Dar es Salaam. Balozi wa Ukraine nchini Kenya Andrii Pravednyk anategemewa kukutana na viongozi wa Serikali ya Zanzibar pamoja na raia wa Ukraine waliokwama nchini humo ili kuona namna wanavyoweza kuwasaidia raia hao ambao awali waliingia Zanzibar kama watalii.
Kwa mujibu wa gazeti la nchini Kenya la The East African, Balozi Pravednyk na Serikali ya Zanzibar wanafanya mazungumzo ya kuwasafirisha raia hao wapatao 900 mpaka nchini Poland ambayo kwa sasa inapokea wakimbizi wengi kutoka Ukraine.
Taifa la Ukraine kwa sasa lipo vitani dhidi ya Urusi iliyoanza mashambulizi ya kijeshi dhidi ya jirani yake huyo mnamo Februari 24, 2024, kwa kisingizio cha kuzuia juhudi za Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (NATO) kujipanua katika Ulaya ya Mashariki.
Kufuatia hatua hiyo ya Urusi, jeshi la Ukraine, likisaidiwa na nchi nyengine kama vile Marekani na Umoja wa Ulaya kwa silaha, ilianzisha operesheni ya kujilinda dhidi ya uvamivi wa Urusi, hali iliyopelekea vita kamili kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Hatua hiyo imepelekea raia wengi wa Ukraine kutafuta hifadhi uhamishoni, huku Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi la UNHRC likisema kwamba mpaka kufikia Machi 2, 2022, jumla ya raia 660,000 kutoka Ukraine wametafuta hifadhi katika nchi zingine kama vile Poland, Hungary, Moldova, Romania, na Slovakia.
Hatua hii inamaanisha kwamba raia wa Ukraine waliokuwa nje ya nchi yao kabla ya vita kuanza hawawezi tena kurudi nchini mwao kwa sasa, hususani ukizingatia hatua ya Serikali ya Ukraine kufunga anga zake kwa sababu za kiusalama.
Mnamo Februari 28, 2022, wakati wa mkutano wa kila mwisho wa mwezi na waandishi wa habari, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi alisema kwamba Serikali yake imepokea maombi kutoka kwa raia takriban 900 waliokwama visiwani humo ambao hawawezi kuondoka kwa sababu ya hali ya vita nchini kwao pia hawawezi kuendelea kubaki Zanzibar kwa sababu pesa zimewaishia.
Mwinyi alisema kwamba tayari Serikali yake imekubaliana na wamiliki wa hoteli visiwani humo ili waendelee kuwapa huduma raia hao bila kuwatoza fedha huku Serikali yake ikiahidi kuwafikiria wamiliki hao kwenye masuala ya kodi.
“Ukweli ni kwamba tunaona umuhimu wa kutoa msaada kwa watu hawa ambao walioko kwao sasa wanaondoka,” alisema Rais Mwinyi huku akiitaja Ukraine kama chanzo muhimu cha watalii wanaotembelea Zanzibar. “Kwa hiyo, huwezi kumwambia mtu rudi kule ndani [wakati wengine wanaondoka]. Ni lazima tutafute njia ya kuwasaidia.”