Dar es Salaam. Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kimewataka waajiri nchini kuzingatia sheria, kanuni, na miongozo mbalimbali inayoongoza masuala ya kazi ili kuhakikisha haki, heshima, na maslahi kwa wafanyakazi.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hapo Machi 31, 2022, Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka TUICO Noel Nchimbi alisema kufanya hivyo kutawasaidia viongozi wa matawi wa wafanyakazi kutokuingia kwenye migogoro isiyokuwa na tija na waajiri.
Wito huo wa Nchimbi unakuja wiki moja tangu The Chanzo ichapishe habari za kufukuzwa kazi kwa viongozi wa wafanyakazi kiwandani hapo, hatua walioihusisha na harakati zao za kupigania haki na maslahi ya wafanyakazi.
Wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo, Said Ibrahim Stawi, ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani (TUICO), tawi la SBC Tanzania kabla ya kufukuzwa kazi alianisha madhila wanayokumbana nayo wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Madhila haya ni pamoja na madai ya kuafanyishwa kazi bila ya mikataba; watu kufanyishwa kazi kama vibarua kwa zaidi ya miaka 20; na tuhuma za rushwa ya ngono ambayo wahanga wakubwa ni wafanyakazi wanawake.
Mengine yanahusisha watu kufanya kazi miaka mingi bila ya kuwepo kwa nyongeza ya mishahara; pamoja madhila ya udhalilishaji mahala pa kazi kama vile kukaripiwa kwa makosa madogo madogo na hata ubaguzi wa rangi unaoelekezwa dhidi ya wazawa.
Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari hapo jana, Mkuu huyo wa Idara ya Sheria kutoka TUICO Noel Nchimbi alisema:
“Baada ya kupokea habari hiyo [iliyoibuliwa na Stawi], mnamo Machi 28, 2022, ofisi ya Katibu Mkuu [TUICO], Katibu wa TUICO Kanda ya Dar es Salaam, uongozi wa kiwanda cha SBC Tanzania Limited, na kwa kushirikiana na ofisi ya Kamishna wa Kazi nchini, tulikutana jijini Dodoma, katika kikao cha ndani.
“Na lengo hasa ilikuwa ni kufanya mashauriano na kujadili masuala yaliyoibuliwa katika habari hiyo iliyotolewa mnamo Machi 23, 2022, na aliyekuwa mwenyekiti wa tawi katika eneo la kazi.
“Sambamba na kutafuta muafaka wa pamoja ili kutatua changamoto zinazo wagusa wafanyakazi wa SBC Tanzania Limited pasipo kuvunja misingi, matarajio na taratibu zilizopo kwa mujibu wa sheria za kazi hapa nchini.
“Katika kikao hicho cha ndani tulitoka na makubaliano kadha wa kadha yaliyokuja na muafaka wa kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza ndani ya [kiwanda cha] SBC Tanzania Limited.
“Hivyo chama cha wafanyakazi, kwa maana ya TUICO, kitaendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza makubaliano hayo ili haki, heshima na maslahi ya wanachama na wafanyakazi vizidi kustawi na wafanyakazi watambue wajibu wao wakati wote wanapokuwa kazini.”
Hata hivyo, Nchimbi hakuweka wazi makubaliano ambayo chama hicho kilifikia na uongozi wa SBC Tanzania Limited na endapo kama makubaliano hayo yatahusisha kurejeshwa kazini kwa viongozi wa wafanyakazi waliofukuzwa kwa kupigania maslahi ya wafanyakazi wenzao kama Stawi na mwenzake Lucas Emmanuel Dundo aliyekuwa Katibu wake.
Kauli ya TUICO inakuja siku moja tangu maafisa wa Serikali kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Idara ya Uhamiaji kufanya ziara maalum kwenye kiwanda cha SBC Tanzania ambapo walifanya ukaguzi kiwandani hapo na kuhoji baadhi ya wafanyakazi.
Mwakilishi wa kampuni ya SBC Tanzania aliyekuwepo katika mkutano huo na waandishi wa habari ulioitishwa na TUICO alisema kampuni hiyo iko tayari kutimiza matakwa yote ya makubaliano ambayo kampuni hiyo imeingia na TUICO na Serikali.
“Nitaheshimu yale maazimio ambayo tumeyafikia baina ya pande zote tatu kati ya Ofisi ya mheshimiwa Kamishna wa Kazi, chama cha wafanyakazi TUICO Tanzania na kampuni ya SBC,” alisema mwakilishi huyo.
“Kuna maazimio ambayo tumeyafikia,” aliongeza. “Kwa hiyo, mimi nitaheshimu hayo na tutayatekeleza na kuendelea kuheshimiana kama jamii moja kwenye jumuiya ya wafanyakazi Tanzania.”
Haya ni Baadhi ya Madhila Wanayopitia Wafanyakazi wa SBC Tanzania
Serikali Yatimba Kiwanda cha Pepsi Kufuatia Malalamiko ya Wafanyakazi
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.