Dar es Salaam. Said Ibrahim Stawi alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO), tawi la SBC Tanzania, ambaye aliachishwa kazi kwa kile alichodai ni harakati zake za kupigania maslahi ya wafanyakazi kiwandani hapo.
Stawi hayuko peke yake kwenye orodha ya viongozi wa wafanyakazi waliowahi kufukuzwa kazi katika kiwanda hicho kilichopo eneo la Vingunguti, Dar es Salaam. Siku chache kabla ya kufukuzwa kwake, aliyekuwa Katibu wake Lucas Emmanuel Dundo pia alifukuzwa kwa madai hayo hayo ya kusimamia masilahi ya wafanyakazi kiwandani hapo.
The Chanzo ilishindwa kupata maelezo ya upande wa pili wa uongozi wa kiwanda baada ya uongozi huo kugoma kujibu maswali yetu mahususi. Hata hivyo, uongozi huo umesema kama kuna madai yoyote dhidi ya kampuni yawasilishwe kwa njia rasmi kwa ajili ya utatuzi.
Madhila mengi
Wakati wakiongea na The Chanzo nyumbani kwa Stawi mnamo Machi 18, 2022, huko Kiwalani, Dar es Salaam, viongozi hao wa wafanyakazi walieleza kwamba wafanyakazi kiwandani hapo wanapitia madhila mengi ambayo yameshindikana kutatuliwa kwani kila anayejitokeza kuyaibua uongozi wa kampuni unamfutia kazi.
Madhila haya ni pamoja na madai ya kuafanyishwa kazi bila ya mikataba; watu kufanyishwa kazi kama vibarua kwa zaidi ya miaka 20; na tuhuma za rushwa ya ngono ambayo wahanga wakubwa ni wafanyakazi wanawake.
Mengine yanahusisha watu kufanyakazi miaka mingi bila ya kuwepo kwa nyongeza ya mishahara; pamoja madhila udhalilishaji mahala pa kazi kama vile kukaripiwa kwa makosa madogo madogo na hata ubaguzi wa rangi unaoelekezwa dhidi ya wazawa.
“Sababu mama ya kunifukuza kazi ni ile tabia yangu ya kusimama kwenye haki za wafanyakazi,” Stawi, ambaye amekuwa akifanyakazi na SBC Tanzania tangu mwaka 2009, anaieleza The Chanzo.
“Yaani kwamba wao mpango wao ni kudhulumu mfanyakazi katika maisha yao ya kila siku,” anaongeza Stawi, ambaye kazi yake ilikuwa ni mtunza vifaa. “Mimi mpango wangu ilikuwa ni kuhakikisha kwamba kila mtu anapata stahiki zake kulingana na sheria inavyosema. Kwa hiyo kitendo hicho cha mimi kusimama katika misingi ya kisheria na wao kusimama kwenye upande wa dhuluma ndicho kinachopelekea leo nafukuzwa kazi.”
Athari za kufukuzwa kazi
Stawi ameileza The Chanzo kwamba uamuzi wa kufukuzwa kazi umemuathiri sana, akidai kwamba uamuzi huo umechangia kumpoteza kaka yake lakini pia ulimzuia binti yake ashindwe kufanya mtihani wake.
Kaka yake huyo alikuwa anaugua ugonjwa wa kiharusi na alikuwa akimtegemea Stawi kwa ajili ya kukidhi gharama za maisha na matibabu.
“Sasa juzi [Machi 16] baada ya kupata taarifa kwamba mimi nimefukuzwa kazi, nasikia alidondoka ghafla na umauti wake ukamkuta papo hapo,” anaeleza Stawi. “Kwa hiyo, jana [Machi 17] wamemzika saa nne asubuhi. Kwa hiyo, haya maana yake kwamba, kaka yangu asingekufa kama sio maamuzi waliyonifanyia Pepsi.”
Stawi pia alipaswa kusafiri kwenda Songea ambako binti yake anasoma ili kutatua sintofahamu iliyokuwa imeibuka baina ya binti yake na uongozi wa chuo kuhusiana na suala la ada. Lakini kutokana na kilichotokea, na kulazimika kupigania ajira yake, alishindwa kufanya hivyo.
“Matokeo yake Jumatatu [Machi 14] wameanza mitihani, mtoto hakuingia kwenye mitihani,” anaeleza Stawi. “Hivi ninavyozungumza [binti yangu] hakufanya mitihani ya stashahada kutokana na jambo hili.”
Kupigania haki kumenigharimu
Kwa upande wake, Dundo anasema kwamba hali ya maisha imekuwa ngumu sana kwa upande wake tangu afukuzwe kazi, ukizingatia ana familia inayomtegemea, ikiwa ni mke na watoto wawili.
“Nilijitoa mhanga kwa ajili ya kuwatetea watu lakini mimi imekuja kunigharimu,” anaeleza Dundo kwa masikitiko. “Naona kama [ni] ushujaa lakini kihali ya maslahi imeniathiri.”
Foti Gwebe ni Msemaji wa kampuni ya SBC Tanzania ambaye baada ya kutafutwa kutoa maelezo kuhusiana na shutuma zilizoelekezwa dhidi ya kampuni alisema: “Wanajua utaratibu wa kampuni. Kama wanaona wananyanyaswa ofisini kuna utaratibu wakufuata, wafuate huo utaratibu.”
Gwebe aligoma kujibu maswali mahususi kutoka The Chanzo.
Stawi na Dundo kwa pamoja wameeleza kwamba Ofisi ya Kamishna wa Kazi inaelewa madhila wanayopitia wafanyakazi wenzao wa SBC Tanzania na licha ya kutoa maelekezo kwamba hatua za kuboresha ustawi wa wafanyakazi zichukuliwe maagizo hayo yamepita bila utekelezaji.
The Chanzo iliitafuta Ofisi ya Kamishna wa Kazi ili kujiridhisha kama madai haya ni ya kweli lakini ilishindikana kupata maelezo baada ya afisa anayehusika kuomba muda zaidi na kuturudia lakini mpaka wa kuandika habari hii hakuwa amefanya hivyo.
Wafanyakazi wasikae kimya
“Kiukweli, [wito wangu] kwa wafanyakazi [ni kwamba] hawatakiwi kukaa kimya kwa sababu hali hii itakuwa ni endelevu; itakuwa ni hali ya kurithishwa,” anashauri Dundo. “Na kwa Serikali [ni] kuweza kupita mara kwa mara na kuona vitu gani vinavyoendelea [kwenye maeneo ya kazi].”
Mbali na kuwataka wafanyakazi wenzake wasikate tamaa katika kudai haki na stahiki zao, Stawi pia alikuwa na haya ya kusema kuhusu mamlaka zinazohusika na kusimamia masilahi ya wafanyakazi nchini:
“Serikali mimi nailamu sana,” alisema Stawi. “Serikali imechangia mimi kufika hapa nilipofika. Kwa sababu siamini kwamba ipo Serikali duniani inayoshindwa kuchukua maamuzi dhidi ya mwananchi wake, au taasisi iliyo ndani ya nchi yake, inapofanya makosa. Serikali ijiangalie. Serikali ipo haja ya kupata meno ya kusimamia hivi vitu.”
Dundo na Stawi wameahidi kupigania haki zao kwa kuanzia katika Mahakama ya Kazi na ikishindikana kupata haki zao hapo wataendelea kwenda mahakama zingine za juu.
One Response
Bora kujiajiri