Dodoma. Wakala wa Uagizaji Mafuta Pamoja (PBPA) umesema kwamba hatua ya Serikali kutegemea mfumo huo katika uingizaji wa nishati hiyo muhimu nchini umeisaidia sana kuiepusha Tanzania na changamoto za ukosefu wa nishati hiyo inayohitajika kwa matumizi mbalimbali.
Haya yalielezwa hivi karibuni na Afisa Ugavi Mwandamizi kutoka PBPA, Sophia Kidimwa, wakati wa maonesho ya 19 ya Wahandisi Tanzania, yaliyofanyika mkoani Dodoma hapo Septemba 23, 2022. Maadhimisho hayo yalifanyika chini ya kauli mbiu isemayo ‘Ubunifu na Uendelezaji wa Ujuzi katika Kuimarisha Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Taifa: Mtazamo wa Kihandisi.’
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na The Chanzo pembezoni mwa maonesho hayo, Kidimwa alieleza kwamba kitendo cha Serikali kutumia mfumo huo kumefanya kiwango cha mafuta yaliyoingia nchini kwa matumizi ya ndani na nje kuongezeka.
Kwa mfano, Kidimwa alibainisha kwamba kwa kipindi cha kuanzia Aprili 2022, PBPA ilipokea wastani wa lita milioni 816 kwa mwezi, ambapo wastani wa asilimia 45 ni matumizi ya ndani ya nchi na wastani wa asilimia 55 ni matumizi ya nje ya nchi.
“Kwa sababu tayari tunaratibu uletaji wa mafuta, na tunaweza kujua mahitaji ya mafuta kwa mwezi, na tunapanga zabuni zetu kila mwezi, kwa hiyo mafuta ya miezi miwili ijayo tayari yanakuwa kwenye bomba.
“Kwa hiyo, kama leo ni Agosti, tayari tunajua mipango ya mafuta ya mwezi huo. Kama leo ni Septemba, tayari tuna mipango ya Septemba. Kwa hiyo, kila wakati sisi tunakuwa kwenye mchakato wa mafuta kuingia.
“Kwa hiyo, hata kama itatokea changamoto hapa katikati ni rahisi kuyaita mafuta ambayo yatakuja Oktoba kuyaambia yawahi,” alisema Kidimwa ambaye kitaaluma ni mhandisi.
Mfumo wa uagizaji mafuta wa pamoja ulianzishwa mwaka 2011 baada ya Bunge kupitisha Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 pamoja na kanuni za uagizaji wa mafuta kwa pamoja. Mafuta yanayoagizwa kupitia mfumo huo ni dizeli, petroli, mafuta ya ndege na mafuta ya taa.
Kidimwa aliiambia The Chanzo kwamba tangu kuanzishwa kwa mfumo huo, Tanzania imepata mafanikio mbalimbali, ikiwemo nchi kuwa kitovu cha biashara ya mafuta kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Kumekuwa na ongezeko la kiwango cha mafuta yanayopita kwenye bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara kwenda nchi jirani na hivyo kupata unafuu kwenye gharama za uletaji wa mafuta. Nchi zinazopitisha mafuta katika mfumo huu ni Rwanda, Burundi, Zambia, DRC Congo, Malawi na Uganda.
“Pia, kumekuwa na kupungua kwa gharama za uagizaji wa mafuta na kudhibiti mfumuko wa bei za mafuta nchini.
“Na pia, tumeweza kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa. Kumekuwa na kuongezeka kwa mapato ya kodi pia yatokanayo na bidhaa za mafuta,” alieleza Kidimwa.
Afisa huyo mwandamizi alieleza pia kwamba matumizi ya mfumo yamesaidia kuokoa wastani wa dola za Marekani milioni 413.20, sawa na takribani Shilingi bilioni 961.15, kila mwaka. Pia, kumekuwa na kupungua kwa gharama za meli kusubiri kushusha mafuta.
Kwa mfano, kabla ya mfumo huo kuanza kutumika, gharama za kusubiri zilikuwa ni wastani wa dola za Marekani 45 kwa tani, ambapo ukilinganisha sasa gharama za meli kusubiri ni wastani wa dola za Kimarekani 2.5 kwa tani.
Lakini pia, nchi ilikuwa ikikumbana na changamoto ya kukosekana kwa mafuta kwa kuwa mfumo uliokuwepo ulitoa nafasi kwa wafanyabiashara kuagiza nishati hiyo mmoja mmoja kwa wakati ambao anaona unafaa kutokana na mahitaji yake.
“Mfumo huu pia umerahisisha kudhibiti ukwepaji kodi katika mafuta yanayoingia nchini na kusaidia kupatikana kwa takwimu sahihi za mafuta yaliyoingia nchini na yanayotarajia kuingia nchini, hivyo kuwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati,” Kidimwa aliiambia The Chanzo.
“Mfumo umeondoa vikwazo katika uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa kuweka usawa wa mazingira ya kufanya biashara pamoja na kuimarisha udhibiti wa upotevu wa mafuta wa upokeaji kutoka kwenye meli kwa kuendelea kuboresha taratibu za ukaguzi na usimamizi,” aliongeza afisa huyo.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.