The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kimesababisha Mgogoro wa Urusi na Ukraine?

Wengi wanaamini mlango wa mazungumzo unaweza ukafunguka tena. Hatua ya hivi karibuni ya nchi za ulaya na marekani kuzuia benki za Urusi kutumia mfumo wa kibenki wa swifti pamoja na NATO kuongeza majeshi karibu na mipaka ya Urusi inaweka shinikizo zaidi kwa Urusi kurudi kwenye mazungumzo.

subscribe to our newsletter!

Kwa wakazi wengi wa mji wa Kiev, Dnipro, Kharkiv na miji mingine ndani ya Ukraine kwa sasa wanaishi katika jinamizi. Wengi wangetamani lingekuwa ndoto walau liondoke wakiamka. Ila ndo maisha halisi. Urusi imeingiza vikosi vyake vya kijeshi Ukraine na kuamua kufanya vita.

Kwa takribani wiki tatu, nchi ya Marekani na washirika wengine wa NATO wamekuwa wakitoa taarifa zao za kiitelijensia kuwa Urusi itavamia Ukraine. Hata hivyo, Urusi iliendelea kukana mpango wa kuingia kivita Ukraine mpaka alipofanya hivyo Februari 24, 2022.

Mapambano katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev yanaingia siku ya tatu huku Rais wa Urusi Vladmir Putin akiwataka wanajeshi wa Ukraine kuacha kupigana na kuing’oa Serikali ya nchi yao au kujisalimisha. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, ameendelea kusisitiza watapigania nchi yao mpaka mwisho huku akiendelea kuyasihi mataifa mengine kutoa misaada na kuiwekea vikwazo vikubwa Urusi ili kuishinikiza iache kuvamia nchi yake.

Waukraine zaidi ya laki moja wameshakimbia nchi yao.  Je, tumefikaje hapa? Ni nini Urusi inataka na kwa nini dunia inaangalia kwa ukaribu mgogoro huu?

Wakazi wa Kharkiv wakiwa kwenye mahandaki ya chini ya njia ya treni ili kujikinga na mashambulio

Msukumo wa kihistoria na tamaduni

Ili kuelewa mgogoro huu unaoendelea ni muhimu kuelewa historia ya mahusiano ya nchi hizi pamoja na mwingiliano wa tamaduni kati yao. Historia ya Ukraine na Urusi inaenda miaka mingi nyuma hata kufikia karne ya 17. Lakini kwa uelewa wa haraka tuanzie miaka ya mwanzo ya 1990.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, Shirikisho la Soviet lilianguka. Shirikisho hili kitovu chake kilikua Urusi. Sovieti ilikua shirikisho la nchi takribani 15 ambazo ni Urusi, Ukraine, Georgia, Belorussia, Uzbekistan, Armenia, Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Moldova, Turkmenistan, Tajikistan, Latvia, Lithuania and Estonia.

Na pia kuna nchi zingine ambazo hazikuwa chini ya shirikisho lakini zilikua  chini ya utiisho wa Soviet, yaani Soviet akisema ruka wanaruka bila kuuliza, ambazo ni  Poland, Romania, Czechoslovakia, Hungary, Bulgaria, Ujerumani ya Mashariki, Yugoslavia na Albania.

Ramani inayoonyesha Shirikisho la Sovieti

Mawimbi ya nchi kujitenga na shirikisho la Sovieti yalisambaa miaka ya mwisho ya 80 mpaka mwanzoni mwa 90. Nchi nyingi zikaamua kutangaza uhuru wake. Hizi zinatajwa kuwa ni nyakati kubwa za aibu kwa Urusi ambapo hadhi yake kama ‘super power’ iliondolewa. Kama ilivyo kwa nchi zingine zilizojitenga, Disemba 1, 1991, wananchi wa Ukraine wanapiga kura ya maoni na kuamua kuwa taifa huru.

Hata hivyo, bado Ukraine wanabaki na uhusiano mkubwa na wa muhimu na Urusi. Wakati wa Sovieti sehemu kubwa za silaha za kinyuklia zilikua zinahifadhiwa nchini Ukraine.  Mwaka 1994, Ukraine iliamua kujihakikishia mamlaka yake kama nchi huru kwa kutoa  silaha zote za nyuklia zilizoachwa na Soviet na kusaini mkataba kwa masharti kuwa Urusi na mataifa mengine makubwa yataheshimu uhuru wake kama nchi.

Mkataba huo uliosainiwa na Urusi, Marekani na Uingereza unajulikana kwa jina maarufu kama Makubaliano ya Budapest. Baadhi ya wachambuzi wenye mrengo mkali wanachukulia hili kama kosa kubwa walilofanya Ukraine.

Ukiacha historia kati ya Urusi na Ukraine, jambo lingine la kuangalia ni mwingiliano wa tamaduni kati ya  watu wa Ukraine na watu wa Urusi.

Walau asilimia 20 mpaka 30 ya wakazi wa Ukraine wanaongea Kirusi kama lugha ya kwanza. Lakini majimbo ya Luhansk, Donetski na Crimea ni majimbo ambayo watu wanajitambulisha na kujitanabaisha kama Warusi pia. Crimea ina historia yake ya pekee.

Mpaka mwaka 1954, Crimea  ilikua sehemu ya Urusi, yaani pamoja na nchi zote  hizi kuwa chini ya Soviet, bado zilikua na mipaka. Kiongozi wa Soviet wakati huo aliamua kuigawa Crimea kwa Ukraine, hasa ikizingatiwa kigeographia Crimea imeungana na Ukraine haijaungana na Urusi.

Ukraine inavyopata uhuru, Crimea inabaki kuwa sehemu ya Ukraine. Tutaona umuhimu wa Crimea, Luhansk na Donetski katika sakata hili mbele kidogo katika makala hii.

Urusi na NATO

Nyakati za anguko la Shirikisho la Soviet zinatajwa kama nyakati za aibu kwa taifa la Urusi. Taifa lao liliabika hasa kwa kuwa na kiongozi aliyeitwa ‘mlevi,’ kuanguka kwa heshima yake kama ‘super power’ pamoja na ukata mzito. Toka wakati huo, Urusi imekuwa ikitafuta namna ya kurudisha hadhi na utukufu wake wa mwanzo.

Kuingia kwa Putin madarakani mwaka 2000, mwanainteligensia wa zamani aliyeweza kutiisha makundi mbalimbali ndani ya Urusi, pamoja na kufanikiwa kuirudisha Urusi kiuchumi, analeta sura mpya ya urudishaji wa hadhi ya mwanzo ya Urusi.

Urusi chini ya Putin inachangamka kwa namna ya kipekee na kuongeza ushawishi ndani na nje ya Urusi. Lakini kuna shida moja kwenye huu muonekano mpya wa Urusi: NATO.

NATO, ambao ni umoja wa kujihami wa nchi za Magharibi ukiongozwa na Marekani, inakuwa mwiba kwa Urusi kwa namna moja au mbili. Umoja huu uliundwa kwa lengo la kukabiliana na Shirikisho la Soviet (Urusi ya zamani).

Mataifa mengi yaliyoondoka chini ya Shirikisho la Sovieti kwa kuzingatia udogo walionao mbele ya Urusi, fursa za biashara na kutaka kulinda uhuru wao wanaamua kujiunga na umoja wa ulaya na pia NATO. Hii inajumuisha nchi kadhaa ambazo zimepakana ubavu kwa ubavu na Urusi.

Geographia ya Urusi ni tofauti na nchi zingine kubwa ambazo zina mipaka ya kigeographia kama mito na bahari zinazotenganisha nchi na nchi. Kwa Urusi sehemu kubwa ya mipaka yake zimetengwa na ardhi ya nchi zingine. Kwa miaka mingi Urusi imekuwa ikijihakikisha usalama wake kwa kuziweka nchi zinazoizunguka chini ya mbawa zake.

Mataifa kama Ukraine na Georgia nayo yanapata msukumo mbalimbali hasa kutoka kwa wananchi wao  juu ya kulandana na nchi za magharibi, jambo ambalo Urusi hairuhusu. Kwani kwa nchi hizi kujiunga na umoja wa ulaya au NATO, moja kwa moja zinadidimiza ushawishi wa Urusi. Hata hivyo, nchi hizi ni huru na zina haki sawa sawa na Urusi.

Urusi chini ya Putin inajiona imerudisha utukufu wake wa mwanzo. Kuzungukwa na NATO ni kama kumbukumbu mbaya ya nyakati za aibu jambo ambalo tutaona linavyokuwa sababu ya mzozo unaoendelea.

Watu wa Ukraine

Baada ya Ukraine kupata uhuru wake na kuamua kuwa nchi ya kidemokrasia inaingia kwenye mabadiliko kadhaa ya mfumo wa kitaifa.

Badiliko la kwanza ni badiliko la kiuchumi kutoka uchumi unaohodhiwa na dola mpaka kwenda kwenye uchumi huria. Mabadiliko haya ya kwenda kwenye uchumi huria yanafanywa kwa namna ambayo baadhi ya vikundi vya watu walio karibu ya uongozi ndio wanaokuwa wanufaika wakubwa.

Rushwa na ubadhirifu, utekwaji wa dola, ukiukwaji wa haki na kutofwatwa sheria vinagubika uongozi mpya. Kashfa kama ile ya uvujishwaji wa mazungumzo ya Rais Leonid Kuchma yaliyoonesha Rais akitoa maagizo ya mauaji ya mwandishi wa habari aliyekuwa akifichua rushwa Serikali, zinaghubika maisha ya Ukraine mpya.

Katika yote haya, viongozi wa Ukraine wanahakikisha wana mahusiano mazuri na uongozi wa Urusi kiasi kwamba hata wananchi wanahoji maswali juu ya uhuru wao kama nchi.

Rushwa inawasukuma watu wa Ukraine kutaka kuona mabadiliko. Wanataka kuwa na nguvu juu ya nchi yao na hatma zao.  Kumbuka, mfumo wa kiutawala wa demokrasia, au mfumo ambao unawapa nguvu zaidi watu, ni mfumo unaoendana zaidi na nchi za magharibi kuliko kwa upande wa Urusi.

Machoni kwa Urusi, hili si jambo zuri kwa mustakabali wa mahusiano kati ya Urusi na Ukraine.

Mwaka 2004, katika uchaguzi wananchi wa Ukraine wanaamua kuonyesha nguvu yao. Mawaziri wakuu wawili wastaafu Viktor Yushchenko and Viktor Yanukovych  wanagombania uchaguzi.

Uchaguzi huu unakuwa na mambo mengi ikiwemo kunywesha sumu kwa mgombea wa upinzani, Viktor Yushchenko, jambo ambalo lilimfanya kunusurika kifo na kubakia na sura iliyoharibiwa kabisa. Huku Urusi na wanainteligensi wa Ukraine wakirushiwa lawama juu ya jaribio hili la kumuaa Yushenko.

Viktor Yushchenko na Yuliia Tymoshenko wakati wa mapinduzi ya Orange

Hata hivyo, uchaguzi unafanyika na chama cha Viktor Yanukovych  kinashinda. Huyu alikua ni mgombea aliyependwa zaidi na Urusi. Kutokana na kasoro kubwa za uchaguzi, wananchi wanapinga uchaguzi huo na kupelekea kile kinachoitwa Mapinduzi ya Orange, ambapo wanaandamana mpaka uchaguzi unaporudiwa na mgombea wa upinzani anashinda.

Mapinduzi ya Orange yanafanya Urusi kuangalia Ukraine kwa jicho la tatu, hasa ukizingatia mapinduzi haya yalikuwa yanasukuma Ukraine kuangalia upande wa magharibi zaidi kuliko upande wa Urusi. Viktor Yanukovych  hakukata tamaa.

Muda unaenda, hatimaye mwaka 2010, Viktor Yanukovych  anachaguliwa kuwa Rais. Yanukovych ni kiongozi ambaye anakua na uhusiano mzuri na Urusi. Ushawishi wa Urusi ndani ya Ukraine unakuwa mkubwa sana. Hata hivyo, wananchi wanaendelea kuisukuma Serikali iangalie upande wa ulaya, hasa kutokana na fursa zinazopatikana.

Mwaka 2012, Umoja wa Ulaya unatoka na pendekezo nono la mkataba wa mahusiano na Ukraine. Kutokana na ushawishi mkubwa toka Urusi, Yanukovych anakataa kusaini mkataba huo pamoja na manufaa ya wazi wazi yanayoonekana.

Wananchi  wengi wanaonyeshwa kutoridhishwa na maamuzi hayo. Kuanzia November 2013, maandamano yaliyopewa jina la Euromaidan au mapinduzi ya heshima yanazuka huku hoja kubwa zikiwa ni juu ya uhuru na mamlaka ya Ukraine kama nchi.

Serikali ya Yanukovych inatumia nguvu kubwa na kufanya mauaji ya waandamanaji, jambo ambalo linachochea makasiriko zaidi ya wananchi. Hata hivyo, maandamano yanazidi nguvu na hatimaye Yanukovych anaamua kuachia nchi na kukimbilia Urusi.

Rais wa sasa wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, wakati wa kumbukumbu ya mauaji wakati wa maandamano ya Euromaidan, Februari 20,2022

Kukimbia kwa Rais aliyekuwa kipenzi kwa upande wa Urusi, inakuwa kama mkuki kwenye moyo wa Putin. Inaamsha kumbukumbu mbaya ya nyakati za aibu. Lakini kubwa zaidi ni maandamano ya watu wa Ukraine, Urusi wanaamua kufanya kitu kukomesha hali hiyo isisambae.

Kutwaliwa kwa Crimea

Mwanzoni nilikuelezea Ukraine kuna upande hasa Crimea, Donetski na Luhanski. Hawa wanajitambulisha kama Warusi na mara zote hufungamana na Urusi. Wengi wao hata vyombo vya habari wanavyofuatilia ni vya Urusi.

Baada ya kuondolewa kwa Rais wa Ukraine, Urusi inatumia ushawishi wake ndani ya haya maeneo kusambaza taarifa potofu kama Serikali ya Kiev inampango wa kuwamaliza,  na wanatumia habari ya Ukraine kutaka kusaini mkataba wa Umoja wa Ulaya kama chambo.

Hata hivyo, tayari kuna makundi ya watu wanaoipinga msimamo wa wengi ndani ya Ukraine wa kuwa na mahusiano mazito na magharibi kama ilivyo na Urusi. Ghafla katika jimbo la Crimea, wanaibuka watu wenye silaha wanaovalia sare za kijeshi za rangi ya kijani, bila utambulisho wanatokea nchi gani au wana mrengo upi, watu hawa wanapewa jina la ‘little green men’, watu wadogo wa kijani. Watu hawa wanaibuka mwishoni mwa mwezi wa pili wa 2014.

Wapambanaji waliopewa jina la “Little Green Men”

Urusi anakataa makundi hayo ni wanajeshi wake, wanawaita ni wazalendo wa maeneo hayo walioamua kusimamia hatma ya nchi yao. Wanafanikiwa kuteka majengo kadhaa ya Serikali wakishirikiana na vikundi vya watu ndani ya Crimea.

Urusi anajitenga kabisa na kusisitiza sio uvamizi, bali ni wazalendo wameamua kusimiamia haki zao. Hata hivyo, wazalendo hawa walikua ni wanajeshi wa vikosi maalum vya Urusi maarufu kama Spetsnaz.

Baada ya kutwaa maeneo yote ya Serikali, wananchi wa Crimea wanaamua kuitisha kura ya maoni ya kujiunga na Urusi, kirahisi tu wanajiunga na kuwa sehemu ya Urusi. Ukraine wanaamua kuwa wapole katika hili ili kuzuia umwagwaji wa damu, huku wakitegemea zaidi shinikizo la mataifa mengine juu ya Urusi, lakini Urusi haikuishia hapo.

Ghafla majimbo ya Donetski na Luhanski nayo yanataka kujitenga na Ukraine, na kujitangaza kama nchi huru huku Urusi akiwapa silaha pamoja na misaada mingine.

Katika hili Ukraine inaamua kuingia vitani ndani ya nchi yake. Kwa makundi makubwa makubwa ya wanamgambo, wananchi wa Ukraine nao wanajitolea kupambana ndani ya nchi yao.

Kwa kiasi kikubwa wanawadhibiti watu hao waliojitangazia uhuru toka Ukraine, vita hii ndani ya Ukraine imekuwa ikiendelea mpaka mwaka huu, huku zaidi ya watu 10,000 wakiuwawa.

Katikati ya hizi changamoto Ukraine inafanya uchaguzi na kumchagua Volodymyr Zelenskyy  mwaka 2019. Anashinda kwa zaidi ya asilimia 70 huku sehemu ya sera zake ni kuisogeza Ukraine karibu na mataifa ya magharibi.

Ukraine kama nchi ina haki ya kufuata maslahi yake. Hata hivyo, kuchaguliwa kwa kiongozi ambaye Moscow haiwezi kumuendesha moja kwa moja huku akiwa na malengo ya kuvuna pia kwa upande wa ulaya haikua habari nzuri kwa Urusi.

Urusi inapoteza ushawishi wake ndani ya serikali ya Ukraine huku wananchi wakiendelea kupigia chapuo mahusiano zaidi na upande wa magharibi. Kwa nje umoja wa ulaya na NATO wanaonekana kuendelea kuwashawishi zaidi Ukraine, jambo hili linazidisha hali ya wasiwasi kwa Urusi, kuanzia Machi 2021 Urusi anaanza taratibu kujiandaa na uvamizi.

Mwanzoni mwa Februari 2022,Rais wa wa Urusi anakutana na Rais wa Ufaransa Emanuel Macron kujadili juu ya Ukraine, umoja wa ulaya na NATO. Putin anataka kuwe na hakikisho kuwa Ukraine haitakaa iruhusiwe kujiunga na NATO, hasa ukizingatia moja ya kanuni ya NATO ni kuwa mwanachama yeyote akivamiwa ni wote wamevamiwa, mazungumzo yanafeli.

Urusi kuvamia Ukraine

Mpaka mwisho wa mwaka 2021, Urusi imekuwa ikifanya mazoezi na kupeleka silaha na wanajeshi wake katika mpaka wake na Ukraine. Pamoja na kupinga kuwa haitavamia Ukraine, mnamo Februari 24, 2022, Urusi anaingia ndani ya Ukraine.

Rais wa Urusi anasema uongozi uliopo unakandamiza watu na ni wa-kinazi. Lakini baada ya muda anaenda mbali na kusema kihistoria Ukraine iko chini ya Urusi na hatambui Ukraine kama nchi huru.

Wataalamu wengi walitengemea Urusi itachukua muda mrefu kabla ya kujaribu kuteka mji mkuu. Ila siku ya pili tu ya kuvamia Ukraine, Urusi inajaribu kuingia mpaka Kiev. Hii ikimaanisha kwa upande wa Urusi wameshafunga kitabu cha mazungumzo.

Uharibifu ndani ya mji wa Kiev

Taarifa za kiinteligensia na chambuzi za wataalamu zinahitimisha kuwa lengo la Rais wa Urusi ni kumuondoa Rais waliyepo na kumweka mwingine. Rais wa Ukraine anatoa taarifa kuwa kuna orodha ya watu watakaouliwa ambapo jina lake ni la kwanza, likifuatia na familia yake.

Urusi ina nguvu kuliko Ukraine. Bila msaada wowote wa maana kama inavyoendelea sasa ni wazi kuna uwezekano mkubwa wa Ukraine kudhibitiwa.

Lakini kuna mambo kadhaa yanayofanya isiwe rahisi kihivyo. Kwanza, Ukraine imekuwa katika hali ya kivita kwa muda mrefu. Uwepo wa makundi ya raia waliokua wakijitolea kupigana, kunafanya vita hii iwe ngumu.

Pili, kwa upande wa Urusi wangetaka vita hii imalizike mara moja, hasa kwa wao kushinda. Kwasababu jinsi wanavyokaa ndani ya Ukraine, ndio nafasi ya mambo kuharibika ndani ya Urusi inavyoongezeka. Hali inaonyesha mipango ya Urusi haijaenda jinsi walivyotarajia hasa katika kuuteka Kiev. Huku nyumbani Urusi tayari kuna maandamano yanayotokea hapa na pale na kuna uwezekano wa kupata nguvu zaidi.

Maandamano ndani ya Urusi kupinga uvamizi unaoendelea

Pia, vikwazo vinavyowekwa tayari vinaanza kufanya kazi, ikiwemo kuzuia sehemu kubwa ya mali na viongozi na baadhi ya watu mashuhuri wa Urusi kuingia Ulaya na Marekani na nchi rafiki.

Tayari meli kadhaa za Urusi zinaripotiwa kukamatwa. Ndege ya kiongozi wa Bunge ilirudishwa katikati ya safari. Kubwa zaidi ni vikwazo juu ya Benki ya Urusi, hii itafanya mambo kuwa magumu kwa raia wa Urusi jambo ambalo litaendelea kumweka matatani pia Rais wa Urusi kwa upande wa nchi yake.

Jambo la tatu kufanikiwa kwa kampeni ya Urusi ndani ya Ukraine inamaanisha anaweza kuendelea na nchi zingine zinazozunguka Urusi na zenye historia na Urusi. NATO hawataruhusu kuwe na ushindi wa moja kwa moja katika hili ingawa pia hawataingia katika vita ndani ya Ukraine.

Nchi zingine

Kuna makundi matatu ya nchi zingine katika mgogoro huu zenye maslahi ya moja kwa moja. Kundi la kwanza ni NATO, kundi la pili ni China na kundi la tatu nchi zenye historia na Urusi.

Kwa upande wa NATO wameshatoa msimamo kuwa hawataingiza majeshi ndani ya Ukraine kupigana. Sababu katika hili zinaeleweka. NATO akiamua kuingiza majeshi ndani ya Ukraine, haiwezi kuwa vita ya kawaida tena, ni vita ya nyuklia maana Urusi hatakubali kushindwa na wote wana silaha za nyuklia. Jambo hili Rais wa Urusi amelisisitiza.

Lakini NATO anamaslahi katika hili. Maslahi yake yanakuja na swali kwamba nini kinamzuia Urusi kuendelea na nchi zingine hasa zilizo pembezoni kabisa ya mipaka kama atafanikiwa kampeni yake ya Ukraine?

Upande mwingine ni China, taifa hilo ni mshirika wa karibu na wa kipekee wa Urusi.  Kwanza China anamuhakikishia Urusi kununua gesi yake kama vikwazo vikiendelea kuwekwa. Lakini pia ushawishi wa China ni muhimu. China na Urusi wamekuwa wakikubaliana katika mambo mengi hasa katika kuzuia ongezeko la ushawishi wa marekani duniani na karibu na mipaka yao.

Laini pia mgogoro huu ni picha nzuri kwa China kupima namna mataifa makubwa yanavyojibu katika matukio kama haya. China amekuwa na mgogoro wa kihistoria na Taiwan, ambapo inaiangalia nchi hiyo kama sehemu ya nchi yake huku Taiwan ikijitambulisha kama nchi huru. China kuwa upande wa Urusi ni muhimu sana kwa sasa, na mpaka sasa imeendelea kuhakikishia Urusi juu ya kumuunga mkono.

Tatu, nchi zenye historia ya kuwa chini ya utawala wa Urusi, hasa ambazo ziko pembezoni ya Urusi, zimeanza kuonyesha hofu yake kama Urusi akifanikiwa ndani ya Ukraine basi zenyewe zitafuatia. Nchi za Baltiki (Estonia, Latvia and Lithuania) zimeonyesha hofu hiyo juu ya mgogoro huo.

Maandamano ya kuiunga mkono Ukraine yalifanyika Februari 26 nchini Estonia,

Kwa sisi wengine nje wa hayo makundi matatu athari kubwa tutakayoiona ni upandaji wa bei za mafuta. Urusi kuwa mmoja wapo wa mzalishaji mkubwa wa mafuta maana yake ni lazima mzozo huu utaathiri usambazaji wa mafuta duniani, hivyo bei kupanda.

Hata hivyo, bado wengi wanaamini mlango wa mazungumzo unaweza ukafunguka tena. Hatua ya hivi karibuni ya nchi za ulaya na marekani kuzuia benki za Urusi kutumia mfumo wa kibenki wa swifti pamoja na NATO kuongeza majeshi karibu na mipaka ya Urusi inaweka shinikizo zaidi kwa Urusi kurudi kwenye mazungumzo.

Tony Alfred K ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

5 responses

  1. Kiukwli Mimi binfsi naona urusi ana haki kumwajibisha ukreni kwakurudisha heshima ya koloni lake maanamalekani anademokrasia kandamizi Sana na ametuchelewwsha Sana hata bara la afrika kimaendeleo kwakutugombanisha Sisi Kwa kutupandikizia migogoro ya vikundi vya kigaidi namigogoro isiyo isha Kwa lengo lakutuibia rasirimali zetu yeye akinufaika Sisi akituachia umaskini na vita mfano: DRC,sudani, Mali,Angola,Somalia,centrel afrika.na no asanteni

  2. kwanini nato ashindwe kuingilia mzozo huu na kuamua kukaa pembeni wakati mara ya kwanza urusi alishindwa kuwashawishi Nato kuwa ukraine asihusike kwa chochote na umoja huu…lakini leo mataifa yenye nguvu nayo yanamuogopa urusi….kwani nguvu kubwa ya nato ipo wapi au wananufaika na hivi vita wakati watu wanapoteza maisha wao wanaleta siasa za kipuuzi huku watu wanazidi kuteketea…..usitake amani wakati wa vita ukraine aendelee kumkazia tu huyo urusi hata kama apewi sapoti ya kutosha asiludi nyuma kamwe…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts