The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

Ripoti za vijana kupotea katika mazingira tatanishi zinakuja wakati ambao Rais Samia anaielezea Zanzibar kama sehemu hatarishi kwa usalama wa nchi.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Pengine hakuna watu waliolipokea kwa mikono miwili agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Polisi kuhusu haja ya kuiongezea Zanzibar ulinzi kama wazazi na ndugu na jamaa ambao mpaka wakati wa kuandika makala haya wanashindwa kupata usingizi kwa kutokujua hatma ya wapendwa wao waliopotea kwa nyakati tofauti katika mazingira ya kutatanisha.

Amiri Jeshi Mkuu huyo alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi mnamo Agosti 30, 2022, mkoani Kilimanjaro alipogusia haja ya Zanzibar kufanywa Kanda Maalum, akisema “Zanzibar ni padogo penye mambo makubwa.”

Samia alisema Jeshi la Polisi linalotegemewa kuvilinda visiwa vya Zanzibar ambavyo amesema viko wazi “ni dhaifu,” akibainisha kwamba kitu pekee polisi wanalinda Zanzibar ni “mawaziri na wakubwa [wengine] tu pale mjini.” Rais Samia alienda mbali zaidi kwa kusema kwamba “Zanzibar ni sehemu hatarishi.”

Kwa familia nyingi zilizopoteza wapendwa wao kwenye mazingira ya kutatanisha kwa siku za hivi karibuni, tathmini ya Rais Samia juu ya hali ya Jeshi la Polisi Zanzibar na hali ya usalama visiwani humo kwa ujumla ni ile ambayo wao wenyewe wamekuja nayo baada ya kushindwa kujua ni wapi wapendwa wao wapo kwa sasa na ni lini wanaweza kurejea na kuungana na familia zao.

Ameshindwa kuwafikiria watoto?

Sabrina Khamis ni mama wa watoto watatu, wote wakike, anayeishi Michenzani, mjini Unguja. Sabrina, anayejishughulisha na uchoraji wa hina kuendesha maisha yake, ameshalia sana. Kwa kumtazama tu utajua kwamba Sabrina si mtu mwenye furaha. Akiwa amekaa kwenye kochi lake sura yake ni ya uchovu huku macho na miguu yake  vikionekana kuvimba.

Sabrina, sasa akiwa na ujauzito wa miezi saba, anaikumbuka vyema siku ya Julai 26, 2022. Hii ni siku ambayo mume wake, ajulikanaye kama Sultan Mussa, alitoweka kwenye mazingira ya kutatanisha na mpaka leo hajaonekana tena.

Mussa, 36, aliyekuwa akifanya kazi kama kinyozi, hakuwa mtu wa dini sana, Sabrina anasema, alikuwa hata akitumia vilevi, kama vile bangi. Hali hiyo, hata hivyo, ilibadilika ulipofika mwezi wa Ramadhan, ambayo ilikuwa Aprili mwaka huu wa 2022.

“Ramadhan yote mawaidha yake yalikuwa ya Aboud Rogo,” Sabrina aliieleza The Chanzo wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika nyumbani kwake. “Na kabla ya siku hajaondoka alikuwa anaulizia kuhusu biashara za Kenya na pia alirudisha mapenzi [kwangu] haswa mpaka nikawa nashangaa.

Aliniaga kuwa anakwenda Dar es Salaam kununua mitumba. Nikampa pesa kisha akatoka. Akiwa kwenye mlango akawa anazungumza na mtu [kwenye simu], akisema nakaribia sasa hivi.”

Sheikh Aboud Rogo Mohammed alikuwa ustadhi wa dini ya Kiislamu kutoka nchini Kenya aliyeshukiwa kuwa na mafungamano na kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab cha nchini Somali, akitajwa kuratibu michango ya kifedha kwa ajili ya kikundi hicho.

Mnamo Agosti 27, 2012, Rogo aliuwawa na watu wasiyojulikana, huku kifo chake kikisababisha maandamano makubwa nchini Kenya. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Rogo alikuwa na ushawishi mkubwa ndani ya Afrika Mashariki na ripoti mbalimbali zinaonesha kwamba mahubiri yake yanaendelea kuwa na ushawishi mkubwa.

Kwa mujibu wa Sabrina, mume wake huyo alimpigia simu na kumjulisha kwamba tayari alikuwa amefika jijini Dar es Salaam. Majira ya saa saba za usiku, Mussa alimpigia tena simu Sabrina na kumwambia mke wake huyo kwamba amuombee na kwamba angempigia tena asubuhi.

“Lakini asubuhi ilipofika hakunipigia na nilipoanza kusikia kuhusu watu kupotea nikaanza kupata wasiwasi,” Sabrina anasimulia kwa uchungu mkali. “Ndipo nikaenda sehemu tunayoweka vyeti na kuona hati yake ya kusafiria haipo. Ndipo nilipojua kuwa mume wangu ameniacha na watoto kwenda huko Jihad.”

“Mume wangu ameondoka bila hata kuwafikiria watoto wangu,” alinung’unika Sabrina huku machozi yakimtoka kama maji yanavyotoka kwenye bomba. “Mume wangu ameondoka bila kunifikiria hata mimi, kweli?”

Sabrina alikuwa hawezi tena kuongea na mahojiano yetu yakaishia hapo.

Sultan Mussa, 36, alitoweka katika mazingira ya kutatanisha huko Zanzibar mnamo Julai 26, 2022, akiacha nyuma mke mwenye ujauzito, Sabrina Khamis, pamoja na watoto watatu. Mpaka leo hajaonekana tena.

Wingu la hofu

Simulizi kama za Sabrina zimetawala visiwani hapa na kutengeneza wingu la hofu na wasiwasi miongoni mwa wakazi wake. Kwa wale ambao ndugu zao tayari wametoweka, hofu yao ni kutokujua hatma yao na kwa wale ambao bado hawajakumbwa na kadhia hiyo hofu yao kubwa ni lini itakuwa zamu yao.

Ni ngumu kufahamu ni vijana wangapi haswa mpaka sasa tayari wametoweka kwenye mazingira kama hayo, huku Jeshi la Polisi likishindwa kuzipa familia zilizojawa na majonzi ya kupotelewa na wapendwa wao majibu yanayoweza kueleweka.

Mnamo Agosti 16, 2022, kufuatia miezi ya malalamiko kutoka kwa wananchi, Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad alithibitisha uwepo wa visa vya watu kutoweka katika mazingira tatanishi visiwani humo lakini aligoma kuhitimisha kwamba vijana hao wanajiunga na vikundi vya kigaidi.

“Inawezekana watu wamepotea, lakini kuna wengine miongoni mwa hao wanaosemekana kwamba wamepotea, inawezekana wameondoka kwa ajili ya kufanya shughuli za halali kabisa,” Hamad aliwaambia waandishi wa habari.

“Sitaki kukataa ukweli kwamba wengine pengine wanaweza wakawa wanajiunga na hivyo vikundi,” aliendelea kueleza afisa huyo mwandamizi wa Jeshi la Polisi. “Lakini sasa tunaweza tukalisema hilo pale tutakapokuwa na ushahidi.”

Juhudi za The Chanzo zilizolenga kufahamu kama polisi wameweza kupata ushahidi wowote au la! ziligonga mwamba baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kujibu maswali yetu mpaka wakati wa kuandika habari hii.

Na wakati The Chanzo haiwezi kuthibitisha kwamba ni kweli vijana hawa wanajiunga na vikundi vya kigaidi, ushahidi uliopo unaonesha kwamba baadhi yao wanafanya hivyo.

Alikuwa anachukia dhuluma

Kama wazazi wengi wa Kizanzibari, Mwanamkuu Abdallah Said alikuwa akijivunia mtoto wake Abdulkadir Salum Seif ambaye alikuwa na sifa zote za mtoto mwema: alipenda kusoma Kurani, alichukia kuona watu wanadhulumiwa na hakufurahia kushamiri kwa uchafu wa kimaadili katika visiwa vya Zanzibar.

Lakini miezi sita kabla ya kutoweka kwake hapo Oktoba 2021, Seif, 19, alianza kuonesha dalili ambazo zilimpa mashaka sana mama yake mzazi, Mwanamkuu, mama wa watoto wanne, ambaye Seif ni mtoto wake wa kwanza.

Abdulkadir Salum Seif, 19, ambaye mama yake Mwanamkuu Abdallah Said amemuelezea kama mtu aliyekuwa hapendi dhuluma, alitoweka Oktoba 2021 huko Zanzibar. Aliacha barua iliyowataka wazazi kuacha kuwa hofu, akiwaambia “Tutaonana kesho kwa Allah (S.W).”

