The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ado Shaibu: Hivi Ndivyo Tanzania Inaweza Kupata Tume Huru ya Uchaguzi

Kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kusisitiza msimamo wa chama chake wa kutanguliza mapambano ya Tume Huru ya Uchaguzi akisema taasisi hiyo ni muhimu kwa sasa ili mapambano ya kudai mabadiliko mengine makubwa kama vile Katiba Mpya yaweze kufanikiwa.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa chama cha upinzani chini cha ACT-Wazalendo Ado Shaibu amesema kwamba kinachopaswa kufanywa ili Tanzania iweze kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ni kuchukua maoni ya wananchi kama yalivyo kutoka kwenye Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuyatumia hayo kutunga sheria mpya ya uchaguzi.

Shaibu alitoa ushauri huo hivi karibuni wakati akiongea na The Chanzo kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake jijini hapa. Wito huo umetolewa wakati ambapo ACT-Wazalendo inajiandaa kusukuma mbele ajenda ya upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoipatia Tanzania Katiba Mpya.

“Tume ya marekebisho ya katiba ambayo ni maarufu kama Tume ya Jaji Warioba ilizunguka nchi nzima, ikakusanya maoni ya wananchi, ikayachambua, ikayachakata tukapata maoni mahususi yanayohusisha mfumo wa uchaguzi,” alisema Shaibu. “Tunachopaswa kufanya hivi sasa [ni] yale maoni ya wananchi katika rasimu ya Jaji Warioba yachukuliwe kama yalivyo baada ya kujadiliwa na kupata maboresho machache yaingizwe kutengeneza sheria ya taifa ya uchaguzi.”

Shaibu alibainisha kwamba mapendekezo hayo kwa ujumla wake yanaweza kuchukuliwa na sheria ya uchaguzi bila kuathiri katiba ya nchi. Yafuatayo ni mazungumzo ambayo The Chanzo ilifanya na kiongozi huyo wa kisiasa. Endelea …

The chanzo: Kwanza kabisa ningependa kupata tathimini yako fupi jinsi chama chenu cha ACT-Wazalendo kilivyouanza mwaka wa 2022. Natambua kwamba ndani ya kipindi hiki kifupi cha mwaka huu chama chenu kimefanya Mkutano wake Mkuu pamoja na uchaguzi wa kujaza baadhi ya nafasi za uongozi. Hivyo kama Katibu Mkuu wa chama unautathimini vipi mwaka huu wa 2022 kwa jinsi chama chenu kilivyouanza?

Ado Shaibu: Asante sana ndugu mwandishi. Mwaka 2022 sisi tuliuanza kwa Mkutano Mkuu maalumu. Kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo, Mkutano Mkuu ndiyo chombo cha juu zaidi cha maamuzi na hua kinakutana mara chache kwa sababu maalumu.

Kwa ACT-Wazalendo, Mkutano Mkuu unakutana mara moja kila baada ya miaka mitano na tulikwishafanya Mkutano Mkuu wetu mwaka 2020 wa kuchagua viongozi wa kitaifa ambao wanaendelea kufanya kazi hivi sasa. Lakini kama ambavyo nchi inajua na dunia inafahamu mwaka 2021 tulipata pigo la kuondokewa na Mwenyekiti wa chama chetu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar.

Kwa hiyo, Mkutano Mkuu ambao tumeuitisha mwaka 2022 ulikuwa unalenga kuziba nafasi iliyoachwa na Maalim Seif Sharif Hamad. Lakini ukiacha kwamba huu ulikuwa ni mkutano wa uchaguzi lakini kwetu sisi Mkutano Mkuu maalumu ulikuwa ni mkutano wa kutengeneza mwelekeo wa chama chetu kwa mwaka 2020 lakini pia kutoa mwelekeo wa masafa marefu kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa, 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Hivyo basi kupitia Mkutano Mkuu ule tumetoka na mambo makubwa manne, ambayo kwa kweli ndio yatakayoongoza mwelekeo wa siasa za chama chetu kwa mwaka 2022 na pia katika kuelekea 2024, uchaguzi wa Serikali za mitaa na 2025, [na] Uchaguzi Mkuu.

Mambo hayo nikiyataja kwa muhtasari la kwanza ni kufanya mageuzi ya kuendesha chama chetu kisayansi na hasa katika eneo la kusajili wanachama ulipaji wa kadi za wanachama na mfumo wa mawasiliano ya ndani na mawasiliano kwa umma.

Kwa hiyo, tumeanzisha programu maalumu inayoitwa ACT Kiganjani ambayo inakusudia kuleta mageuzi makubwa katika uendeshaji wa chama. Hivi sasa chama cha ACT-Wazalendo tumeachana na kadi za karatasi na wanachama wetu watajisajili kielektroniki kupitia simu zao, wataweza pia kulipa ada zao za uanachama kupitia simu na wataweza kupata taarifa mbalimbali za ndani ya chama na zile ambazo zinastahili umma kupitia simu zao.

Kwa hiyo, programu hiyo tunaiita ACT Kiganjani na ninashukuru kwamba imepata mapokeo makubwa kutoka kwa wanachama na viongozi wetu wanachama hivi sasa wanaendelea kujiorodhesha katika programu ya ACT Kiganjani na tunadhani kwamba itakuwa ni nyenzo muhimu katika kutuhakikishia kwamba tunajipanga katika kupata ushindi wetu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Jambo la pili ambalo limetoka katika Mkutano Mkuu ni kuiwajibisha Serikali. Tumefanya  utafiti baada ya Uchaguzi Mkuu na tumejiridhisha kwamba vyombo vya uwakilishi wa wananchi, kwa maana ya mabaraza ya halmashauri pamoja na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, havitekelezi majukumu yake sawasawa ya kuisimamia na kuiwajibisha Serikali na sisi ACT Wazalendo tunadhani ni kwa sababu ya jinsi viongozi wenyewe walivyopatikana.

Uchaguzi wa 2020 ulikuwa hauna sifa hata moja ya kuitwa uchaguzi huru wa haki na wakidemokrasia. Kwa hiyo, wabunge waliopatikana, madiwani waliopatikana kwa sehemu kubwa hawawajibiki kwa wananchi kwa sababu hawakupatikana kutokana na matakwa ya wananchi na idadi ya wapinzani katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni ndogo sana, idadi ya wabunge wa kuchaguliwa katika bunge vyama vyote vya upinzani ni wabunge nane tu.

Kwa hiyo, ni vigumu kutengeneza utaratibu uliozoeleka ndani ya bunge wa kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kupitia Baraza la Mawaziri kivuli.  Kwa hiyo, ACT-Wazalendo tumeanzisha kamati maalumu ya kuisimamia na kuiwajibisha Serikali yenye wasemaji wakisekta ambayo itahakikisha kwamba kila waziri na kila wizara anakuwa na mtu kutoka ACT-Wazalendo ambaye anaisimamia na kuimulika na kuiwajibisha kupitia kuikosoa na kutoa mbadala kwenye wizara husika ya Serikali. Na katika utafiti ambao tumeufanya katika mikoa tumeona kwamba shida nyingi zinatokea katika wizara mbalimbali lakini muundo wetu wa sasa wa chama chetu na wa vyama vingine hautuwezeshi kuweza kuisimamia Serikali vizuri na kuiwajibisha Serikali.

La tatu ambalo tumetoka nalo tumesema na tumetangaza kwa umma kwamba kwetu sisi ACT-Wazalendo mwaka 2022 utakuwa ni mwaka wa kujenga chama. Kwa hiyo, tutakuwa tunajikita katika ngazi za chini, katika matawi, katika kata, katika majimbo kuhakikisha tunatengeneza mtandao madhubuti wa chama chetu kwa ajili ya kuweza kufanikisha malengo ya chama chetu hasa kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

Na hili kwa kweli tumelianza kupitia ziara mbalimbali za viongozi. Mnaofuatilia mtaona hivi sasa tumo katika ziara ya kuwatambulisha viongozi wetu wakuu kwa maana Mwenyekiti wa chama pamoja na Makamu Mwenyekiti wa chama kwa upande wa Zanzibar ndugu Juma Duni Haji pamoja na ndugu Othman Masoud Othman ambao wamechaguliwa na Mkutano Mkuu kwenda katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kukutana na wanachama na viongozi na kutambulishwa.

Tumekwisha fanya hivyo kwa kanda ya Kusini ambako alipokelewa vizuri pale Lindi. Tumefanya hivyo kwa Unguja, kwa Pemba na Kanda ya Pwani ambako tumefanya kwa mkoa wa Tanga. Kinachofuata hivi sasa tarehe 19, Machi [mwaka 2022] tumejipanga kuwa na tukio kubwa ambapo mbali ya kuwapokea Juma Duni Haji pamoja na Othman Masoud Othman  Sharif lakini pia tutazindua oparesheni yetu ya kupigania Tume Huru ya Uchaguzi.

Na la mwisho kwa kulitaja ambalo tumetoka nalo ni kwamba tumeamua kwamba ACT-Wazalendo tutabeba ajenda kama ilivyotaja ya kuipigania Tume Huru ya Uchaguzi kama turufu ya mageuzi ya kisiasa katika nchi. Kwa hiyo, haya manne niliyoyataja ndio yatakayoongoza mwelekeo wa siasa za chama chetu na ndio tumeanza nayo 2022.

The Chanzo: Nikitambua kwamba chama chenu hivi sasa kimesimama na ajenda ya kupigania Tume Huru ya Uchaguzi, ningependa kufahamu ni kwa namna gani sasa tunaweza tukaipata hiyo Tume Huru ya Uchaguzi. Na pengine labda mapendekezo yenu ni yapi au mnapendekeza nini haswa kama chama juu ya mchakato mzima wa upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi?

Ado Shaibu: Asante sana. Kwanza, ACT-Wazalendo tumeweka bayana kwamba katika kuelekea mageuzi ya kisiasa, katika kurekebisha hali ya kisiasa ambayo iliharibiwa sana katika miaka saba iliyopita ya utawala wa Hayati John Pombe Magufuli, ajenda ya kuanza nayo ni Tume Huru ya Uchaguzi.

Na tumeweka wazi sababu za kuanza na Tume Huru ya Uchaguzi na kwa mtu yeyote ambaye atafanya tafakuri ya kina atakubaliana na sisi kwamba sababu zetu ni za msingi. La kwanza tumesema ni muhimu kuanza na Tume Huru ya Uchaguzi kwa sababu tunahitaji Katiba Mpya na ili tupate Katiba Mpya ni lazima tuwe na chombo ambacho ni huru na kinachoaminika, kinachoweza kusimamia mchakato wa kura ya maoni ya Katiba Mpya na chombo hicho si kingine isipokuwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Sababu ya pili tumesema ukitazama kipindi ambacho tumebaki nacho, hii ni 2022 mwakani 2023, mwaka unaofuata 2024 kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za mitaa na 2025  Uchaguzi Mkuu, tumesema tunahitaji Tume Huru ya Uchaguzi ili kwa sababu yoyote ile iwapo kuanzia sasa mpaka 2025 hapatoweza kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi basi tuwe na chombo ambacho kitasimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu na kuhakikisha kwamba chaguzi zote hizi mbili zinafanyika katika mazingira ya huru na ya haki.

Na sababu ya tatu ambayo tumeitoa ni kwa sababu panahitajika kuwa na matayarisho fulani ya uchaguzi, mathalani kwa mujibu wa sheria Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapaswa kuboresha daftari la wapiga kura mara mbili katika kipindi cha miaka mitano. Sisi ACT-Wazalendo haturudhiki na mchakato wa uchaguzi ambao unaanza kwa kuboresha daftari ufanyike chini ya tume hii ya uchaguzi.

Kwa hiyo, tunapambana kuhakikisha kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine wa siasa vyama vingine vya siasa na wadau wa demokrasia kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunatoa msukumo ili Tume ya Uchaguzi ipatikane mwaka huu wa 2022.

Sasa itapatikanaje? Kwanza upo mjadala na mjadala ni suala la afya, ni suala zuri sana katika taifa kwamba Tume ya Uchaguzi ni zao la katiba na misingi madhubuti ya tume huwa inawekwa katika katiba. Lakini hiyo haimaanishi kwamba katika kipindi cha mpito kuelekea 2025 hatuwezi kupata Tume Huru ya Uchaguzi.

Kwa hiyo, mapendekezo ya ACT-Wazalendo kwanza ni lazima sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi ziandikwe upya. Hatutaki zifanyiwe maboresho. Hatutaki ziwekwe viraka. Tunataka kuandikwa kwa sheria mpya ya uchaguzi hapa Tanzania. Tunapaswa kuanza upya. Tunapaswa kujadiliana.

Tunapaswa kuwa na makubaliano ya namna gani tunataka chaguzi Tanzania ziendeshwe na yale makubaliano yanayotokana na maoni ya wananchi ndio yajumuishwe katika sheria mpya ya uchaguzi ambayo baadae itafuatiwa na kanuni za uchaguzi na bahati nzuri tunapo pa kuanzia.

Tume ya marekebisho ya katiba ambayo ni maarufu kama Tume ya Jaji Warioba ilizunguka nchi nzima, ikakusanya maoni ya wananchi, ikayachambua, ikayachakata tukapata maoni mahususi yanayohusisha mfumo wa uchaguzi. Tunachopaswa kufanya hivi sasa [ni] yale maoni ya wananchi katika rasimu ya Jaji Warioba yachukuliwe kama yalivyo baada ya kujadiliwa na kupata maboresho machache yaingizwe kutengeneza sheria ya taifa ya uchaguzi na utaona mapendekezo yale kwa ujumla wake yanaweza kuchukuliwa na sheria ya uchaguzi bila kuathiri katiba ya nchi.

Kwa mfano, sisi ili kuchokoza mjadala kuna mapendekezo mahususi ambayo ndio tunayoyasukuma ACT-Wazalendo na nitayataja hapa kwa muhtasari.

Moja, tunasema hiyo sheria mpya ya uchaguzi ni lazima ihakikishe inatengeneza chombo. Chombo ambacho kitakuwa kamati  maalumu ya uteuzi wa viongozi wakuu watakaosimamia uchaguzi hapa Tanzania. Katika tume tunafahamu patakuwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, kutakuwa na makamu wa tume ya uchaguzi, kutakuwa na makamishna wa tume ya uchaguzi.

Sisi tunasema hawa wote wasiteuliwe moja kwa moja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni lazima pawe na mchakato ambao ni shirikishi, mchakato ambao ni wa wazi, mchakato ambao unaaminika, mchakato ambao tunaupendekeza utakuwa na ngazi tatu.

Ngazi ya kwanza ni lazima paundwe hiki chombo, kamati maalumu ya uteuzi halafu pili watu wenye sifa watume maombi ya kuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi,  ya kuwa makamishna, ya kuwa mkurugenzi wa uchaguzi. Na hii kamati maalumu ya uchaguzi ndio yenyewe sasa iendeshe mchakato ambao utakuwa wazi na uzoefu huu tumeupata Kenya ambako watu wanaoomba kushika nafasi nyeti katika Tume ya Uchaguzi wanatuma maombi na mchakato wa kuchujwa kwao na kupendekezwa kwao unakuwa wazi kwa umma kupitia vyombo vya habari.

Hii ni ngazi ya kwanza, na kuna sifa maalumu za hao watu tunaotaka wawe viongozi wakuu na kuna sifa maalumu za tunaotaka wawe wajumbe wa hicho chombo ambacho kitasimamia uteuzi. Kwa mfano, sifa maalumu za hiyo kamati ya uteuzi tunataka iongozwe na Jaji Mkuu. Tunataka Jaji Mkuu asaidiwe na Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Tunataka pawe na uwakilishi wa chama cha Wanasheria [Tanganyika] TLS. Tunataka pawe na uwakilishi wa asasi yenye kuheshimika ya kupigania haki za binadamu. Tunataka pawe na uwakilishi unaoakisi jinsia pia. Tunataka kiwe chombo ambacho Watanzania wakikiona watakiamini.

Lakini pia tunataka hao watu watakaotuma maombi ya kuwa viongozi wakuu wa tume wawekewe vigezo vya kuhakikisha kwamba wanakuwa sio mashabiki na wanachama au viongozi wa vyama vya siasa. Wawe ni watu ambao wanasifa zilizo bainishwa. Watu wenye rekodi inayoheshimika ambayo tunaweza tukawakabidhi mchakato wa uchaguzi.

Kwa hiyo, hii ni ngazi ya kwanza. Ngazi ya pili tunataka Rais afanye uteuzi na tunataka Bunge liidhinishe kwa hizi ngazi tatu tunaamini kwamba tume kitakuwa ni chombo huru. Lakini pia katika ngazi za chini tunataka tume iwe na watendaji wake wenyewe tofauti na hali ilivyo sasa. Ukienda katika ngazi ya wilaya, tume ya uchaguzi pale inawakilishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ambao wengi tunafahamu ni makada wa Chama cha Mapinduzi.

Imekuwa ni mtindo hapa Tanzania watu walioshindwa uchaguzi katika kura za maoni za CCM ndio hupewa zawadi ya kuwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri. Mtu ambaye ameshiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi wa CCM anawezaje yeye kuwa ndie msimamizi wa uchaguzi, anawezaje kumtangaza mipinzani kuwa mshindi?

Mfano mwingine mdogo. Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Rais akiachiwa ateue moja kwa moja, Rais Magufuli alifikia kiwango cha kumteua Balozi Ramadhan Mapuri ambaye aliwahi kuwa mkuu wa propaganda kwa maana ya katibu mwenezi wa Chama cha Mapinduzi kuwa kamishna wa Tume ya Uchaguzi. Unatarajia ni kwa namna gani Mapuri anaweza kutenda haki kwa ACT-Wazalendo na CHADEMA?

Kwa hiyo, tunapaswa kubadilisha mambo haya na bahati nzuri kuna maelewano miongoni mwa wadau. Sisi wapinzani tulisusia uzinduzi wa ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa sababu ya kuonesha hisia zetu jinsi uchaguzi ule ulivyoendeshwa. Lakini ripoti ile ukiisoma, ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, baadhi ya haya mambo tunayoyasema yamependekezwa mle na NEC [Tume ya Taifa ya Uchaguzi].

NEC imependekeza kwenye ripoti ile kwamba ni lazima sheria ya uchaguzi iandikwe upya. NEC imependekeza kwamba iwe na watendaji wake katika ngazi za chini na Rais aliafiki mapendekezo haya.

Kwa hiyo, sisi ACT-Wazalendo tunaamini ukiunganisha utashi wa kisiasa na utayari ambao Rais Samia aliuonesha kupitia kikao cha wadau wa siasa pale Dodoma na majadiliano ya siku tatu tuliyoyafanya ya siku tatu mwishoni mwa mwaka jana na makubaliano tuliyoyafanya ambayo hapakuwa na ubishani juu ya ajenda ya Tume Huru ya Uchaguzi, tunaamini kwamba Tume Huru ya Uchaguzi ni eneo muhimu la kuanzia na ndilo ambalo litaweza kusawazisha mazingira ya kisiasa tukaweza kupata katiba mpya.

Tukiwa na utashi madhubuti wa kisiasa tukaipata Katiba Mpya mapema tutafurahi na kushukuru. Lakini kama haiwezi kupatikana mapema katika mwaka mmoja, miwili ijayo itakuwa pia ni fursa ya kuwa na bunge lililochaguliwa na wananchi wenyewe. Kwa hiyo, wawakilishi wale wanaweza kupewa wajibu wa kutengeneza mchakato mzuri wa kupata katiba ambayo itakuja kuhudumia Tanzania na kutuongoza kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa miaka mia moja ijayo.

Mchakato wa katiba wa sasa tuangalie angalau miaka mia moja ijayo. Tuwe na katiba ambayo inaweza ikatupeleka huko tutakakokwenda. Kwa hiyo, hivyo ndivyo ACT-Wazalendo tunavyoona mambo na katika kuhitimisha sisi baada ya kukusanya maoni ya wanachama wetu, baada ya kufanya tafakuri ya kina katika vikao, tumeona sasa ni wakati wa kuelimisha umma.

Kwa hiyo tarehe 19, Machi, tutazindua Oparesheni Tume Huru ya Uchaguzi. Tutakwenda kila mkoa. Tutakwenda kila jimbo. Tutakwenda mijini na vijijini kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuanza na Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba Mpya yenye maoni ya wananchi.

The Chanzo: Umezungumzia juu ya suala la upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi ikiwa ni pamoja na mapendekezo yenu katika huo mchakato. Sasa ningependa kufahamu hayo mageuzi unayoyazungumzia ya Tume Huru ya Uchaguzi peke yake yanatosha kuhakikisha kuwa kunakuwa na uchaguzi huru na haki? Au yaambatane na mabadiliko mengine katika sekta nyingine ili kukamilisha mchakato wa kupata uchaguzi huru na wa haki?

Ado Shaibu: Sisi tumelitazama hilo kwa umakini sana ndio maana katika kikao cha wadau wa vyama vya siasa na tasnia ya siasa kwa ujumla tulikwenda na hoja nne. Zile hoja ukizitazama kwa umakini ndizo ambazo zinaenda kujibu suala la mchakato wa uchaguzi Tanzania.

Kwa hiyo, kwanza unahitaji chombo, Tume Huru ya Uchaguzi, ndio maana tunaanza na ajenda hiyo. Lakini tumezungumza juu ya mageuzi ya Jeshi la Polisi na tumeweka bayana kwamba tunataka sheria zinazoongoza Jeshi la Polisi ziandikwe upya na ni ajenda ambayo ukitazama masuala yaliyoibuliwa kwenye kikao kile ambayo yalisomwa na Mwenyekiti wa kikao kile Profesa [Rwekeza] Mkandala hilo lilikuwemo.

Lakini jingine ambalo tumesema tunataka uhuru wa kufanya siasa. Kwa hiyo, kwa maana kwamba sheria ya vyama vya siasa iandikwe upya na tunashukuru kwamba Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) tumesikia kupitia mawasiliano ambayo wanafanya na sisi makatibu wakuu wa vyama wamo wamejifungia kuandika sheria za mfano, sheria ya vyama vya siasa mpya na sheria ya uchaguzi mpya.

Tunadhani tukirekebisha haya, na kurekebisha tabia ya vyombo vya dola, tutafika pazuri na haya pia hayahusishi mabadiliko ya sheria tu. Yanahusisha mabadiliko ya utamaduni wa uendeashaji wa Serikali na utamaduni wa uendeashaji wa siasa. Unaweza ukawa na sheria nzuri, unaweza ukawa na taasisi lakini bado hamna utamaduni wa kuheshimu sheria.

Tunayo mifano. Sheria ya vyama vya siasa inaturuhusu sisi kufanya mikutano ya hadhara lakini mikutano ya hadhara haifanyiki. Sio kwa sababu hatuna sheria. Sio kwa sababu hatuna taasisi. Ni kwa sababu tu hatuna utamaduni wa kuheshimu sheria. Kwa hiyo, mageuzi tunayoyasema yatakuwa ni pamoja na mageuzi ya kisheria, mageuzi ya kitaasisi na mageuzi ya utamaduni wa kuheshimu na kutii sheria.

Sheria zilizopo hazitoshi lakini hizo hizo sheria mbovu ambazo zingetekelezwa hata nusu tu bado tungekuwa na mazingira mazuri sana lakini Jeshi letu la Polisi ni jeshi la kikoloni. Fikra za Jeshi la polisi ni za kikoloni. Jeshi la Polisi na vyombo vyetu vya dola vilipoanzishwa wakati wa ukoloni lengo lake lilikuwa ni kurahisisha unyonywaji wa rasilimali za Mwafrika.

Kwa hiyo, Jeshi lilikuwa haliulizi kama madini inabidi yaondoke, kama ardhi inabidi itwaliwe Jeshi lilitumika kupiga watu, kuumiza watu ili mradi rasilimali za Afrika zichukuliwe. Kwa bahati mbaya, tumepata uhuru lakini bado Jeshi letu linafikra za kikoloni, bado ni jeshi la piga, ua. Bado ni jeshi la Tanganyika jeki.

Yaani ndugu mwandishi ukiwa unatuhumiwa ili Jeshi la Polisi liridhike kwamba lenyewe ni jeshi lazima likupotezee utu wako. Litakuja litavamia. Sheria inasema lazima wawe na kibali, wapate idhini ya kuja kupekua wawe na kibali cha kukamata. Lakini kwa sababu ni jeshi lenye fikra za kikoloni watakuja hawana kibali cha kukagua, watakuja hawana kibali cha kukamata, watakukamata, watakupiga Tanganyika jeki yaani unainuliwa utembelee vidole, watakupiga makofi.

Tumeona taswira na ninashangaa Wizara ya Mambo ya Ndani haizungumzi sisi ACT-Wazalendo tunamtetea yeyote. Tumeona tukio maarufu hapa yuko mtu mmoja anajiita Mchungaji Zumaridi. Tunaweza kupuuza mambo haya ya mtu ambaye anatuhumiwa ameenda kukamatwa anavuja damu mwili mzima halafu tunajenga taifa ambalo linaweza kuona ni kitu cha kawaida cha mtu ambaye alama za maumivu, alama za majeraha zinaonekana wazi wazi na amefanywa hivi akiwa mikononi mwa polisi.

Kwa hiyo, tunahitaji mabadiliko makubwa katika Jeshi la Polisi, usipokuwa na mabadiliko haya utakuwa na Tume ya Uchaguzi, utakuwa na taasisi, tume itasema atangazwe Ado Jeshi la Polisi lenye fikra za kikoloni litashinikiza vinginevyo.

Lakini swali litakuja haya yote yanawezekana katika kipindi hiki, uzoefu umetuonesha na hili wenzetu baadhi hawakutuelewa lakini nadhani sasa tunakwenda pamoja kwamba katika siasa zetu za Kiafrika hauwezi kupuuza nafasi ya utu, hauwezi kupuuza nafasi ya utashi wa kisiasa wa viongozi wetu.

Ndio maana tulianza na Rais Julius Kambarage Nyerere, akafuatia Rais Ali Hassan Mwinyi. Nyerere hakuwa Mwinyi. Hivyo hivyo Rais Benjamin Mkapa hakuwa Rais Jakaya Kikwete na Kikwete hakuwa Rais John Magufuli. Utashi wa kisiasa unaweza kutumika kusukuma mageuzi mnayoyataka.

Kwa hiyo, sisi Rais Samia Suluhu alivoingia madarakani tulitega sikio kwa umakini mkubwa sana tumsikie katika hotuba yake ya kwanza atasema nini na katika hotuba yake ya kwanza alizungumza juu ya kufungua ukurasa mpya na amerudia lugha hiyo angalau mara tatu kwa sisi tunaofauatilia.

Kwa hiyo, sisi tukasema tumpe faida ya mashaka. Huyu ni mtu ambaye anajiwasilisha kwetu kwamba yeye sio Rais Magufuli. Kwa hiyo, twende nae tuweke mezani ajenda zetu kwamba tunataka mageuzi katika mfumo wa kusimamia uchaguzi; tunataka sheria mpya ya uchaguzi; tunataka mageuzi ya uendeshaji wa Jeshi la Polisi; tunataka Katiba Mpya; na tunataka siasa zenye tija.

Pia, tunataka siasa za kistaarabu; tuweke hoja mezani na hili unaweza kulifikia kwa mazungumzo, haukimbii meza ya mazungumzo unakwenda katika meza ya mazungumzo ukiwa na ajenda halafu unamtazama mtawala ajenda ulizoziwasilisha zinamwingia kichwani anaonesha utayari wa kushiriki na sisi tuliokwenda kikao cha wadau Dodoma wako watu wanadogosha tukio lile, wako watu wanataka kulipuuza tukio lile.

Lakini tukio lile limepanda mbegu nzuri sana ya kuanzia. Mathalani tangu mwaka 1992 Tume ya Jaji Nyalali ilisema kabla ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi ni lazima kutengeneza miondombinu itakayohakikisha hivyo vyama vingi vinafanya kazi yake na moja alilosema lazima pawe na Katiba Mpya, lazima pawe ma Tume Huru.

Ni lazima sheria kandamizi na ziliorodheshwa zote ziondolewe katika kitabu cha sheria cha Tanzania. CCM walifanya nini? Waliweka pamba masikioni. Waliyakataa yote haya Tume ya Nyalali wameiunda wenyewe kupitia Rais Ali Hassan Mwinyi imewaambia hakuna vyama vingi bila Katiba Mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na sheria kandamizi ziondolewe [CCM] walikataa na tangu mwaka 1992 wimbo wa vyama vya upinzani umekuwa ni katiba na Tume Huru ya Uchaguzi toka mwaka 1992. CCM imekuwa ikiweka pamba masikioni.

Hapa katikati mnakumbuka kulikuwa na Tume ya Jaji Kisanga, katumwa kazi na Serikali kaja kaleta maoni ya mageuzi ya mfumo hata utu wake ulitezwa kwa wanaofuatulia historia. Leo hii tunakuwa katika kikao, tunapeleka ajenda ya Tume Huru halafu CCM, mwakilishi wa CCM, mjumbe wa kamati kuu, Waziri Mkuu mstaafu anasema kwa hili la tume wapinzani tumewasikia.

Unaweza kupuuza mambo haya? Huu ni mwanzo mzuri. Muhimu tusibweteke. Muhimu tusiridhike. Huo ni mwanzo mzuri na tumewaambia tunataka chombo cha kuhakikisha haya tuliyoyazungumza yanachakatwa vizuri, yanafanyiwa kazi, yanawasilishwa kwa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Rais katika salamu zake za kuukaribisha mwaka mpya alisema yale yote mtakayoniletea nitayatekeleza. Tusipuuze mambo hayo. Hiyo nayo ni hatua nyingine ya pili muhimu. Tunaambiwa kikosi kazi kinaendelea kuchakata na hivi karibuni kitapeleka Baraza la Vyama halafu kwa Mheshimiwa Rais ambaye amijipa kazi kwamba yote atakayopelekewa atayafanyia kazi.

Muhimu, narudia, tusibweteke na haya maneno tuyatumie kama nyenzo muhimu ya kusukuma mabadiliko na mimi nashukuru wenzetu mwanzoni mimi binafsi na chama chetu hatukufarijika tumekwenda Dodoma baadhi ya vyama havipo. Ni muhimu mchakato wa mabadiliko tunayoyataka utujumuishe sote. Tuwemo sote na ninaziona dalili kwamba tutakuwa sote na tutafika mahala pazuri pa kurekebisha mazingira ya siasa.

Sisi tuliwaambia hatuwezi kutumia guruneti lilelile ambalo tulitumia kupambana na Magufuli. Silaha zitaendana na mazingira ya utawala. Mwanzoni tulipuuzwa [na] tulibezwa. Lakini kauli hizi tulizozisema mwanzoni ndizo zinazoimbwa hivi sasa za maridhiano za kuja mezani pamoja kujenga taifa letu kwa manufaa ya wote.

The Chanzo: Umezungumza vizuri sana. Sasa nije kwenye hilo suala la maridhiano. Natambua kwamba Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia imeonesha juhudi hivi sasa za kutaka uwepo wa maridhiano kati yake na vyama vya upinzani. Mfano, Rais Samia ailihudhuria kikao cha wadau wa siasa, lakini pia kuna huu mkutano wa Kituo cha Demokrasia ambao atakwenda kuufungua.

Tumeona kwa Mbowe baada ya kutoka gerezani alikwenda kuonana na  Rais Samia hivyo kuonesha kwamba Serikali hii inahitaji kupata maridhiano. Sasa nilitaka kufahamu kwako wewe unadhani ni hatua gani binafsi kama Serikali itazichukua utaamini kweli Serikali hii ina mpango wa kubadilisha mfumo wa kidemokrasia ya vyama vingi hapa nchini?

Ado Shaibu: Mambo mawili tu. La kwanza ndio kubwa. Unapokwenda kwenye maridhiano, ni lazima uhakikishe kwamba mnaweka jambo mezani ambalo mtakwenda nalo wote. Na sisi tunadhani jambo hilo kwa mwaka 2022 ni Tume Huru ya Uchaguzi, tena tungefarijika sana tunavyokwenda katika bunge la bajeti sheria mpya ya uchaguzi ipitishwe, kwa sababu hiyo Tume Huru ya Uchaguzi itakayoundwa inayomajukumu ya kuandaa mchakato wa uchaguzi.

Mchakato wa kuandaa uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ambayo yanapaswa kuanza sasa, tunapaswa kuanza na mikono safi. Kwa hiyo, [mwaka] 2022 jambo pekee ambalo Mama Samia atawafuta machozi wadau wa siasa la kuanza nalo, ambalo ninaamini kwamba linawezekana na linakubalika na wadau wote, ni Tume Huru ya Uchaguzi.

Jingine la pili ni sheria ya vyama vya siasa. Twende sote tukafanye siasa za chini, tukajenge vyama vyetu, Mama Samia alizungumza juu ya kwamba mikutano ya hadhara ni haki yetu, ni kweli ni haki yetu. Nimemuona Katibu Mkuu wa CCM Comrade [Daniel] Chongolo na sekretarieti yake wanakwenda chini, wanafanya mikutano ya hadhara.

Lakini hawa ni viongozi wa kisiasa, Chongolo ni Katibu Mkuu, Ado ni Katibu Mkuu, [John] Mnyika ni Katibu Mkuu [wa CHADEMA]. Sote ni sawa mbele ya sheria ya vyama vya siasa. Kwa nini Katibu Mkuu wa CCM anakwenda kufanya mikutano ya hadhara lakini mimi Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo nikiinua mguu nikienda kufanya hata makongamano na vikao vya ndani lazima nibugudhiwe lazima nikamatwe?

Mara zote nikifanya ziara mimi mkoa mmoja, miwili lazima polisi waingilie ziara yetu. Lazima tukamatwe. Hatuwezi kutengeneza kiwango maradufu katika nchi yetu tuweke uwanja sawa na sisi tunakubali rai ya Mheshimiwa Rais kwamba kitu muhimu ni lazima tufungue ukurasa wa siasa za kistaarabu na sisi tunaamini katika siasa za kistaarabu, siasa za kutoa mbadala, siasa za maendeleo.

Unakwenda Songea. Songea ni wakulima wa mahindi hawana mbolea. Mbolea imepanda kwa zaidi ya asilimia mia moja kutoka [Shilingi] elfu hamsini mpaka laki moja. Ukiiacha CCM iliyolala inakwenda Songea kuimba nyimbo za kusifu na kuabudu ukatuzuia sisi kwenda kuwashajihisha wananchi wa Songea wadai kushuka kwa bei ya mbolea anayeumia ni mkulima wa Songea kwa sababu Serikali haitaki kutatua kilio cha mwananchi wa Songea cha mbolea na wajibu wa upinzani kutoa mbadala.

Ukienda Tunduru unamkuta Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ni Mungu mtu na CCM inamchekea. Pale Tunduru kuna kiwanda cha korosho akina mama maskini waliajiriwa katika kiwanda cha kubangua korosho, wakaondolewa mamia kwa mamia kinyume na sheria ya kazi. Walioondolewa wakadai stahiki zao za kuondolewa Mkuu wa Wilaya ameunda tume.

Tume ile imejenga hitimisho kwamba kuna haki fulani wanastahiki japo sisi tilipochungulia nyaraka zile kuna haki wanastahili na wanazo wamenyimwa. Sasa unabaki mchakato wa malipo. Mkuu wa Wilaya anakwenda kuwaambia wale akina mama kwamba hawawezi kulipwa kwa sababu mwekezaji hataki kulipa.

Akina mama wale wanadai haki zao wameongea na vyombo vya habari Mkuu wa Wilaya anawakamata wale akina mama anawaweka ndani. Sasa ukizuia mikutano ya hadhara, ukizuia siasa mbadala, hawa akina mama zaidi ya mia moja wa kiwanda cha korosho cha Tunduru atawasemea nani?

Kwa sababu CCM inacheka cheka haki za kina mama mia nne zinapotea. CCM inawachekea. CCM ilani ipo inapewa uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara inawaona akina mama wale wanyonge wanakamatwa. Wameandika barua kwa Mheshimiwa Rais mpaka hizi barua zimfikie Mheshimiwa Rais lini?

Wameandika barua CCM. Sisi tunakwenda kule kufanya vikao wanatuzuia. Kwa hiyo, tunavyosema kwamba tunataka sheria ya vyama vya siasa irekebishwe na sisi tusiingiliwe na polisi tunasema tunataka kuleta siasa za kistaarabu za maendeleo kwa sababu chini kuna machozi mengi.

Sisi tumekwenda, nitatoa mfano mwingine wa mwisho mdogo, Lindi tunaimba tunaipongeza Serikali kuna mradi wa Liquefied Natural Gas (LNG), kubadilisha gesi asili kuwa kimiminika mradi mkubwa wa matrilioni ya shilingi nadhani sabini zinafika.

Lakini wizara husika inakwenda kukubaliana na makampuni ukiangalia yale makubaliano wanafanya pale humuoni mwananchi wa Tanzania katika yale makubaliano. Sisi tumekwenda Lindi, tumezungumza na wana Lindi hatujamuona mwana Lindi akiwa na uelewa. Kwa hiyo, rasilimali ile itaondoka pale Lindi mradi mkubwa wa trilioni sabini lakini wananchi wa Lindi hawajaandaliwa ili waweze kupata manufaa ya mradi ule mkubwa wa gesi.

Hii CCM, Serikali ya CCM inayokwenda kukubaliana bila kumkumbuka mwananchi wa Lindi na Mtanzania itaamshwa lini kama utaua mfumo wa siasa, kama unaua siasa za ukosoaji?

Kwa hiyo, ukienda chini tutakesha. Sisi tumekwenda katika Jimbo la Newala, Newala Mjini nadhani, yaani Serikali inasema kwamba mradi huu wa kituo cha afya unakwenda Kijiji A, halafu mbunge wa eneo lile anaamua tu kwamba huu mradi hauendi Kijiji hicho unakwenda katika Kijiji nilichozaliwa, [George] Mkuchika, tena anayeyafanya hivi ni mwanasiasa mkongwe wa muda mrefu.

Haya machozi ya wananchi wa Newala atayasemea nani? Mkoma Kijiji kinaitwa Mkoma 1 nani atayazungumzia machozi ya wananchi wa Mkoma 1? Kwa hiyo, tukizungumza sisi kwamba siasa zifungiliwe, mikutano ya hadhara ifunguliwe, tunataka kuisaidia Serikali kuionesha mbadala. Ukienda huko Kigoma huko watu wanakamatwa, wanapigwa, wanaumizwa ardhi ya kwao ya kulima na watu wa hifadhi wanauawa watu. Ndio maana tunasema siasa zikifunguliwa zitaleta tija katika nchi.

Kwa hiyo, la pili Mama Samia afungulie siasa na yeye mwenyewe amesema katika kikao cha wadau kwamba anafahamu kuwa demokrasia ni nyenzo ya maendeleo. Rais Magufuli fikra yake ilikuwa kwamba demokrasia ni kero. Huo ndio ukweli kwake yeye demokrasia ilikuwa ni kitu kinachochelewesha maendeleo, ukitaka maendeleo ua demokrasia na kwa kweli alikuwa kwenye mpango huo ya kuiua demokrasia.

Sisi tunamwambia Rais Samia demokrasia ni rafiki wa maendeleo na hilo litapatikana kwa kujikita na siasa safi, siasa mbadala, siasa za masuala ambazo sisi ACT-Wazalendo tuko tayari nazo. Kwa hiyo, mambo mawili: moja, Tume Huru ya Uchaguzi [na] mbili tufungulie siasa, yaani tupimwe kulingana na uwezo wa vyama vyetu sio mmoja abebwe na dola.

Kwa hiyo, hayo ndio mawili na kwa kweli sisi kwa kujua kwamba mageuzi yanahusisha mambo mengi, sisi tutakwenda na hayo mawili tu tukiamini kwamba yanawezekana na tayari yameshaanza kupata uungwaji mkono miongoni mwa wadau kutoka pande mbalimbali.

The Chanzo: Sawa, kwa sababu tulianza kwa kupata tathimini jinsi mlivyouanza mwaka huu wa 2022, tukiwa tunakwenda kumalizia, ningependa kufahamu labda tutegemee nini kutoka kwenu ACT-Wazalendo kwenye huu mwaka wa 2022 mpaka tutakapo kuja kuumaliza mwezi Disemba?

Ado Shaibu: Mtarajie ACT-Wazalendo ambayo itakuwa bize kusuka mtandao wa chama, sisi viongozi mtatuona tupo bize vijijini kuanzia Katibu Mkuu ambaye ni mtendaji mkuu na makatibu wake wa idara mpaka ngazi zinazofuatia za chini.

Kwa hiyo, kwa maana ya matarajio ya huu mwaka mtakiona chama ambacho kipo bize vijijini na mijini kusuka mtandao wa chama. Lakini mtarajie, na bila shaka, mmeshaanza kuona dalili chama ambacho kinaongoza kuisimamia na kuiwajibisha Serikali.

Tunaamini kwamba ile likizo ya Serikali, maana yake Serikali ilikwenda likizo ya kuwajibishwa, inaweza ikafanya mambo yake ikaamua kuendesha zoezi la machinga kwa uholela, machinga wakawa hawana mtetezi, wizara husika ikawa haisimamiwi wakaamua tu kuziacha bei za bidhaa zipande zinavyopanda.

Na Serikali ikawa inafurahia bei zipande. Huko chini ukienda bidhaa za ujenzi, bidhaa za muhimu [kama vile] mafuta ya kula, bidhaa zote muhimu zimepanda bei. Hii ni dalili ya Serikali iliyolikizo na mimi nampa rai Mama Samia, nimemsikia majuzi anasema bidhaa zinapanda kutokana na hali inayoendelea duniani, vita na kadhalika.

Mimi nashauri atazame kwa makini bidhaa zimepanda sana hata kabla ya vita ya Ukraine [na Urusi]. Bidhaa zimepanda sio kwa sababu ya UVIKO-19. Bidhaa zimepanda kwa sababu ya mfumo mbovu wa kodi na tozo zetu. Unapotoza mafuta ya petroli unakuza bei za bidhaa maradufu na aangalie kwa makini eneo hili kwa sababu bei zinavyopanda juu nguvu ya kununua inaporomoka [na] umaskini unatamalaki.

Sidhani kama yeye atakuwa tayari kuwa Rais ambaye anaona Watanzania wengi zaidi wakidumbukia katika dimbwi la ufukara. Kwa hiyo, tuangalie kodi zetu. Tuangalie tozo zetu. Lakini pia tuangalie udhibiti wa bei za bidhaa muhimu. Hili ni muhimu sana. Muhimu sana. Muhimu sana.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts