The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Maana ya Ukimya wa Afrika Kwenye Mgogoro wa Urusi na Ukraine?

Baadhi ya wadau wangetegemea nchi za Afrika ziitete Ukraine ambayo katika mgogoro huu ni taifa dhaifu kuliko hasimu wake Urusi. Mantiki hii inatokana na busara kuwa nchi zisizo na nguvu zinateteana. 

subscribe to our newsletter!

“Kama namba zingekuwa farasi, Afrika ingetawala katika ulimwengu wa kidiplomasia duniani.”

Hayo ni maneno ambayo aliwahi kuyasema Rais wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere alipokuwa akizungumzia kwa nini, pamoja na wingi wao ndani ya Umoja wa Mataifa, nchi za Afrika hazikuwa na nguvu yoyote kidiplomasia, hususan kwenye kujitetea pale zinapoonekana kuonewa.

Mwalimu Nyerere alikuwa akipigwa na butwaa kuona nchi nyingi za Afrika, kwa umoja wao, zikiwa zinashindwa kuchukua misimamo yenye maana kwenye maswala muhimu ya kimataifa, hata yale yanayogusa  maslahi ya moja kwa moja ya Afrika.

Dunia imebadilika na Afrika ya kipindi cha Nyerere sio ya sasa. Nchi mbalimbali za Afrika zimeanza kujihusisha na utatuzi wa migogoro mbalimbali duniani kwa kiasi fulani, ikiwemo kuchangia vikosi vya kulinda amani.

Lakini ugumu wa nchi za Afrika kujihusisha na migogoro duniani, hata kwa kutoa matamko tu, bado upo. Hasa pale migogoro hiyo inapohusisha mataifa makubwa.

Mzozo wa Ukraine/Urusi

Alhamisi ya Februari 24, 2022, nchi ya Urusi ilivamia rasmi nchi jirani ya Ukraine. Alfajiri ya siku hiyo, majeshi ya Urusi yalivuka mpaka na kuingia Ukraine. Mashambulizi yalisikika katika baadhi ya miji ya Ukraine na kuzua taharuki kwa wakazi wa miji hiyo.

Jumamosi ya Februari 26 majeshi ya Urusi yaliingia rasmi mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, jambo lililopelekea kuzuka kwa mapigano ya mitaani na majeshi ya Ukraine.

Pamoja na nchi za Ulaya na Marekani kutoa matamko ambayo yamelaani uvamizi huo, nchi za Afrika zimebaki kimya, kwa ujumla wao. Hata Umoja wa Afrika (AU) haukutoa tamko mara moja.

Umoja huo ulitoa tamko fupi lenye aya tatu tu likiitaka Urusi na dola nyingine kuheshimu sheria za kimataifa, mamlaka na uhuru wa taifa la Ukraine. Tamko hilo liliwekwa jioni ya Februari 24 kwenye tovuti ya umoja huo.

Ni kweli kuwa wakati Urusi inajiandaa kuivamia Ukraine nchi tatu za Afrika ambazo ni Ghana, Gabon na Kenya zilitoa matamko katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika Februari 22.

Wawakilishi wa nchi zote hizi tatu walilaani kitendo cha Urusi kutishia usalama wa nchi huru ya Ukraine. Matamshi ya balozi wa Kenya Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, ndiyo yaliyopata umaarufu mkubwa baada ya kuitaka Urusi ijifunze kutoka Afrika kuhusu somo la umuhimu wa kuheshimu mipaka ya nchi ambayo ilibadilishwa na tawala zilizopita.

Pamoja na kuwa nchi hizo tatu zinawakilisha nchi nyingine za Afrika katika Baraza la Umoja wa Mataifa, lakini kwa vyovyote vile matamko ya mabalozi wa nchi hizo walikuwa wakiwakilisha misimamo ya Serikali zao.

Ukimya wazua jambo

Ukimya wa Afrika umezua mjadala mkubwa kwenye majukwaa mbalimbali. Kuna wanaodai kuwa ukimya wa Afrika unafanya Bara hili lidharauliwe na lisichukuliwe kwa umakini katika masuala ya kimataifa.

Hata kama Afrika inakaa kimya kwa nia ya kutokutaka kuingilia uhuru au migogoro ya mabara mengine bado, wadau wanadai, jumuiya ya kimataifa inaweza kutafsiri ukimya huo kama uwoga wa kutokutaka kuchukiza mataifa makubwa.

Baadhi ya wadau wangetegemea nchi za Afrika ziitete Ukraine ambayo katika mgogoro huu ni taifa dhaifu kuliko hasimu wake Urusi. Mantiki hii inatokana na busara kuwa nchi zisizo na nguvu zinateteana.

Lakini wengine wangetegemea nchi za Afrika angalau zitoe tamko la kuchochea suluhu na maridhiano kwenye mgogoro.

Afrika na Urusi

Nchi ya Urusi ina uhusiano wa kihistoria na baadhi ya nchi za Afrika, hasa zile zilizokuwa zinafuata siasa za mrengo wa kushoto wa kisoshalisti. Baada ya kuvunjika kwa uliokuwa Muungano wa Kisovieti uhusiano kati ya Urusi na Afrika ulipungua.

Sasa hivi Urusi sio kati ya nchi zenye kufanya biashara kubwa na nchi za Afrika. China, Ulaya, Marekani, Uingereza, India na nchi nyingine zinafanya biashara zaidi na Afrika. Bidhaa kubwa ambazo Urusi inaiuzia Afrika ni silaha na ngano ghafi.

Pia, Urusi haitoi sana misaada ya kibajeti na ya miradi kwa Afrika kama zilivyo hizo nchi nyingine.

Pamoja na hayo bado kuna ukaribu kati ya Urusi na Afrika ambao ni mgumu kidogo kuuelezea, wadau wanasema. Kwanza, mgogoro kati ya Urusi na Ukraine ni wa miaka mingi. Una zaidi ya miaka saba.

Tatizo linaloendelea

Ni wazi kuwa kidiplomasia nchi nyingi za Afrika zinauchukulia mgogoro huu kama tatizo linaloendelea. Kama nchi hizi zilishindwa kuchukua msimo thabiti tangu mwanzo kuna uwezekano wa uwepo wa hisia kwamba kuchukua msimo sasa ni kama kudandia treni kwa nyuma.

Pia, tangu mgogoro ulipoanza nchi ya Urusi imewekewa vikwazo vingi na nchi za Magharibi. Swala la vikwazo ni nyeti sana Afrika. Baadhi ya nchi, kama vile Zimbabwe na Uganda, ziko ndani ya vikwazo kwa muda sasa.

Nchi za Afrika zinachukulia suala la vikwazo kama ubabe usiokubalika unaotumiwa na nchi za Magharibi kuadhibu nchi zilizodhaifu kiuchumi.

Lakini pia katika masuala kadhaa ya kimataifa nchi ya Urusi imewahi kusimama kidete kuitetea Afrika. Katika mgogoro wa Libya uliopelekea kuuwawa kwa Muamar Gaddafi, kwa mfano,  Urusi ilipinga hatua ya majeshi ya NATO kuingilia mgogoro huo.

Kwa hakika katika dunia ambayo nguvu kubwa za kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia zimelalia upande mmoja wa nchi za Magharibi ni wazi kuwa nchi za Afrika zinajihisi katika hatari.

Kwa mantiki hiyo, nchi hizi zinajisikia salama kidogo zinapokuwa karibu na nchi zenye nguvu zinazopinga sera za Magharibi kama Urusi na China.

Baadhi ya nchi, zikiwemo za Afrika, zinaunga mkono wasiwasi wa Urusi kuhusu kupanuka kwa Umoja wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi, yaani NATO. Nchi kama Brazili, Iran na Syria zimeongea waziwazi na kuunga mkono hatua ya Urusi “kujikahikishia usalama wake” katika kipindi ambacho NATO inazidi kujitanua kuelekea nchi zinazopakana na Urusi.

Nchi nyingi duniani zinaichukulia Nato kama alama ya ubabe wa kijeshi wa nchi za Magharibi. Ni ngumu kwa nchi za Afrika kujitokeza na kuinga mkono waziwazi, na hivyo kuamua kukaa kimya.

Damas Kanyabwoya ni mchambuzi wa siasa kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa maoni, anapatikana kupitia dkanyabwoya@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *