Arusha. Mitandao ya kijamii inaendelea kubaki sehemu muhimu ambazo wanawake wajasiriamali Tanzania wanaweza kuzitumia kufanikisha malengo yao ya kibiashara licha ya uwepo wa changamoto kadhaa zinazoikumba biashara ya mtandao nchini.
Hayo yamebainishwa na Carol Ndosi, mjasiriamali na mdau wa maendeleo wakati akiongea na The Chanzo kuhusiana na namna bora wajasiriamali wanawake wanaweza kuzishinda changamoto zinazozikumba biashara zao mtandaoni ili kuzipeleka kwenye mafanikio wanayoyataka.
Hatua hiyo inafuata baada ya wajasiriamali wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya biashara zao mkoani hapa kulalamikia changamoto zinazozikabili biashara zao hizo, hali inayochangia kuwapunguzia faida na kurejesha nyuma kwa kiwango fulani juhudi zao.
Moja kati ya wajasiriamali hao ni Joyce Kimaro, 24, mkazi wa Njiro mkoani hapa anayejishughulisha na biashara ya kutengeneza na kuuza sabuni za maji zinazojulikana kama Jojo Multipurpose Soap kwa kutumia mitandao ya WhatsApp na Instagram.
“Changamoto kubwa ninayoiona mimi ya kutumia mitandao inahusu uaminifu,” anasema Joyce ambaye amekuwa akifanya biashara hiyo kwa kipindi cha miaka miwili sasa. “Kwamba wateja ni vigumu sana kukuamini na kukutumia hela ili wapate mzigo wao. Wanaona mtu anaweza akawa tapeli wa mtandaoni.”
Akitaja changamoto nyingine, Joyce anasema kwamba anadhani kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zake inachukua muda mrefu sana kwa biashara hizo kujulikana.
Changamoto ya kukosekana kwa uaminifu pia imetajwa na Anastasia Mtalemwa, ambaye amekuwa akitumia mitandao ya WhatsApp na Instagram kufanya biashara yake ya nguo tangu akiwa Chuo Kikuu.
“Watu wanakuwa wagumu kuamini bidhaa za mtandaoni kutokana na uzushi kwamba vitu vya mtandaoni mara nyingi siyo halisi,” anasema Anastasia. “Watu wana hofu kwamba wanaweza kuona nguo au viatu mtandaoni vizuri lakini ukiagiza inakuja bidhaa tofauti kabisa. Inafanya tuonekane wajasiriamali wa mitandaoni kama matapeli.”
Fursa zilizopo mitandaoni
Lakini kwa Carol Ndosi, ambaye amekuwa akifuatilia suala hili la biashara za mtandaoni kwa karibu sana, anaamini kwamba licha ya changamoto hizi ambazo anakiri kuwakumba wajasiriamali wengi, wengi kati yao wameweza kuboresha biashara zao kwa kutumia mitandao ya kijamii kiasi cha kuweza kuwa na ofisi zenye anuani zinazofikika.
“Kuna fursa kubwa sana ya kukua zaidi ya hapo kwa kuzipanua biashara zao kwa kutumia nyenzo muhimu za masoko ya kidijitali na kufanya majukwaa hayo yafanye kazi kwa ajili ya wajasiriamali,” Ndosi anaieleza The Chanzo.
Tanzania inakadiriwa kuwa na watumiaji wa intaneti wapatao milioni 28.47 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2021 kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), huku Watanzania takriban 51.29 wakiripotiwa kutumia simu za mkononi, kitu ambacho Ndosi anaamini ni mwelekeo mzuri kwa wajasiriamali wa mtandaoni.
“Ni muhimu kwa hawa wajasiriamali wachanga kufahamu zana mpya za kidijitali zinazoendelea kubuniwa ili waweze kuzitumia kwenye kutangaza na kukuza biashara zao,” Ndosi anaieleza The Chanzo. “Zana hizi zinaweza kuwasaidia kufanya bidhaa zao zionekane zaidi kwa wateja au hata kuongeza mwingiliano kati ya wajasiriamali hao na wateja wao.”
Changamoto zipo na mafanikio pia
Mbali na kukumbana na changamoto mbalimbali, wajasiriamali wanaotumia mitandao kufanya shughuli zao ambao The Chanzo imeongea nao wanakiri kwamba mitandao ya kijamii imekuwa mkombozi kwao kwani imewasaidia kuendesha maisha yao kiurahisi.
“Binafsi naona ni vizuri kutangaza biashara yako na kufanya biashara mtandaoni,” anasema Joyce wa Jojo Multipurpose Soap. “[Mitandao] inasaidia sana kwani huu ni ulimwengu wa kidijitali. Watu ni rahisi kuingia Instagram na kuagiza bidhaa fulani kuliko kwenda dukani.”
Mama Khairat anakiri kwamba biashara yake ya ‘mama ntilie wa kidijitali’ imemsaidia kuendesha maisha yake, kama vile kulipa kodi ya nyumba, kuingia kwenye michezo mbalimbali ya kukopeshana, na kuhudumia familia yake.
“Wito wangu ni kwamba wanawake wasiitumie mitandao ya kijamii kuangalia udaku au kuchati umbea tu,” anashauri. “Watumie [mitandao] kufanya biashara mbalimbali kwani wakifanya hivyo wataepukana na changamoto ya kuwategemea waume zao.”
Iman Hemed ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Arusha anayepatikana kupitia rashidiman377@gmail.com.