Dar es salaam. Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Zanzibar) Salum Mwalimu amesema kwamba chama hicho cha upinzani kimemuandikia barua Spika wa Bunge Tulia Ackson kikimtaka atekeleze azimio la Baraza Kuu la chama hicho la kuwafukuza kutoka bungeni waliokuwa wanachama wake 19 ambao pia ni Wabunge wa Viti Maalum.
Suala hili linakuja mara tu baada ya taarifa ya hukumu iliyotolewa hapo Jumatano, Juni 22, 2022, na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali pingamizi lilowekwa na wabunge hao wakipinga kuondolewa bungeni mara tu baada ya chama hicho kuwavua uanachama.
“Sisi kwa upande wetu [CHADEMA] wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha kwamba basi taarifa ile ya hukumu iliyotolewa jana inafika kwa Spika wa Bunge la Tanzania na tayari tumekwisha fanya hivyo,” amesema Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni.
“Tunamtaka sasa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza barua ya CHADEMA ya tarehe Mei 12, 2022,” aliongeza Mwalimu.
Barua hiyo ndio iliyobeba azimio la kuwavua uanachama wabunge hao 19 wa viti maalumu wakiongozwa na Halima Mdee ambaye aliyewahi kuwa Mbunge wa Kawe (CHADEMA).
Mbali na kupeleka barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika, Mwalimu amesema pia pia chama hicho kimepeleka nakala zake kwa Ofisi ya Msajili wa vyama pamoja na ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya taarifa.
Akizungumza kuhusiana na Bajeti Kuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyotangazwa Juni 14, 2022, na Waziri wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Saada Mkuya, Mwalimu alisema kwamba bajeti hiyo haioneshi mkakati madhubuti wa kwenda kumsaidia mwananchi wa kawaida ili aweze kuondokana na umaskini lakini pia kupambana na suala la mfumko wa bei.
“Huoni hizo juhudi za mikakati thabiti ukweli ya kukabiliana na mfumuko wa bei,” anasema Mwalimu. “Na huoni mkakati thabiti wa kuona namna gani wanakwenda kuwasaidia Wanzanzibari wa kawaida kuondokana na umaskini wa kipato. Huoni kwa kiwango hicho ambacho ungetamani uone kwa hali halisi iliyopo.”
Mwalimu anaeleza kwamba kwa sasa Zanzibar pamoja na wananchi wake wanakabiliwa na changamoto kubwa ya umaskini unaotokana na mfumuko mkubwa wa bei katika bidhaa muhimu kama vile mkate, sukari pamoja na mafuta lakini bajeti mpya imeshindwa kuonesha namna gani itamkomboa Mzanzibari katika hali hiyo.
Mwalimu ameeleza kuwa chama hicho kinaunga mkono sera ya uchumi wa buluu ikiwa ni eneo ambalo chama hicho kinadhani Wazanzibar wanaweza kunufaika sana na eneo hilo lakini amebainisha kwamba kunahitajika mjadala wa kitaifa kwa Serikali na wananchi ili kuweza kufanikisha jambo hilo.
“Tunaunga mkono juhudi za uchumi wa buluu na maono ya uchumi wa buluu. Serikali inapaswa kufikiria zaidi na zaidi kwenye uchumi wa buluu.
“Tunazungumza kujenga bandari za wavuvi mbili, tunazungumza kununua boti za uvuvi, tunazungumza kujenga kiwanda cha kusarifu samaki, nadhani bado ni vitu vidogo vidogo.
“Tunahitaji kuwekeza kweli kweli kwenye uchumi wa buluu. Serikali itoke na isione aibu ifungue milango itengeneze mjadala wa kitaifa kwamba tunafanyaje kwenye uchumi wa buluu?”
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.