“Aliacha kuungana na waumini wengine wa Kiislamu kwenye ibada ya sala na [kuanza] kusali peke yake,” Mwanamkuu aliieleza The Chanzo kwa taabu sana. “Alikuwa akisema masuala ya kujiunga na makundi hatarishi ya Al-Shaab. Alikuwa akizungumzia masuala ya bastola na mambo ya mujahideen yalikuwa mengi.”

Mujahideen ni neno la Kiarabu ambalo tafsiri yake isiyokuwa rasmi ni Waislamu wanaojitolea kupigana kwa niaba ya dini yao au kwa niaba ya jamii ya Kiislam, au ummah, kama jamii hiyo inavyojulikana kwa Kiarabu.

Tukiwa tunaendelea na mahojiano sebuleni kwa akina Seif, The Chanzo iliweza kuona ukutani picha ya familia; Mwanamkuu akiwa na mume wake wakiwa wameketi na Seif na binamu zake na ndugu zake wengine wakiwa wamesimama.

“Mara nyingi alitoka akiwa na msala wake na siku hiyo alipoondoka kwenda Paje aliniaga na kunikumbatia na kusema nimuombee,” Mwanamkuu anakumbuka. “Sikujua kama anaweza kuniacha na kwenda huko. Ni maumivu sana ninayopata na baada ya matangazo kuna watu kadhaa walinipigia simu na kuniambia wamemuona Nairobi.”

Maneno yanayoonekana ndani ya kabati la nguo la Abdulkadir Salum Seif.

Lakini Mwanamkuu hakuwa na haja ya kuamini waliokuwa wanampigia simu na kumweleza habari za kijana wake. Alipaswa tu kusoma barua ambayo Seif mwenyewe aliacha kabla ya kuondoka, akiwasihi wazazi wake wasiwe na wasiwasi na kumjulisha kwamba wataonana “kesho kwa Allah (S.W).”

Ukurasa wa kwanza wa barua ya kurasa nne ambayo Abdulkadir Salum Seif aliwaachia wazazi wake kabla ya kwenda kusikojulikana.

Akiwa anaendelea na mahojiano na The Chanzo, Mwanamkuu alipokea simu iliyomjuza kwamba kuna vijana wengine wawili, mmoja kutoka Kikwajuni na mwengine Michenzani, ambao nao walikuwa wamepotea.

Maandishi ya A.K 47, aina ya silaha, ambayo Abdulkadir Salum Seif ameandika kwenye mlango wa chumbani kwake.

Abdulkadir mwenyewe, baadaye ilikuja kugundulika, aliondoka  na rafiki yake Nudrik Mkubwa Salim, aliyekuwa na umri wa miaka 23. Wawili hawa wanatajwa kuondoka siku moja, muda mmoja. Salim alikuwa analelewa mtaa wa tatu karibu na nyumbani kwao Seif.

Nudrik Mkubwa Salim, 23, anayetajwa kuondoka siku moja, muda mmoja, na Seif. Mpaka sasa wote wawili hawajulikani walipo.

Vijana wa vijiweni walengwa

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na The Chanzo, iligundulika kwamba sehemu kubwa zinazotumika kuwinda vijana hawa na kuwashawishi kuondoka Zanzibar ni vijiweni, sehemu ambazo vijana wa makamo hukaa kwa pamoja na kujishughulisha na tabia kama vile za kutumia mihadarati, ikiwemo bangi.

The Chanzo ilibahatika kuzungumza na mmoja wa vijana aliyefuatwa na watu hawa ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe, ambaye alisema kwamba watu hao wana ofisi zao mjini Darajani na wamekuwa wakitembelea vijiwe vingi ambapo vijana wapo na kuwashawishi wajiunge na vikundi vya kigaidi.

“Huwa wanakuja maskani tukiwa tumekaa na kuanza kutuambia kuhusu hayo mambo ya mujahideen; ni watu wapo na wana ofisi zao hapa mjini,” alisema kijana huyo. “Unajua mimi sitaki kwenda huko nikamuacha mama yangu. Mama yangu hana mtu na kusema ukweli wananisumbua sana.”

Mama na ndugu wa kijana huyu unaweza kusema ni watu wenye bahati. Hata hivyo, siyo wazazi wengi visiwani hapa wenye bahati kama hiyo.

​​Jua limeshazama tayari, siku ya kwanza ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ikiwa imeshapita, nami naingia kwenye dalala ya Bububu – Fuoni.

Lengo la safari hii ni kwenda kuonana na Fatma Hassan Yussuf, mama wa watoto wanne mkaazi wa Michenzani. Mnamo Julai 27, 2022, mtoto wa pili wa Fatma, Hassanali Khalid Ahmed, mwenye umri wa miaka 21, naye alipotea kwenye mazingira ya kutatanisha.

“Kwanza aliacha kazi, akawa amezidisha kusali na kukaa maskani,” Fatma ananieleza wakati wa mazungumzo yetu. “Maana yeye amesomea mambo ya ubaharia akawa anasema juu ya mambo yanayoendelea nchini Nigeria na Kenya. Aliwahi kuniambia kuhusu kwenda Dar es Salaam kubadilisha vyeti vyake vya ubaharia. Alingojea mpaka nimetoka kwenda kazini ndipo akaondoka.”

Fatma hakushtuka mpaka alipoanza kuwa hampati kijana wake kwenye simu. Kibinadamu, Fatma akajipa matumaini kwamba labda siku ya pili yake angempata kijana wake. Hakumpata mpaka wakati anaongea na The Chanzo.

Hassanali Khalid Ahmed, 21, naye anasemekana kupotea katika mazingira yasiyoeleweka hapo Julai 27, 2022. Mpaka sasa hajulikani alipo.

Fatma alipoweka tangazo la kupotelewa na kijana wake ndipo alipogundua kwamba kijana wake na Mussa, yule mume wake Sabrina aliyetoweka kwenye mazingira tatanishi pia, ni marafiki. Sabrina alikiri kwa The Chanzo kumuona Hassanali nyumbani kwake mara kadhaa akizungumza na mume wake.

‘Ondoka kabla baba yako hajajua’

Kwenye mkutano wake na waandishi wa habari hapo Agosti 16, 2022, Kamishna wa Polisi wa Zanzibar Hamad Khamis Hamad aliwaambia wananchi kwamba “Jeshi la Polisi ni chombo cha kwao,” akiwataka watoe ushirikiano kwa jeshi hilo katika kuchunguza matukio hayo.

Lakini Hamad anaweza kuanza kuchukua uzoefu kutoka kwa afisa mwenzake kutoka Idara ya Zimamoto kwani hata maafisa waandamizi wa Serikali hawajasalimika kwenye juhudi hizo za kuwinda watu wanaoweza kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Mnamo Agosti 8, 2022, kwa mfano, Ibrahim Ali Hassan, ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Zanzibar, alipotelewa na mtoto wake mwenye umri wa miaka 19 aitwaye Ali Ibrahim Ali.

Ali amemaliza kidato cha nne mwaka huu wa 2022 na baba yake alikuwa na mipango ya kumpeleka nchini Uturuki kwa ajili ya kusoma. Hata hivyo, majira ya saa tano asubuhi ya siku ya tukio, Ali aliondoka na kuna ujumbe ambao ulionekana kwenye simu yake akizungumza na mtu juu ya safari hio.

“Aliondoka kwenda kwa Sheha kuchukua barua kwa ajili ya kwenda nayo uhamiaji ili kuweza kutengeneza pasi ya kusafiria,” baba yake Ali aliiambia The Chanzo.

Kwa Zanzibar, Sheha hufanya kazi zinazofanywa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa kwa Tanzania Bara.

“Ila hapo hapo akakimbia na mpaka sasa hajulikani alipo,” aliendelea kueleza baba huyo. “Ila dada yake alikamata simu yake na kuona ujumbe ulioandikwa jitahidi uondoke kabla baba yako hajajua na namba ya jina hili limeandikwa Fahad ila kila tukipiga haipatikani.”

Jihad

Sheikh Abdallah Haji ni Mwalimu wa Fiqh – fani ya elimu inayoshughulikia na kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za Uislamu katika maisha ya kila siku – kutoka Mombasa, Zanzibar.

Sheikh Haji ameieleza The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba ameshtushwa na habari za vijana hao wa Kizanzibari wanaotelekeza familia zao kwa kisingizio cha kujiunga na Jihad, akisema kwamba kwa sasa hakuna Jihad inayoendelea duniani.

Jihad ni neno la Kiarabu ambalo linaweza kuwa na maana mbili. Maana ya kwanza ni vita takatifu inayopiganiwa kwa niaba ya dini ya Kiisalamu kama wajibu wa kidini. Maana ya pili ni mapambano binafsi katika nafsi ya mtu ambayo yanaweza kuhusisha nidhamu ya kidini.

Kwa mujibu wa Sheikh Haji, Jihad inayowezekana kwa sasa ni hiyo ya pili tu kwani ili hiyo ya kwanza ifanyike ni lazima kuwe na tamko la kiongozi wa juu wa kidini, tamko ambalo kwa sasa anasema halipo.

“Hivyo, watu wanaowashawishi vijana kuhusu Jihad ni waongo na wapotoshaji,” alibainisha Sheikh Haji. “Hili linalofanyika hivi sasa [hapa Zanzibar] lishawahi kutokea huko nyuma. Ni muhimu viongozi wa dini na Serikali kuunganisha nguvu kuzuia hii hali. Hiyo siyo tu itaokoa vijana wetu lakini pia tutaimarisha usalama wa nchi yetu.”

Peter Bofin ametumia miaka 12 iliyopita kutafiti masuala ya ugaidi katika nchi za Tanzania, Kenya na Mozambique ambaye ameiambia The Chanzo kwamba kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na ushindani kwenye kusajili miongoni mwa vikundi vya kigaidi vya Al Shabaab na vile vinavyohusiana na Islamic State kwenye nchi za Mozambique na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Kwenye miaka hii miwili – mwaka jana na mwaka huu – Al Shabaab wametoa video kadhaa zinazowalenga wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kwa lengo la kupata vijana wa kuwasajili,” alisema Bofin.

“Al Shabaab wanaweza wakawa na mafanikio zaidi kwenye kusajili kwa sababu kwanza wana pesa nyingi,” aliongeza mtaalamu huyo wa masuala ya ugaidi. “Wanatoza kodi kwenye maeneo wanayosadikiwa kuyadhibiti. Hii inawawezesha kusajili kwa urahisi, kutoa motisha, na huduma fulani angalau kwa viwango vya Somalia.”

Zanzibar kuwa Kanda Maalum?

Rais Samia anadhani ili kufanikisha hili lengo la kuimarisha usalama wa nchi, vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji, vinapaswa kuiangalia Zanzibar kwa jicho la tatu.

“[Zanzibar] kuko wazi kabisa,” Rais Samia alisema wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi hapo Agosti 30, 2022. “Kuna kesi ambapo silaha kubwa kubwa [zimechukuliwa] zikafichwa visiwani [humo]. Kama ni eneo hatarishi, Zanzibar ni eneo hatarishi. Inahitaji kupewa uangalizi maalum.”

Samia alionya kwamba watu ni rahisi kuingia Zanzibar, akibainisha kwamba wakati kuna maeneo yanalindwa, yapo maeneo ambayo hayalindwi kabisa, na hivyo watu kuweza kuingia kwenye visiwa hivyo kwa urahisi.

Hii inakuja na athari kubwa sana kwa nchi, alikiri Rais Samia.

“Madawa [ya kulevya] ni rahisi kupitia Zanzibar,” alidokeza Rais Samia. “Usafirishaji haramu wa binadamu [pia ni rahisi kufanyika]. [Ni lazima tujue] watu gani wanaingia [Zanzibar], watu gani wanatoka.”

Ni wazi kwamba vyombo vya ulinzi na usalama kwa sasa vitakuwa vinatafakari namna vinavyoweza kutekeleza agizo la Rais Samia.

Wakati vikifanya hivyo, Sabrina Khamis, Mwanamkuu Abdallah Said, Fatma Hassan Yusuf,  Ibrahim Ali Hassan na wazazi wengine waliopoteza vijana wao katika mazingira ya kutatanisha visiwani hapa watakuwa wanavitegemea vyombo hivyo hivyo kufanikisha kurejea kwa vijana wao ili waungane nao kwa mara nyengine tena.

Hii itafanya vilio, simanzi, huzuni na majonzi ambavyo kwa sasa vimetawala nyumba zao kukoma na kutoa nafasi kwa familia hizi kuendelea na majukumu ya ujenzi wa taifa!

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts