The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Migogoro Isiyokwisha Kilosa Yawasukuma Wakulima Kutafuta Kikao na Majaliwa

Migogoro ya ardhi Kilosa yaelezwa kudumu kwa takriban miaka 10, ikifanya maisha ya wenyeji wa huko, wengi wao wakiwa ni wakulima na wafugaji, kuwa magumu.

subscribe to our newsletter!

Morogoro. Wakulima wilayani Kilosa mkoani hapa wameunda kamati ndogo itakayokuwa na kazi ya kufanikisha kikao baina ya wakulima hao na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ikiwa ni sehemu ya jitihada za wakulima hao kutafuta suluhu ya kudumu ya migogoro ya ardhi inayoelezwa kudumu wilayani humo kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Hatua hiyo inatokana na wakulima hao wadogo kukosa imani na mamlaka za ngazi za wilaya na mkoa kwamba zina nia ya dhati ya kutatua migogoro hiyo ambayo wakulima wanasema imekuwa ikiwafanya wawe na maisha magumu huku wakishindwa kuishi kwa amani na furaha ndani ya nchi yao.

Haya yalidhihirika hapo Juni 23, 2022, wakati wa mkutano ulioandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) ambao uliwakutanisha wakulima wadogo kutoka wilayani kilosa kwa lengo la kutathmini kwa pamoja namna bora wakulima hao wanavyoweza kumaliza migogoro ya ardhi inayoendelea wilayani humo hivi sasa.

Wakiongea wakati wa mkutano huo, wakulima walieleza hofu yao ya kuibuka kwa machafuko kati yao na wafugaji yanayoweza kusababishwa na uhaba wa ardhi ya matumizi. Uhaba huo, kwa kiasi kikubwa, unatajwa kusababishwa na “wawekezaji” ambao wamekalia maeneo mengi ya ardhi bila ya kuyaendeleza, hali inayotengeza “uhaba bandia wa ardhi.”

Mkulima kutoka kijiji cha Kimamba B Salum Ally, kwa mfano, alibainisha wakati wa mkutano huo kwamba wenyeji wa Kilosa wamelalamika sana kuhusu migogoro hiyo kwenye mamlaka za wilaya na mkoa bila ya kuwepo kwa mafanikio yeyote yaliyo patikana.

“Ni kupoteza muda kama kuendelea kushughulika na viongozi wa ngazi ya wilaya au mkoa,” alisema Ally. “Ni lazima tupelekee kilio chetu ngazi za juu, Waziri Mkuu ni mtu muhimu sana kumfikia na kumueleza kilio chetu.”

Migogoro ya siku nyingi

Wilaya ya Kilosa ni moja kati ya maeneo yenye migogoro ya siku nyingi ya ardhi nchini Tanzania. Migogoro hii imekuwa ikitokea kati ya wakulima na wafugaji; wenyeji na wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kukalia ardhi kubwa bila ya kuziendeleza; pamoja na wenyeji na mamlaka za Serikali, kama vile Jeshi la Magereza, ambazo zinadaiwa kukalia ardhi ambazo kisheria ni za wanavijiji.

Matokeo ya migogoro hii ni maisha magumu kwa wanavijiji, hali inayowafanya wawe na makasiriko na simanzi kubwa, hali zinazotakana na hisia zao za kusalitiwa na kuachwa nyuma na Serikali yao. Wakati wa mkutano huo wa Juni 23, haikuwa ngumu kuona ni kwa namna gani wakulima hawa wamechoshwa na migogoro hii.

“Tunaiomba Serikali iwadhibiti hawa wanaoitwa wawekezaji wenye tabia ya kupora na kuchota maeneo halali ya wakulima,” alisema Abdul Tumbo, ambaye ni mkulima wa mpunga na mahindi kutoka kijiji cha Mvumi.

“Wakulima wadogo ndiyo tunaoathirika kiuchumi,” aliongeza. “Itafutwe suluhu ya kudumu ya mipaka katika sura zake zote [iwe inahusu] wawekezaji, matajiri [au] taasisi za Serikali. Ni wakati sasa wa kukomesha mauaji ya wakulima wadogo yanayojitokeza pindi wanapo dai haki zao.”

Wakulima hawa wamekuwa wakichukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba wanapambana dhidi ya jitihada za kuporwa kwa ardhi yao. Hata hivyo, katika kufanya hivyo, wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kufunguliwa mashitaka ya aina mbalimbali na Serikali.

Nuru Pipino ni Afisa Sheria kutoka MVIWATA ambaye amekuwa akishughulika na kesi nyingi zinazofunguliwa dhidi ya wakulima wanapodai haki zao juu ya matumizi ya ardhi au umiliki wa ardhi.

“Katika hii wilaya ya Kilosa kuna kesi 77 zilizosimamiwa katika kipindi cha mwaka 2018 mpaka 2021,” Pipino aliiambia The Chanzo pembezoni mwa mkutano huo. “Na kesi hizo zilihusisha wakulima wapatao 89, ambapo wanawake walikuwa 14 na wanaume walikuwa 75.”

Kati ya kesi hizo, 51 zilihusisha mashitaka ya jinai ya kuingia kwa nguvu kwenye ardhi, aliongeza Pipino. Na kwa kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021, kesi ambazo hazikuwa na sifa ya kuwa jinai zililikukwa 26. Na katika kipindi cha mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Juni, MVIWATA imepokea kesi jumla ya 22 kutoka wilaya ya kilosa.

Akiongea katika mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa, Afisa Mifugo na Uvuvi Kelvin Emanuel alisema kwamba ni muda sasa matatizo ya ardhi wilayani yanapaswa kupatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, Emanuel hakuzungumzia shutuma mahususi zilizoelekezwa kwa Serikali na wakulima hao. Alisema: “Kuna utatuzi wa haraka na kuna utatuzi ambao tunatakiwa tushirikiane pamoja na nyie [wakulima]. Kukaa pamoja kama hivi inawezekana tukaenda mbele zaidi.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts