The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Hasa Kilipelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?

Hofu ilitoa mchango mkubwa sana katika kufanikissha tukio hilo kubwa katika historia ya Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Watanzania wengi hawafahamu kwamba Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mnamo Disemba 10, 1963, lakini utawala ukabaki kwa Sultan kama Mkuu wa Nchi. Mnamo Januari 12, 1964, Sultan akapinduliwa na kuikimbia nchi kulikopelekea kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, dola kamili ya Wazanzibari iliyokuwa na Serikali yake, wimbo wake wa taifa, na Rais wake.

Bahati mbaya dola ya Zanzibar haikudumu. Mnamo Aprili 26, 1964, Muungano ulitangazwa wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunayoijua sasa. Na huo ukawa mwisho wa Zanzibar kama nchi huru.

Zanzibar, kwa uamuzi ule, ilipoteza nguvu ya kujiamulia mambo yake. Ikapoteza utambulisho miongoni mwa mataifa. Kuelewa umuhimu wa hili, rejea mkasa wa Zanzibar kutaka kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC). Kwa upande wake, Tanganyika ni kama tu iliongeza ukubwa wa himaya yake na kubadili jina, kwani yenyewe, kama mshirika mkubwa, ilivaa koti maarufu la Muungano.

Wazanzibari hadi hii leo wanalalamika kuwa makubaliano ya awali ya kimuundo katika Muungano hayakutekelezwa. Wao, alisema hayati Maalim Seif Sharif Hamad katika hotuba zake, walidhani wanakabidhi mamlaka kwa Serikali ya Muungano ili Tanganyika ifanye hivyo hivyo na kuundwe mamlaka ya tatu katika muundo wa shirikisho. Badala yake Tanganyika wakawa ndiyo Muungano.

Muungano umebakia suala gumu, tata, linalogusa hisia na linalobishaniwa zaidi katika siasa za Tanzania. Na hii ni ishara ya ukubwa wa uamuzi ule wa kuunganisha nchi hizo mbili na athari zake, hasa kwa Wazanzibari.

Moja kati ya maswali magumu yanayoulizwa hadi leo ni nini hasa kilipelekea muungano kutokea? Faida gani ilikuwa ikitafutwa? Je, huu ulikuwa ni muungano wa hiari au kulikuwa na mbinyo aidha wa ndani au wa nje ambao uliwaacha wahusika, hasa Abeid Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar huru, bila chaguo jingine?

Msimamo rasmi wa Serikali ambao pia ni wa chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM), kama anavyotaja Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, ni kwamba huu ni Muungano wa hiari na asemaye tofauti ni mzushi asiyefahamu vizuri historia. Hata hivyo, hao ‘wasiojua historia’ na wenye maelezo mbadala na tofauti nao ni wengi.

Nini hasa kilipelekea Muungano?

Maelezo rahisi zaidi yanayotolewa ni kuwa Muungano huu ni wa hiari unaotokana na maono ya waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume na ni hatua katika kuetekeleza Umajumui wa Afrika, nadharia iliyokuwa katika fasheni kipindi hicho. Ni vigumu kuamini sababu hii kwa sababu kama maono yalitosha ungefanikiwa Muungano wa Afrika ya Mashariki au Afrika nzima.

Kingine kinachotajwa kuchagiza Muungano ni shughuli za kiuchumi sawa zilizowaunganisha kama uvuvi na biashara na utamaduni wa pamoja, ikiwemo kuunganishwa na lugha moja ya Kiswahili. Kadhalika, inatajwa kuwa watu wa pande hizi mbili wote walipitia historia ya madhila ya aina moja chini ya ukoloni.

Jambo jingine linalotajwa kuchochea Muungano ni uhusiano wa karibu na kirafiki uliokuwepo kati ya vyama vya TANU kwa upande wa Tanganyika na ASP kwa Zanzibar vilivyopigania uhuru kabla ya kuungana mwaka 1977 na kuunda CCM.

Katika hili, mwandishi Amrit Wilson katika kitabu chake Tishio La Ukombozi anathibitisha kuwa ASP iliitegemea TANU kwa uchambuzi wa kisiasa, ingawa baadhi ya wanachama wa ASP hawakufurahia hali hiyo.

Hoja zote hizi ni nzuri ingawa bado tunaweza kuhoji kuwa hata nchi nyingine pia zilikuwa na ukaribu wa kijiografia, utamaduni wa pamoja na hata walipitia madhila sawa nyakati za mkoloni lakini miungano  bado haikuwezekana.

Mwandishi Wilson katika Tishio La Ukombozi anapinga vikali hoja hizo, kwa kusema: “Kuuelezea Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika kuwa ni wazo la Nyerere la kujenga Umoja wa Umajumui wa Afrika, kama baadhi ya waandishi walivyofanya, ni jambo la kipuuzi.”

Hofu mbalimbali za kiusalama

Ukiacha sababu hizo ‘za kiserikali,’ suala la usalama linatajwa kama sababu kuu iliyopelekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Suala hili lina pande kadhaa. Kwanza, Karume alitaka kulinda nafasi yake ya uongozi, akihofia maadui wa Serikali yake waliotokana na mapinduzi na matukio, baadhi ya kikatili sana, yaliyofuatia yaliyoacha makovu mengi.

Lakini kubwa zaidi, kulikuwa na tishio kutoka kwa viongozi waandamizi wa Serikali yake kutoka chama cha Umma Party walioamini katika itikadi ya Ukomunisti, hususan Waziri wake wa Mambo ya Nje na Biashara, Abdurrahman Babu, ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika uendeshaji wa nchi. Kwa kuhofia upinzani, Karume alitumia fursa ya Babu kusafiri nje ya nchi kuingiza Zanzibar katika Muungano.

Inadhaniwa kuwa Karume aliona kuitoa sadaka dola ya Zanzibar kwa kaka mkubwa, Tanganyika, ilikuwa ni njia bora zaidi ya kumdhibiti Babu, ambaye baadaye alihamishiwa Bara na kupewa uwaziri chini udhibiti ya Ofisi ya Rais Nyerere.

Fikra za siasa za mrengo wa kushoto za kikomunisti hazikukubalika siyo tu kwa Karume bali hata kwa Nyerere aliyekuwa na msimamo wa wastani akiamini katika siasa za mrengo wa kushoto lakini zenye vionjo vya Uafrika.

Kwa upande mwingine, Nyerere aliamini visiwa hivyo vikikaliwa na adui,  Tanganyika ingekabiliwa na hatari kutoka bahari ya Hindi. Nyerere alikuwa na wasiwasi huo muda mrefu, hata kabla ya uhuru wa Tanganyika, ambapo alinukuliwa akisema: “Kama ningeweza kukitupa kile kisiwa cha Zanzibar katikati ya Bahari ya Hindi, ningefanya hivyo. Kiko dhaifu sana kwenye kupokea ushawishi wa nje. Naogopa kitatuumiza kichwa sana.”

Fikra hizi zingalipo hata Tanzania ya leo, kama alivyothibitisha mwaka 2014 aliyewahi kuwa waziri mwandamizi na kada wa CCM William Lukuvi aliysema kwamba Zanzibar haiwezi kuachwa ijitawale kwa sababu asilimia 95 ni Waislamu, hivyo Waarabu watarudi na watazalisha siasa kali na hatimaye kutusumbua sisi Wabara.

“Zanzibar ni nchi ndogo sana,” alisema Lukuvi kwenye hafla hiyo ya hadhara. “Unaweza ukauliza kwa nini sisi tunaing’angania? Madhara ni makubwa kuiacha Zanzibar kama ilivyo. Kile ni kisiwa. Visiwa hivi vinasumbua sana. Huwezi kujua kitu gani kitaingia kule na kitavuka na kuingia huku. Kwa sababu, hamna uwezo wa kulinda mipaka ya bahari, ni mipaka mipana sana.”

Katika maelezo yake hayo aliyoyatoa kanisani, Lukuvi hakuficha kuhusu aonayo kama haki ya Watanganyika kuwa ndiyo dola: “Sisi ni wakubwa, lazima tuvae koti la Muungano. Hata jeshi hili ni la kwetu sisi! Rais huyu wa Tanzania Bara ndiye ataendelea kuwa Rais wa Muungano, ataendelea kuwa Amiri Jeshi Mkuu. Hatuwezi kumyonyoa. Na ataendelea kuwa mawakilishi wa kiti chetu UN.”

Ipo pia fikra kwamba Muungano ulikuja kwa matakwa ya Marekani na Uingereza na uliratibiwa na majasusi wa nchi hizo ili kuzuia hatari ya Zanzibar kuangukia katika himaya ya ushawishi wa Wakomunisti na kuwa ‘Cuba ya Afrika’ itakayosambaza  fikra hizo eneo la Afrika ya Mashariki katika kipindi hicho cha vita baridi. Jambo hili limeandikwa kwa kirefu na mwandishi Amrit Wilson.

Kungetokea nini bila Muungano?

Ukiangalia ushahidi mbalimbali, utaona kuwa zile sababu za kiserikali zinazotajwa kupelekea Muungano, hazina nguvu sana. Kwa maoni yangu, huu ulikuwa zaidi ni Muungano wa hofu kuliko kitu kingine chochote. Karume alihofia kupokwa nafasi yake siyo tu na wakomunisti bali pia  wafuasi wa Usultan akataka Tanganyika kubwa yenye nguvu imkinge.

Nyerere, kwa upande wake, alikuwa na hofu ya ushawishi wa mawazo ya ukomunisti na kusambaa Tanganyika, lakini pia alihofia usalama wa Tanganyika kutoka baharini. Mataifa ya Magharibi nayo yalitaka kumdhibiti adui yao China kujenga himaya kama Cuba visiwani hapo.

Hofu hizi ni halisi au visingizio tu? Nini kingetokea bila  kuwepo muungano? Binafsi naamini huenda tungeshahudia mapinduzi mengine kadhaa kama Zanzibar ingebaki peke yake. Fikiria hasira za walioathiriwa na mapinduzi. Fikiria kuhusu mkorogano na visasi ambavyo vingefuata baada ya kuuliwa Karume. Hivyo, sina shaka kuwa Muungano ulisaidia kuituliza Zanzibar.

Hata hivyo, sina hakika kama inakubalika gharama ambayo Zanzibar ililipia kupata utulivu huu hivi sasa kwa kutoa sadaka dola yake kupitia muundo wa Muungano wa Serikali mbili badala ya shirikisho, huku Tanganyika ikifanya maamuzi muhimu, ikiwemo nani anatawala. Bahati mbaya ni kuwa leo hii Zanzibar walau kurekebisha tu mfumo huu wa Muungano ni ngumu kwa sababu amekuwa mshirika mdogo na dhaifu.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia +255 735 420 780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Muungano ni jambo mtambuka, na hata kifo cha Karume NI Mapinduzi yalikuwa Tu, ILA tunu kubwa ya Muungano ni Amani na usalama pande zote mbili za muungano

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts