The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

ACT-Wazalendo: ‘Bajeti Hii Inawaweka Wananchi Kwenye Njia Panda’

Chama hicho kinadai bajeti imeshindwa kutoa muelekeo sahihi ambao Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaelekea.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kimewapa pole wananchi wa Tanzania ambao kimedai kuwa wamewekwa njia panda na bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, kwa kushindwa kutoa muelekeo sahihi ambao Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaelekea.

Emmanuel Mvula, msemaji wa masuala ya fedha na uchumi kutoka chama hicho, aliwaambia wanahabari jijini hapa leo, Juni 16, 2022, kwamba bajeti hiyo ya pili ya Serikali ya awamu ya sita inadhihirisha ni kwa namna gani Serikali haiko tayari kugawana na wananchi kwenye kubeba mzigo unaotokana na gharama za maisha.

“Tunaitaka Serikali kuacha kuwahadaa wananchi kwa sababu nyepesi za vita ya Urusi na Ukraine [na] janga la UVIKO-19 na badala yake kuweka mikakati madhubuti ya kuwaondoa wananchi kwenye ugumu wa gharama za maisha na hatimaye waondokane na kuishi kwa tabu na umasikini,” alisema Mvula wakati wa hafla ya kuchambua bajeti hiyo.

Mnamo Juni 14, 2022, Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaotegemewa kuanza Julai 2022, ambapo Shilingi trilioni 41.48 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo ya Serikali.

Miongoni mwa hatua za kikodi zilizotangazwa na Dk Nchemba hapo Jumanne na kupongezwa na wananchi ni pamoja na kufutwa kwa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita; kupunguzwa kwa tozo zinazotokana na miamala ya simu kwa asilimia 43; kubadilisha mfumo wa manunuzi ya umma; na kudhibiti matumizi ya vyombo vya moto vya Serikali.

Mbali na hatua hizi, bajeti hii pia inakuja na mipangilio mipya ambayo wadau wanahofu kwamba inaweza kuwaumiza wananchi zaidi badala ya kuwasaidia. Mipangilio hii ni kama vile kutoza kodi kwenye mikopo inayotolewa nje ya mfumo wa mabenki; Sh1,000 mpaka Sh3,000 kuwekwa kama ada ya king’amuzi; kuongezwa kwa ushuru wa nywele bandia pamoja na hatua zingine kama hizo.

Katika uchambuzi wake ambao umebainisha mambo 10 katika bajeti hiyo mpya ya Serikali, ikiwemo sababu za Serikali kushindwa kufikia malengo yake kwenye kukusanya mapato, Mvula alisema kwamba Tanzania ina utajiri wa kutosha kuiwezesha Serikali kuboresha hali za maisha za watu wake.

“Nchi yetu inazo rasilimali nyingi na uwezo wa kutoka kwenye mikwamo ya kiuchumi endapo kama wananchi wataamka na kukataa muendelezo wa hadaa za Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo kila bajeti yake haiakisi uhalisia ya maisha ya Mtanzania wa kawaida,” alisema Mvula.

Kwenye uchambuzi wake huo, ACT-Wazalendo, chama mshirika wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) huko  Zanzibar, kimependekeza kufutwa kabisa kwa tozo za miamala ya simu zilizoanzishwa na Serikali, ikisema hatua hiyo itachangia kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kumuondoshea mzigo mwananchi.

Chama hicho pia kimependekeza kupunguzwa kwa kiwango cha kodi ambacho wafanyakazi na waajiriwa wamekuwa wakikatwa ikiwa ni njia ya kuwapunguzia mzigo wananchi wa kawaida.

Akizungumzia namna bora ya kudhibiti ubadhirifu wa fedha za umma serikalini, Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe alisema ipo haja ya kufanya mabadiliko ya kikatiba ili kazi za udhibiti na usimamizi wa matumizi ya Serikali zitenganishwe.

Zitto anataka kazi ya udhibiti ifanywe na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali na kazi za ukaguzi zifanywe na Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Zitto anadhani hii itampa nguvu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kwa sababu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha hataweza kupata fedha bila Mkaguzi Mkuu kusema fedha zitoke.

“Hili ni tatizo la kikatiba,” alibainisha Zitto. “Na ndiyo maana tunaona matatizo haya ni mengi. Hoja za ukaguzi hazijibiwi. Hii yote ni kwa sababu tuna tatizo la kikatiba, ambalo ni kurundika majukumu ambayo yanapaswa kuwa tofauti kwa mtu mmoja.”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts