Dodoma. Kwa mujibu wa muhtasari wa taarifa ya mwenendo wa utolewaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini, iliyotolewa hapo Septemba 10, 2022, mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kuwa na asilimia nyingi ya wananchi waliokamilisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa hatari hadi kufikia Septemba 3.
Ukiongoza kwa asilimia 101.5, mkoa wa Dodoma, ambao ndiyo makao makuu ya nchi, unafuatiwa na Ruvuma ( asilimia 91.1) na Mwanza (asilimia 79.5).
Mkoa wa Rukwa, kwa upande mwengine, ndiyo unaongoza kwa kuwa nyuma kwa kuwa na asilimia 23.3 tu ya wananchi wake waliopata chanjo ya UVIKO-19, ukifuatiwa na Tanga (asilimia 31.2) na Manyara (asilimia 35.1).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoangalia kipindi cha kati ya Julai 23, 2021, na Septemba 10, 2022, asilimia ya wananchi waliokamilisha chanjo hadi Septemba 3, 2022, kitaifa, ilikuwa ni asilimia 58.92 tu.
Ripoti hiyo inakuja siku chache baada ya The Chanzo kufanya mahojiano maalum na Mratibu wa Huduma za Chanjo kwa mkoa wa Dodoma Francis Bujiku ili kufahamu sababu ya Dodoma kufanikiwa katika zoezi hilo.
“Ni ushiriki wa viongozi mbalimbali, tukianza na kiongozi wetu ngazi ya mkoa, ambaye ni Mkuu wa Mkoa,” alisema Bujiku wakati wa mahojiano hayo na The Chanzo yaliyofanyika hapo Agosti 29, 2022.
“Tumekuwa na vikao vya uhamasishaji katika ngazi ya mkoa vikihusisha pia wenzetu wa wilaya, ambapo Wakuu wa Wilaya wanakuwepo kwenye vikao,” aliongeza afisa huyo wa Serikali.
Bujiku aliongeza pia kwamba wao kama mkoa walihusisha wadau mbalimbali kwenye kuhamasisha watu kuchanja kama vile viongozi wa dini, waandishi wa habari na makundi mbalimbali ambao walisaidia kwa kiasi kikubwa kuelimisha kuhusu chanjo.
“Pia, tulikuwa tunatoa vyeti kwa wanaofanya vizuri,” aliendelea kufafanua Bujiku. “Kwa hiyo, wale ambao hawafanyi vizuri wanajitahidi, ili nao wapate vyeti wakati mwingine.
Kwa hiyo, kila siku tukishapata zile takwimu tunazichakata asubuhi, wanapewa viongozi wetu ngazi ya mkoa. Wanapeleka pia kwenye ngazi ya wilaya na halmashauri, wajione wamefanya nini na waeleze changamoto.”
Bujiku alieleza pia kwamba kama mkoa walitumia huduma ya mkoba ya kuwafuata watu katika maeneo yao ambayo ilisaidia watu kujitokeza kuchanja.
“Ukisubiri kwenye kituo ili uwapatie chanjo wakati mwingine wananchi wanashughuli mbalimbali za kiuchumi,” alibainisha Bujiku. “Kwa hiyo, wanakosa ile fursa ya kwenda kwenye vituo na vituo vingine viko mbali na makaazi yao. Kwa hiyo, sisi tulichofanya ni kuwafuata kwa kutumia huduma ya mkoba na huduma tembezi.”
Naye Afisa Programu Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Juliana Mshama aliiambia The Chanzo kwamba sababu ya Dodoma kuongoza kwenye uchanjaji wa chanjo hiyo ya UVIKO-19 ni kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu.
“Dodoma ni sehemu ambayo inamuingiliano sana,” alisema Mshama. “Sisemi kwamba kwa asilimia 100 hii ndiyo sababu lakini moja ya sababu ni kwamba hata kipindi cha maambukizi katika mikoa ambayo ilikuwa na athari Dodoma ni moja wapo ukilinganisha na mikoa mingine.”
Juliana alibainisha kwamba mikoa mingine kuna vikwazo vinavyosababisha mtu kushindwa kuchanja kama vile imani potofu, akisema kwamba watu wamekuwa wakipata taarifa zisizo sahihi kuhusu masuala ya chanjo hali inayopelekea watu kutojitokeza kuchanja.
Kwa mujibu wa muhtasari huo wa taarifa ya mwenendo wa utolewaji wa chanjo ya UVIKO-19 nchini, iliyotolewa hapo Septemba 10, 2022, hadi kufikia Septemba 10, 2022, jumla ya dozi 27,315,820 kati ya dozi 27,658,170, sawa na asilimia 99, zilizopokelewa zilikuwa zimesambazwa mikoani kwa matumizi. Dozi zilizotumika hadi Septemba 9 zilikuwa ni 24,536,514.
Idadi ya waliopata dozi kamili mpaka kufikia Septemba 10, 2022, kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni 18,570,560 kati ya watu 30,740,928, sawa na asilimia 60.41, huku lengo likiwa ni kuchanja asilimia 70 ya Watanzania wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea.
Hadi kufikia Septemba 10, 2022, pia, watu waliopata dozi kamili kwa Tanzania Bara ni 18,374,894 kati ya watu 59,517,754, sawa na asilimia 30.87 huku watu 246,734 kati ya 2,828,594, sawa na asilimia tisa, waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm hawakurudi.
Watu 476,827 kati ya 1,800,371, sawa na asilimia 26, waliotakiwa kurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer hawakurudi.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.