Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kitendo cha Serikali kuonyesha nia ya kuwaondoa wenyeji wa Hifadhi ya Ngorongoro kwa madai ya kulinda urithi wa dunia kutokana na kile kinachodaiwa ni uharibifu unaofanywa na wananchi ni kinyume na uanzishwaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Chama hicho cha upinzani kilibainisha hilo kwenye taarifa ya Msemaji wake wa Sekta ya Maliasili na Utalii Juliana Donald juu ya mapitio ya utekelezaji wa bajeti na hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2022/23 iliyowasilishwa bungeni siku ya Ijumaa, Juni 3, 2022.
“Tumeona Serikali inafanya kila njama za kuwaondosha wafugaji jamii ya Wamaasai katika eneo lao la asili kwa madai ya kulinda masharti ya kimataifa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ilimnukuu Juliana, ikisisitiza kuwa siyo kweli kwamba uwepo wa wakazi hao una hatarisha uendelevu wa hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa ACT-Wazalendo, mpango wa kuwahamisha wenyeji wa Ngorongoro umekuja baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuonyesha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo ya kumaliza changamoto ya matumizi mseto ya ardhi ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro hapo mwaka 2021.
Akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa bajeti na bajeti ya mwaka 2022/23 bungeni hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana alisema kupitia majadiliano ambayo Serikali imefanya na wadau mbalimbali, ikiwemo wananchi wa Ngorongoro, tayari wameandikisha kaya 278 zenye wakazi 1,439 ambao wapo tayari kuhama kwa hiari yao kwenda kuishi katika maeneo yaliyotengwa ya Handeni, Tanga na Kitwai, Manyara.
Hata hivyo, ACT-Wazalendo wanaona wenyeji wa Ngorongoro ni sehemu muhimu ya kuendeleza uhifadhi wa Ngorongoro na NCAA ina wajibu wa kusimamia shughuli za uhifadhi, kuendeleza utalii na ustawi wa jamii zinazoishi ndani ya eneo la hifadhi hiyo.
ACT-Wazalendo kimekuwa kikidai kwamba maamuzi mengi yamekuwa hayawashirikishi wenyeji wa Ngorongoro ambao ndiyo wadau muhimu wa hifadhi hiyo.
Mnamo Februari 15, 2022, ACT-Wazalendo ilitoa mapendekezo mbalimbali juu ya namna bora ya kushughulika na suala la Ngorongoro, ikiwemo kuhisi za ushirikishwaji wa wenyeji katika maamuzi yanayohusu hifadhi.
Chama hicho cha upinzani pia kilipendekeza Serikali kuachana na mapendekezo yaliyotolewa na Ripoti ya Matumizi Mseto ya Ardhi ya Ngorongoro ambayo ilishauri kuondolewa kwa watu katika hifadhi ya Ngorongoro.
ACT-Wazalendo pia inataka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ivunjwe ikidai kwamba mamlaka hiyo imekuwa chanzo cha matatizo ya matumizi mseto ya ardhi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 kwa kuwa sheria imeipa nguvu kubwa mamlaka hiyo kuliko Wanajamii wanaoishi kwenye hifadhi .
Badala yake, ACT-Wazalendo inashauri iundwe kampuni yenye kumilikiwa kwa ubia kati ya wenyeji waNgorongoro na Serikali.