Kwa majina naitwa Msafiri Elia Mchera, mimi ni mzaliwa wa Dodoma na hapa ndipo ninapoishi na kufanya kazi zangu kwa sasa. Mimi nilizaliwa mwaka 1994 nikiwa mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto watano.
Mimi nilizaliwa nikiwa mzima kabisa lakini ilipofika mwaka 2000 nilianza kuugua macho. Niliumwa ugonjwa ambao ulikuwa haueleweki ni ugonjwa wa aina gani. Unajua kipindi kile wazazi wetu hawakuwa na elimu yeyote kuhusu ugonjwa uliokuwa ukinisumbua.
Kwa hiyo, hiyo ilifanya ishindikane mimi kupatiwa matibabu ninayostahiki. Badala yake, wazazi wangu wakaanza kunipeleka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kupata matibabu. Hapo ndipo nilipoanza kutumia dawa za kienyeji kutibu matatizo ya macho huku wazazi wangu wakiamini kwamba zitanisaidia.
Hali ilipozidi kuwa mbaya zaidi, hiyo ilikuwa mwaka 2001 sasa, wazazi wangu waliamua kunipeleka hospitali ya macho ya Mvumi iliyopo hapa Dodoma kwa ajili ya kuangalia hali yangu ili niweze kupata tiba.
Tulipofika pale daktari akanipima na kuwaeleza wazazi wangu kwamba nina ugonjwa wa surua. Hata hivyo, daktari alisema nilipelekwa hospitalini hapo nikiwa nimechelewa sana na hivyo haitakuwa rahisi kwa mimi kupata tiba.
Daktari alisema kwamba dawa za macho ambazo nilikuwa natumia hazikuwa sahihi kwa ajili ya kutibu ugonjwa ule. Kwa hiyo, akawaambia wazazi wangu nimeshachelewa na hata operesheni sitaweza kufanyiwa tena kwa sababu surua imeshaweka kikovu kwenye macho yangu.
Lakini hata uwezo wa kuona vitu kwenye macho yangu ulishakufa. Mnamo mwaka 2003, wazazi wakanipeleka shule ya wasio ona Buigiri iliyopo hapa Chamwino Ikulu, Dodoma.
Safari ya kuwa mwandishi wa habari
Nikasoma pale tangu mwaka huo hadi nilipo hitimu masomo yangu ya elimu ya msingi mwaka 2009.
Lakini wakati namaliza shule ya msingi walikuja Wachina kuja kutupima macho kuhusiana na mtoto wa jicho. Wachina waliniambia kwamba wanataka wanipeleke hospitali nchini China kupata matibabu.
Baada ya kuniambia hivyo wazazi waliitwa kuambiwa lakini hawakukubali jambo hilo la mimi kwenda China kutibiwa macho. Kwa hiyo, nilikwama na sikwenda. Baada ya hapo ilinibidi nikae nyumbani kusubiri matokeo yangu ya kumaliza elimu ya darasa la saba.
Bahati nzuri Mungu alinisaidia nikafanikiwa kufaulu na kujiunga na shule ya sekondari Mvumi DCT hapa mkoani Dodoma. Ilipofika mwaka 2010 nikaanza masomo ya kidato cha kwanza mpaka mwaka 2013 nikahitimu. Baada ya kumaliza matokeo ya kuhitimu kidato cha nne yalitoka na nilifaulu kwa kupata daraja la tatu.
Lakini sikutaka kusoma kidato cha tano na sita. Mimi niliwaambia wazazi wangu kwamba nahitaji kwenda chuo moja kwa moja ili kupunguza muda wa kusoma ili nijiajiri kama ni kupata kazi nipate.
Baada ya pale ilifipoka mwaka 2015 nikaenda chuo mkoani Morogoro kusoma masomo ya uandishi wa habari kwa ngazi ya cheti na astashahada katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph. Baada ya kumaliza chuo nikasubiria matokeo na baada ya kutoka nilifanya vizuri.
Kisanga cha kutafuta kazi
Ilinibidi mimi nirudi nyumbani Dodoma kwa ajili ya kufuatilia masuala ya kazi. Sasa katika kufuatilia mambo ya kazi nilijaribu kutuma kwa kweli maombi ya kazi sehemu nyingi, redio za aina mbalimbali, kote walikuwa wananiambia kwamba nafasi za kazi hakuna.
Sehemu nyingine sikurudishiwa majibu kama nafasi za kazi zipo ama hakuna. Kutokana na jinsi nilivyo, inaonekana watu wanao miliki vituo vya habari yawezekana bado hawajaamini kwamba mimi nina uwezo wa kufanya kazi kama watu wengine. Kwa hiyo, bado sijapata kazi.
Kujiajiri
Kiukweli baada ya kuona kazi kupata ni changamoto, niliamua kujiajiri mwenyewe, napambana kidogo kidogo. Baada ya kukaa muda mrefu bila kupata kazi niliamua kufungua biashara ya ufugaji wa kuku na njiwa.
Lakini pia, sasa hivi nauza mafuta ya petroli [na] mihogo. Lakini nina mpango wa kutengeneza tambi na bisi niuze. Vyote hivi ninafanya mwenyewe. Niliamua kufanya biashara ili na mimi niweze kujiingizia kipato kwa sababu huwezi ukakaa ukamtegemea mtu. Ni lazima ufanye kazi.
Biashara yangu inakwenda vizuri japo kuna changamoto ya upandaji wa vitu bei. Ninauza kuendana na bei na sijawahi kudhulumiwa eti kutokana na hali yangu. Hakuna, sijawahi.
Pamoja na changamoto zote hizi ninamshukuru Mungu nimepambana nimejenga nyumba yangu ya vyumba vitatu, yaani nimepambana mwenyewe mpaka nimefanikiwa.
Kuhusu unyanyapaa, mimi kama mlemavu wa macho kwa kwali kwangu sijawahi kuupitia unyanyapaa. Ninaishi vizuri tu na kila mtu. Hakuna shida kama hiyo.
Kwangu mimi changamoto kama hizo hakuna labda itokee tu kutokuelewana na mtu. Lakini mambo ya kusema kwamba kuna shida ya unyanyapaa, hapana, hakuna.
Changamoto za mahusiano
Nilikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke mmoja mwaka 2020 nilitaka kumuoa. Lakini shida ilikuwa kwa wazazi wangu walikuwa hawamtaki huyo mwanamke.
Mimi nilikuwa nimempenda na tunapendana. Tulikuwa tukisaidiana kwenye mambo mengi, tukishirikiana vitu vingine vya maisha vizuri tu.
Wazazi wangu wakaniambia kwamba huyu mwanamke sisi hatumtaki. Wakaniambia mwanamke anaonekana ni mjanja sana atakuwa hajatulia. Walimkataa kutokana na wanavyomuona. Basi, tukaachana.
Kiukweli nilikuwa sielewi. Baada ya kutokea suala hilo kiukweli niliumia sana kwa sababu ni mwanamke ambaye nilikuwa nampenda na yeye alikuwa akinipenda.
Mimi kwa sasa kwa kweli nahitaji kuwa na kazi ya uhakika kwa sababu kuna vitu bado sijavitimiza. Nitakapo kuwa nimepata kazi ninaamini nitafanya kazi kwa ajili ya kuyatimiza malengo yangu.
Lengo langu ni kuwa na mimi niwe na watu wa kuwaajiri na ndio shauku yangu kwa kiasi chochote kile nitakacho kipata.
Wito kwa walemavu, Serikali
Mimi nawashauri walemavu wenzangu watengeneze mtazamo mzuri kwenye jamii iwe kwa wanaume ama wanawake na watu wote ambao wanawazunguka. Wanatakiwa wajitume, yaani wafanye kitu ambacho ni zaidi ya vile ambavyo wanatakiwa wawe.
Sisi walemavu tunapaswa kufanya tofauti na mtu mwingine ambavyo anafanya. Kwa hiyo, vikashafanyika vitu kama hivyo basi mimi nadhani jamii itawaheshimu watu wenye ulemavu na hakutakuwa na changamoto kama ambavyo watu wanasema.
Kwa upande wa Serikali, wito wangu ni kwamba Serikali inabidi itengeneze sheria ambayo inaweza ikatusaidia watu wenye ulemavu kama sisi kupata kazi kwa urahisi. Yaani hakuna mfumo rasmi wa Serikali ambao utamsaidia mtu mwenye ulemavu kupata kazi au kujitegemea mwenyewe.
Kwa sababu kuna zile asilimia ambazo walizitamka wao kwamba asilimia tatu kuhusiana na watu kama sisi. Hizo asilimia kiukweli hazifanyiwi kazi. Kwa hiyo, wameziandika kwenye makaratasi ila hawazifanyii kazi ya aina yoyote. Kwa hiyo, kama Serikali ikiwajibika itakuwa vizuri sana.
Kingine pia ni kwa Serikali, au jamii kwa ujumla, iwasaidie watu wenye ulemavu kupata mitaji. Hiyo itakuwa nzuri kwa sababu hicho ndiyo kitu ambacho kinatusumbua. Sasa hivi ninatamani nifungue kibanda cha chipsi au duka la urembo lakini sasa pesa ndiyo sina.
Msafiri Mchera amesimulia simulizi hii kwa mwandishi wa The Chanzo mkoani Dodoma. Kwa maoni, unaweza kumpata Jackline kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni jackline@thechanzo.com.