The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Safari Bado Ndefu Kukabiliana na Ukatili Dhidi ya Wazee Tanzania

Ipo mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo ilipitishwa katika mikutano ya wakuu wa nchi ili kuhakikisha ustawi wa wazee duniani. Hata hivyo, mikataba hii haijaridhiwa na Serikali ya Tanzania na hivyo kutotekelezwa.

subscribe to our newsletter!

Ukatili dhidi ya wazee ni janga ambalo limekuwa likiitafuna jamii yetu kwa miaka mingi sana lakini limekuwa ni jambo lisilotiliwa mkazo unaostahili katika kukabiliana nalo.

Ukatili huu umekuwa ukitendwa katika ngazi ya kaya na watu wa karibu ambao ndiyo hutambulika kama wasaidizi wa karibu wa wazee katika ngazi hiyo, mara nyingi bila kujua kwamba kitendo hicho wanachofanya ni ukatili.

Inasadikika kuwa kati ya wazee wanne duniani kote, mmoja wao hufanyiwa ukatili kila mwezi na mtu wa karibu, jamii au taasisi miongoni mwa eneo analoishi. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio Namba 66/127 la mwaka 2011 kama sehemu ya kukabiliana na janga hili.

Azimio hilo liliitenga Juni 15 ya kila mwaka kama siku maalum ya uelimishaji na kupinga ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee duniani. Azimio hilo ulikuwa ni uthibitisho wa kutambua na kukubaliana kuwa wazee katika maisha yao wanapitia chagamoto mbalimbali.

Mwaka huu ni mwaka wa saba (tangu 2016) kwa hapa kwetu Tanzania na ni mwaka wa 11 (tangu 2011) kidunia kuadhimisha siku hii.

Sisi HelpAge ni miongoni mwa mashirika mtandao duniani ambalo dira yake ni kuona dunia ambayo kila mzee anaishi maisha yenye afya, hadhi na salama ambalo pia hapa Tanzania ni mdau mkubwa katika kuhakikisha wazee wanakuwa salama na kuheshimiwa.

Katika kutekeleza azma hiyo, tunatekeleza afua tano ambazo ni jumuishi katika kuleta usalama na heshima kwa wazee.

Afua hizi ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na bora kwa wazee; kupinga vitendo vya ukatili na manyanyaso dhidi ya wazee; kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga; kuhakikisha usalama wa kipato; na kuchagiza harakati za mabadiliko.

Ukatili dhidi ya wazee umegawanyika katika makundi matano kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Makundi haya ni pamoja na kutelekezwa; ukatili wa kisaikolojia; ukatili wa kipesa; ukatili wa mwili; na ukatili wa kingono. Kwa mujibu wa Umoja wa Matifa, mzee ni mtu yeyote ambaye ana umri kuanzia miaka sitini na kwenda juu.

Utokomezaji wa ukatili wa wazee Tanzania

Moja kati ya hatua ambazo sisi kama wadau tumekuwa tukichukua kukabiliana na ukatili huu dhidi ya wazee ni pamoja na kujengea uwezo mashirika yanayojihusisha na masuala ya wazee, mabaraza ya wazee ngazi ya mikoa na wilaya, asasi za kutetea haki za binadamu na kuchukua juhudi za kuielimisha jamii juu ya haki za wazee na umuhimu wa kumlinda mzee.

Tunafanya kazi kwa karibu na Serikali na taasisi zake kuandaa na kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya wazee nchini (2019-23).

Tunashirikiana na Serikali pia kwenye kufuatilia utoaji wa huduma za wazee, ikiwemo kujua hali ya vitendo vya ukatili na mauaji katika meneo yaliyotembelewa ili kujadiliana na viongozi mikakati waliyonayo kukabiliana na vitendo hivyo.

Tumefanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuandaa sera na sheria ya wazee ambayo inalinda usalama wa kipato kwa mzee. Tayari HelpAge, kwa kushirikiana na Shirika la Kazi duniani (ILO), tumeandaa mfumo wa utoaji wa Penshion Jamii Zanzibar.

Pia, tumeshirikiana na taasisi za utafiti, kama vile vyuo vikuu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Mzumbe, kuchambua mahitaji na uwezekano wa kuanzisha na kuendeleza pensheni jamii kwa wazee hapa nchini.

Tumekuwa tukiwasaidia wazee kuanzisha na kuendeleza miradi ya kujiongezea kipato kama vile ufugaji kama vile wa kuku, nyuki, mbuzi na ngombe; kilimo cha mbogamboga; utengenezaji wa sabuni; dawa za kuchua; na usindikaji wa vyakula vya binadamu na wanyama. Hii imefanyika kwenye mikoa ya Morogoro, Mwanza, Kagera, Kigoma, Tanga na Ruvuma.

Katika kuchagiza mabadiliko chanya, shirika linashirikiana na Serikali na vyombo vya habari kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu uzee na kuzeeka, ikiwemo kujenga uhusiano na taasisi na idara za Serikali, mashirika na mitandao ili kusaidia kuhamasisha kuheshimu haki za wazee.

Changamoto bado ni nyingi

Pamoja na kufanikiwa kwa sehemu kubwa katika utekelezaji wa afua hizo, bado jamii inamtazamo hasi kuhusu uzee na kuzeeka na mzee anaonekana kama mzigo. Bado kuna mashirika machache sana nchini Tanzania yanayojihusisha na masuala ya wazee na hivyo kasi ya uchechemuzi kuwa ngumu.

Kwa mashirika yaliyopo, hali zao za kifedha siyo nzuri. Mashirika haya yanategemea fedha za wafadhili ambazo hata hivyo hazitabiriki na wakati mwingine wafadhili huwa na vipaumbele tofauti na vile vya mashirika husika.

Kwenye mipango ya Serikali, ikiwemo bajeti, wazee bado hawajapewa kipaumbele stahiki kama yalivyo makundi mengine. Kwa mfano, uhakika wa kipato au mgawao wa asilimia 10 za halmashauri.

Pia, ipo mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo ilipitishwa katika mikutano ya wakuu wa nchi, kama vile the African Protocol on Older People Rights, ambayo imelenga kuboresha ustawi wa wazee. Hata hivyo, bado mikataba hii haijaridhiwa na nchi yetu na hivyo kutotekelezwa. Mikataba hii ina mambo mazuri kwa mstakabali wa maisha ya wazee hapa nchini.

Vyombo vya habari nchini pia vimekuwa na mwako mdogo kwenye kutoa taarifa chanya kuhusiana na masuala ya wazee. Mara kadhaa, vyombo vya habari vimekuwa vinatumia lugha za kunyanyapaa wazee hata pale mzee anapoonyesha kufanikiwa jambo fulani la kupigiwa mfano, ikiwemo matumizi ya maneno kama vile ajuza, kikongwe nakadhalika.

Bado vitendo vya ukatili na mauajai ya wazee vinazidi kujitokeza na kusambaa katika maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na shida hiyo. Kwa mfano, ni matukio ya mauaji ya bibi wazee watatu – Agnes Msengi, 84, Windila Saidi, 80,  na Winfrida Gigila, 80, – katika kijiji cha Kisharita, wilayani Iramba, mkoani Singida.

Hii yote inamaanisha kwamba ni muhimu sana tukaungana kuhakikisha kwamba mambo haya yanakoma ili wazee wetu wafurahie maisha yao kama ilivyo kwa makundi mengine yote katika jamii zetu.

Uzee na kuzeeka haukwepeki, ni muhimu wote tukatimiza wajibu wetu!

Victor Mapile ni afisa habari wa shirika la HelpAge International TZ. Anapatikana kupitia Victor.Mapile@helpage.org au +255 753067086. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na siyo lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *