The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Eduardo dos Santos: Rais Aliyeyafisidi Mapinduzi ya Angola 

Ni nini Afrika kama bara inaweza kufanya kuiepusha na viongozi wa aina ya kina Dos Santos? Jibu linaweza kuwa gumu kuliko swali.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Julai 8, 2022, Rais wa awamu ya pili wa taifa la Kusini mwa Afrika la Angola José Eduardo dos Santos alifariki dunia.  Dos Santos, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 79, alikuwa moja kati ya viongozi wa Afrika waliotawala kwa muda mrefu sana, huku uongozi wake ukiambatana na kujilimbikizia mali yeye binafsi, familia yake na maswahiba wake.

Angola ni taifa lililokumbwa na vita kwa kipindi kirefu, kwanza vile vya ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wareno, vita iliyopiganwa chini ya  Movimento Popular de Libertacao de Angola (MPLA), au Chama cha Umma cha Ukombozi wa Angola, kilichoongozwa na Dk Agostinho Neto aliyefariki dunia mwaka 1979.

Vita ya pili iliyoikumba Angola ni ile vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza mwaka 1975, punde tu baada ya Angola kupata uhuru wake kutoka kwa Mreno, iliyopiganwa baina ya MPLA na waasi wa Chama cha Taifa cha Ukombozi Kamili wa Angola (UNITA) kilichoongozwa na Jonas Savimbi.

Kulikuweko na chama cha tatu, Chama cha Kitaifa cha Ukombozi wa Angola ((FNLA), ambacho kiongozi wake alikuwa Holden Roberto. Dk Neto alifariki dunia mwaka 1979 na ndipo Kamati Kuu ya MPLA ilipomteuwa José Eduardo dos Santos kuwa Rais, wakati huo akiwa kijana wa miaka 37.

Kwa hakika, wengi walifikiria mrithi wa Neto angekuwa Katibu Mkuu wa MPLA Lucio Lara, mwanamapinduzi muasisi wa MPLA aliyehakikisha nadharia ya Karl Marx iliyokuwa ikifuatwa na chama hicho inaendelezwa.

Lakini Lucio Lara, kwa mshangao, alilikataa pendekezo hilo na mbele ya kikao cha Kamati Kuu alichokiongoza akiwa Katibu Mkuu, mtu mwenye madaraka na usemi mkubwa chamani, alipotamka, “Näo proponho camadara Dos Santos assuma a lideranca,” ambayo kwa tafsiri isiyo rasmi alimaanisha, “Hapana, napendekeza ndugu Dos Santos achukuwe uongozi.”

Dos Santos ndani ya viatu vya Neto 

Alipoapishwa na kukamata hatamu kama Rais wa pili wa Angola, Dos Santos, aliyesoma na kuhitimu uhandisi wa shughuli za uchimbaji mafuta kutoka Chuo Kikuu cha Baku Azerbaijan, enzi ya uliokuwa Muungano wa Jamhuri za Kisovieti (Soviet Union), aliwashangaza  wana MPLA alipoanza kuwafyeka vigogo, akiwemo Lucio Lara ambaye aliteuliwa kuwa Spika wa Bunge na Lopo do Nascimento aliyekuwa Waziri Mkuu.

Ilionekana dhahiri ameazimia kuyadhibiti madaraka! Wakati vita vikiendelea dhidi ya waasi wa UNITA, hatimaye ulipatikana mkataba wa amani uliosainiwa Lisbon, Ureno, uliopelekea kufanyika kwa uchaguzi, huku UNITA ikiahidi kuachana na mapigano na kuwa chama cha kisiasa.

Kiongozi wake, Jonas Savimbi, akawa Makamu wa Pili wa Rais. Lakini Savimbi akawa anasita sita kurudi Luanda. Muda si mrefu kukaibuka vita vyengine vilivyodumu hadi 2002, vita iliyopelekea kifo cha Savimbi aliyekufa kwenye uwanja wa mapigano.

Kuuwawa kwa Savimbi kulisaidia kufungua ukurasa mpya ambapo yalipatikana makubaliano mapya ya amani na jeshi la UNITA likajumuishwa katika jeshi la taifa na UNITA kugeuka kuwa chama cha kisiasa na wajumbe wake kuchaguliwa kuingia bungeni katika uchaguzi uliofuata.

Dira  ya MPLA ilionekana kuanza kubadilika wakati  Rais Eduardo dos Santos, ambaye alikuwa kiongozi asiyezungumza sana na mtu asiye kubali ushauri, alipofanikiwa kuwaondoa wapinzani wake wote chamani.

Mshauri wake mkubwa na wa karibu alikuwa ni binti yake Isabel dos Santos mwenye umri wa miaka 49, aliyezaa na mkewe wa kwanza Tatiana  Kukanova aliyekutana naye akiwa masomoni Urusi ya zamani na kutalakiana naye mwaka 1979.

Isabel ndiye aliyeteuliwa na baba yake kuliongoza Shirika la Mafuta na ukawa mwanzo wa safari ya familia ya Dos Santos kujirundikizia utajiri mkubwa usio na kifani. Isabel alitajwa kuwa mwanamke tajiri kabisa barani Afrika, akiwa na ushawishi katika uongozi wa baba yake.

Familia ya Dos Santos ikajijengea himaya ya utajiri mkubwa pia Ulaya na katika mataifa ya Ghuba. Mali kadhaa za familia ya Dos Sangtos zimezuiliwa kwa sasa huku uchunguzi dhidi ya Isabel na wengine ukiendelea.

Ilipokuwa ikizungumzwa kwamba Luanda, mji mkuu wa Angola, ndio jiji lililo ghali kabisa duniani, binafsi nikihisi kama kutiwa chumvi. Miaka yote nikiliona jiji la Paris, Ufaransa ndilo ghali zaidi.

Lakini rafiki yangu mmoja kutoka Angola, kada wa MPLA, alinihakikishia kwamba ni kweli mji wa Luanda umegeuka kuwa mji wa matajiri pekee na Waangola wanaoishi kwenye vitongoji vya mji huo wanaendelea kuwa katika hali duni, akisikitika kwamba hayo yanatokea katika nchi iliyo ya pili kwa uchimbaji mafuta barani Afrika na mchimbaji mkubwa wa madini ya almasi.

Nilimuuliza nini chanzo cha hali hiyo? Jibu lake likuwa uongozi mbaya wa MPLA ulioyazika mapinduzi ya Angola na matumaini ya Waangola, viongozi kutumbukia katika dimbwi la ufisadi na rushwa. Kama yalivyotokea kwengineko, Eduardo dos Santos aliukumbatia upepari na utandawazi na kuzizika fikra za kimapinduzi, chimbuko la  MPLA.

Lourenço na vita  dhidi ya ufisadi

Mwaka 2016, Eduardo dos Santos aliamua kuondoka madarakani kwa sababu ya hali mbaya ya afya na kumpendekeza João Manuel Gonçalves Lourenço aliyehudumu kama Katibu Mkuu wa MPLA kwa miaka kadhaa na Waziri wa Ulinzi kuchukua nafasi yake.

Lourenço akawa mgombea wa MPLA katika uchaguzi wa mwaka 2017 na kumrithi Dos Santos. Akikerwa na kukithiri kwa rushwa, Lourenço alianza kuchukua hatua kali, akiwaandama vigogo kadhaa. Katika kundi hilo, Isabel na familia ya mtangulizi wake haikunusurika.

Lourenço alianzisha uchunguzi katika shirika la mafuta la taifa, akimsimamisha kazi binti huyo wa Dos Santos na kuzizuwia mali za familia hiyo. Pia, alitangaza kuyachunguza makampuni ya mafuta ya kigeni ambayo Isabel alikuwa na uhusiano nayo.

Sambamba na hayo, vita dhidi ya mafisadi havikuishia kwa familia ya Dos Santos pekee. Rais Lourenço aliwafukuza kazi Waziri wa Usalama na Mkuu wa Idara ya Usalama na Intelijensia na hata aliyekuwa Mkuu wa  Idara ya Usalama jeshini Apolinario Jose Pereira.

Benki Kuu ikatangaza kuanzisha uchunguzi baada ya kugundua kulitolewa kitita kikubwa cha fedha kutoka Benki ya Biashara na kuingia mikononi mwa maafisa wa kijeshi kutoka Idara  ya Usalama ya Ikulu ya Rais. Kwa ujumla, kabla ya Dos Santos kuachia ngazi, maafisa kadhaa serikalini walihakikisha wanajichotea fedha kwa kiasi wanachoweza.

Dos Santos  aliondoka kwenda kuishi ng’ambo, akitibiwa ugonjwa uliomsumbua kwa muda mrefu, mjini Barcelona, Hispania. Lakini  alimuachia kibarua kigumu mrithi wake cha kupambana na ufisadi uliokuwa umekidhiri katika kipindi cha karibu miaka 40 ya uongozi wa  Rais Dos Santos.

Wadadisi wanasema miaka mitano baada ya kuchukua uongozi wa taifa hilo, Lourenço ameshindwa kuwapa matumaini Waangola na sababu kubwa ni kwamba rushwa na  ufisadi vinatokana na mfumo ulioota mizizi.

Wapinzani wake wanasema kinachohitajika ni mabadiliko ya utawala. Angola inatarajia kufanya Uchaguzi Mkuu Agosti 24 mwaka huu. Tayari vyama vya upinzani vimelalamika Serikali kujaribu kufanya mizengwe ili kuvihujumu kwa kuvitumia vyombo vya dola.

Dos Santos anaacha alama gani Afrika?

Ni dhahiri kifo cha José Eduardo dos Santos wiki iliyopita kinaacha hisia tafauti kwa wananchi wa Angola. Kuna wale watakaomkumbuka kama mmoja wa wanaharakati waliopigania ukombozi wa taifa hilo.

Wengine watamkumbuka kama kiongozi aliyevunja matarajio yao na kuwaacha katika dimbwi la umasikini na hali duni. Kwa Afrika, kifo cha Dos Santos kinaacha kumbukumbu ya mtu aliyejitajirisha kama marais wengine kadhaa ambao waliingia madarakani kwa ahadi nyingi za kutetea rasilimali za nchi zao na Afrika.

Matokeo yake wameondoka madarakani wakiwa na utajiri mkubwa na wengine kuendelea kubakia madarakani kwa lengo la kujihudumia badala ya kuutumikia umma uliowaweka madarakani na hata kuukandamiza. Kweli madaraka matamu na wakati mwengine ni matamu zaidi.

Swali kubwa ni vipi Afrika itaweza kujikomboa kutokana na viongozi wa aina ya kina Dos Santos? Bahati mbaya hata baadhi ya wanaojigamba kuwa wanamapinduzi na  wanaumajumui wa Kiafrika nao sasa vitendo vyao vinaekewa alama ya kuuliza.

Mohammed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts