Kwa takriban miaka kumi hivi tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, palikuwa pakifanywa uhalifu mkubwa hapa Zanzibar kwa jina la Mapinduzi hayo. Moja ya eneo maarufu ambalo lilikuwa limeshtadi kwa mateso na ukatili ni gereza la Kwa Bamkwe.
Huku gerezani Kwa Bamkwe, misamiati huruma na ubinadamu ilikuwa haifahamiki. Binadamu kama sisi walikuwa wanakatwakatwa, wananyongwa na kufukiwa wakiwa hai. Wako wengi walioonekana wakipelekwa Kwa Bamkwe lakini hawakuonekana tena wakirejea hadi leo hii.
Tokea kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania, Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya kihalifu, mateso, uwekaji watu vizuizini, ubakaji na mauwaji vinavyotekelezwa na vyombo vya dola, hususan kabla na baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Uhalifu huu wa kidola umekuwa ukizua taharuki kubwa ndani ya Zanzibar na kupelekea chuki, uhasama na mifarakano baina ya watawala na raia kwa upande mmoja; na baina ya kambi mbili za kisiasa zilizopo Zanzibar, kwa upande wa pili.
Mwaka 2010, viongozi wetu wapenzi, wenye ghera na uzalendo wa nchi yao, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Amani Karume na Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, walidhamiria, kwa dhati kabisa, kukomesha siasa hizo kupitia Maridhiano ya Novemba 5, 2009, ambayo, pamoja na mambo mengine, yalizaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Azma hii, hata hivyo, haikudumu kwa muda mrefu kwani waliokabidhiwa hatamu za nchi yetu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, walijali zaidi maslahi ya vyeo na matumbo yao badala ya maslahi mapana ya nchi yetu. Pamoja na misingi mizuri iliyowekwa kufuatia Maridhiano hayo, nchi yetu ilirejeshwa tena katika mkwamo mpya wa kisiasa baada ya kuvurugwa kwa makusudi kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Kama sote tunavyokumbuka, kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2020, hali ya kisiasa ilikuwa mbaya zaidi kote Tanzania Bara na Zanzibar. Utawala wa kidikteta chini ya Hayati John Magufuli uliweza kutamalaki nchini kuliko ilivyowahi kutokea tangu nchi yetu iingie katika ushindani wa vyama vingi vya siasa, na mara nyengine taswira ilikuwa ya kutisha hata kuliko tokea tupate uhuru.
Utawala huo wa mkono wa chuma usiojali sheria, Katiba wala ubinadamu, uliweza kumdhibiti kila aliyetamani kuona haki, demokrasia na utawala bora vinamalaki ndani ya nchi yetu. Hivyo basi, hali hiyo ikapelekea nchi kuingia katika giza nene lililopelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 kuwa wa kibabe zaidi, usiojali sheria zaidi, wa kihalifu zaidi na mauwaji.
Mimi ninayeandika makala haya ni mmoja tu kati ya mamia ya wahanga wa uhalifu uliofanywa na vyombo vya dola kupitia jina la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa Zanzibar.
Pamoja na kuonywa sana na kutishiwa kurejeshwa tena Kwa Bamkwe pindipo tukithubutu kuyahadithia mateso tuliyotendewa, nimeona ipo haja ya kuhadithia kwa urefu ili kumbukumbu ziwekwe na wapenda haki za binadamu na demokrasia ndani ya nchi yetu na duniani kwa manufaa ya sasa na ya baadaye ya nchi yetu.
Mateso wakati wa uvamizi
Nilikuwa mmoja wa vijana 40 waliokabidhiwa jukumu la kusimamia kituo cha kujumlisha na kuhakiki matokeo ya Uchaguzi Mkuu (Party Tallying Center) ya Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Tulikabidhiwa jukumu hilo na chama na kituo chetu cha kufanyia kazi hiyo kilikuwa ni Hoteli ya Mazsons iliyopo Shangani, Zanzibar. Hoteli ya Mazsons mara kadhaa hukodiwa na ACT-Wazalendo kwa ajili ya kufanya shuguli zake mbali mbali za kichama.
Kituo cha kujumlisha na kuhakiki matokeo ya Uchaguzi Mkuu ambacho mwandishi wa makala haya na wenzake 40 walikuwa wakifanya kazi kabla ya kuvamiwa na kuteswa. Kituo kilikuwa katika Hoteli ya Mazsons iliyopo Shangani, Zanzibar. PICHA | KWA HISANI YA MWANDISHI
Usiku wa Oktoba 28, 2020, hapo Mazsons Hotel, kiasi cha saa nne usiku, tukiwa tunakaribia kufunga jukumu tulilokabidhiwa la kujumlisha na kuhakiki matokeo ya Mgombea wa Urais wa Zanzibar wa ACT-Wazalendo, tulivamiwa na kundi kubwa la askari wanaokadiriwa kufikia mia moja waliokuwa wamevalia sare kama zile za JWTZ.
Askari hawa walikuwa wameziba nyuso zao na wameshikilia silaha nzito za kivita mikononi, ikiwemo marungu, vipande vya nondo na nyenzo nyengine mbali mbali walizozitumia kwa ajili ya kutugeuza kuwa kama mateka wa kivita.
Askari hao walituvamia kijeshi kwa kufyatua risasi na kupiga mateke mlango mmoja baada ya mwengine hadi walipofika katika ukumbi mdogo tulipokuwa tukifanyia kazi yetu.
Waliyotufanyia wanajeshi hao ni ya kusikitisha na kuhuzunisha. Bila ya kutueleza wametumwa na nani, au kosa letu ni nini, walianza kututishia kifo, kuvunja vunja vifaa na miundombinu yote tuliyokuwa tunafanyia kazi, kutupiga, kutukatakata kwa visu na singe za bunduki zao, kutuvunja miguu, uti wa mgongo, kutupasua midomo, kututumbua macho nakadhalika.
Kwa upande wangu mateso ya uvamizi yaliniathiri uti wa mgongo kwa kupata maumivu makali na shida ya kuendelea hata kukaa kitako katika eneo hilo. Kwa namna nilivyokuwa nikijiskia maumivu kila mkao ninaokaa, sikutegemea kama nitaondoka nikiwa hai sehemu ile.
Wakati tumelazwa kifudifudi, mwanajeshi mmoja aliyekuwa karibu yangu aliniwekea buti lake juu ya shingo yangu na kuanza kunishindilia kwa nguvu zake shingoni. Nilipopiga kelele kwa maumivu na kukosa pumzi, aliniambia, “Wewe gaidi, nyamaza kimya.”
Shingo yangu hadi sasa naandika makala haya haiwezi kugeuka kulia wala kushoto kwa ukamilifu pamoja na tiba ya viungo (physiotherapy) ya muda mrefu. Tindi zinazofanya kazi sehemu ya shingo zimepishana kusiko kawaida, nyengine zikizidi nyuma na nyengine zikizidi mbele.
Miongoni mwetu walikuwemo wanawake watano kati yao ni wadogo wasiozidi miaka 20. Hawa, bila huruma au kujali jinsia yao, walivunjwa vunjwa na kukaa walemavu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Pia, watesi wetu walidhamiria kuwadhalilisha kijinsia mbele yetu wakati wa uvamizi pale Mazsons Hotel. Askari mmoja alimwendea mtoto mmoja wa kike na kumuagiza avue nguo zake zote.
Kwa sababu walifyatulia risasi taa zote, na kelele za piga piga lilidumu kwa muda mrefu, na kila mmoja wetu alikuwa katika taharuki yake, sikufahamu tena muendelezo wa kitendo kilichokuwa kinaendelea kati ya askari huyo na huyo binti, kama aliweza kumbaka au la!
Sakafu yote katika horofa tuliyofanyiwa uhalifu huu ilitapakaa damu zetu kila upande. Mateso ya Mazsons Hotel yalidumu kwa takriban saa tano, kuanzia saa nne usiku hadi kiasi ya saa tisa usiku. Mara baada ya kumaliza kutuadhibu kwa kiasi walichopenda pale Mazsons Hotel, watesi wetu wakatufunga mikono nyuma na vitambaa vya macho.
Hapo sasa wakatuamrisha tutoe kila kitu tulichokua nacho na tuwakabidhi ikiwa ni pamoja na simu za mikononi na fedha taslim. Binafsi nilikuwa na kiasi cha Sh1,200,000 mfukoni. Pesa hizi ni msahara wangu ambao nilikuwa nimetoka kuuchukua benki na pesa za malipo kwa baadhi ya shughuli za uchaguzi za ACT-Wazalendo nilizokuwa nikizisimamia.
Pesa hizi walizotupokonya pale Mazsons Hotel hatukuziona tena hadi leo. Jeshi la kufanya uvamizi kama huu, kuwavunja vunja watu wasio na hatia, waliokuwa hawakugoma kukamatwa na baadaye kuwapora, linaweza kuwa ni jeshi lenye upekee hapa duniani.
Safari kuelekea Gereza la Hanyegwa Mchana
Baada ya kukamilika kwa mateso ya uvamizi pale Mazsons Hotel, yalifuata mateso ya kutusafirisha kutupeleka katika Gereza la Hanyegwa Mchana, Wilaya ya Kati, Unguja. Tukiwa hivyo tulilazimishwa kutembea kuelekea yalipo magari ya kijeshi ambayo hatuyaoni na kila aliyekosea muelekeo alipigwa rungu moja baada jengine mpaka alipofanikiwa kuligusa gari.
Kazi ya kuyapanda magari makubwa ya kijeshi huku tukiwa hatuoni na tumefungwa mikono nayo ilikuwa sehemu muhimu katika mateso yetu. Unalazimishwa uruke na utue katika kingo za gari la kijeshi kwa tumbo lako au kifua na ujiingize katika gari kwa kujisukumiza na kujiviringisha.
Zoezi la kupanda gari la wafungwa lilikuwa gumu kwetu sote hivyo tulijikuta tunaruka na kuanguka chini mara kadhaa huku tukiangukiana vifuani na vichwani na kuumizana wenyewe kwa wenyewe. Halkadhalika, kila aliyeshindwa kuingia katika gari wakati akiwa anahangaika kupanda alikua anapigwa rungu ili kumuhimiza kuingia katika gari.
Wengi wetu tulijikuta tunaanguka chini ya gari na kunyanyuka mara kadhaa bila kufanikiwa kupanda. Baadhi yetu mwishowe waliweza kujiingiza garini kwa mateso makubwa huku wengine wakikamatwa na wanajeshi na kulengwa katika gari kama viroba.
Ndani ya gari tulikaa mkao wa mateso na maumivu makubwa. Tulikuwa wengi na gari ilikuwa ndogo kwa mateka 40. Tulilaliana kama viroba vya viazi kila mmoja akimkalia mwenzake ama kichwani, tumboni au kifuani.
Kila mmoja alikuwa anapiga kelele za maumivu angalau aweze kupata msaada wa kubadili mkao ndani ya gari hilo lakini hakuna mtesi aliyejali. Ukipiga kelele kusema “Afande naomba nisaidie amenikalia kichwani huyu,” unajibiwa, “Wewe nyamaza,” huku anakupiga mkono wa bunduki.
Pamoja na kwamba Hanyegwa Mchana siyo mbali sana kutoka mjini safari yetu ilichukua zaidi ya dakika 45. Nadhani njia zilizotumika zilikuwa za mzunguko sana ili kutufanya sisi tusiweze kujua sehemu halisi tunapopelekwa.
Tukiwa ndani ya gari la wafungwa tuliendelea kufungwa mikono kwa nyuma na vitambaa vyeusi machoni katika safari yote ya kuelekea gerezani.
Muonekano wa nje wa Gereza la Hanyegwa Mchana ambalo mwandishi wa makala haya alikaa kwa muda wa siku nane: Jumatano, Oktoba 28, 2020, hadi Jumatano, Novemba 4, 2020. “Siku nane hizi tuliziona sawa na mika nane kutokana na ukubwa wa mateso tuliyokuwa tukipewa.” PICHA | KWA HISANI YA MWANDISHI
Kuwasili gerezani
Tulifika gerezani Hanyegwa Mchana kiasi cha saa tisa usiku. Hapo tulitenganishwa na wanawake na hatukuwaona tena hadi siku ya kuachiwa. Tulidhalilishwa kwa kulazwa kwa matumbo yetu sakafuni ndani ya uzio wa gereza bado tukiwa na maumivu na vidonda vya mateso ya Mazsons Hotel na bado tukiwa tumefungwa vitambaa vya macho na mikono ikiwa imefungwa kwa nyuma.
Waliendelea kutupiga mateke na mikwaju. Hapa ndiyo kwa mara ya kwanza nilimuona Nassor Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), ambaye tulikamatwa pamoja naye. Mazrui alikuwa pembeni yangu anapata mateso ya aina yake. Watesi wake walikuwa wanampiga na hata kumpandia mgongoni.
Alikuwa anapiga mayoe akisema, “Wanangu basi tena, mtaniuwa, mimi ni mgonjwa.” Wale watesi walikuwa wanamcheka na kumwambia, “Wewe si ulituita wasenge pale katika uwanja wa Mnazi Mmoja? Basi leo utatuona wasenge.”
Katika chumba cha gereza alichoingizwa, Mazrui, sasa Waziri wa Afya wa Zanzibar, muda wote alikuwa akisikika akipiga mayoe na kulia kwa ukali wa mateso waliyokuwa wanampa mchana na usiku. Kwa kweli siwezi kuyasimulia kwa ukamilifu mateso waliyompa Mazrui.
Baada ya hapo walitufungua mikono na kutuondolea vitambaa vya macho. Tulitakiwa tuvue nguo zote na tubakishe zile za ndani tu. Baadaye tukaingizwa katika vyumba vya gereza. Hatukujua tupo wapi kijiografia, ila tulifahamu tupo gerezani. Tulilala katika sakafu yenye baridi kali.
Usiku mzima tulikuwa tunatetemeka kwa baridi kali kwa muda wa siku zote nane za maisha ya gerezani. Ndani ya chumba cha gereza tuliwakuta wenzetu kiasi 30 hivi wakiwa wameshatangulizwa humo kutoka maeneno mbali mbali ya Unguja kutokana na visa vya uchaguzi.
Baada ya kuchangayika na sisi, tulifikia idadi ya watu 65 hivi kwa jumla ndani ya chumba hicho kimoja cha gereza.
Maisha, mateso gerezani
Tulikaa gerezani hapo kwa muda wa siku nane, yaani kuanzia siku ya Jumatano, Oktoba 28, 2020, hadi Jumatano, Novemba 4, 2020. Siku nane hizi tuliziona sawa na miaka nane kutokana na ukubwa wa mateso tuliyokuwa tukipewa.
Picha inayoonesha mgongo wa mwandishi wa makala haya ukiwa na majeraha yaliyotokana na vipigo kutoka kwa watesaji. PICHA | KWA HISANI YA MWANDISHI
Ni sawa tu na yale tunayoyasoma vitabuni ya Kwa Bamkwe katika zama za Mapinduzi. Tuliwekewa ratiba maalum ya kupigwa na kuadhibiwa kwa kila siku. Tulikuwa tunapigwa mara mbili kwa siku. Mara moja ni kabla ya kunywa chai ya asubuhi na mara ya pili ni kiasi saa tisa hivi baada ya chakula cha mchana.
Katika mara zote mbili, kiasi cha watesi 20 wenye sare za aina tofauti zilizofanana na zile za vyombo vya ulinzi vya Jamhuri ya Muungano na vikosi vya SMZ huingia ndani ya chumba chetu cha gereza wakiwa na bunduki, marungu, waya, vipande vya mbao na vipande vya nondo.
Hapo sote hutakiwa tukae mikao wanayotaka wao kama vile kulala kifudifudi na kusimama huku tukiegemea ukutani kwa tumbo kwa ajili ya kupigwa waya na marungu katika makalio na mgongoni.
Mkao mwengine ni kitako na kunyoosha miguu na kusimama kuegemea ukuta kwa migongo kwa ajili ya kupigwa vipande vya mbao na vyuma katika vifundo vya miguu na mikono. Walitupiga sana walitupasuapasua kwa kadri walivyopenda bila huruma na chumba cha gereza kilitapakaa damu ambazo tulikuwa tunazisafisha kila siku.
Walitaka watajiwe miongoni mwetu waliokuwa na dhamana ya kusimamia shughuli za kituo cha ujumlishaji matokeo pale Mazsons Hotel. Vijana wenzetu, kwa sababu ya mateso makali waliyokuwa wakiyapata na pengine wasipotaja wanapewa mateso zaidi, walitaja majina manne, likiwemo lile la kwangu.
Sisi wanne tulipata mateso maalum. Baada kipigo cha jumla kumalizika, tulikuwa tunaitwa sisi peke yetu na kupigwa upya. Wakati wanatupiga, walikuwa wakisema, “Nyinyi ndiyo wakuu wa uchakachuaji wa uchaguzi wetu. Sisi tunachagua Rais wetu, nyinyi mnabadilisha.”
Mateso wakati wa mahojiano
Gerezani kuliendeshwa zoezi la mahojiano pia. Wakati wa kupelekwa na kurejeshwa katika chumba cha mahojiano tulifungwa vitambaa vya macho na mikono nyuma. Tulilazimishwa kutembea kichura tukiwa hatuoni mbele huku tunapigwa waya na marungu mpaka tunafika katika chumba cha mahojiano.
Ndani ya chumba cha mahojiano tulikuwa tunatakiwa kukaa kitako na kunyoosha miguu kuwaelekea maafisa walioonekana kuwa ni wa usalama kiasi ya ishirini hivi ambao ndiyo walikuwa wanatuhoji. Kabla ya mahojiano walitufunguwa kitambaa cha macho na kamba za mikono.
Maafisa hao ambao hawakuziba nyuso zao na ambao wengine tunawatambua walikuwa wanatuuliza maswali kwa kipindi kisichopungua saa moja. Maswali yao ni mengi lakini ukiyatathmini utagundua walikuwa wanalenga kubaini mambo yafuatayo.
Mosi, pamoja na uchaguzi wote kuharibiwa na mawakala wa upinzani kupigwa na kufukuzwa katika vituo vya kuhesabia kura, ni kwa vipi matokeo ya uchaguzi yaliweza kuwafikia ACT-Wazalendo?
Pili, ni akina nani walioko ndani ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ambao wanashirikiana na ACT-Wazalendo wakati kwa uchaguzi huu hakuna afisa yoyote mwenye mafungamano na chama hicho?
Tatu, matokeo ya uchaguzi ambayo mwanaharakati anayejulikana kama Kigogo kwenye mtandao wa Twitter alikuwa anayatoa yalitokana na ACT-Wazalendo kupitia kituo chao cha kujumlishia? Na kama ndiyo ni akina nani ndani ya ACT-Wazalendo walikuwa wakifanya kazi na Kigogo?
Nne, maafisa hao walikuwa na dhamira ya kutushawishi na kutulazimisha tukubali uongo kwamba pamoja na kazi ya kujumlisha matokeo tuliyokuwa tunaifanya, Mazsons Hotel pia ilikuwa ni kituo cha ACT-Wazalendo cha kuhifadhia mabomu.
Wakati wa mahojiano, maafisa wa usalama walitulazimisha tutoe majibu wanayoyataka wao na kama hatukufanya hivyo tulikuwa tunapata mateso mwanzo hadi mwisho wa mahojiano.
Wakati mahojiano yakiendelea, mtesi aliyevalia kijeshi, mwenye bunduki, rungu, alikuwa amesimama nyuma ya mhojiwa kwa ajili ya kupokea amri ya kupiga. Askari huyu alikuwa akitupiga mgongoni na katika nyayo za miguu kwa marungu bila huruma.
Baada ya mahojiano kumalizika tulikuwa tunalazimishwa kujaza fomu ya mashtaka ambapo tulipewa mashtaka ya uongo ya kukutwa na mabomu.
Kutoka gerezani
Baada ya CCM kumaliza kufanya walichokusudia kufanya na Rais kuapishwa, sisi mateka wa uchaguzi sote tulitolewa magerezani huku hali zetu za afya zikiwa ni mbaya sana. Kwa juhudi za ACT-Wazalendo na familia zetu tulianza matibabu ya awali katika hospitali mbali mbali, za hapa Zanzibar na zile za Bara.
Kati yetu wapo waliopata athari za kudumu katika miili yao kama vile kusumbuliwa na uti wa mgongo, macho, kichwa, miguu nakadhalika. Baadhi yetu hadi sasa hatukupata matibabu ya uhakika ya kuondoa athari hizo kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Siku ya kuachiwa huru, kuna maafisa walikuja katika chumba chetu cha gereza na kutuonya. Walitueleza kuwa tusikubali kutumiwa na Marehemu Maalim Seif kwa sababu yeye hawezi kukamatwa, kwamba analindwa na itifaki za kidiplomasia za kimataifa, hivyo tutakaouliwa ni sisi.
Walitusisitiza kuwa baada ya kutoka gerezani tukae kimya na yeyote atakayethubutu kufungua mdomo wake atarejeshwa gerezani.
Ahadi hewa za fidia za Mwinyi
Baada ya uhuni ulioitwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kumalizika, sisi wahanga tukiwa bado tuko vitandani na hospitalini tulipata taarifa kwamba Rais Hussein Mwinyi alimwita Marehemu Maalim Seif kuzungumza naye juu haja ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kutibu vidonda vilivyotokana na Uchaguzi Mkuu.
Maalim Seif, kwa uungwana wake na kwa kuweka maslahi ya taifa mbele na baada ya kushauriana na viongozi wenzake na wanachama walioridhia wito huo wa Rais Mwinyi, aliitikia wito huo na ACT-Wazalendo kikafanya uwamuzi wa kuingia katika SUK.
Hata hivyo, Marehemu Maalim Seif aliwekeana makubaliano kadhaa na Rais Mwinyi kabla ya kukubali kuingia katika SUK ili kuridhiana na kusameheana yaliyotokea na kusonga mbele. Baadhi ya makubaliano hayo ni yale yanayotuhusu moja kwa moja sisi wahanga wa mateso yaliyotokana na uchaguzi mkuu.
Marehemu Maalim Seif na Rais Mwinyi waikubaliana wahanga wa mateso na udhalilishaji katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 walipwe fidia na Serikali. Kwa masikitiko makubwa sana, suala hilo la ulipaji fidia halijatekelezwa mpaka wakati wa kuandika makala haya.
Watanzania wanaona
Fidia ilipwe au isilipwe, ni muhimu kwa CCM na Serikali yake kutambua kwamba Watanzania hawapo mbali na dunia na wanaona kila kinachoendelea ulimwenguni kote. Upole, ukimya na uungwana wa Watanzania haumaanishi uzembe au woga bali una mshindo mkubwa.
Utulivu na uvumilivu wa Watanzania haumaanishi wao ni wanyonge na ambao wanaweza kutawalika kwa mabavu milele. Ipo siku wanaweza kusema hapana na nchi yetu ikaingia katika maafa makubwa.
Watawala hawana budi wajitafakari kama bado wanahitaji kuendelea kuendesha nchi kwa kutumia gereza na mtutu wa bunduki. Dunia inabadilika kwa kasi katika kila nyanja inayogusa maisha ya mwanadamu, hivyo na Tanzania inalazimika kufuata upepo huo wa mabadiliko.
Tanzania ijifunze kutoka hata kwa jirani zetu kama Kenya badala ya kubaki na kung’ang’ania ukiritimba na ubabe katika kuongoza nchi.
Ninazipongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuanzisha mchakato wa mazungumzo na vyama vya siasa sambamba na kuanzisha mchakato wa kutafuta maoni yenye dhamira ya kufanya mabadiliko ya mifumo ya kisheria na kidemokrasia ndani ya nchi yetu.
Ninaunga mkono juhudi hizi na ninaiomba sana Serikali iweke udhati wa kutimiza dhamira hii ili tuweze kupata mabadiliko ya Katiba, sheria na mifumo ya kidemkrasia itakayoiweka nchi yetu pahala salama zaidi na kuepusha migogoro siku za usoni.
Ahmed Omar kwa sasa anafanya kazi kama msaidizi wa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Juma Duni Haji. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia eddyommy@gmail.com au kupitia Twitter kama @ahmed_omar80. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.