Dodoma. Wito umetolewa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya maboresho ya kisheria na kisera ambayo yataweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali wanawake wanaofanya biashara kwenye mipaka mbalimbali iliyopo kwenye nchi zinazounda jumuiya hiyo za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani ya Kusini.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la EASSI lenye makao makuu yake Kampala, Uganda linalojihusisha na kuimarisha uwezo wa wanawake kiutawala na kiuchumi wanaamini kwamba sheria na sera ambazo zimekuwa zikipitishwa na vyombo vya EAC kama vile Sekretarieti na Bunge la Afrika Mashariki zimekuwa hazizingatii suala la jinsia pamoja na wafanyabiashara wadogo.
Hili lilidhihirika mnamo Februari 22, 2022, jijini hapa wakati wa mdahalo ulioandaliwa na mashirika hayo kujadili changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake wanaofanya biashara zao maeneo ya mipakani na kutafakari kwa pamoja namna bora za kutatua changamoto hizo kwa maslahi mapana ya wajasiriamali hao.
Kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na EASSI, wanawake wajasiriamali wengi (asilimia 68) wanaofanya biashara mipakani hutegemea biashara hiyo kama shughuli ya msingi ya kiuchumi.
Asilimia 42 ya wajasiriamali hawa hujihusisha na biashara za kilimo wakifuatiwa na wale wanaouza nguo (asilimia 21.5) na bidhaa zingine (asilimia 18.5).
Baadhi ya changamoto
Lakini wakati wa mdahalo huo ilibainika kwamba wajasiriamali hao wanakabiliwa na changamoto kubwa zinazowakwamisha kufikia malengo yao.
Hizi ni pamoja na ukosefu wa soko na mitaji; ukatili wa kingono na wanawake kukamatwa kimakosa mipakani na kutokupatikana kwa taarifa kuhusu biashara na viwango vidogo vya kujua kusoma na kuandika kwa baadhi ya wajasiriamali.
Changomoto nyingine zinahusiana na unyonywaji unaofanywa na mawakala dhidi ya wajasiriamali wanawake mipakani pamoja na kutokuwepo kwa uratibu wa pamoja kati ya nchi na nchi mipakani.
Sylivia Daulinge ni Meneja Mipango na Mikakati kuktoka TAMWA ambaye anaamini kwamba changamoto hizi kwa kiasi kikubwa zinatokana na sheria na taratibu zinazoongoza shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo hazitoi kipaumbele siyo kwa wajasiriamali wadogo tu bali pia kwa wanawake.
“Kuna sera na sheria ambazo zipo zinatungwa au zinatekelezwa lakini ukiangalia kwa upana wake zinawaangalia zaidi wafanyabiashara wakubwa na siyo hawa wakina mama,” Daulinge aliiambia The Chanzo pembezoni mwa mdahalo huo.
“Sera na sheria hizi kwa kiasi kikubwa zimewaweka nyuma wajasiriamali hawa. Unaweza kukuta kwamba hata wakati wa kutungwa kwake [hawa wajasiriamali] hawakuhusika,” ameongeza Daulinge.
Mabadiliko yanayotakiwa
Baadhi ya mabadiliko ya kisera na kisheria ambayo EASSI na TAMWA wamekuwa wakiishawishi EAC iyatekeleze kupunguza changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake mipakani ni pamoja na kupitiwa upya kwa Mfumo wa Biashara Uliorahisishwa wa EAC ili kukabiliana na athari za ugonjwa wa UVIKO-19.
EAC imetakiwa pia kuzingatia suala la jinsia wakati wa utoaji wa msaada wa kifedha na hatua nyengine kuwaokoa wafanyabiashara wadogo.
Wadau pia wanataka EAC iwasilishe tena katika Bunge la Afrika Mashariki kwa Mswada na Sera ya Usawa wa Jinsia na Maendeleo ya EAC pamoja na kuipitisha na kuitekeleza.
Hatua pia zichukuliwe kuimarisha ushirikiano wa usalama baina ya nchi na nchi mipakani. Pia kuwe na msukumo unaoonekana dhidi ya nchi wanachama wa EAC katika utekelezaji wa mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo pamoja na Mkataba wa Soko la Pamoja.
EAC pia imetakiwa kutunga sera na kuja na mkakati itakayotawala uvukaji wa mipaka ndani ya jumuiya hiyo na kuharakisha ufanikishwaji wa fedha ya pamoja ya EAC ili kuepukana na athari zitokanazo na kupanda na kushuka kwa thamani za fedha za nchi wanachama.
Mabadiliko mengine yanahusiana na uoanishwaji wa taratibu za kodi kati ya nchi wanachama; kuanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya mipakani; pamoja na kuharakisha upitiwaji mpya wa mfumo wa biashara uliorahisishwa wa EAC.
Kukomesha dhuluma
Suzani Kibandi ni Afisa Mradi Msaidizi kutoka EASSI ambaye aliiambia The Chanzo pembezoni mwa mdahalo huo kwamba hatua hizi ni muhimu kama EAC na nchi zake wanachama wamedhamiria kukomesha kile alichokiita “dhuluma” dhidi ya wajasiriamali wanawake wanaofanya shughuli zao mipakani.
“Kuna dhuluma wanawake [wa mipakani] wanazipitia,” anasema Kibandi. “Mama anaweza kufika [mpakani] akaambiwa atoe rushwa. Ndiyo maana unaona kuna ushawishi unaofanywa kubadilisha hali hii. Kwa mfano, hili la kuwa na madawati ya jinsia ni takwa lililoibuliwa na wanawake wajasiriamali wenyewe.”
Veronica Maro ni mjasiriamali mwanamke anayefanya biashara zake katika mpaka wa Horohoro ambaye anaamini kwamba hatua kama hiyo ya kuanzisha dawati la jinsia ni muhimu akibainisha tishio la ukatili wa kijinsia kwa wajasiriamali kama yeye ni kubwa sana.
“Unaweza ukavuka, ukakutana na askari anakwambia labda bila pesa fulani huwezi kupita hapa,” Maro anaiambia The Chanzo. “Zaidi ya hapo anaweza kukuomba mapenzi. Tayari anakuwa amesha kukosea adabu. Binafsi nilishakutana na hali hiyo lakini nilijitahidi kuwa ngangari na kurudi nilikotoka.”
Serikali itusaidie
Monica John, mjasiriamali mwengine anayefanyia shughuli zake mpakani, analalamikia kudaiwa ushuru usiyo rasmi na maafisa wa mipakani. Wanaposhindwa kutii amri hizo, basi huzuiliwa kufika eneo lao la biashara na hivyo kuathirika kama mjasiriamali.
“Serikali ituwekee njia rahisi ya kuvusha bidhaa zetu,” anaomba John. “Na kule kwenye masoko tunapo kwenda tusikutane na vipingamizi vya aina yeyote ili kwetu iwe rahisi kupambana na ukali wa maisha.”
Christopher Mramba ni Afisa kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ambaye katika wasilisho lake wakati wa mdahalo huo alibainisha nia ya Serikali kuwasaidia wajasiriamali hao kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri, ikiwemo kwa kuwaelimisha taratibu za kisheria wanazopaswa kuzifuata.
“Changamoto nyingi ni za uwelewa wa zile sheria zinazo tawala biashara na kanuni zinazotawala biashara,” alisema Mramba. “Siyo ngumu kiasi hicho [kuzielewa]. Ni suala la kuendelea na mashauriano ya aina hii kwa lengo la kuwawezesha kuzitambua na kuzielewa kanuni zenyewe na kuzifuata.”
Jackline Kuwanda mwandishi wa habari wa The Chanzo jijini Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.