Dar es Salaam. Lilikuwa ni tukio la kipekee kuwahi kufanyika katika historia ya uandishi wa kazi za fasihi nchini Tanzania pale watunzi wa kazi hizo walipokutana na wapenzi na wasomaji wao katika hafla iliyofanyika jijini hapa hapo Jumapili, Julai 3, 2022.
Ikifanyika chini ya mwavuli wa UWARIDI, ambao ni Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira, hafla hiyo iliwakutanisha waandishi wakongwe na chipukizi pamoja na wasomaji wao na wadau wengine wa kazi za fasihi nchini ili kujadili kwa pamoja mambo yanayowahusu na mustakabali mzima wa aina hiyo ya sanaa.
Riwaya jumla ya tano zilizinduliwa siku hiyo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo iliyopewa jina la Elite Mjue Mtunzi – Msimu wa Pili, iliyodhaminiwa na duka hilo la vitabu la Elite pamoja na AZAM TV na Simulizi na Sauti (SnS).
Pia, jumla ya waandishi watatu wa kazi za fasihi – Elizabeth Mramba, Joseph Shaluwa na Ibrahim Gama – walikabidhiwa ngao za heshima kama ishara ya kutambua mchango wao katika kukuza fasihi ya Kiswahili nchini kupitia kazi zao za uandishi wa vitabu.
Watatu hawa, pamoja na waandishi wengine, walipata fursa ya kuelezea kwa ufupi safari zao za kiuandishi, wote wakigusia namna fani hiyo walivyoanza nayo tangu utotoni; simulizi hizi zilikuwa hamasa tosha kwa wale waliokuwa wanatamani kuingia kwenye fani hiyo lakini wakiwa hawajui pa kuanzia.
Waandaji wa hafla hiyo walifanya hivyo kwa makusudi kwani, kama alivyozungumza Katibu Mwenezi wa UWARIDI Maundu Mwingizi, yeye mwenyewe akiwa ni mwandishi wa kazi za fasihi: “Tumekutana hapa kuja kumjua mtunzi. Lakini siyo kumjua jina au sura yake. Ni kujua mchakato mzima wa maisha yake ambao unahusu uandishi. Kwa sababu maisha ya mtunzi ndiyo uandishi wenyewe.”
Tukio la furaha, kifamilia
Waandishi wa kazi za fasihi waliohudhuria hafla hiyo walitoka sehemu mbalimbali za nchi – kuanzia Arusha hadi Pemba – wengi wao wakija na familia zao, hali iliyofanya tukio zima kuchukua sura ya kifamilia – badala ya ile ya kitaaluma – na kuwavutia washiriki wake wengi, akiwemo Profesa Mkenda mwenyewe.
“Kilichonifurahisha zaidi kwa kweli ni kuona watu wamekuja na familia,” Preofesa Mkenda alielezea hisia zake waziwazi. “Naona watoto wapo humu [ukumbini]. Yaani imekuwa ni kama tamasha kwa kweli. Kuna wake, waume, wazazi. Ni kitu kimoja kizuri na najisikia vizuri sana kukiona.”
Moja kati ya tukio muhimu lililowafurahisha wengi wakati wa hafla hiyo ni pale Ibrahim Gama, mwandishi wa kitabu maarufu cha Balaa, alipojitambulisha kwa njia ya kughani, akiimba:
Jina langu Ibrahimu wa Gama wa Marijani
Kwa kabila Mzaramo wa Bagamoyo Mjini
Ni mimi muadhamu kindakindaki wa Pwani
Katibu wa UWARIDI na pia wa shirikisho.
Hussein Issa Tuwa ni mwandishi mashuhuri wa kazi za fasihi nchini Tanzani ambaye pia anafanya kazi kama Rais wa UWARIDI.
Akieleza kwa nini wameamua kujiita Umoja wa Waandishi Riwaya wenye Dira, mwandishi huyo wa riwaya pendwa ya Mfadhili alieleza kwamba lengo lao ni kudhamiria kuandika riwaya zinazofuata taratibu za kiuhariri, kiuchapishaji, kiaamdili na kufanya uandishi wa riwaya kuwa ajira inayoheshimika.
“Anapotokea mwandishi yoyote akaandika kwa malengo haya, yeye ni mwandishi mwenye dira hata kama siyo mwana UWARIDI,” alisema Tuwa. “Kwa sasa kazi yetu ni kutambua waandishi waliopo [Tanzania] ambao ni wanachama wa UWARIDI na wale ambao siyo wanachama.”
Daftari la kudumu la wasomaji riwaya
Tuwa alibainisha kwamba moja kati ya mikakati waliyonayo kama umoja kwa sasa ni kuanzisha daftari la kudumu la wasomaji riwaya ili waweze kuwa na kanzi data mahususi ya wasomaji wa kazi zao nchi nzima.
“Tulianzisha hili daftari mwaka 2020 kwenye [hafla] ya Mjue Mtunzi – Msimu wa Kwanza na majina ya wote waliohudhuria pale tuliyaweka kwenye orodha ambayo imehifadhiwa,” alisema Tuwa.
“Na waliohudhuria leo [Julai 3, 2022] orodha yao itawekwa pale,” aliongeza Tuwa. “Huu ni mwanzo tu, lakini tunafikiria namna ya kuja na njia bora zaidi ya kukusanya idadi ya wasomaji wote wa riwaya nchi nzima ili baadaye tuwe na takwimu za kuonesha idadi halisi ya wasomaji riwaya Tanzania.”
Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Profesa Mkenda alisema kwamba Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kuwa na waandishi wachache sana wa kazi za fasihi ukilinganisha na nchi kama Nigeria na Ghana, akisema kwamba ni “lazima Serikali isaidie” kubadilisha hali hiyo.
Mkenda alisema tayari Serikali imefanya kikao na wadau kilicholenga kuainisha mbinu ambazo Serikali inaweza kuzitumia kuweka vivutio zaidi ili kuwe na uandishi na usomaji zaidi wa vitabu nchini Tanzania.
Kugharamia kazi za fasihi
“Kikubwa ambacho tumeshafanya, na ambacho tumekiweka kwenye bajeti, [ni kwamba] tumeamua sasa tutakuwa tunachagua waandishi waliofanya kazi nzuri halafu tutagharamia uchapaji ya vitabu hivyo,” alisema Mkenda. “Kwa asilimia mia moja.”
Profesa Mkenda ameeleza kwamba baada ya Serikali kutoa gharama hizo ni jukumu la mwandishi sasa kujipanga pamoja na wasambazaji wake ili waweze kuuza kazi hizo ikiwa faida yote itakayopatikana itaenda kwa mwandishi pamoja na msambazaji.
“Na tunafanya hivyo ili UWARIDI ioneshe kwamba unaweza kuendesha maisha yako kwa kuwa mwandishi tu,” aliongeza Profesa Mkenda. “Kwa hiyo, kama unaweza kuandika kitu kizuri, halafu kikachapwa bila kuingia gharama yoyote, hiyo inaweza kufanikisha dira hiyo. Kwa hiyo, hilo tumeliweka kwenye bajeti [ya Wizara ya Elimu kwa mwaka 2022/2023].”
Zoezi hilo litasimamiwa na kamati maalum iliyoundwa na Profesa Mkenda na ambayo inasimamiwa na Profesa Penina Mlama, moja kati ya waandishi mashuhuri nchini Tanzania na gwiji la kazi za fasihi za Kiswahili.
Mkenda alisema kwamba mnamo Jumatano, Julai 6, 2022, kutakuwa na kikao cha menejimenti ya wizara yake na kamati ya Profesa Mlama ambayo tayari imeshaanza kazi kwa ajili ya kupitia andiko ambalo kamati hiyo imewasilisha serikalini.
“Nitoe wito kwa taasisi na makampuni mengine kusaidia pia shughuli hizi za uandishi na uchapishaji,” Profesa Mkenda alisema. “Na pahali pa kuanzia papo. Tuanze na UWARIDI. Hawa tayari wapo na wamejipanga, watafanya kazi zao mkiwasaidia au msipowasaidia. Kuwasaidia [UWARIDI] ni kusukuma gari moshi ambalo limeanza mwendo tayari.”
Kwisha kwa shughuli hiyo kulikuwa ni mwanzo kwa washiriki kuchangamana ambao wasomaji wa kazi za fasihi walipata fursa ya kubadilishana mawazo na waandishi wao pendwa pamoja na kupiga nao picha. Pia, ilikuwa ni fursa kwa wasomaji kununua vitabu kadhaa vya fasihi vilivyokuwa vinauzwa kwenye shughuli hiyo.
Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.