugu mwandishi kuwa sisi Jeshi la Polisi ile siku ya tukio tulienda pale kwa sababu wananchi walikuwa wamefanya uharibifu na tuliwakamata watu watano. Tunao [mikononi mwetu hivi sasa].”

Japhet Hasunga ni mbunge wa jimbo la Vwawa linalojumuisha kijiji cha Isela kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) anayeamini kwamba mgogoro huo unaweza kumalizwa endapo tu kama mamlaka za nchi zitakaa chini na wananchi wanaokataa kuhama na kufanya nao mazungumzo.

“Haya mambo ya kutumia nguvu hapana,” alisema Hasunga aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo wakati akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu. “Ili uhame lazima uwe umefidiwa. [Uwe] umefanyiwa tathmini na umeambiwa thamani ya mali zako ni hizi na utapewa hiki.”

Hasunga aliongeza kwa kusema kwamba ardhi yote ni mali ya Serikali na kwamba kama Serikali itataka kupanua hifadhi basi lazima taratibu za kawaida zizingatiwe na wananchi waondolewe kwa utaratibu unaokubalika, ikiwemo kupatiwa fidia zao.

Kutoka Mbozi mpaka Ngorongoro

Taarifa kwamba Serikali inataka kuhamisha watu kwa nguvu katika kijiji hicho cha Isela wilayani Mbozi zinakuja wakati ambao kuna taarifa pia kwamba Serikali imepanga kuwahamisha Wakazi  kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro, ikisema kwamba kuendelea kuwepo humo na kufanya shughuli zao za kibinadamu kunahatarisha hifadhi hiyo kupoteza hadhi yake.

Mjadala mkubwa unaendelea nchini hivi sasa ambapo wadau wamegawanyika sehemu mbili kati ya wale wanaotaka watu hao wabaki kwenye eneo hilo na wale wanaotaka waondolewe na kupelekwa sehemu nyengine. Joseph Oleshangay ni wakili na mwanaharakati ambaye amekuwa akijihusisha kwa karibu sana na vuguvugu la kushinikiza Wamasaai wabaki kwenye eneo hilo.

The Chanzo ilimuuliza Oleshangay, ambaye asili yake ni kutoka Ngorongoro, kama anaona mfanano wowote kati ya kile wananchi wa Isela wanakabiliana nacho na kile wao kama Wamasaai wanakumbana nacho huko Ngorongoro.

“Kuna uhusiano mkubwa,” alijibu Oleshangay ambaye anafanya kazi na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). “Matukio yote mawili yanadhihirisha jinsi ambavyo mamlaka zetu za nchi zisivyozingatia masilahi ya binadamu pale zinapojaribu kuchukua hatua zinazoitwa za kiuwekezaji, hatua zakuziingizia mamlaka hizo fedha.”

Fidia siyo kila kitu

Akizungumzia suala la fidia alilogusia Hasunga, kwamba watu wahame baada ya kulipwa fidia, Oleshangay anasema kwamba watu hawakatai kuhama kwa sababu hawalipwi fidia.

Anasema kwamba sababu kubwa inayowapelekea watu kukataa kutoka kwenye maeneo yao ni kwa sababu watu hao wanamahusiano ya kijamii na kiutamaduni na sehemu yao na hivyo kuwahamisha kwa lazima ni sawa na kukiuka haki zao za msingi za kibinadamu.

“Kuna watu inawezekana wanaabudu, kuna watu wameweka miili ya ndugu zao wakidhani kwamba ni nyumbani, kwa maana ni kwao, ndiko nyumbani kwao,” anabainisha Oleshangay.

“Nyumbani siyo sehemu yoyote yenye jengo,” anaongeza. “Ni sehemu ambayo unamahusiano nayo kama binadamu. Kwa hiyo, unapofikiria kuwaondoa ni lazima ufikirie siyo tu masilahi unayopata kama nchi kiuchumi lakini masilahi ya watu wale kiimani, kiutamaduni nakadhalika.”

Umuhimu wa ushirikishwaji

The Chanzo ilimtafuta Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dk Freddy Manongi ili kufahamu mikakati mamlaka hiyo itakayotumia kufanikisha zoezi lao hapo Isela baada ya wananchi kugoma kuhama lakini simu yake ilikuwa inaita tu bila kupokelewa.

Hata hivyo, akizungumza mnamo Januari 13, 2021, wakati wa mkutano wa kijiji hapo Isela baada ya wananchi kugoma kuhama, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dk Christopher Timbuka alikiri kwamba sehemu kubwa ya mgogoro unaoendelea kijijini hapo unasababishwa na uwepo wa ushirikishwaji mdogo wa wananchi kuhusu jambo husika.

“Kinachokosekana ni kwamba ushirikishwaji bado haujawa wakutosha,” alisema Dk Timbuka. “Kuna haja ya kujadiliana. Kujadiliana kwenyewe ndiyo kama hivi tulivyofanya [kwa kuwa na mkutano na wanakijiji]. Lazima [wananchi] wajue kwamba na sisi [watu wa hifadhi] tunathamini maoni yao.”

Alipoulizwa maoni yake kuhusiana na mgogoro huo, Atanas Andrea Cheyo, mwenyekiti wa kitongoji cha Isela, alisema: “Mimi ninachoomba ni kwamba Serikali isikie na ielewe kwamba suala hili wananchi walishalikataa. Isikilize. [Serikali] iwe inasikiliza na mawazo ya wananchi. Isikandamize kilio cha wananchi badala yake wakithamini.”

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *