The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Ukatili Baina ya Wapendanao Siyo Jambo la Kifamilia

Kati ya wanawake na wasichana 87,000 waliouwawa ulimwenguni kote kwa mwaka 2017, zaidi ya theluthi moja walifariki kwenye mikono ya wapenzi au waume zao wa sasa au wa zamani. Hili siyo suala la kifamilia. Hili ni janga la kijamii.

subscribe to our newsletter!

Ni janga kubwa na lisilo na kifani. Linaleta uchungu na mateso kwa wanawake na familia zao. Linaharibu jamii katika kila nchi na tamaduni. Lakini cha kushangaza, ni mara chache linazungumziwa, na kwa hakika halishughulikiwi kwa uharaka, tofauti kabisa na janga lingine lolote, ambalo limewahi kuwepo angalau kwa miaka miwili iliyopita.

Tanzania ni mfano wa nchi ambayo janga hili limejikita sana lakini linafichwa. Katika nchi kama hii yenye mandhari nzuri, visiwa vya kupendeza, na wanyama wa porini wa kuvutia, kufichwa kwa janga hili kunaleta kizungumkuti.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linatanabaisha kuwa asilimia 38 ya wanawake nchini Tanzania wameshawahi katika maisha yao kukumbana na ukatili kutoka kwa wapenzi au wenza wao wa karibu.

Takwimu za WHO pia zinaweka wazi kuwa katika kipindi cha miezi kumi na mbili iliyopita, mwanamke mmoja kati ya wanne nchini Tanzania, ameshawahi kufanyiwa vitendo vya kikatili. Hii ni mara mbili ya wastani wa kimataifa na juu ya wastani kwa kanda ya Afrika.

Taarifa hizi zimepatakana baada kufanyika kwa utafiti mkubwa zaidi kuwahi kutokea duniani, juu ya kuenea kwa ukatili dhidi ya wanawake. Utafiti huu ulifanyika kuanzia mwaka 2000 hadi 2018. Kufuatia ujio wa janga la UVIKO-19 hali ya ukatili dhidi ya wanawake ilizidi kuwa mbaya, kwani janga hili kwa ujumla wake lilizidisha hali ya watu kunyanyapaliana.

Athari kwa afya ya umma

Ukatili dhidi ya wanawake ni suala linaloathiri afya ya umma. Kati ya wanawake 87,000 wakiwemo wasichana waliouawa duniani kote mwaka wa 2017, zaidi ya theluthi moja walikufa mikononi mwa wapenzi wao wa kiume au waume zao, wa sasa au wa zamani.

Ikilinganishwa na idadi ya watu wote duniani, Afrika ilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha mauaji ya wanawake yaliyosababishwa na wenzi wao. Katika Afrika, kwa wastani, kila baada ya dakika 48 mwanamke au msichana mmoja aliuawa na mpenzi au mwenzi wake.

Wanawake wanaonusurika na kifo kufuatia vitendo vya kikatili dhidi ya wapenzi au wenza wao wa kiume, mara nyingi hubaki na madhara ya kiafya ambayo yanaweza kudumu maishani mwao. Madhara haya yanajumuisha majeraha makubwa mwilini mwao, shinikizo la damu, na hata msongo wa mawazo. Hivyo ninaposema kuwa “kuna vita dhidi ya wanawake,” isieleweke kuwa natia chumvi.

Sehemu ya tatizo hili la ukatili dhidi ya wanawake, linasababishwa na namna dhana yenyewe inavyoeleweka. Kwa muda mrefu sana, ukatili dhidi ya wanawake umechukuliwa tu kama “suala la familia.”

Tunahitaji kwenda mbali zaidi ya hapo na kuliita tatizo hili kama linavyostahili. Pale mwanaume anapomnyanyasa mwenzi wake kimwili au kingono, hilo si “suala la familia.” Pia sio tu “vurugu za nyumbani” bali ni kosa la jinai, uhalifu dhidi ya utu na jambo lisilo na mashiko.

Namna tunavyozungumzia ukatili dhidi ya wanawake unaakisi uhalisia wa tatizo hili kwa mapana zaidi. Tunaishi katika ulimwengu ambao wanaume ndiyo wanatunga sheria na mfumo dume umekita mizizi katika jamii nzima.

Nchini Tanzania, kama ilivyo katika sehemu nyingi duniani, jeshi la polisi lililosheheni wanaume linashindwa kushurutisha utiifu wa sheria dhidi ya ukatili wa wanawake, hasa ukatili huo unapotokea katika mazingira ya majumbani mwao. Sheria kwa ujumla pia haipo bayana kuhusu suala la wanaume kuwabaka wake zao wa ndoa.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba watu wengi, wanawake wakiwemo, mara kwa mara hutoa visingizio kwa kuwatetea wanaume wanaofanya vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake: utasikia kwa mfano, “alikuwa na hasira,” “alikuwa amelewa; hakumaanisha,” mwanamke anaambiwa; “hukupaswa kumkasirisha,” mwanamke anaambiwa; “ulitarajia nini ulipomkosea heshima kama siyo kipigo?”

Utamaduni huu unachochea unyanyasi wa wanaume dhidi ya wanawake na unaweka mazingira magumu kwa wanawake kujinasua kutoka kwa wanaume wanaowanyanyasa.

Kifungo cha kiwewe

Tatizo hili linachangiwa na hali ya kisaikolojia inayomkuta mtu ambaye amekuwa akinyanyaswa kwa muda mrefu, inayojulikana kwa kitaalamu kama traumatic bonding. “Traumatic bond” kwa Kiswahili kisicho rasmi ni sawa na “kifungo cha kiwewe.” Kifungo cha kiwewe ni kifungo cha kihisia cha mnyanyaswaji dhidi mnyanyasaji kinachotokana na unyanyasaji wa kila mara.

Mnyanyasaji wakati mwingine anaweza kuamua tu kuanzisha ugomvi, kuwa na wivu kupita kiasi au kumtisha mnyanyaswaji, ambaye kwa muktadha huu ni mwanamke. Kwa upande wake, mwanamke anayenyanyaswa sana wakati mwingine anajawa na hofu kubwa hata kujaribu kujipendekeza kwa mnyanyasaji.

Katika hali kama hii mara nyingi unyanyasaji unazidi. Unyanyasaji unaweza kuwa wa kimwili, kihisia au kimaneno. Wakati mwingine hofu ya mateso inapozidi mnyanyaswaji anaweza kujaribu kuondoka au kutafuta msaada. Katika hatua hii mnyanyasaji anapoona madhara anayosababisha ni makubwa anaweza kujuta, kuomba radhi na kuahidi kubadilika.

Hii inaweza kumpelekea mnyanyaswaji kumuhurumia, kumsamehe na wakaanza kuishi tena kama wapo fungate kwa mapenzi na mahaba. Hatua hii inampa tumaini mnyanyaswaji na anataka kuamini kwamba mtesi wake anaweza kubadilika, na kwamba siku moja watakuwa na uhusiano wa upendo anaotarajia, na zaidi hasa ikiwa anamtegemea mwanaume huyu kuendesha maisha yake.

Kwa kawaida, ingawa inasikitisha, jambo hili huwa linajirudiarudia, na kila linapojirudia linakuja na vurugu zaidi na linachukua muda mrefu kuisha.

Ishara kubwa kwamba uko katika ‘kifungo cha kiwewe’ ni kwamba unajaribu kuhalalisha unyanyasaji na kumkinga mnyanyasaji baina ya mateso anayokusababishia. Unaweza hata kujitenga na familia na marafiki ambao wanataka kukusaidia kujinasua na mateso unayopitia.

Unadiriki hata kuwachukia ikiwa watajaribu kuingilia kati na kukusaidia kupambana na mnyanyasaji wako. Unaweza kufikiri kwamba yeye ndiye kipenzi cha maisha yako na yote anayofanya ni kwa sababu tu anakupenda sana na hawezi kudhibiti hisia zake.

Unaweza kufikiri kwamba wewe ni sababu ya tabia yake, na kwamba ukibadilika yeye pia hatimaye atabadilika. Ukweli ni kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba vurugu zitaendelea, na huenda zikaongezeka. Anapokuonyesha yeye ni nani, mwamini mara moja tu! Mtu anayekunyanyasa hakupendi. Katika upendo wa kweli, hakuna mahali pa vurugu.

Kukiepuka ‘kifungo cha kiwewe’ si rahisi kama kutoka nje ya mlango na inaweza kuchukua muda mrefu, ingawa inawezekana. Badala ya kubaki kuwazia nyakati nzuri za zamani au matumaini ya wakati ujao, ni vema ukatae unyanyasaji wa sasa unaofanyika juu yako. Jitunze na tambua thamani yako.

Tafuta vyanzo vya faraja yako mbali kabisa na mnyanyasaji wako, kama vile kufanya mazoezi ya viungo, kukaa na marafiki unaowaamini na kuzungumza nao. Jifunze mengi uwezavyo kuhusu mahusiano dhulumishi, na jinsi mtu anavyoweza kuyatofautisha na mahusiano mazuri (kwenye mtandao kuna utajiri wa taarifa nzuri na ushauri kwa wanawake walioathirika na ukatili).

Tengeneza mikakati ya kuboresha usalama wako na – hatimaye – kufanya mpango wa kuondokana na mateso unayopata. Yote haya yanaweza kukugharikisha, ndiyo maana ni muhimu kujua kwamba msaada unapatikana, na kwamba hauko peke yako. Kuna wataalam wa matibabu, vikundi vya usaidizi, na mashirika ambayo yanaweza kukusaidia.

Jukumu muhimu la kutekeleza

Kama jamii, tuna jukumu muhimu la kutekeleza. Wanaume na wanawake lazima wafanye juhudi za pamoja ili kujenga utamaduni ambao hauvumilii ukatili dhidi ya wanawake. Juhudi hizi lazima ziwe shirikishi kwa kada zote, kuanzia mtu kibinafsi, kundi la watu, taasisi na itikadi fulani.

Ni lazima pia tujivike ujasiri wa kutambua kwamba baadhi ya imani na mitazamo tuliyonayo ni hatarishi na tuwe tayari kuweka mikakati ya kuzibadilisha, hata kama zinatukosesha raha.

Katika ngazi ya watu binafsi, lazima tusimame na kuzungumza tunapofahamu au hata kushuku kuwa mtu fulani ananyanyaswa, na lazima pia tuwalee watoto wetu wa kiume na wakike kufanya vivyo hivyo.

Katika ngazi ya kitaasisi, lazima tusisitize Serikali na taasisi nyingine za umma kufanya jitihada za makusudi kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuwa tayari kuwajibishwa iwapo watashindwa.

Katika ngazi ya kiitikadi, ni lazima tupinge tamaduni za kijamii pamoja na mifumo ya imani ambazo zinashiriki katika kuendeleza ukandamizaji wa wanawake. Kazi ni ngumu. Lakini je, tuna chaguo? Ukatili wa wanaume dhidi ya wanawake lazima ukomeshwe.

Rainer Ebert ana Shahada ya Uzamivu kwenye Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Rice, huko Texas. Kati ya mwaka 2017 na 2019, Ebert alikuwa ni Mhadhiri wa Falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Unaweza kumfikia kupitia www.rainerebert.com au kupitia Twitter @daktari_rainer. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *