The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wanahabari Epukeni Makosa Haya Mnapokitumia Kiswahili

Wanahabari wanadhima ya kukieneza Kiswahili kikiambatana na ustaarabu, usahihi, usanifu, ufasaha, utamaduni na kunga zake.

subscribe to our newsletter!

Lugha kama chombo kikuu cha mawasiliano na kupashana habari, huchukuwa nafasi adhimu kwenye sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Kiswahili, kama moja ya lugha kuu za kimataifa, kinashuhudiwa kasi yake, jinsi kinavyokata mbuga katika tasnia ya habari ulimwenguni.

Hivi sasa, Kiswahili kinatumika kama lugha ya kutangazia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, vile vya ndani na nje ya nchi, kama ambavyo utakuwa umeshuhudia matangazo yakifanyika kwa Kiswahili kwenye mashirika kama vile BBC, DW, VOA nakadhalika.

Wakati Kiswahili kinazidi kupasua anga za kimataifa, hususan katika sekta hiyo ya habari, ipo hatari ya lugha hiyo kupoteza uasili wake. Hii ni kutokana na kukumbana na changamoto kubwa ya kutumiwa visivyokuwa sahihi, iwe ni kwenye eneo la usanifu, ufasaha au utamaduni wake.

Lugha itumikapo nje ya usanifu na ufasaha wake hupotosha hata ule ujumbe uliyokusudiwa uwafikie wasikilizaji au wasomaji wa taarifa inayotolewa na huharibu utamaduni wa jamii husika. Hapa ndipo hatari ilipo na ni msingi wa makala yangu hii.

Yapo madai kwamba umuhimu wa lugha ni mtu kuelewa kinachowasilishwa, kwa hiyo, si lazima kuchunguza usanifu na ufasaha wake. Bila shaka, umuhimu wa lugha ni mawasiliano ingawa mawasiliano ya hakika hayawezi kufikiwa kwa kuitumia lugha visivyokuwa sahihi. Kama ni hivyo, kulikuwa na umuhimu gani wa kukisanifisha Kiswahili?

Unaweza kukiuka ufasaha na usanifu wa lugha kwenye mazungumzo na ukasamehewa. Hali haiwezi kuwa hivyo kwenye lugha ya usemaji na uandishi. (Usemaji huhusisha utangazaji, uhubiri nakadhalika). Kwenye lugha hizi mbili, ni lazima kuchunga mipaka ya usanifu, ufasaha na utamaduni wa lugha inayohusika.

Kwa wanahabari, umuhimu wa kuzingatia lugha sanifu na fasaha hauwezi kusisitizwa zaidi. Hii ni kwa sababu shughuli zao ni rasmi. Pia, makosa yanayotendwa na vyombo vya habari huchukua nafasi ya kusambaa takriban pande zote za ulimwengu, tena kwa haraka mno.

Jambo la kusikitisha ni kuona vyombo vya habari vya Tanzania vinajumuishwa katika matumizi mabovu ya lugha ya Kiswahili. Matarajio ya wengi ni kwamba wanahabari wa Tanzania wawe mstari wa mbele katika kusimamia na kudhibiti uenezi wa Kiswahili sahihi na fasaha. Lakini hali iko kinyume na matarajio hayo.

Baadhi ya makosa mengi yanayofanywa na watumiaji rasmi wa Kiswahili, hususan vyombo vya habari, ni matokeo ya kasumba ya kuwa Kiswahili hakina mwenyewe. Makosa, hususan ya maana za misamiati, tungo, istilahi na matumizi ya maneno nje ya muktadha, hutokana na matumizi ya lugha nje ya kanuni zilizokubaliwa na jamii husika.

Hapa ndipo unapokutana na maneno kama vile mbeleni, katoto kadogo, kusimikwa, ukarabati, masaa na mengineyo ambayo kimsingi hayaendani kabisa na usanifu na ufasaha wa lugha ya Kiswahili, hasa katika jamii za asili ya uzawa wake.

Ni vyema wanahabari kuitambua miktadha inayoonesha matumizi yasiyo sahihi ya Kiswahili. Kwa kuitambua miktadha hii kutawasaidia kubaini namna bora ya kukitumia Kiswahili katika usahihi wake ili kiwakilishe siyo lugha tu, bali hata utamaduni, silka, adabu na falsafa ya Mtanzania.

Usahihi na ufasaha wa maneno

Maneno mengi hunukuliwa yakitamkwa kinyume na usahihi na ufasaha wa lugha yenyewe. Athari yake hujitokeza hata kwenye maandishi. Maneno hayo ni kama vile themanini, salasini/thelathini, arobaini, tahir, asumani, tofauti, maharibi, kustahafu, ahsante, sentensi, thoruba/dhoruba, afisi, feza, zamana, zambi, zahabu, mmomonyoko, kigelegele nakadhalika.

Usahihi na ufasaha wa maneno hayo ni: thamanini, thalathini, arubaini, Twahir, Athumani, tafauti, magharibi, kustaafu, asante, sentesi, dharuba/dharba, ofisi, fedha, dhamana, dhambi, dhahabu, mmong’onyoko, na kigeregere.

Yapo maneno mengi yanayolazimishwa kuwekewa kiambishi cha wingi katika maumbo yake, kinyume na sarufi ya Kiswahili inavyotaka. Kwa mfano, maneno kama masaa, mapungufu, madhaifu, maboresho, madawa nakadhalika. Haya yalitakiwa yawe saa, upungufu, udhaifu, uboreshaji, dawa.

Maneno mengine huwekewa maumbo ya umoja, kinyume na kanuni za usanifu na ufasaha wa lugha. Maneno kama: zoezi (kazi za kujipima), zoezi (la viungo vya mwili), dhumuni, dhehebu, shindano, tumizi nakadhalika. Haya yalitakiwa kuwa mazoezi, madhumuni, madhehebu, mashindano, matumizi.

Muktadha wa tungo na sentesi

Tungo mara nyingi huwa ni kifungu cha maneno ambacho huhitaji kufungamana kisarufi ili ipatikane maana na muudo sahihi wa tungo hiyo.

Mfano wa tungo ambazo siyo sahihi ni kama vile Kumi na mmoja; Maji taka; Weka sahihi; Kwa niaba yangu; Kuweka dawa kidonda; Chandarua kimewekwa dawa; Nawashukuruni wote; Hadi hapa nawaageni wote; Naomba niwasalimieni wote; Habarini za asubuhi; Kutuma barua; Nikiwa kama mwenyekiti; na Nawaomba mufanye usafi.

Ili kukidhi usanifu na ufasaha, tungo na sentesi hizo zilipaswa kuwa: kumi na moja; maji machafu; tia sahini; Binafsi/kwa nafsi yangu; Kutia dawa kidonda; Chandarua kimetiwa dawa; Nakushukuruni nyote (nyinyi)/nawashukuru wote (wao); Hadi hapa nakuageni nyote (nyinyi) au nawaaga wote (wao); Naomba nikusalimuni nyote; Habari za asubuhi; Kupeleka barua; Nikiwa mwenyekiti; na Nnakuombeni mufanye usafi.

Maana za istilahi na msamiati

Baadhi ya dhana hupewa istilahi zenye maana ama tafauti na kinachokusudiwa au kinyume na ustaarabu na adabu za jamii. Kwa mfano, istilahi kama barua pepe, isimu, kitabu (cha kuandikia), ni istilahi zenye maana tafauti na kilichokusudiwa. Istilahi hizi zilitakiwa kuwa; baruapeperushi, lughawiya, daftari.

Pia, istilahi kama kifirio, pembe msimiko, (ya tiba), kidadavuzi mpakato (laptop) ni istilahi zinazotoa tafsiri ya matusi kwa jamii za Waswahili.

Kwa upande wa msamiati, baadhi ya maneno hubadilishiwa miktadha ya matumizi, hususan kwa maneno yanayofanana lakini yanasawiri maana tafauti. Kwa mfano, maneno kama kughairisha na kuakhirisha; hafla na ghafla; onyesha na onesha; baada na badala; wakilisha na wasilisha; pambanua na fafanua; dhana na zana na mengine mengi.

Maneno haya ni sahihi lakini kwa kutojua, hutumiwa sehemu isiyo sahihi na hivyo kuharibu lugha na kupotosha maana. Unaweza kumsikia mtangaazaji akisema, “Sasa Waziri wa Fedha na Mipango anakwenda kuwakilisha taarifa ya bajeti yake” akiwa na maana ya kwenda kuwasilisha.

Kujumuisha na kutenganisha maneno

Katika muktadha huu maneno muambatano hutenganishwa na yasiyo muambatano huambatanishwa. Maneno kama Mwinyi Mvua; Mwinyi Chande; Bata mzinga; Popo bawa; Chozi gomba; Asili mia; Mwana genzi; Mwana nchi; Mfa maji; Mwenda wazimu, Wana habari, Wana siasa na Mwana funzi. Maneno haya kiusanifu huambatanishwa na kuwa neno moja kitu ambacho ni kosa.

Kadhalika, baadhi ya dhana ambazo maneno yake hutenganishwa, waandishi wengi hufanya makosa pasi na kujua kwa kuyajumuisha. Maneno kama Polepole; Sawasawa; Hapahapa; Harakaharaka; Mbalimbali; Kimyakimya; Kidogokidogo; Mbiombio; na Taratibutaratibu, na mengineo.

Usanifu na ufasaha wa maneno haya ni kutenganishwa na siyo kujumuishwa.

Nini hupelekea makosa haya

Ni vigumu kuainisha makosa yote yanayofanywa na vyombo vya mawasiliano ya umma katika Kiswahili sanifu na fasaha. Hivyo, inaweza kuwa busara kubainisha sababu za makosa hayo ili iwe dira ya kuyaepuka. Baadhi ya sababu ni pamoja na uelewa hafifu wa lugha ya Kiswahili kisarufi na kiutamaduni.

Sababu kubwa zaidi ya makosa ya kiusanifu na kiufasaha yanayofanywa na wanahabari na watumiaji rasmi wengine wa Kiswahili ni kukosa maarifa ya stadi za lugha na utamaduni wake.

Kwa mfano, kwa upande wa sarufi, mtangazaji anaposema “Hadi wakati ujao nawatakia jioni njema” katika kitenzi “nawatakia” kiambishi wa- kinadhihirisha urejeshi wa nafsi ya tatu wingi (wao).

Kimsingi, mtangazaji wa kipindi hata kama haonani na wasikilizaji au watazamaji lakini kimawasiliano ni sawa na kuzungumza nao ana kwa ana. Hivyo, alitakiwa kutumia kiambishi cha nafsi ya pili wingi (nyinyi). Hivyo, sentesi ilitakiwa kuwa “Hadi wakati ujao nakutakieni jioni njema.”

Sababu nyengine ni athari za kuchanganya Kiingereza na Kiswahili, kwa mfano: Okay, ndugu wasikilizaji sasa tunakuleteeni mchezo wa drama; Well, nimekusikia ndugu mtazamaji, lakini kwa upande mwengine, perhaps, watu wana mtazamo mwingine juu ya issue hiyo.

Pia, lugha za vijana (rejesta; vijiweni, sokoni, barabarani, hotelini) kuingilia matumizi rasmi ya lugha sanifu na fasaha. Kwa mfano, Mambo akimaanisha uhali gani. Poa yaani Sijambo. Au Vipi!Fresh au Hamna noma.

Kuthamini cha kwetu

Kama nilivyosema, makosa ni mengi na sababu zake ni nyingi pia. Itoshe tu kusema kwamba makosa ya matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha yanayofanywa na vyombo vya habari hukishushia hadhi Kiswahili licha ya kukua na kuenea kwake.

Ni wajibu wetu watumiaji wa lugha, hasa wanahabari ambao wamekuwa na dhima kubwa ya kuisimamia na kuieneza lugha hii, kuhakikisha kwamba tunajifunza Kiswahili sanifu na fasaha ili kutoa mwanga kwa watumiaji wengine ulimwenguni kote.

Tuna dhima ya kukieneza Kiswahili kikiambatana na ustaarabu, usahihi, usanifu, ufasaha, utamaduni na kunga zake, kama ilivyo kwa Kiingereza, Kiarabu, Kiitaliana, Kifaransa na lugha nyenginezo.

Inastaajabisha kuona mtu anapokosea, au kuharibu, lugha ya Kiingereza huchekwa na kubezwa lakini anapoharibu lugha yake ya Kiswahili huchukuliwa kawaida pasi na kutanabahi taathira zake kilugha, kijamii, na kitaaluma.

Tujifunze Kiswahili sanifu na fasaha ili tuilinde lugha yetu adhimu. Usipokithamini mwenyewe hakitathamniniwa. Kikithaminiwa pasi na kukithamini mwenyewe kitakuponyoka. Hekima za wahenga!

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Nikushukuru kwa makala nzuri yenye kukipigania Kiswahili chetu. Nami pia najishughulisha na matumizi ya lugha katika vyombo vya habari hasa vya Tanzania, nikimanikia makosa. Kwa ufupi, makala yako ina machango mzuri sana ambao unalenga kuboresha lugha ya Kiswahili. Hata hivyo, kuna baadhi ya mifano uliyotoa na kudai kuwa ni makosa lakini katika usanifu na ufasaha wake iko sawa. Nitaandika jibu la kuonesha baadhi ya mifano hiyo nikipata muda.
    Hongera sana kwa makala yako nzuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts