The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bila Uhuru wa Mwanafasihi, Fasihi Haiwezi Kuwa Chombo cha Ukombozi wa Umma

Ukosefu wa uhuru wa mwanafasihi hupelekea kushamiri kwa fasihi pendwa ambayo haina msaada kwa jamii kama yetu ya Kitanzania yenye matatizo lukuki ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

subscribe to our newsletter!

Uhuru wa mwanafasihi ni dhana inayohusiana na hiari na utashi wa mwanafasihi katika utunzi na uwasilishaji wa kazi yake bila ya kuingiliwa, au kushurutishwa, na mtu au chombo kingine chochote, akiwa ndani ya mipaka ya uhuru wake.

Na mwanafasihi hapa tunamaanisha mtunzi na mwasilishaji wa kazi ya fasihi, iwe fasihi simulizi au fasihi andishi. Mwanafasihi anaweza kuwa mwimbaji, msimulizi, muigizaji na hata mwandishi.

Mwanafasihi anakabiliwa na dhima kadhaa ikiwa ni pamoja na kufichua na kujadili maovu na matatizo yaliyopo kwenye jamii; kupanua wigo wa maendeleo; kukosoa na kuonya tabaka lolote lile; kuamsha na kuhamasisha watu katika kutatua matatizo sugu yanayowakabili; na kuikomboa jamii (kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni).

Lakini ili mwanafasihi huyu aweze kuyafanya haya kwa ustadi ni lazima awe huru kuamua nini cha kutunga na namna gani awasilishe alichokitunga pasi na kuyumbishwa au kuingiliwa na chombo chengine chochote.

Kinyume na hapo, mwanafasihi huyo ama atazama katika mawazo ya kikasuku, atatumia lugha ngumu iliyojaa taswira na mafumbo au atachagua kutunga fasihi pendwa zisizojadili masuala mazito yanayosababisha mikwamo katika maisha ya jamii, zaidi ya kuburudisha.

Wengi wetu tunadhani kwamba wanafasihi nchini Tanzania wapo huru kwa kule kuongezeka kwa idadi ya wasanii wa muziki, maigizo na waandishi. Kadhalika, wingi wa kazi za fasihi, hasa nyimbo na maigizo, unaashiria uhuru wa wanafasihi katika akili za wasioangalia mambo kwa jicho pevu na yakinifu.

Lakini kwa kiwango kikubwa kuna viashiria vingi vinavyobainisha kubanwa kwa uhuru wa mwanafasihi Tanzania. Viashiria hivi vinaweza kutokana na mazingira, mtunzi binafsi au kazi zenyewe.

Nguvu za dola

Moja ya viashiria vikubwa ni nguvu za dola kuingilia sanaa na taaluma ya fasihi. Mara kadhaa tumeshuhudia kazi mbalimbali za wasanii wa Kitanzania zikizuiliwa ama wao wenyewe kuingia makuchani mwa vyombo vya dola.

Wasanii kama Nay wa Mitego, Stamina, Roma wameshawahi kutiwa nguvuni au kuzuiliwa kwa kazi zao kwa kile kilichoitwa kukashifu viongozi wa Serikali.

Tafsiri ya kashfa hizo ni kule kuibua kwao maovu yaliopo kwenye jamii ikiwemo rushwa, unyonyaji, ukandamizaji, kutowajibika, ubadhilifu wa mali ya umma, utawala usiyofuata sheria na mengineo.

Hali hii imewafanya wanafasihi wengi kutumia taswira nzito, lugha fiche iliyojaa wingi wa mafumbo, tamathali na jazanda. Jambo hili, hata hivyo, huiwia vigumu hadhira ya kawaida kung’amua kilicho nyuma ya lugha ya wanafasihi. Wanaoweza kufahamu ni wachache hasa wanafasihi na wahakiki.

Hivi utakubaliana nami nikikueleza kuwa wimbo wa Msiniseme wa Ali Kiba au Muziki wa Darasa ni miongoni mwa nyimbo zinazozungumzia masuala ya kisiasa na kiutawala? Hakika nadhari za wengi zinaweza kunisuta juu ya ukweli huu.

Hii ni kwa sababu, wasanii hao wametumia mafumbo makubwa na taswira nzito katika mashairi yao kiasi cha kufichama kwa maudhui halisi ya kazi zao, ili kulinda usalama wa uhuru wao.

Matumizi makubwa ya kitaswira na lugha fiche katika kazi nyingi za kifasihi hasa nyimbo na maigizo, husababisha fasihi kusalia kama burudani pekee na kudhoofisha dhima ya kuikomboa jamii katika nyanja zote za maisha.

Matumizi haya pia yanaashiria hofu na woga wa wanafasihi dhidi ya usalama wao. Kwa minajili hii ni wazi kuwa uhuru wa mwanafasihi upo matatani. Hivyo, fasihi hushindwa kusimama kama chombo cha ukombozi wa umma.

Kushamiri kwa fasihi pendwa

Kwa kuhofia uhuru wao, tunashuhudia sasa wanafasihi wengi wakijitenga na udhati wa maisha halisi ya jamii. Badala yake hukithirisha maudhui ya kimapenzi, ngono, majigambo, upelelezi, ujasusi, kutupiana vijembe na kusutana.

Kinachodhihiri hapa ni kuwa maudhui ya namna hiyo hayana taathira kubwa katika kuikomboa jamii dhidi ya madhila, mateso, umasikini, ukandamizaji na uongozi mbaya usiyozingatia misingi ya utawala bora, haki na uadilifu. Hivyo kuifanya fasihi ishindwe kusimama kama chombo cha ukombozi kwa umma.

Wakati jamii ikiendelea kuathiriwa na umasikini, uonevu na uvunjwaji wa sheria na haki za binadamu, tunashuhudia mamia ya wanafasihi, hasa wa nyimbo na maigizo, wakidhaminiwa na kununuliwa ili kutetea maslahi ya matabaka ya wafadhili wao.

Kudhaminiwa na kununuliwa kwa wasanii ni kuporwa kwa utashi wa mwanafasihi ambao ndio kigezo kikuu cha uhuru wake.

Mwanafasihi akidhaminiwa na tabaka fulani, kamwe hawezi kujadili maovu ya tabaka hilo wala mikwamo ya maendeleo ya jamii inayosababishwa na mdhamini wake na hivyo kuigeuza fasihi ambayo ni mali ya jamii kuwa bakora ya kuiadhibu jamii yake badala ya kuikomboa.

Baadhi ya wanafasihi ni chanzo cha kuuweka uhuru wao matatani pia. Wanafasihi waliyowengi, hasa wa fasihi simulizi, hawakidhi vigezo vinavyotumiwa kupima uhuru wa mwanafasihi.

Utashi binafsi, kuitawala sanaa ya utanzu husika, kuilewa lugha na utamaduni wake na kuwa na falsafa inayoeleweka ni nyenzo na vigezo visivyoweza kuepukika katika kulinda na kupima kiwango cha uhuru wa mwanafasihi.

Wimbi kubwa la wanafasihi kukosa vigezo hivi husababisha wachache walionavyo kuonekana maadui, wasaliti na wapinzani wa mifumo ya kiutawala. Ilihali ndiyo wanaoitendea haki taaluma na sanaa ya fasihi kwa jamii zao. Kadhalika, wale wasiokidhi vigezo hivi hujikosesha uhuru binafsi wa mwanafsihi.

Hatimaye kazi zao hujaa matusi, lugha chafu, upotoshaji na uchapwa wa kisanaa. Hapo uhuru wao nao huingia matatani kwa kushindwa kuitawala vyema lugha na sanaa yake katika kazi zao.

Itakumbukwa wimbo wa Nyegezi wa Diamond na Rayvany, Chura wa Snura na baadhi ya filamu kwa kukosa ustadi wa kisanaa, lugha na utamaduni wake, ziliwahi kuingia matatani.

Udhibiti badala ya uthibiti

Hatuwezi kuulinda uhuru wa mwanafasihi ikiwa mabaraza ya sanaa, lugha na mamlaka husika zitajikita katika mwelekeo wa udhibiti badala ya uthibiti. Mwelekeo wa udhibiti unatoa nguvu na uhalali wa kufungiwa kwa kazi za fasihi au na mwanafasihi, ikiwa tu kazi hiyo inakinzana na falsafa, mitazamo na mielekeo ya mifumo ya kiutawala.

Mwelekeo wa uthibiti utazifungia kazi na mwanafasihi kwa kuchunguza vigezo vya kitaaluma, lugha, utamaduni na ustaarabu wa jamii husika. Vigezo ambavyo kama havikukidhiwa ni halali kwa kazi ya fasihi kufungiwa.

Hii ni kwa sababu fasihi ni zao la jamii na ni chombo cha kutunza utamaduni wa jamii husika, lugha na taaluma ya sanaa yenyewe. Kwa hivyo, kwa namna yoyote ile, fasihi haiwezi kukinzana na jamii. Ikitokea hivyo hiyo si fasihi na inapaswa kuzuiliwa.

Mwelekeo wa uthibiti utatoa dira na kutanabahisha kuwa mwanafasihi anapoibua maovu yaliyopo katika jamii yake na kubainisha mikwamo ya maisha, hakusudii kukashifu tabaka lolote.

Itaonekana kwamba anachokusudia ni kubainisha makosa na mitelezo iliyopo ili wenye mamlaka wayaone, wayasikie na wachukue hatua ama za kurekebisha mienendo au kutatua matatizo yanayojadiliwa.

Ni wajibu wa wanafasihi pia kuendelea kujifunza zaidi kuhusu lugha na kunga za sanaa husika. Kufanya hivyo kutasaidia kulinda uhuru wao na kuifikia dhima kuu ya fasihi ya kuikomboa jamii kuliko ilivyo sasa, ambapo fasihi imebakia kama chombo cha burudani.

Sambamba na hili wanafasihi lazima wazingatie kuwa uhuru usiyo na mipaka si uhuru salama. Mpaka wa uhuru wa mtu ni pale tu uhuru huo unapoanza kuingilia au kuhatarisha uhuru wa mwengine. Mathalani, uhuru wa mtunzi wa kazi za fasihi lazima pia uzingatie utamaduni, maadili na mahitaji ya jamii kwa wakati huo.

Uzingatie pia mabadiliko ya nyakati na mazingira, saikolojia ya maisha na falsafa ya ulimwengu kulingana na mazingira ya jamii. Vyenginevyo, chambilecho wahenga, tutakuwa tunabeba maji pakachani kama si kuchezea kusi kwa tanga bovu.

Kamwe hatutaifikia bandari tunayoiazimia!

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 responses

  1. Mimi ni mdau na msomaji mzuri wa makala ya “The chanzo initiative”, naomba kama kuna namna ya kuweza kupata updates kila wakati panapokuwepo na habari au taarifa mpya. Nilikuwa nikifuatilia makala iliyowekwa ambayo inazungumzia uandishi wa fasihi na changamoto zinazowakumba waandishi au watunzi.

    1. Habari Joseph

      Unaweza kufuatilia kurasa zetu za mitandao ya kijamii (@thechanzo) kuona kila tunapoweka makala unazozifuatilia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts