Zanzibar. Wafanyabiashara visiwani hapa wameishauri Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusiana na utaratibu mpya unaowataka kutoa stakabadhi za malipo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama VFMS pamoja na kuharakisha agizo la Rais Hussein Mwinyi la kutaka wafanyabishara waruhusiwe kulipia mashine hizo kwa awamu.
Rais Mwinyi alilazimika kutoa agizo hilo mnamo Februari 28, 2022, wakati akiongea na waandishi wa habari kufuatia kile alichokiita ni upinzani ambao Serikali imeendelea kukumbana nao kutoka kwa wafanyabiashara kuhusiana na utaratibu huo mpya unaolenga kuingozea mapato Serikali visiwani humo na kuondoa mianya ya upotevu wa mapato.
“Tunasema tusigombane kwa hilo, tutatafuta utaratibu wa watu walipe kwa awamu,” alitamka Rais huyo wa awamu ya nane wa Zanzibar. “Lakini Sh400,000 lazima ilipwe kwa sababu kifaa kile hakitolewi bure. Ukitumia kifaa hiki baada ya muda mfupi sisi tutaipata hiyo Sh400,000. Naitaka [Bodi ya Mapato ya Zanzibar] ZRB itengeneze utaratibu wa kuwalipisha [wafanyabiashara] kwa awamu.”
Mfumo huo wa utoaji stakabadhi kielektroniki kwa kutumia mashine maalum umeanza utekelezaji kwenye mwaka unaendelea wa fedha wa 2021/2022 hapo Julai 1, 2021, na kuja kupata umaarufu zaidi mwanzoni mwa mwezi Februari 2022 baada ya mamlaka husika kuanza ufuatiliaji wa kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia mfumo huo.
Lakini licha ya ufuatiliaji huo na elimu inayoendelea kutolewa juu ya umuhimu wa matumizi yake bado wafanyabiashara wengi visiwani hapa wanaonekana kuwa wazito kuutumia, huku wengi wao wakitaja gharama ya Sh400,000 kama sababu ya kushindwa kwao wakisema ni kubwa isiyolingana na biashara zao na hawawezi kulipa kwa mkupuo.
Matumizi hafifu ya mashine
Utafiti mdogo uliofanywa na The Chanzo katika maeneo ya Vikokotoni, Mchangani, Mtendeni na Makontena kisiwani Unguja umebaini kwamba wafanyabiashara wengi wa kipato cha chini na cha kati hawajaanza kutumia mfumo huo huku wakibainisha kwamba wanasubiri mashine hizo zitolewe kwa mkopo ndiyo waanze kutumia mfumo huo.
Seif Suleiman ni mfanyabiashara wa nguo katika eneo la Vikokotoni, Darajani ambaye anadhani kwamba Serikali inapaswa itoe ufafanuzi kwa umma juu ya nani haswa anastahiki kutumia mashine hizo mpya ili kuepusha taharuki anayodai imewakumba wafanyabiashara wenzake visiwani humo.
“[Huu mfumo] unamlenga hata mfanyabiashara tu mwenye kimeza hapo njiani au ni wale wenye maduka tu?” anauliza Suleiman. “Kuna watu hiyo Sh400,000 ambayo Serikali inataka watu walipie hizo mashine ndiyo mtaji wao mzima. Je, hawa wanapaswa kununua hizo mashine pia?”
Suleiman anashauri kwamba kama Serikali imedhamiria mashine hizo zinatumiwa na wafanyabiashara wote, basi izitoe kwa bei nafuu na kama inawezekana basi wafanyabiashara wakopeshwe na kutakiwa kulipa madeni yao kwa awamu.
“Nia ni kujenga nchi,” anasema Suleiman. “Sisi wananchi wa Zanzibar ni watu waelewa sana. Ni watu wakarimu sana. Lakini ni muhimu Serikali ikatuchukulia kama marafiki, watufanye kama ndugu. Wasitusukume sukume tu. Twende taratibu. Mambo haya yanahitaji muda. Wasitunyanyase.”
Baadhi ya wafanyabiashara visiwani hapa wanajiuliza ni kwa nini Serikali imeshindwa kutoa mashine husika bure kwa wafanyabiashara kama imejiridhisha faida ya matumizi ya mashine hizo ni kubwa. Mmoja kati ya wafanyabiashara hawa ni Barik Ali Omar, mfanyabiashara wa vifaa vya michezo.
“Sh400,000 kwa biashara zetu za Zanzibar ni kubwa sana,” anasema Omar. “Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanaogopa au wanasikitika sana kwa sababu hii mashine ni ghali sana. Bei ya mashine ni lazima ipunguzwe au itolewe bure kabisa.”
Omar ana maoni kwamba endapo kama mashine hizo zitatolewa bure basi watu wengi watahamasika kuzitumia, kitu ambacho anasema kitakuwa ni faida kwa Serikali na kwa nchi kwa ujumla.
“Suala la kodi kwa ujumla siyo suala baya,” anaongeza Omar. “Nchi zote zilizoendelea duniani zimeendelea kutokana na kodi za wananchi wenyewe. Lakini Serikali ingerahisisha upatikanaji wa mashine hizi kwa wafanyabiashara kwa kuweka utaratibu ambao hauwaumizi wafanyabiashara.”
Kodi ni lazima ilipwe
Kwenye mkutano wake huo na waandishi wa habari uliofanyika Februari 28, 2022, Rais Mwinyi alieleza kwamba mfumo huo unawalenga wale wafanyabiashara ambao kiwango cha fedha wanachoingiza ni zaidi ya Shilingi milioni 10 tu na kuacha wafanyabiashara wanaoingiza chini ya kiwango hicho.
“Ndugu zangu kodi [ya ongezeko la thamani] VAT ni muhimu sana,” Rais Mwinyi aliwasihi Wazanzibari. “Kama kuna kodi ambayo inaweza kuongeza pato kwa Serikali ni hii kodi ya VAT kwa sababu tunailipia kwenye kila bidhaa. Kwa hiyo, hili siyo jambo la kusema kama tutakaa [na] kutafakari liendelee au lisiendelee. Lipo kisheria na ni lazima liendelee.”
Abdallah Bakari Hassan ni mchambuzi wa masuala uchumi na kodi kutoka Umoja wa Ushauri wa Walipa Kodi Zanzibar (UWAKOZA) ambaye licha ya kukubaliana na Rais Mwinyi kuhusiana na utaratibu huu na faida zake kwenye ukusanyaji wa mapato Zanzibar anashauri wafanyabiashara kupewa muda kidogo ili waweze kujipanga kununua mashine hizo.
“Ingekuwa [wafanyabiashara] wanalipishwa kidogo kidogo kwa miezi minne,” anashauri Hassan. “Hicho kichache alichonacho ukikimega ukasema kwamba lazima utuletee sisi kwanza unamuacha akiwa hana fedha za kendeshea biashara yake.”
Hassan pia ameisihi Serikali kuacha kutumia nguvu katika kufanikisha zoezi hili badala yake iendelee na juhudi za kutoa elimu pamoja na kutekeleza ushauri mwengine unaotolewa na wafanyabiashara na wadau wengine kwenye ufanikishaji wa zoezi husika.
Salim Khamis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Anapatikana kupitia salimkombo437@gmail.com.