The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Namna Fasihi ya Kiswahili Ilivyo Changa Kidhima Licha ya Kuwa Kongwe Kihistoria

Warsha za ufundaji wa fanani, watunzi na wahakiki, uwekezaji wa kutosha, uhamasishaji na usimamizi bora vitasaidia sana katika kuimarisha ufahamu wa kitaalamu na utambuzi mpana katika utunzi, uwasilishaji na uhakiki wa kazi za fasihi, kwa kuzingatia kunga zake.

subscribe to our newsletter!

Fasihi ni matokeo ya usanii wa lugha. Lengo kuu la fasihi ni kufikisha ujumbe fulani kwa jamii kuhusu kadhia kadhaa zinazotokea. Inategemewa kazi za fasihi zisikilizwe, zitazamwe au zisomwe na watu wote wa jami inayohuska. Kwani fasihi ni sanaa inayoyasawiri maisha ya kila mwanadamu katika nyanja zote. Si kwa makundi maalumu kama inavyodhaniwa na wengi.

Fasihi ni muhimu sana katika kuimarisha mfumo wa utambuzi wa kifikra na kimtazamo kuhusu falsafa ya maisha na ulimwengu. Fasihi ni taaluma na sanaa inayofundisha namna ya kuikwamua jamii kutoka hali moja kwenda hali nyengine bora zaidi katika nyanja zote za maisha.

Kwa kuwa fasihi ni zao la lugha, ni wazi kuwa imefuatana na mifumo yote aliyoipitia mwanadamu katika maisha yake (ujima, utumwa, ukabaila, ujamaa na ubepari). Fasihi ya Kiswahili ina historia ndefu sana. Imeanza tangu kuanza kwa jamii za Waswahili. Hivyo ni kongwe na ina maendeleo yake.

Hata hivyo, bado fasihi ya Kiswahili inakumbana na changamoto kubwa ya kukidhi kikamilifu mahitaji na matokeo ya taaluma yenyewe katika kumbadilisha mwanadamu kifikra na kimazingira hasa katika nyakati za sasa. Fasihi ya Kiswahili ni kongwe kihistoria lakini changa kidhima. Nitafafanua kwa uchache.

Fasihi kama chombo cha ukombozi

Moja kati ya dhima kuu ya fasihi na mwanafasihi ni kuitoa jamii kutoka hatua moja hadi hatua nyengine nzuri zaidi (ukombozi). Fasihi husimama kama chombo cha ukombozi wa jamii kwa kule kujadili kwake na kukemea maovu na machafu yote yatendekayo katika jamii pamoja na kutoa mwelekeo thabiti wa maisha kutoka wakati mmoja hadi mwengine.

Katika kusawiri dhima hii, fasihi ya Kiswahili bado iko nyuma. Watunzi na wazalishaji wengi wa fasihi ya Kiswahili hujadili mambo yasiyo ya msingi ili kuburudisha na kuteka hisia za hadhira ili mradi tu kazi ziuzike kwa haraka na wao waweze kupata fedha/faida.

Badala ya kujadili na kukemea maovu kama vile unyanyasaji, usaliti, uongozi mbaya, rushwa, mmong’onyoko wa maadili, athari za utandawazi, umasikini, utabaka, ubadhirifu wa mali ya umma nakadhalika, wanafasihi wengi, hususan wale wa nyimbo na filamu, hujadili zaidi masuala ya mapenzi, ngono, udaku, upelelezi, ubabe nakadhalika. Hali hii inaifanya fasihi ya Kiswahili kukosa uimara wa kuikomboa jamii kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.

Fasihi ya Kiswahili pia imegubikwa na wimbi la fanani wasiyozingatia mila, dasturi na ustaarabu unaoashiria utamaduni wa jamii katika utunzi na uwasilishaji wa kazi zao.

Wakati mmog’onyoko wa maadili unazidi kuhatarisha mustakbali wa maisha ya vijana wengi wa Kitanzania, ndiyo kwanza tunashuhudia watunzi na fanani wengi wa fasihi ya Kiswahili kuwa miongoni mwa watu wa kupigiwa mfano katika ukosefu wa maadili hata kwenye kazi zao.

Wasanii wengi wa muziki na filamu hawawakilishi utamaduni wa jamii zao katika kazi zao; mavazi yao, mikato ya nywele zao, mitindo ya maisha yao, lugha yao, na hata kashfa zinazowakabili kila uchao na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Hawawezi kuwa kioo cha jamii kama ilivyolenga sanaa yao. Kazi zao zimejaa matusi ya wazi, kiasi cha kutosikilizika au kutazamika mbele ya watu wa aila yako.

Hali hii inajitokeza hata katika baadhi ya kazi za fasihi andishi. Ingawa si kwa kiwango kikubwa. Malengo ya waandishi wengi ni kipato cha haraka na si kuzingatia miiko na kunga za sanaa na taaluma wanayoitumia.

Kuhusu nini wanaifunza jamii na kitaleta athari gani haisumbui sana vichwa vya waandishi wengi wa kazi za fasihi katika utunzi na uandishi wao. Hali hii inaleta uchanga wa fasihi ya Kiswahili katika kuthamini, kutunza, kuendeleza na kuwakilisha utamaduni wa jamii husika.

Fasihi kama chombo cha ukuzaji lugha

Fasihi kama sanaa ya lugha ina nafasi kubwa katika kuchangia ukuaji, uenezaji na uendelezaji wa lugha inayohusika. Pia, ina nafasi kubwa ya kuidumaza lugha. Lugha ya kifasihi inatakiwa isheheni msamiati wa lugha husika tena ufinyangwe kiusanii na kiusanifu.

Matumizi ya lugha za kigeni na uteuzi mbovu wa maneno na tungo yamechukua nafasi kubwa katika baadhi ya tanzu za fasihi ya Kiswahili, hususani nyimbo na maigizo. Kwa mfano, nyimbo kama African Beuty ya Diamond Platinum, Nitekenye ya Harmonize na nyimbo nyingi za Hip Hop hasa za Darasa na Fid Q, utakuta matumizi makubwa ya lugha ya Kiingereza tena yasiyo na msingi wowote.

Kutozingatia stadi za lugha katika kazi za fasihi ni ishara ya umiliki mdogo wa lugha na kutojielewa kwa fanani wengi wa fasihi ya Kiswahili. Hatimaye kudhihirisha uchanga wa fasihi hiyo licha ya upevu wa kihistoria.

Uchache wa kazi za fasihi ya Kiswahili, hususani kazi za fasihi andishi, unasababisha uchanga wa fasihi ya Kiswahili pia. Tatizo hili linasababishwa na uchache wa waandishi nguli wa kazi za fasihi na uvivu wa wataalamu wa Kiswahili katika fani ya uandishi.

Wataalamu wengi wa Kiswahili hawajishughulishi na uandishi.

Hali hii iimechangia kwa kiasi kikubwa kuzuka kwa wimbi la watunzi na waandishi wasiyomahiri na wasiyo na vigezo vya uwanafasihi, kuiingilia fani fasihi ya Kiswahili. Ukizingatia historia ya fasihi ya Kiswahili tangu kuwepo, ukilinganisha na idadi ya waandishi pamoja na kazi zao hupati ulinganifu stahiki.

Kadhalika ni wachache katika Waswahili, hususan Watanzania, wenye utamaduni wa kujisomea. Hasa kazi za fasihi. Usomaji wa kazi za fasihi, kwa kiasi kikubwa umeachiwa wanafunzi na walimu wa lugha ambao hujisomea kazi chache zilizoteuliwa ili kutimiza tu malengo ya ufundishaji na ujifunzaji.

Uchache wa waandishi, vitabu na wasomaji unadhihirisha uchanga wa fasihi ya Kiswahili kidhima licha ya upevu wa kihistoria.

Nafasi ya wahakiki wa kazi za fasihi

Wahakiki ni daraja baina ya mtunzi wa kazi za fasihi na hadhira yake (jamii). Wakati kazi za fasihi hutumia usanii wa kimfumo na kimtindo na lugha ya mficho kupitia taswira, semi na tamathali, mhakiki hufumbua usanii huo na kuyaweka wazi maudhui ya kazi hizo ili hadhira ifahamu kwa undani kile kilichokusudiwa na mtunzi baada ya kuburudika.

Wahakiki wengi wa kazi za fasihi ya Kiswahili wanaishia kutafsiri yale yaliyofumbwa kifasihi na mtunzi asilia, badala ya kuhoji, kudadisi, kukosoa na kubainisha kufaulu na kutofaulu kwa mtunzi pamoja na kupendekeza njia za uboreshaji ili zipatikane kazi zenye tija kwa jamii.

Kwa upande wa fasihi simulizi – nyimbo, filamu, tamthilia, vichekesho, ngonjera nakadhalika – ambazo hupatikana kwa wingi, huvutia wengi na kusambaa kwa haraka mno, bado hakujawa na wahakiki mahususi na wastadi, jambo ambalo husababisha kazi hizo kubaki kama burudani zaidi kuliko kuzingatiwa kwa ujumbe na mafunzo yake kwa jamii.

Fasihi ya Kiswahili inakumbwa na changamoto kubwa katika muktadha wa udhibiti na uhuru wa kazi za fasihi pia. Imeshudiwa mara nyingi baadhi ya kazi za fasihi, kama nyimbo na filamu zikifungiwa kwa mnasaba wa ama kukiuka misingi na falsafa za kisiasa za wakati husika au huwekewa misingi ya udhibiti ili zisivuke mipaka iliyowekwa.

Fasihi ni sanaa huru ya lugha inayokusudia kuwasilisha fikra nzito za jamii kwa njia ya ufundi na ubunifu utakaoburudisha hisia na kufikirisha nadhari. Fasihi haidhibitiwi au kufungiwa kwa kuwa tu imesadifu mguso hasi kwa makundi fulani ama yenye nguvu za kiutawala au kifedha.

Au haikuendana na falsafa ya mfumo wa kisiasa na kiutawala. Fasihi ni chombo cha kusifu kilicho bora na kukosoa chochote kisichobora kwa maslahi mapana ya jamii. Fasihi ni taaluma. Inahukumiwa kwa misingi ya kitaaluma au pale inapokiuka misingi ya nidhamu na ustaarabu wa jamii husika.

Udhibiti wa kazi za fasihi na watunzi wake kwa misingi isiyo yakinifu, unaidunisha fasihi na wanafasihi pamoja na kuinyima uhuru wake. Hatimaye kuendelea kuwa changa licha ya historia yake kongwe.

Isiyoota chafu, isiyozalisha pofu

Huu ni msemo wa Waswahili waliyoupigia mfano wa mbegu. Msemo unatutanabahisha kuwa unapoibua jambo kisha hata lisichomoze, misingi ya jambo hilo ni batili. Likichomoza na kunawirika lakini lisikidhi dhima yake basi kiini cha utekelezaji wake hakijatendewa haki.

Fasihi ya Kiswahili ilishachomoza na kunawirika tangu enzi. Hivyo haina misingi batili. Tunapoona taathira yake ni ya kiwango cha chini kwenye maisha halisi ya jamii, tutanabahi kuwa kuna shida katika kiini cha utekelezaji wake.

Warsha za ufundaji wa fanani, watunzi na wahakiki, uwekezaji wa kutosha, uhamasishaji na usimamizi bora vitasaidia sana katika kuimarisha ufahamu wa kitaalamu na utambuzi mpana katika utunzi, uwasilishaji na uhakiki wa kazi za fasihi, kwa kuzingatia kunga zake.

Yakifanyika haya kwa nia ya dhati na ya makusudi itakuwa chachu ya kuipevusha fasihi ya Kiswahili kidhima kupitia miktadha iliyojadiliwa kwenye makala haya. Vyenginevyo, itabaki tu kuwa sehemu ya ajira kwa wachache lakini isiyo na tija kwa maslahi mapana ya jamii.

Nihitimishe safu hii kwa kusema kwamba fasihi ya Kiswahili ikipevushwa kidhima inaweza kuchagiza manufaa makubwa kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiteknolojia na hata kidiplomasia. Tuanze sasa, hatujachelewa!

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts