Katika kile kinachoonekana kama ni mwendelezo wa ubaguzi unaofanywa na mamlaka za nchi dhidi ya wenyeji wa Ngorongoro, Serikali hivi karibuni imewapatia barua za uhamisho wafanyakazi kumi wazawa wa Ngorongoro wanaofanya kazi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) zikiwajulisha kuhamishiwa taasisi nyingine za kihifadhi na zile siziso za kihifadhi.
Wafanyakazi hao walipewa barua za uhamisho mmoja mmoja tangu Mei 9, 2022, huku wakitakiwa kuripoti kwenye vituo na taasisi mpya zao za kazi kuanzia Mei 18. Mpaka muda wa kuandika makala haya, wafanyakazi wazawa wanne tu ndiyo wamesharipoti kwenye vituo vyao hivyo vipya vya kazi, kwa mujibu wa taarifa nilizonazo.
Wafanyakazi waliopatiwa barua za uhamisho ni Joshua Olembario, ambaye amepelekwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA); Arpaakwa Sikorei, ambaye ameshahamia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA); na Ngorisa Sandei, ambaye naye anapelekwa TAWA, huyu alipewa uhamisho akiwa masomoni!
Wengine ni Mathayo Ndari ambaye anahamishiwa TAWA; James Oloju aliyepelekwa Baraza la Sanaa (BASATA); Yohana Shaudo aliyehamishiwa TAWA-Gurmeti; Moinga Olesasi, ambaye amepelekwa Bodi ya Utalii (TTB), Tobiko Sane aliyepelekwa TTB pia; Abisaye Lomayani amepelekwa Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) mkoani Dodoma; na Soka aliyehamishiwa TARURA pia.
Fomu za kuainisha idadi ya mali
Uhamisho huu unafuatia barua ya Aprili 27, 2022, iliyowataka wafanyakazi wazawa wa Ngorongoro kujaza fomu maalum za kuainisha idadi ya mali, kama vile nyumba na mifugo, wanazomiliki ndani ya hifadhi. Mwisho wa kuwasilisha fomu hizo ilikuwa ni Aprili 29, 2022.
Maelekezo hayo yanafuatia kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa wafanyakazi wazawa waliojenga makazi ndani ya hifadhi, nyumba zao zitabomolewa bila fidia na hawatafidiwa kama wananchi wengine kwenye mchakato wa kuhamisha raia wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Kwa ujumla, kati ya wafanyakazi 10 wanaohamishwa, tisa ni wa kabila la Kimaasai. Hii kwa Wamaasai wengi inajenga picha kwamba zoezi hili limebeba sura ya ukabila.
Wakati wa mazungumzo yangu na baadhi ya wafanyakazi hao waliokumbwa na kadhia hiyo, wengi wao wamenieleza kwamba uhamisho wao umefanywa kwa hila, wakisema kwamba ni mwendelezo wa mambo kadhaa ya hujuma inayofanywa dhidi ya wenyeji wa Ngorongoro.
“Uhamisho huu ni wa kibaguzi,” mmoja kati ya wafanyakazi waliohamishwa alinieleza bila kutaka jina lake kutajwa mitandaoni. “Nasema hivi kwa sabau [huu uhamisho] umewalenga wafanyakazi wazawa na zaidi wa kabila la Kimaasai.”
Hoja hii inapata nguvu kwa kuangalia matendo mengine yanayofanywa na mamlaka za nchi.
Umaasai unapokuwa tatizo
Kwa mfano, wakati wa kupeleka askari wilayani Handeni, mkoani Tanga kwa ajili ya kusimamia mradi wa Serikali wa nyumba za kuwahamishia Wamaasai wa Ngorongoro, kuwa mfanyakazi Mmaasai ilikuwa ni kigezo kikuu cha kutofuzu kwenda kusimamia mradi wa Handeni.
Hata operesheni maalum zinazotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, wafanyakazi wazawa wamekuwa wakitengwa kwa makusudi. Hali hii imepelekea mahusiano kati ya wenyeji, mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na Serikali kwa ujumla kuendelea kuwa ya mashaka makubwa.
Wafanyakazi hao wamehamishwa licha ya kugomea uamuzi huo kwa kukataa kujaza fomu maalumu ambazo ziliwataka kutoa idadi ya mifugo wanayowamiliki.
Wafanyakazi wameeleza kwamba walipinga kujaza fomu hizo kwa kuwa ni wafanyakazi wazawa peke yao tu ndiyo walitakiwa kuainisha mali wanazomiliki ili kurahisisha mchakato wa kubomoa makazi yao bila fidia.
Kwa utaratibu wa kawaida, mwajiri hana mamlaka yeyote na mali binafsi ya mwajiri. Mchakato wa kutambua mali za mfanyakazi kama kuna haja hiyo ni lazima ufuate sheria.
Tatizo siyo uhifadhi
Mchakato huu dhidi ya wafanyakazi Wamaasai ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ni kielelezo kingine tosha kuwa mchakato wa kuwahamisha Wamaasai ndani ya Ngorongoro hautokani na madai ya uhifadhi bali hujuma dhidi ya Wamasai.
Kama tatizo lingekuwa uhifadhi basi kusingekuwa na sababu ya kuwalenga wafanyakazi wa kabila flani.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2018, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitoa maelekezo kwa taasisi, hasa za kitalii zinazofanya shughuli zao ndani ya hifadhi, yasitoe ajira kwa wenyeji wa Ngorongoro na kwamba wale waliokwishaajiriwa wahamishwe nje ya eneo la Ngorongoro.
Pia, kuna tetesi kuwa majina ya wafanyakazi wazawa wengine watakaohamishwa kutoka Ngorongoro kwenda taasisi nyingine zitatolewa baadae.
Mwanzoni wa mwezi Mei, Majaliwa akiwa mkoani Tanga katika eneo la Msomera, Handeni, alisema kuwa wafanyakazi wazawa waliojenga nyumba za kudumu ndani ya hifadhi kinyume cha kile alichokiita kinyume na sharia za hifadhi wavunje wenyewe na kwamba hawatapata fidia yeyote.
Wenyeji wamepokea jambo hili kwa masikitiko makubwa.
Tangu mwaka 2019, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro haijawahi tena kutoa nafasi za ajira kwa wenyeji wote wenye vigezo zote katika nafasi za ajira zilizotoka.
Pia, mwaka 2019 mamlaka ilishirikiana na uongozi wa mkoa wa Arusha kutoa waraka kwa wamiliki wa hoteli na loji kusitisha utoaji wa ajira na kuwaondoa kazini wenyeji waliokuwa wanafanya kazi katika maendeo yao.
Kwa maoni yangu, mambo mengi yameharibika kutokana na uhusiano mbaya kati na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wenyeji.
Tangu mwaka 2014 baada ya ujio wa mhifadhi mkuu aliyepo kwa sasa Dk Freddy Manongi, miradi mingi ya maendeleo kwa miaka mitatu sasa imehamishiwa katika tarafa nyingine ya halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro na hasa katika wilaya ya jirani ya Karatu ambapo ndipo yalipo makao makuu ya mamlaka.
Julius Moses Lolchumuya ni mwenyeji wa Ngorongoro kutoka kabila la Wamaasai. Kwa maoni, anapatikana kupitia mosesjulius04@gmail.com au Twitter kama @JOleshangai. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa mawasiliano zaidi.