Dar es Salaam. Serikali ya Zanzibar inatumia vifaa vya kieletroniki visivyo na rubani vinavyojulikana kwa kitaalamu kama drones katika utafutaji, ugunduzi na uwekaji wa kumbukumbu za kiramani za maeneo ambayo yanaweza kuwa na mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa hatari wa malaria.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tovuti inayochapisha habari zinazohusiana na drones inayojulikana kama DroneDJ.
Zoezi hilo ni sehemu ya mradi wa pamoja kati ya Mpango wa Kutokomeza Malaria Zanzibar, Chuo Kikuu cha Aberystwyth cha nchini Uingereza, Shule ya Dawa za Kitropikali ya Liverpool, Shule ya Usafi na Dawa za Kitropikali ya London, Zzapp Malaria, Tanzanian Flying Labs na Mosquito Consulting.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka shirika la Innovative Vector Control Consortium ambapo Wakfu wa Bill & Melinda umechangia jumla ya dola za kimarekani milioni 50, ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 115.7 za Kitanzania, kama ruzuku ya awali.
Wataalamu wanabainisha kwamba ili juhudi za kutokomeza malaria ziweze kuzaa matunda ni lazima mamlaka zinazohusika na afya ya umma ziwe na taarifa sahihi za wapi kuna mazalia ya mbu. Drones zinatajwa kuwa na uwezo wa kubainisha mazalia haya kwa haraka.
Mamlaka zinazohusika zinaweza kutumia taarifa hizi zilizokusanywa na drones kupitia app maalum inayopatikana kwenye simujanja, au smartphone, na kuweza kuainisha makazi husika ya watu yanayohitaji kutibiwa.
Dk Andy Hardy ni mtaalam kutoka Idara ya Jiografia na Sayansi za Dunia kutoka Chuo Kikuu cha Aberystwyth ambaye ameieleza DroneDJ kwa nini teknolojia hii ni muhimu kwenye juhudi nzima za kukabiliana dhidi ya malaria.
“Moja ya changamoto kubwa wanazokumbana nazo wadhibiti magonjwa ni kutambua maeneo madogo ya maji ambayo mbu [wanaosababisha malaria] huyatumia kuzaliana,” anaeleza Dk Hardy.
Anaongeza kwa kusema: “Hapa ndipo drones zinapoingia. Kwa mara ya kwanza, picha zinazotokana na drones zinaweza kuchukuliwa mara kwa mara na Mpango wa Kutokomeza Malaria Zanzibar [na] kutengeneza ramani sahihi ya mazalia haya.”
Kwa mujibu wa Dk Hardy, drone moja ina uwezo wa kutafiti shamba moja la mpunga lenye ukubwa wa ekari 30 kwa muda wa dakika 20 tu. Picha zinazochukuliwa zinaweza kuchakatwa ndani ya muda huo huo ili kugundua na kutengeneza ramani ya mazalia ya mbu.
Dk Hardy, hata hivyo, anabainisha kwamba ili teknolojia hii iweze kusaidia utokomezaji wa malaria ni lazima iambatane na hatua nyengine kama vile kulala ndani ya vyandarua vilivyowekwa dawa pamoja na kupuliza dawa za kuulia mbu badala ya kutumika kama mbadala wake.
Hata hivyo, utaratibu huu wa kutumia drones kutambua mazalia ya mbu Zanzibar umedhihirika kuwa imara na sahihi sana kiasi ya kwamba Mkurugenzi wa Operesheni za Kisayansi kutoka Chama cha Udhibiti wa Mbu Afrika (PAMCA) Dk Silas Majambere ameieleza DroneDJ kwamba anatamani utaratibu huo ungetumika pia kwenye nchi zingine za Rwanda, Tanzania, Uganda, na Ghana.
“Tunapoliendea lengo la kutokomeza malaria [ni muhimu] kuangalia mbinu na teknolojia mpya ambazo zitasaidia kuiboresha mikakati yetu,” anasema Dk Majambere. “Upigaji ramani wa kutumia drones unasaidia kupatikana kwa taarifa sahihi na kuwezesha tathmini pana ya wapi palipo na maeneo ya maji, hatua ambayo ni muhimu sana katika zoezi zima la kudhibiti mbu.”
Mnamo mwaka 2020, takriban watu 627,000, wengi wao wakiwa watoto, waliripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa wa malaria barani Afrika. Kwa mujibu wa ripoti ya malaria ya hivi karibuni kutoka Shirika la Afya Duniani watu wapatao milioni 241 wanaripotiwa kuwa na malaria ulimwenguni kote kwa mwaka 2020.
Zanzibar inatajwa kama moja kati ya nchi chache barani Afrika iliyoweza kwa mafanikio kudhibiti ugonjwa wa malaria ambapo inaripotiwa kwamba watu wachache sana visiwani humo, hususan wageni, hukutikana na ugonjwa huo unaosababishwa na mbu.
Kwa upande wa Tanzania Bara, idadi yote ya wananchi wanaoishi nchini humo wanahisiwa kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa malaria. Tanzania Bara pia inatajwa kuwa miongoni mwa nchi 10 za Afrika zinazoongoza kwa kuwa na kesi nyingi za malaria na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo hatari.