Zanzibar. Idadi ya watalii wanaowasili visiwani hapa imeripotiwa kuongezeka maradufu, hali ambayo inahusishwa na kupungua kwa vizuizi vya kusafiri ambavyo mataifa mengi duniani yalikuwa yameviweka kama sehemu ya juhudi za kupambana na ugonjwa hatari wa UVIKO-19.
Kwa mujibu wa takwimu ambazo The Chanzo imeweza kuzipata kutoka Kamisheni ya Utalii, taasisi ya Serikali ya Zanzibar yenye wajibu wa kuiwezesha na kuitangaza sekta ya utalii visiwani humo, idadi ya watalii waliowasili Zanzibar kwa miezi ya Aprili, Mei na Juni mwaka huu ni kubwa ukilinganisha na idadi ya watalii waliopokelewa katika kipindi hicho hicho mwaka 2021.
Kwa mfano, Zanzibar ilipokea watalii 13,839 tu mnamo Aprili 2021. Mwezi kama huo mwaka huu, jumla ya watalii 20,540 walipokelewa visiwani humo. Mnamo Mei 2021, ni watalii 9,280 tu ndiyo waliopokelewa Zanzibar. Mei 2022 ni watalii 20,450. Juni 2021, Zanzibar ilipokea watalii 20,416 wakati Juni mwaka huu jumla ya watalii 34,013 walitembelea visiwani hapa.
Mnamo Agosti 17, 2022, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) pia ilitoa ripoti iliyoonesha kwamba mpaka kufikia Julai 2022, jumla ya watalii 742,133 waliingia nchini ikilinganishwa na watalii 456,266 walioingia nchini katika kipindi kama hicho mwaka 2021.
Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka NBS Daniel Masolwa aliwaambia waandishi wa habari kwamba kati ya watalii hao 742,133, jumla ya watalii 222,449 waliingia Tanzania kupitia Zanzibar, akisema hiyo ni sawa na asilimia 30 ya watalii wote.
TAZAMA: Idadi ya Watalii Yaongezeka kwa Asilimia 62.7 Katika Kipindi cha Januari-Julai 2022
Kufuatia taarifa hizi, The Chanzo ilipata shauku ya kutaka kusikia kutoka kwa watu wanaofanya kazi kwenye sekta ya utalii hapa Zanzibar ili kufahamu kwamba takwimu hizi zinaendana na uhalisia wao.
Mnamo Septemba 27, 2021, The Chanzo ilizungumza na wafanyakazi kadhaa wa sekta ya utalii visiwani hapa ambao walieleza namna kuathiriwa kwa sekta hiyo na janga la UVIKO-19 kulivyoathiri maisha yao, hali iliyotokana na kufungwa kwa biashara pamoja na makampuni ya utalii na hoteli kupunguza wafanyakazi wao.
SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo UVIKO-19 Inavyoliza Wafanyakazi Sekta ya Utalii Zanzibar
The Chanzo iliamua kuwatafuta watu wale wale iliyoongea nao hapo Septemba 27, kuona kama maisha yao yamebadilika kwa namna yoyote kufuatia taarifa hizi za kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar.
Wote walikiri kwamba hali ya sasa ni tofauti sana na mwaka jana.
Mambo ni mazuri
Juma Mohammed, 28, anayefanya kazi ya kutembeza watalii, alizungumza na The Chanzo Septemba 2021 akiwa hajui hatma yake baada ya kupunguzwa kazini kutokana na athari za UVIKO-19. Mambo, kwa sasa, anasema ni mazuri. Anaeleza:
“Kwa sasa mambo ni mazuri. Kwanza, unabahati kunikuta hapa [Forodhani]. Nina zaidi ya mwezi sijaja hapa. Maana wageni ni wengi sana na kazi ni nyingi. Tangu Juni [2022] mpaka leo niko na kazi za kutembeza watalii.
“Mimi napata kazi nyingi kwa sababu nazungumza Kifaransa na hao ndiyo wageni wengi hapa Zanzibar. Sijaweza kurudi kwenye kampuni ile [iliyoniachisha kazi] kwa sababu wakati wa [UVIKO-19] niligundua ukiwa mtembeza watalii huru unapata sana pesa kuliko kuwa chini ya kampuni.
“Kwa takribani miaka mitatu ya kuwa mtembeza watalii, nilikuwa nikilipwa Sh450,000 kwa mwezi. Ila sasa safari moja ya kuwatembeza watalii wasiozidi 10, kwa masaa yasiyozidi sita, ni Sh35,000 kwa maeneo ya mjini na shamba ni Sh45,000.”
Kheri Bakari Kheri, 63, aliiambia The Chanzo hapo Septemba 2021 kwamba kazi ya utalii imekuwa ngumu visiwani humo kuliko kipindi chochote cha maisha yake. Kheri, baba wa watoto watatu, alianza kufanya kazi hiyo akiwa na umri wa miaka 19 tu.
“Saa hivi mimi ndiyo napanga bei maana kwenye makampuni wanabei za juu kidogo ila mimi, kwa sababu ya kujua lugha nyingi, basi napata kazi nyingi,” Kheri aliiambia The Chanzo kwa ufahari.
“Kwa kweli, wakati mwingine hata nyumbani sirudi,” aliendelea kuzungumza Kheri. “Na hapa nina simu nyingi za kazi ila huwa nawaambiwa sina nafasi kwa sababu ya wageni. Sasa bei zangu ni Sh55,000 mpaka Sh65,000 kwa safari moja. Mambo ni mazuri.”
Diana Bahati, 25, ambaye alikuwa miongoni mwa wafanyakazi waliopunguzwa kwa sababu ya UVIKO-19, na kulazimika kurudi nyumbani kwao Dar es Salaam, ameimbia The Chanzo kwamba kampuni yake aliyokuwa anaifanyia kazi na nyingine zimeweza kumtafuta ili arudi kazini.
Bahati anasema alirudi Zanzibar lakini alikaa kwa mwezi mmoja tu kabla ya kurudi jijini Dar es Salaam na kuendelea na biashara yake aliyoianzisha wakati wa UVIKO-19 na ambayo kwa sasa inafanya vizuri.
“Licha ya ofisi kunirudisha kazini ila nashukuru kwa sasa suala la kazi yangu ya mkono limesimama haswa, tofauti na nilipoanza,” alisema Bahati wakati wa mahojiano ya njia ya simu na The Chanzo.
“Mimi nauza sana shanga zangu kwa watu kwa sasa,” aliongeza. “Ila mambo yakikiwa sawa, nitarudi [Zanzibar] kuendelea na kazi.”
Tunakataa wageni
Hoteli ya Shangani ni moja kati ya hoteli mashuhuri visiwani hapa. Mnamo Septemba 2021, meneja wa hoteli hiyo Florence Ruwa alilamikia kukosekana kwa wateja, akisema, kwa mfano, kwa wiki wanaweza kuuza vyumba vitatu tu.
Hali hii ilipelekea matatizo mengi. Mbali na kupoteza mapato, Ruwa anasema pia walilazimika kupunguza wafanyakazi wao kutoka 20 na kubaki na saba tu.
The Chanzo ilirudi tena hotelini hapo wiki hii kutaka kusikia kutoka kwa Ruwa kama kumekuwa na mabadiliko yoyote, na hapa anaeleza mabadiliko yaliyotokea:
“Hali za uendeshaji, kwa upande wetu, zimerejea na tumeweza kuwarejesha kazini wafanyakazi wetu wote, wale 20, ambao tuliwapunguza kutokana na janga la UVIKO-19.
“Kwa mfululizo wa miezi mitatu, kuanzia Juni hadi sasa [Septemba, 2022], tunajaza wageni hotelini mpaka tunakataa wageni kwa sababu hatuna pakuwaweka.
“Hali imerudi na biashara ni nzuri na wafanyakazi wamerudi na majukumu yanaendelea.”
Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.