The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Zanzibar Yaimarisha Ulinzi Kufuatia Taarifa za Vijana Kutoweka Katika Mazingira Tatanishi

Taarifa mpya zaibuka pia zinazoonesha uwezekano wa vijana wanaotoweka kurubuniwa kuhusu fursa za kazi Ulaya.

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Vyombo vya ulinzi na usalama visiwani hapa vimeanza operesheni maalum inayolenga kusambaratisha mtandao unaodaiwa kuhusika na utoroshaji wa vijana katika mazingira ya kutatanisha na kuacha familia zao zikiwa kwenye huzuni na majonzi makubwa.

Taarifa za mamlaka zinazohusika na usalama wa nchi kuanza kuendesha operesheni hiyo zinakuja siku takriban nne baada ya The Chanzo kuripoti kwamba makumi ya vijana kutoka Zanzibar wamepotea kwenye mazingira ya kutatanisha.

Katika taarifa hiyo, The Chanzo ilinukuu wazazi waliopoteza vijana wao na wake waliopoteza waume zao wakiziangukia mamlaka za nchi ziwasaidie kuwarejesha wapendwa wao ambao wanadhani kwamba wanaweza kuwa wamejiunga na vikundi vya kigaidi.

Taarifa hizo pia zinakuja ikiwa ni takriban wiki moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama – ikiwemo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji – kuingozea Zanzibar ulinzi, akisema visiwa hivyo ni “hatarishi” na ni rahisi kwa “usafirishaji haramu wa binadamu,” pamoja na uhalifu mwengine, kutokea.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, tayari watu wanaokadiriwa wanne wanaohusishwa na mtandao huo wamekamatwa visiwani hapa, huku msako mkali ukitajwa kuendelea.

“Tangu ile habari [ya The Chanzo] itoke maafisa [wa Jeshi la Polisi] wamehamanika,” kilisema chanzo chetu ambacho kilikataa jina lake kutajwa mtandaoni akisema yeye siyo msemaji rasmi wa Jeshi la Polisi. “Inaonekana kuna dhamira ya kutaka kukomesha hivi vitendo.”

Polisi visiwani hawakukubali wala kukanusha taarifa hizo huku Said Kondoro, Msemaji wa Kamishna wa Polisi Zanzibar, akisema Jeshi la Polisi litatoa taarifa kuhusiana na suala hilo muda muafaka ukifika.

Leo, Septemba 6, 2022, Jeshi la Polisi lilikuwa lifanye mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumzia “hali ya usalama” Zanzibar, lakini uliaghirishwa ndani ya dakika chache kabla ya kuanza bila ya kutolewa sababu zozote.

SOMA ZAIDI: Vijana Zanzibar Watoweka Katika Mazingira Tatanishi. Wazazi, Polisi Watoa Kauli Kinzani

Kwenye agizo lake hilo alilolitowa wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi mnamo Agosti 30, 2022, mkoani Kilimanjaro, Rais Samia alisema kwamba angetoa agizo hilohilo kwa Idara ya Uhamiaji siku akikutana na maafisa wake.

Tumepokea agizo

The Chanzo ilimuuliza Afisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Shariff Bakar Shariff kama chombo hicho kilicho na dhamana ya kushughulikia suala zima la uhamiaji kimeanza kuchukua hatua zozote zinazolenga kufanyia kazi agizo hilo la Amiri Jeshi Mkuu.

“Idara ya Uhamiaji imepokea maelekezo kutoka kwa Rais [Samia] juu ya kusimamia suala la kiusalama [visiwani hapa],” alisema Shariff wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika ofisini kwake Kilimani, Zanzibar. “Tayari maagizo hayo yameanza kutekelezwa kwa kuweka ulinzi mkali kwenye mipaka yote inayoizunguka Zanzibar.”

Ingawaje amekiri kusikia taarifa za vijana kutoweka kwenye mazingira ya kutatanisha, Shariff alisema kwamba mpaka sasa hawana taarifa zozote juu ya kuwepo kwa suala la usafirishaji haramu wa binadamu visiwani humo. 

“Hakuna kesi yoyote ya malalamiko juu ya kusafirishwa kwa watu kwa nguvu,” alieleza Shariff kwenye mahojiano hayo. “Wote waliosafiri, au kuondoka, wameondoka kwa hiyari yao. Maana mtu anaweza kutafuta hati ya kusafiria na huku akiwa na vielelezo vyote vya kwenda sehemu husika kwa kuonesha uthibitisho. Hiyo hatuwezi kusema ni usafirishwaji haramu wa binadamu.”

Kwenye uchunguzi wake, The Chanzo ilibaini uwepo wa mtandao unaowalenga vijana wenye umri kati ya 18 na 40 visiwani hapa, hususan wale wanaojihusisha na utumiaji wa mihadarati, kwa lengo la kuwasajili na kuwaunga kwenye vikundi vya kigaidi.

Familia zilitaja kubadilika kwa mienendo ya vijana wao kabla ya kutoweka, ikiwemo kuwa karibu sana na mambo ya dini, kitu ambacho hawakuwa nacho kwa siku za nyuma, kama ishara kwamba vijana wao wameondoka na kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Vijana wengine waliacha barua kwa ajili ya wazazi wao kabla ya kutoweka kusikojulikana, wakiwaambia wasihofu kuhusu wao na kwamba wataonana mbele ya Mwenyezi Mungu. 

Vijana wanarubuniwa?

Lakini siku takriban nne tangu The Chanzo ichapishe habari hiyo, taarifa mpya zimeibuka zinazoweza kuonesha kwamba siyo vijana wote wanaondoka Zanzibar wanafanya hivyo kwa kujua kwamba wanaenda kujiunga na vikundi vya kigaidi.

Wengine, The Chanzo imegundua, wanaweza kuwa wamerubuniwa kwa kuahidiwa kazi kwenye nchi za Ulaya, kama vile Poland. Abbas Salum* ni moja kati ya vijana waliowahi kukutana ana kwa ana na watu hao waliomuahidi kazi nchini Poland.

Salum, ambaye kitaaluma ni daktari, alikuwa tayari kusimulia uzoefu wake baada ya kusoma habari iliyochapishwa na The Chanzo. Anasema kwamba mnamo Novemba 2021, mfanyakazi mwenzake alimuambia kuhusu safari ya kwenda Poland kikazi. 

Salum anasema alishawishika na kazi hiyo ambayo aliambiwa mshahara wake kwa mwezi ulikuwa ni Dola za Kimarekani 1,000, sawa na Sh2,332,000. Lakini alipata wasiwasi baada ya mwenzake huyo kushindwa kujibu maswali mengi ambayo Salum alikuwa nayo kuhusu kazi hiyo. 

“Pia, nilipata hofu baada ya kuniambia kwamba hakuna gharama ambazo natakiwa kuchangia,” alieleza Salum. “Pia, nilipofanya utafiti nikagundua kuwa aina hio ya kazi hakuna huko Poland. Yupo daktari mwenzangu kutoka huko alikuja hapa [Zanzibar] nakumuuliza kuhusu jambo hilo na akaniambia hakuna aina hio ya kazi huko kwa sasa.”

Kuna shida sehemu

Salum anasema kwamba mfanyakazi mwenzake hayuko peke yake kwenye kuwarubuni watu kama yeye kwani aliwahi kwenda saluni siku moja na kusikia hadithi kama hizo, huku watu wanaorubuni vijana wengine wakiwa tofauti na yule mfanyakazi mwenzake.

“Nilijua kuna shida sehemu,” alisema Salum. “Inawezekana hawa watu wanawalaghai vijana kwa kuwaambia kuhusu hizo kazi za Poland.”

Shariff kutoka Idara ya Uhamiaji Zanzibar ametoa wito kwa wananchi wote kuripoti kesi yoyote inayowatia mashaka kwenye kituo cha polisi kilicho karibu nao ili kusaidia juhudi za kukomesha vitendo hivyo.

“Taarifa zote za kiuhalifu huanza kuripotiwa kwenye vituo vya polisi,” alisema Shariff. “Huko ndiyo sehemu sahihi ya kutoa taarifa. Iwapo suala linatuhusu sisi [Idara ya Uhamiaji] basi nasi hupata taarifa kutoka huko [polisi]. Ni muhimu watu wakatoa taarifa polisi.”

*Siyo jina lake halisi.

Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na makala haya, unaweza kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts