The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ras Inno: Hatutungi Nyimbo Tukaziimbe Rumande

Mwanamuziki huyo anaelezea A-Z ya sakata zima la yeye kuwa mikononi mwa polisi baada ya kufananishwa na mtuhumiwa mwengine.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa miondoko ya reggae nchini Tanzania Innocent Richard Nganyagwa, maarufu kama Ras Inno, amesema kwamba atachukua hatua dhidi ya askari aliyemlazimisha aimbe akiwa rumande, akisema kwamba kazi yake siyo kutunga nyimbo ili aende akaimbe rumande.

Ras Inno alisema hayo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hapo Septemba 17, 2022, yaliyolenga kufahamu sakata lake la kukamatwa na polisi akiwa mkoani Iringa baada ya polisi kumfananisha na mtuhumiwa mwingine.

“Lazima tutalipana,” Ras Inno aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. “Studio nalipa mimi. Jukwaani watu wanalipa kuniangalia. Siwezi nikamuimbia askari. Hatutungi nyimbo tukaziimbe rumande. Tutakapofika kwenye hatua za mbele, [yule askari] atalipa zile nyimbo mbili nilizomuimbia.”

Siku hiyo ya Agosti 30, 2022, Ras Inno alikamatwa akiwa anafanya mazoezi nyumbani kwake, na kupelekwa kituo cha polisi ambako alidai kuteswa, kunyanyaswa na kubaguliwa. Baadhi ya vitu alivyofanyiwa ni pamoja na kupigwa ngumi ya mdomo, kulazimishwa aimbe na kutishiwa kunyolewa rasta zake.

Yafautayo ni sehemu ya mazungumzo hayo yaliyofanyika katika studio za The Chanzo zilizopo Msasani, Dar es Salaam. Endelea …

 

The Chanzo: Bwana Ras Inno, asante sana. Labda kwa kuhofia, naweza nikawa sijazungumza vizuri, au sijakutambulisha vizuri kwa watazamaji wetu. Labda pengine kwa ufupi ungetuambia Ras Inno ni nani kwa ufupi?

Ras Inno: Mimi kwa jina kamili naitwa Innocent Richard Nganyagwa, [hilo] ndiyo [jina] lliipo kwenye vyeti na vitu vingine. Jina ninalofahamika zaidi ni Ras Inno Nganyagwa kutokana na muziki. Mimi nafanya muziki wa reggae. [Mimi] ni miongoni mwa wanamuziki wa awali kabisa wa muziki wa reggae nchini.

Lakini nje ya kufanya muziki, mimi nilijiongeza zaidi ya kufanya muziki. Kama hivyo mimi ni mtafiti wa masuala ya jamii naitwa mwana anthropolojia. Mimi ni mshauri wa kitalaam wa muziki. Lakini pia ni mtangazaji wa vipindi redioni. Nafanya vipindi katika redio ya Kiingereza iliyoko chini ya Shirika la Utangazaji la Taifa [TBC], inaitwa TBC international. Mimi pia ni jaji mzoefu wa mashindano ya kusaka vipaji. 

Lakini mimi ni Katibu wa Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT), [mtandao] unaojumuisha utetezi wa masuala ya haki za wasanii kupitia sheria zinazoendesha sanaa. Pia, ni Katibu wa mtandao wa wanamuziki unaitwa TAMUNET, na ni mshauri mkuu wa chama cha wanamuzuki wa reggae na Dancehall Tanzania kinaitwa KOREDA. Kwa kifupi, naweza kujitambulisha hivyo. 

The Chanzo: Umevaa kofia nyingi sana kusema ukweli. Na hiyo inapelekea moja kwa moja kwenye swali langu. Inawezekana vipi kwa mtu kama wewe, kwenye nafasi yako, mwanamuziki ambaye unajulikana, mtangazaji wa radio, inawezekana vipi polisi kukukamata kwa kudai kwamba wamekufananisha na mtuhumiwa mwingine? Labda kwa namna yoyote pengine ilikushangaza labda? Ilikushtua? Ulijisikiaje labda kuona kwamba polisi wanakukamata kwa kukufananisha na mtuhumiwa mwingine?

Ras Inno: Sikujisikia vizuri. Kwa sababu waliponikamata nilichokuwa nakifanya ni kitu ambacho nimekuwa nikikifanya tangu mwaka 2019. Kwa sababu mwaka 2019 nilipata maradhi yaliyotishia mimi kupata ugonjwa wa kiharusi. Kitalaam, kitabibu, [huo ugonjwa] wanaita peripheral neuropathy, yaani kutikisika na kuyumba kwa mfumo mkuu wa mshipa ya fahamu unaotoka chini ya kisogo unaenda kufuata uti wa mgongo. 

[Ugonjwa huu] ulipelekea upande wa kulia wa mwili usiwe na hisia, nisiweze kusikia [hisia]. Sasa, moja kati ya vitu ambavyo nilishuriwa kwenye tiba, mojawapo, vilikuwa vinne, [moja wapo] ni kufanya mazoezi ya mwili. Kwa hiyo, tangu 2019 nafanya mazoezi na nimepunguza idadi tu kwa sababu wakati fulani maungo yalikuwa yanauma, niliporudi tena kwa daktari wangu akasema mazoezi yanaenda na umri, punguza kiwango cha mazoezi. 

Kwa hiyo, nikiwa pale nyumbani kwangu, kitongoji cha Ndiuka D, kata ya Igumbilo, mkoani Iringa, manispaa ya Iringa, pale mjini, wakazi wote na majirani wanaonizunguka wanafahamu kwamba mimi huwa nafanya mazoezi. 

Kwa sababu Iringa ni sehemu ambayo naenda mara nyingi kwa sababu za kifamilia na sababu zangu nyinginezo. Ukichukua idadi ya siku ambazo naishi Iringa, ukizikusanya, ukazijumuisha kwa pamoja, inatimia miezi sita. 

Kwa hiyo, ina maana mimi miezi sita huwa sipo katika hili jiji [hili la Dar es Salaam]. Kwangu ilikuwa ni mshituko mkubwa.

The Chanzo: Kwa hiyo, walikuja saa ngapi asubuhi? 

Ras Inno: Asubuhi ile nilianza mazoezi saa 11:07, wao walikuja saa 11:17. 

The Chanzo: Na kwa hiyo, walikuambiaje labda walipofika? 

Ras Inno: Wakati wanakuja na gari yao, mimi nilikuwa natokea upande wa mwisho wa ukuta, narudi upande wa kuelekea barabara. Waliponiona, walisimamisha gari. Waliposimamisha gari, wakashuka, nikamsikia kulikuwa askari wa kike anasema ndiyo huyo huyo. Mimi nikajiuliza ndiyo nani? 

Wakaja wakanisalimia, tena nakumbuka walinifuata wakasema Ras vipi? Nikamjibu safi. Akanambia kwa nini uko hapa? Nikamuambia nafanya mazoezi. Kwa nini unafanya hapa? Nikamwambia ni nyumbani mimi naishi nyumba hii. Wakasema twende kituoni, nikauliza kufanya nini? [Wakajibu] wewe twende kituoni usiwe mbishi.  

Nikawaambia mmenikuta nafanya mazoezi, niko nyumbani kwangu, nikawaambia naomba nichukue simu, ilikuwa juu ya dirisha. Wakasema simu tutakuchukulia. Wakachukua simu, wakatia mfukoni. Nikawaambia basi naomba nimuage mke wangu, wakanikatalia. Wakasema wewe unaleta ubishi, wakanifunga pingu pale pale nyumbani. 

Nikasema sawa, naomba nimuage mjumbe wa Serikali ya Mtaa. Kwa upande niliokuwa naongea nao nimetazamana nao ni mgongoni kwangu, yaani ni mahali nyuma tu ya mgongoni kwangu hatua tano. Wakakataa. Nikasema naomba nimuage mama wa jirani ambaye anakaa nyumba ya pili kutoka nyumba yetu kutoka kwenye kona ya barabara, napo wakakataa. 

Wakaniamrisha kuingia kwenye gari. Gari ile ina nafasi kwa nyuma, wangeweza kuniambia nipite kwa kule nyuma lakini wakanilazimisha, kuna ngazi ya pembeni, nikapanda. Sasa kukawa na amri zinazokinzana. Mmoja anakuambia chuchumaa, mwingine [anakwambia] simama, mwingine kaa chini. 

Wakawa wananiambia nijiburuze kupitia chini ya kile kiti nitokee upande wa pili. Nikawaambia mimi hali yangu siyo nzuri na ndiyo maana nalazimika kufanya mazoezi. Hawakutaka kusikia. 

Vitu vikanijia kichwani kwamba endapo nachukuliwa bila kuiambia familia yangu, na pia niliwatajia nina dada yangu ambaye anaishi pale, ikiwa hatupo pale yeye ndiyo ni kama anaangalia hiyo nyumba na anaishi na mume wake na mtoto. 

[Sasa hapo] sielewi hawa watu wana dhamira gani. Nafsi ikaniambia piga kelele. Nikaita neno ‘mama’ mara tatu. Nikaita jina Michael Honde, ndiyo huyo mjumbe wa Serikali ya Mtaa, mara tatu. Nikaita mama Sambara, anaitwa Imelda, maarufu zaidi wanamfahamu mama Elina mara tatu [nikaita]. 

Wale [polisi] wakasema unatupigia kelele unamuita mama yako atakuja? Nikawaambia mama yangu mzazi alifariki mwaka jana Agosti 6. Ila mimi mke wangu huwa namuita mama. Tena huyo askari ambaye ndiyo alikuwa mstari wa mbele akaleta kebehi. 

Kwa hiyo, mke wako unamuita mama? Nikamwambia we sijui kama una mke au huna lakini mimi mke wangu nikitaka maji namuambia mama nataka maji. Hivyo hivi ndivyo navyomuita. Kwa hiyo, gari ikaanza kutembea.

The Chanzo: Na wakati mnaelekea huko pengine hawakukupiga wala nini? 

Ras Inno: Mpaka hapo yule dada askari akanambia ili utokee upande wa pili nyoosha miguu. Kwa hiyo, nikanyoosha miguu. Akasema haya jiburuze. Nikiwa na pingu ukumbuke mkononi!

The Chanzo: Wamekufunga kwa nyuma? 

Ras Inno: Kwa mbele. Nikajiburuza, nikatokea upande wa pili. Sasa kwenye ile shule ya msingi kuna uwanja wa mpira. Gari likaenda, likasimama kwenye goli la magaharibi. Zile kelele nilizopiga zikasikiwa na watu. 

Kwanza, kuna mzee mmoja anaitwa Mzee Mzigilwa anakaa pale eneo la duka. Kuna mtu anaitwa Dauson karibu na duka lake akawa amesimama, akauliza vipi? Wakasema wewe mzee nenda kalale. Akaja mjumbe mwingine wa Serikali ya Mtaa. 

The Chanzo: Alikuja kwenye gari? 

Ras Inno: Ndiyo. Yaani gari lilisimama kwa sababu watu walikuja.

The Chanzo: Sawa!

Ras Inno: Akaja mjumbe mwingine anaitwa Jane Mlula. Akaja yule mjumbe Michael Honde akaja [na] mke wangu. [Polisi] wakawauliza mnataka nini? Michael Honde akauliza huyo mnayemchukua ni mwananchi wetu, ni raia mwema hana shida. [Polisi] wakasema mtamfuata kituoni. 

Wakamuuliza mke wangu wewe unataka nini? Akasema huyo ni mume wangu ana kawaida ya kufanya mazoezi. Sasa nikiwa mle ndani ya turubai, ukumbuke kwa nyuma kuna turubai, nikawa namuambia mama utakuja na vitambulisho hivi wakanambia nyamaza. 

Nikawambia siwezi kunyamaza kwa sababu watu wanaomchukua mtu kwa nia njema kwa sababu ya kwenda kumuhoji hawataikatalia familia yake isijue. Kwa hiyo, wale watu wakarudi kujiandaa kuja kituoni. Gari likageuka kuanza kuelekea kituo cha polisi mjini. Ndiyo vile vituko vilipoanzia hapo.

The Chanzo: Vituko gani?

Ras Inno: Kwanza walinihoji kwa nini wewe unakata watu mapanga halafu unakimbia? Nikawauliza mapanga gani? Huyo askari akaniuliza wewe hujapita darajani? Nikamuambia sijapita. Akasema una uhakika gani? Nikamuambia Iringa nimefika Agosti 6. Akaanza pale vibweka, [akisema] leo tutakukata nywele. 

Ukumbuke nilivyolazimishwa kupita chini ya kiti mguu huu ukawa umeumia goti, mguu wa kushoto, akanikanyaga mguu huu nikiwa na mchubuko hapa, akanipiga ngumi ya mdomo, akanivua kofia, akasema wewe unakuja huku unafanya uovu, unajificha ulifikiri hatutakupata? 

Nikamuambia mimi sijui hicho unachokisema. Sasa badaye akasema lazima tukukate nywele. Alikuwa ameshika kichuma fulani ambacho sina uhakika kama ni mkasi au vipi akawa anajaribu kufanya hivi. Nikamwambia hapana. [Akawa anasema] nitakupiga sijui nini, wewe si unajifanya mtu mzima? Akashika rungu. 

Wakati tunaendelea na ile gari tunapanda kwa sababu niko kwenye turubai sioni nje. Sasa mimi njia pekee ya kufanya nikasema hapa ngoja nisali. Mimi nina kawaida ya kusali kila mara ndiyo maisha yangu yalivyo. Alikuwa amevuka upande wa pili wa kiti. Wakanimulika na tochi. Wakasema wewe, unasema nini? Nyamaza! 

Nikamwambia mimi nasali. Wakauliza, huwezi kusali kimya? Nikaambia kusali kimya ni njia yako. Njia yangu mimi siyo kusali kimya kimya. Ndiyo vikafika vitisho vingine, akasema unajua hapa uko wapi? Ndiyo kwa kupitia kwenye turubai naona ile alama ya polisi ya pale kituoni. Nikaamrishwa nishuke. 

Kwa hiyo, nikashushwa kwa njia ile ile. Nikapata tena maumivu kwa sababu kiti chenyewe kiko kwa chini, ujibiruze. Nimeshuka [polisi] akawa ananitishia tena kunikata nywele. Nikamgeukia. Akasema twende. Nikafika nyuma ya kaunta ya polisi na pingu zangu, wakasema huyu tumemleta. 

Askari aliyekuwepo pale ambaye aliyeachiwa lindo au kituo sijui, yule dada akaanza kumsimulia kwa ufupi yule askari. Akaniuliza huyu tumemkuta hivi na hivi. Akaniuliza kwa nini unafanya mazoezi nyumbani? Nikamuambia mimi siku zote nafanya mazoezi nyumbani. Kwa nini usifanyie kule barabarani kwenye maduka? Nikamuambia huko ndiyo ningeonekana kabisa nina dhamira tofauti. 

[Wakauliza], kwa nini unafanyia mazoezi kwenye giza? Nikamuambia taa ya jirani ilikuwa inawaka, ile nyumba niliyokuwa nafanya mazoezi na ambayo mmenikuta haina umeme. Akasema kinachokulazimisha ufanye mazoezi nyumbani ni kipi? Nikamuambia maelekezo ya daktari wangu. Akasema kwa nini na ndiyo nini nikamuambia kwa sababu ya peripheral neuropathy.  

Akasema ni kitu gani? Sasa nilivyomuangalia kwa sababu alikuwa ni mtu anayekunyanyasa pasi na sababu na mimi niligundua uwezo wake kwenye lugha ni mdogo nikamjibu tena ni tilting of the main nerves system, akabaki ananiangalia. Aakaniuliza maana yake nini? Nikamtafsiria kwa Kiswahili. Akasema wewe unatokea wapi? 

Nikamuambia natokea Dar es Salaam. Akaniuliza, Iringa unafanya nini? Nikamwambia ni kwetu, mbona huwa nakuja hata miezi mingapi mara nyingi nakuja. [Akasema] sasa hatukuelewi  Dar es Salaam mbona nikijibu unajibu majibu marefu. Nikamuambia siwezi kukujibu jibu fupi kwa sababu peripheral neuropathy ndiyo inavyoitwa, nikikujibu kwa Kiswahili kuyumba kwa mfumo mkuu wa mshipa wa fahamu ni sentensi.

Sasa wakasema tunataka tukuweke rumande lakini tukukate nywele. Nikauliza nywele zangu zinahusiana nini na kukamatwa kwangu? Kwanza mmenikamata kinyume na sheria. Wakaja tena askari, walikuwa watatu waliokuwa wananinyanyasa, yule wa kwanza na wengine wawili wakawa wananitishia kunikata nywele, wakashika kama vyuma hivi, nilikuwa nimefungwa pingu. 

Mimi nikainuka, wakaniuliza wewe selo gani uliona watu wanaingia hivi [na nywele]? Nikamwambia wewe kwanza we huna haki ya kuniingiza huku mpaka uniambie mimi nimefanya kosa gani. 

Yule dada akasema busara itumike, wakafungua ile pingu, nikaambiwa nikae chumba cha askari wapelelezi, chumba ambacho huwa kinatumika na askari wapelelezi kuandika maelezo. Basi nikajitaja jina langu. Wakachukua simu yangu wakaikabidhi pale, wao wakaondoka kwenda kutafuta watu wengine.

The Chanzo: Hiyo ilikuwa saa ngapi sasa saa 12? 

Ras Inno: Saa 12 hasa ilikuwa haijatimia kwa sababu mwendo haukuwa mrefu sana ni kama dakika 15 kutoka pale ni dakika kumi na tano hadi ishirini. Nikaenda, nikakaa kwenye kile chumba, wao wakaendelea na mambo yao, wakatoka na ile gari. Sasa kuna vitu pale pale nikasema lazima nivishike kichwani kwa ajili ya baadaye. 

Askari yule aliyechukua simu nilishika namba yake, nilisoma, sikuona zile herufi, lakini niliona namba yake na ile gari nilichungulia niliiona namba yake wakaondoka. Kwa hiyo, wakaniacha mimi nimekaa pale. Baadaye wakarudi, akaja yule yule askari aliyenitishia rungu, aliyenikanyaga, hapa akasema kuna neno wanasema yeye ni mkunda wa nini sijui yaani mchunga watu, nikasikia wenzake wanamuita jina Mussa. 

Akaniambia Ras wewe ni mtu mbaya. Nikamuambia ubaya wangu kitu gani? Akaniambia pale umeandikisha wewe ni mwanamuziki, niimbie nyimbo mbili. Nikamuimbia wimbo unaoitwa Gila, ndiyo wimbo ambao watu wengi sana wanaufahamu, ukiutaja tu Gila wanajua huyo ni mimi. Kuna wimbo mwingine unaitwa Tupendane.

Tena wakati naimba Gila akasema huo wa kihehe? Nikamwambia ndiyo. Akaniambia umesema wewe ni Katibu wa CINT, inashughulika na nini? Nikamtajia kirefu cha CINT akasema najua mambo ya intellectual property copyright. Alikisia nafikiri. Akaniambia nimtajie sababu tatu za kufuga natural dreds, yeye alitamka sababu tatu za kufuga Ras, nikamjibu. 

Akasema fanya mikono hivi, nikaweka. [Akasema] wewe [ni] mtu mbaya, umeua mtu na nini. Nikamwambia mimi nimeua mtu wapi? Na nikiwa pale nikawa nasikia kwa sababu kwenye gari walisema ulimkata mtu mapanga, lakini nikiwa pale nikawa nasikia nimekaa kwenye kile chumba baada ya kuondoka na gari kuna askari anaongea na simu sijui na radio call anasema sasa huyu mtu mwenyewe mnasema amekufa mbona hajafa, yupo.

Inaonesha mtu aliyepigwa mapanga walihisi amekufa lakini baadaye wakathibitisha kwa mawasiliano kwamba amejeruhiwa vibaya yuko wodini na ndipo nilipojua kwamba yule mtu ama anahusika na wao ama ni mmoja wao. Kwa hiyo, picha ikanijia kwamba kuna rasta mwingine huwa anafanya mazoezi daraja la kuvuka la chini la Kitanzini, hii jiografia kwa watu wanaoijua Iringa wanaijua vizuri sana, ana kikundi chake cha vijana wanaotembea na mapanga.  

Kwa hiyo, walimcharanga mtu mapanga lakini wasijue kwamba huyo mtu anahusiana na mamlaka za usalama, askari sijui, wanaitwa. Kwa hilo mimi nililifikiria nikalishika kichwani. Sasa baadaye kukawa kumekucha, akaja mke wangu, mjumbe Michael Honde, na kijana mwingine wa mambo ya ulinzi shirikishi anaitwa Frank. Akaja na dada yangu tulimpigia simu kwa sababu nilichukua simu ya mke wangu tukampgia anaitwa Zaina Nganyagwa akaja. 

Yule mjumbe alivyofika moja kwa moja kwa afisa mpelelezi wa wilaya pale kituoni, unapanda ghorofani akamueleza alichomueleza yule bwana, akaja pale akaniambia yule mjumbe wa Serikali unaitwa. Niakenda, nikahojiwa baadhi ya maswali, nikajibu, nikarudishwa pale pale miongoni mwake [mwa hayo maswali yalikuwa] Iringa umefuata nini? Kwa nini umekuja hapa, nakadhalika. 

Kutoka hapo wakatumwa vijana watatu wakaniita tukawa tumesimama nje ya mlango wa kituo, wakaniuliza ilivyokuwa, nikawajibu, wakaondoka mara ya tatu akaniita tena yule afisa upelelezi kipindi mara ya kwanza nilivyoenda mke wangu anasisitiza kuna askari alikuwa anamzuia asiingie, akafungua mlango akaingia yule afisa akamuuliza kwa nini umeingia hapa, akamuambia huyu ni mume wangu, ndicho alichomjibu. 

Lakini mara ya tatu yule akasisitiza niende peke yangu kabla ya hizo mara tatu nilizoitwa na huyu afisa upelelezi wa wilaya, yule askari aliyekuwa anafanya vituko vyake na vibweka vyake wakati huo kitambulisho changu kilikuwa kishakuja sasa kwa sababu nilimuambia mke wangu mama naomba uje na kitambulisho nikamuonesha kitambulisho kile la kwanza. 

La pili nikamuambia kwenye ile simu ukitaka kuhakikisha kama mimi ni mwanamuziki kuna nyimbo zangu, kuna video zangu kwa sababu mimi simu ni kama ofisi. Cha tatu nikamuambia kwamba ukitaka kuhakikisha mimi nafanya vipindi TBC International, kutoka kituo kile cha polisi cha pale sokoni Iringa mjini mpaka  jengo ambalo kuna ofisi ya TBC ya mkoa ni mita chache sana, ni kitendo cha dakika kumi, unafika, nenda kamulize dada anaitwa fulani ndiyo muakilishi wa TBC Iringa. 

Na nikija huwa ninatabia ya kupita ofisini yote haya hakutaka kusikiliza. Sasa hitimisho ikawa nilivyoenda kule kwa mara ya tatu niliulizwa maswali yale yale ambayo niliyafafanua, hususan suala la Iringa nakuja kufanya nini, nikamjibu Iringa ni kwetu kwa asili. Baba yangu ni mzaliwa, mkulia na alimalizia maisha yake hapa, alifia Iringa na akazikwa Iringa. 

Iringa nimesoma mwaka wa mwisho shule ya msingi. Iringa nimesoma sekondari. Iringa nilikuwa miongoni mwa vijana wacheza madisko maarufu na nikawataja mpaka watu ambao tulicheza madisko miaka hiyo wapo wengine mpaka sasa pale Iringa mjini. Nikamtaja mtu anaitwa Adam Manyata. Nikamtaja mtu anaitwa Hassan Ngoe. Iringa ndiyo nimezalia mwanangu wa kwanza. Nikamuambia Iringa ndiyo ukweni kwangu sasa hivi  nyumbani kwa wazazi wa mke wangu na cha mwisho nikamuambia Iringa ndiko nnakolima, akaniuliza unalima nini? Nikamuambia mahindi, alizeti [na] maharage. 

Kwa hiyo, nilimjibu hoja kumi kwa swali lake moja. Mwisho akasema mimi nachoona wewe hakuna chochote kinachoendelea uende tu. Hapo kushakucha  zaidi ya saa 12 [asubuhi] kwa sababu nakumbuka wakati wanataka kunitoa kwenye kaunta kunipeleka kwenye kile chumba saa niliyokuwa naangalia pale inasema saa 12. 

Nikaanza kusali siyo kwa kupiga kelele unaona tu mdomo kuna askari alikuwa amesimama upande wa pili wa kaunta akasema wewe unasema nini nikaambia nasali. Akaniambia kwa nini usali? Nikamuambia I pray by the clock. Kwa hiyo, ikifika 12 kamili nina aina ya sala lazima nisali. 

Basi wakasema ndiyo tunakuachia. Ndiyo nikarudishiwa simu yangu na nikaachiliwa kwenda nyumbani. Wale wajumbe na wakazi wengine wa kile kitongoji wakaenda njia yao sisi tukaenda mahali tu mimi, mke wangu, dada yangu baada ya hapo ndio nikarudi nyumbani. 

The Chanzo: Kwa hiyo, hii ilikuwa mara yako ya kwanza ya kukutana na vitimbi, kwa kukosa neno zuri zaidi, kutoka kwa polisi au ulishawahi kwenye maisha yako kukumbana na kadhia inayofanana na hii kwa namna moja au nyingine? 

Ras Inno: Niliwahi lakini siyo katika kiwango hicho, siyo kiwango cha kufungwa pingu, halafu ilikuwa ni jambo la kuzungumza, la kinyumbani ambalo walisema hili mkamalize nyumbani.

The Chanzo: Na labda hili sakata lote, kuanzia mwanzo pale wanakuja mpaka wanakuachia, wewe limekuachia mafunzo gani, limekuachia hisia gani labda kwa mtazamo wako?

Rass Inno: Cha kwanza ni kwamba ulikosekana umakini wa kufanya kazi kwa mujibu wa polisi wa katika kudhibiti usalama katika eneo lile, jambo la kwanza. Jambo la pili hamkani na hisia walizozibeba nafsini kwa sababu aliyecharangwa mapanga wananasaba naye ya kikazi ambayo mimi hainihusu kwa sababu muda inatokea kucharangwa mapanga nilieleza tarehe nilizokuwa pale Iringa na zina ushahidi. 

Jambo la tatu, hakutumia weledi kwa sababu kama mtu ameshajieleza mimi ni fulani, hapa nyumbani kwangu, zote unakataa, humpi nafasi ya kumsikiliza, unaponiuliza naumwa nini yaani nashindwa kuelewa. 

Sijui, mimi nafikiri kufikia kiwango fulani cha askari kwenda juu ndiyo wanaonesha weledi kwa sababu kama askari mpaka anafikia kiwango kile hajui mifumo ya kuongea lugha za kigeni, mimi naamini wanakwenda chuo, wanasoma, kwa hiyo nakujibu wa mujibu wa daktari wangu kwa sababu mimi ninaye daktari ndiye anayenitibu kila nikipata matatizo. 

Sasa hisia zilizoniijia ni kwamba, ninafikiri, kile kilichofanyika ni uhuni, yaani uhuni. Kwa sababu ziko njia za askari kushughulika na kazi yake na wana Police General Orders (PGO) siku hizi, wanajua. 

Na katika askari saba, watatu hawa ndiyo walikuwa wananinyanyasa, [wale wengine] wanne wangeweza kuwazuia wale watatu. Aliyekuwa anawaongoza ni yule dada kidogo, [alikuwa akisema], wewe pita chini ya kiti, [au] huyu msimueke huku, mueke huku. 

Mimi ndiyo nilimuona mdada fulani, siyo mdogo wala siyo mkubwa. Halafu niliingia na kutoka nimekamatwa na kuachiwa mimi sijaandikiwa maelezo yoyote, ilikuwa mpaka ile siku natoka ni siku hiyo hiyo nimeingia na kutoka kama nilituhumiwa basi ningeliandikiwa si ndio? Halafu ningeonekana siyo wangenichunguza halafu wangeniona siyo mimi wangeniachia.

The Chanzo: Walikuomba samahani? 

Ras Inno: Baada ya kuachiwa, kabla hata sijafika nyumbani, simu nilivyoiwasha ndiyo zikaanza kuja simu kutoka Dar es Salaam, simu za pole. Mimi nilikuwa sijui kama limefika Dar es Salaam, kumbe nilivyokamatwa wamesambaziana limefika Dar es Salaam, Dar Salaam likawekwa  kwenye mitandao ya kijamii. 

Sasa simu zikaanza kuja mtu mmoja akasema ni vyema ukasema neno ili watu watulie maana yake hawajui huku una hali gani vipi vipi. Ndiyo nikaweka chapisho refu kwenye ukurasa wangu wa Facebook kwamba ilikuwa hivi hivi mpaka sasa hivi iko hapa. 

Kama kawaida ikadakwa, ikaanza kuzunguka. Sasa kilichokuja kutokea, kesho yake asubuhi nilikuwa naota jua kule hali ya hewa inakuwa ni ya baridi, nimekaa na mke wangu pale nje, akaja mjumbe yule wa Serikali ya Mtaa akiwa ameongozana na watu wengine watatu, wanne. 

Mmoja ni mtu niliyesoma nae shule, mwingine ni mtu anayezidi wa makamu kidogo, mwingine ni mdogo wangu. Nikafikiri walikuja kunisabahi. Yule kijana akasema nimekuja kwa sababu nimepata ujumbe kutoka kituoni. Nikamuuliza ujumbe gani? Akasema yule kamanda pale aliyekuachia amesema mbona hizi habari unazisambaza kwenye mitandao? 

Nikamuambia habari zipi? [Akasema] za kukamatwa kwako. Nikamuambia sikiliza mimi nimekamatwa Iringa, watu walikuwa wanasambaza zile habari Dar es Salaam na nilijibu ile ili watu watulie. Mwambie mimi ni mtu wa watu. Nina watu wanaonipenda, wamekasirishwa na kughadhibishwa. Kwa hiyo, mimi niko Iringa siwadhibiti hawa watu wa Dar es Salaam. Nahusikaje? 

Cha pili nikaambiwa niende kule tuzungumze, nikawaambia siyo kituo kile na siwezi kwenda. Cha tatu, nikamuambia yule kijana sikiliza mimi shida yangu na askari watano. Wale watatu wa kwenye gari na wawili wa kituoni. Sina shida na hicho kituo wewe na polisi wa Iringa na wote sina shida nao. 

Muda huo kabla ya yule kijana hajaja nilipigiwa simu sasa na askari mwingine ambaye ananifahamu, alisikia maana yake zile habari zilikuwa zinazunguka si Dar es Salaam tu, zinazunguka mpaka kwa watu wengine, hata sikutarajia mimi watu wa ukubwa ule wataweza kutaka kujua taarifa zangu. 

Yule mtu akanipa pole akasema sasa kwa nini hukusema kwamba umepata tatizo? Nikamuambia simu ilikuwa imechukuliwa. Kwa hiyo, watu wengi ambao nina mawasiliano nao, hata ambao wako ndani ya Jeshi hili la Polisi, namba ziko mule. 

Akaniuliza kama nimetibiwa, nikamuambia hapana. Akaniuliza tena kwa hiyo utaenda kuchukua PF3? Nikamuambia sitaki hata kukiona kile kituo. Akasema basi nenda mkoani, mtafute RCO, mueleze suala lako basi tukaachana na yale. 

Baada ya muda yule kijana na mjumbe wa Serikali ya mtaa akaja akaniambia tunaitwa, wapi, ofisini mkoani, ufanye haraka. Nikamuambia siwezi kuharakishwa. Kwanza leo haikuwa siku yangu ya kutoka. Hicho kitongoji ni lazima ushuke ndiyo ukifikie. 

Baadaye tulikwenda mimi na wana Ndiuka wengine na mke wangu tukaambatana tukafika kule, tuliwakuta maafisa, akiwemo Afisa Upelelezi wa Wilaya, alikuja RCO kaimu, kaimu RPC, Muendesha Mashitaka wa pale, tukakaa kikao ofisini. 

Wakasema bwana tunaomba radhi vijana wetu walikosea, tutachukua hatua za ndani za Jeshi la Polisi. Walichosema na tutakutaarifu. Sasa RPC akaniuliza uliandikiwa maelezo? Afisa upelelezi wa wilaya akasema ndiyo inawezekana vijana wake walimjibu vile mimi nimjibu siyo na ukweli sijaandikiwa maelezo. Ulipewa PF3? Nikasema sijapewa. Akaagiza kwamba haya yafanyike. Wakaenda kushughulika na mambo ya PF3 ilikuwa jioni, sikufanikiwa kupata matibabu hiyo nazungumzia Jumatano ya tarehe 31. 

Halafu Alhamisi tena tukaenda hospitali nyingine tukakutana na daktari na ile PF3 lakini ninachohisi sijui itakuwa ni kitu kinachotisha kwamba Tanzania ni watu wanaoishi kwenye miji tu ndiyo wanauelewa. 

Kwa sababu, daktari yule tulichotaka kufikia kubishana nimemwambia mimi nimeumizwa goti la kushoto na michubuko kwenye mguu  wa kulia  mpaka hapa nimeumia hapa mdomoni nimepigwa ngumi halafu niko na mawenge kwa sababu mimi kulala kwangu maisha yangu yanafuata ratiba kama mfumo. 

Saa tatu nikilala ili saa 10: 39 kuelekea saa 11 niamke lazima niwe nimelala masaa nane. Lakini nikilala masaa mawili nikisikia gari inapita mbele ya nyumba kichwani inakuja picha ya lile gari la polisi. 

Yule dokta akaanza kuleta ubishi, akasema wewe kwa sababu ulisema unaumwa peripheral neuropathy watu wakiumwa hiyo wanakuwaga na mawenge. Nikamuambia nilivyougua peripheral neuropathy mpaka nainuka naanza kujua kufanya mazoezi sijawahi kupata mawenge hata siku moja. 

Na nilipougua shida ilikuwa ni upande wa kulia wa mwili hili goti la kushoto halikuwa na shida. Akasema hilo suala ni la kumuona physician, nendeni hospitali ile ya rufaa. Tukaenda, kufika kule nikatajiwa bei zao fulani hivi nikasema hapana. Mimi ninachojua hii inatakiwa kwa sababu hii ni fomu ya polisi nikairudisha kwa afisa upelelezi. 

Kesho yake ndiyo tukaenda huko Freelimo ndiyo yakatokea haya nilikuja kufanikiwa kumuona siku ya nne Ijumaa physician akanipeleka kwa daktari wake mfawidhi akaitwa daktari mwingine akanicheki nikaeleza suala la trauma. Akamuita mwanasaikolojia, mwanasaikolojia akanihudumia kwa muda wa masaa mawili tukarudi tukamalizana pale.

The Chanzo: Ukalipia gharama mwenyewe au polisi walilipia?

Ras Inno: Nililipia. Hawajalipia polisi.

The Chanzo: Kwenye taarifa yao, Mtandao wa Sekta Bunifu ulisema kwamba ungemuandikia barua rasmi IGP Camillus Wambura kumueleza kuhusiana na hilo jambo na kwamba alichunguze na wale waliohusika ambao wamekiuka sheria wachukuliwe hatua. Hiyo ni hatua ambayo CINT waliifanya?

Ras Inno: Ile taarifa wakati inatolewa ikumbukwe mimi bado nilikuwa kule na siku ile ile ni taarifa ya Mwenyekiti na jopo lililokuwa limesalia huku [Dar es Salaam] katika hatua za kuchukua. 

Zile zilizokuwa zinafanyika pale ni za uongozi wa polisi wa mkoa. Kwa hiyo, ilikuwa lazima nirudi licha ya hiyo taarifa ambayo watu wanaiona tu kwenye mtandao. Lakini lazima nirudi nisema uso kwa macho ndiyo watu wajue hasa nini kilichopo kwa sababu sio vitu vyote niliviweka kwenye mtandao.

The Chanzo: Unadhani ni kwa kiasi gani kisa chako kinaakisi malalamiko yanayoendelea, au malalamiko ya siku nyingi, dhidi ya Jeshi la Polisi na maafisa wa polisi kwa kutokufuata sheria na kanuni wakati wa kutekeleza majukumu yao? 

Malalamiko ambayo kusema ukweli mpaka Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyatambua na kulitaka hadharani kabisa Jeshi la Polisi lijirekebishe na ameunda mpaka tume ambayo inalenga kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa utoaji haki Tanzania. 

Unadhani ni kwa kiasi gani kisa chako kinaakisi haya malalamiko ambayo wananchi wengi wamekuwa wakiyatoa? 

Ras Inno: Kwa kiasi kikubwa. Kwa sababu, muda ambao Mheshimiwa Rais anafanya kikao na wakuu wa polisi wa mikoa na muda mimi niliofanyiwa tukio yaani viko hapa na hapa. Sikumbuki hasa kikao chake kilikuwa lini lakini ninachokumbuka [tukio] limetokea Agosti 30, 2020. Hicho cha kwanza. 

Cha pili, kama hili siyo kwenye mitandao kuna baadhi ya magazeti yalikuja yaliandika ile habari nao walichota kule kule kwenye mtandao ile ambayo mimi niliisema kwenye ukurasa wangu [wa Facebook]. 

Cha tatu, nilianza kusikia stori nyingi kuhusu vitendo vinavyofanana na hivyo mkoani Iringa na watu wakawa wanasema ikiwa wewe ni mtu unayefahamika sana vipi sisi wananchi wa kawaida? Wanasema ama kwako limekuwa na kelele kubwa kwa sababu una jukwaa kubwa, unafanya muziki, sijui mtangazaji wa vipindi redioni, sijui upo CINT. 

Kuna watu wa kawaida vipi na vingine siwezi kuvisema hapa kwa sababu kuna maeneo mbele nitakuja kuvisema lakini inaakisi kwa sehemu kubwa na mimi siyo msanii pekee kufanyiwa hivyo. Wako wamefanyiwa wanamuziki wengine siyo wanamuziki na shida inakuja mimi mpaka nikawa najiuliza ikiwa askari anaweza kukuambia kama wewe ni mwanamuziki muimbie hivi siku akimkamata nesi atamuambia nichome sindano ili nijue kama we ni nesi? Yaani vitu fulani vya ajabu hivi. 

Ile kufikiria kwao sijui inatokea wapi ni upolisi wa kizamani haupo. Mimi shaka yangu ni moja huu mwenendo ukiendelea tutakuja kugeuka kama Marekani. Nafikiri uliona wakati ule Barack Obama anaacha madaraka anaingia Donald Trump ilikuwa sasa inaanza kugeuka vita baina ya polisi na wananchi. 

Kwa hii tabia inaakisi kwa sehemu kubwa na makelele ni mengi sana na imefikia mahali kukawa na shinikizo kubwa sana ingawaje shinikizo hilo ajabu ilikuwa inaletwa kwangu kwamba watulize watu kwenye mtandao. Siwezi kuwatuliza mimi similiki Facebook, similiki Twitter, similiki kingine. Mimi mwenyewe ni mtu tu ninayetumia. 

Lakini kukawa na shinikizo ya watu wengine wanasema muachie Mungu. Lakini kukawa na presha kubwa sana ya watu wanasema hapana kwa saababu kupitia wewe ndiyo madhila yetu yatafahamika, hakukuwa na presha kwenye upande wa familia. 

Lakini shangazi zangu na baba zangu, ndugu za baba waliniita tukakaa kama familia ilikuwa sasa ni siku ya Jumapili wakasema ni kitu kimoja kama familia unastahili kuchukua hatua, msimamo wa familia kama wewe utaridhia utaliacha hivi hivi hatuwezi kukupinga. 

Lakini fikiria watu wangapi wamekuja nyuma yako na fikiria watu wangapi wamewahi kufanyiwa kama ulivyofanyiwa wewe. Sasa pana ahadi ya hatua za ndani za [polisi] kutolewa taarifa mpaka naongea na wewe muda huu hakuna taarifa imekuja kwamba hatua gani imechukuliwa.

The Chanzo: Pale askari wanashuka kwenye gari, wanakuja wakakuita Ras si ndiyo, sasa sijui kama hiyo walijua kwamba wewe ni Rastafarian ama vipi? Lakini ninachotaka kuuliza ni kwamba wewe ni Rastafarian, una amini, ni imani yako, na Dreds ni alama muhimu kwenye imani yako na kuna polisi pale walitishia kukukata hizo nywele. 

Ras Inno: [Walitishia] zaidi ya mara ya mara tano sijui. 

The Chanzo: Na wewe siyo Rastafarian wakwanza kuzungumza naye, tushawahi kufanya mazungumzo na mtu mwingine ambaye anaamini Urastafarai na amelalamikia kuhusiana na kutokuwepo kwa hiyo kuthaminiwa, kwa kukosa neno sahihi, uelewa wa jamii kuhusiana na imani ya Rastafarai. Unadhani ni kwa kiasi gani hicho kitendo cha polisi, kwa mfano, kukutishia kukata nywele zako ambalo ni tishio la moja kwa moja kwenye imani yako na mapokeo ambayo nyinyi kama Rastafarai mnayapata kwenye jamii tunazoishi?

Ras Inno: Mimi nasema hivi kuna vitu unaweza kuniona labda nimetumia maneno mabaya lakini kwanza ni watu kutokujielimsha. Kwa mujibu wa Katiba hakuna mtu anapangiwa nywele zako ziwe hivi hivi na sheria zote zinatokana na sheria mama Katiba kwa kuwa na Dredlocks aidha upo ndani ya imani au umefuga tu nini haiendi kinyume na sheria yoyote, yoyote. 

Kuna baadhi ya maeneo mpaka kuna watoto wenye imani za Kirastafarai wapo shule baada ya mawasiliano ya wazazi na walimu, cha kwanza. Cha pili, nywele hazihusiani hata kama ningekuwa ndiyo mimi huyo hazihusiani, ushaona? 

Kingine nilichowaambia niliwaambia nywele hizi nimezifuga kwa muda wa miaka 30 hizi nywele zina miaka 30 za mwaka 1992. Cha mwisho, ni kukudhalilisha kisaikolojia kwa sababu mtu hawezi kuja kukukata nywele ambazo mimi nimezitunza miaka 30 na kama mimi ningekuwa ni mtu wa matukio nisingekuwa na nywele za miaka 30, zingekuwa zishakatwa siku nyingi. 

Hizo ni sababu ambazo mimi nawaona wale baadhi ambao wanakiuka utaratibu walitishia hivyo hawakuweza kufanya hivyo lakini hata kama wangeweza kufanya hivyo mimi ningewafungulia mashtaka kwa sababu hawajui mimi nimetumia gharama kiasi gani mpaka nywele ziko hapa. 

Hizi nywele zinakwenda na usafi na matunzo, haziwi safi, hazirefuki. Kingine huko hawakugusa lakini waligusa kwenye nyimbo. Lazima tutalipana. Studio nalipa mimi. Jukwaani watu wanalipa kiingilio kuniangalia. Siwezi nikamuimbia-, hatutungi nyimbo tukaziimbe rumande. Tutakapofika kwenye hatua za mbele atalipa zile nyimbo mbili nilizomuimbia. 

Tena katika zile nyimbo mbili moja ndiyo nyimbo yangu maarufu, yaani ukiigusa tu kila mtu anaijua huyo ni nani. Mimi nasubiri yao [ni] yao na yangu ni yangu. Kama Mtanzania, yao ni yao na yangu ni yao. 

Na kingine siwezi kutishiwa kuogopa kwenda Iringa. Iringa ni kwetu. Nitaenda sana tu ndiyo kwenye asili ya baba yangu. Nafikiri kama eneo lile lina uhalifu wanatakiwa wakune kichwa wapate mbinu za kudhibiti uhalifu siyo kwenda kupiga watu wasiokuwa na hatia. 

Kwa sababu kwanza watu wamechukizwa,  inawezekana kabisa hawatapata ushirikiano wanaoutaka kwa sababu ya kuumiza watu wasiohusika na inaleta taswira mbaya sana kwa Jeshi la Polisi siyo tu nchi nzima hususan mkoani Iringa inaleta taswira mbaya haifai hiyo taswira.

The Chanzo: Ras Inno, mimi nakushukuru sana kwa muda wako, imekuwa ni mazungumzo mazuri sana kwa upande wa mitazamo yako kuhusiana na hilo sakata ambalo limekutokezea. Nilikuwa nataka tumalizie mazungumzo yetu kwa kukuuliza wewe kama mwanamuziki, kama Mtanzania, labda ungependa kuona Tanzania ya aina gani ikijengeka? Ni nchi gani ambayo wewe ipo kichwani mwako na ambayo ungependa itokeze nchini kwetu? 

Ras Inno: Ningependa kuiona Tanzania ya amani kabisa. Watu wakiishi huru kwa sababu unajua inachekesha nilipokuwa naulizwa Iringa nafuata nini, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si lazima ninukuu kifungu, mtu yeyote yupo huru kwenda mahali popote ilimradi havunji sheria. 

Kwa hiyo, hata ningeamua kwenda Bukoba, kila wakati nimeamua. Amani inaenda na haki na haki inakwenda na wajibu. Mimi kama Mtanzania nina haki ya kufanya mazoezi kwa sababu ni tiba. Kitu kingine wasichojua, unaweza ukaja na shtaka la kuhatarisha afya yangu lakini sasa kilichonifanya nipige makelele huwezi kujua unaweza kumpiga mtu tu kichwani buu! akazimia pale. 

Kwa hiyo, hata kama ungesema nataka kuomba radhi ningekuwa nimekufa, wangekuja kuomba radhi maiti au wangewaambia nini ndugu zangu? Haki inakwenda na wajibu kama wao wana haki ya kufanya kazi za usalama wawe na wajibu wa kufuata Police General Orders (PGO) yao inavyoeleza. 

Unajua ilivyo kuna kitu huwa kinakwenda tu kwa muda unaweza kufikiria utakifanya lakini kina mwisho wake. Mimi watu wengi walijaribu kumiwekea tafsiri mdomoni kuhusiana na kilichotokea na wengine bado kwa sababu sijaongea na mengine hata sijayasema. 

Mimi ni miongoni mwa watu ambao ni mashuhuda wa kitu ambacho Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu] amekuwa anakilalamikia. Kwa hiyo, mimi siwezi kuwa kinyume na Mheshimiwa Rais kwa kuongea hivi, maana yake mimi naunga mkono alichokisema Mheshimiwa Rais na ule wito alioutoa kuhusu weledi kwenye jeshi. 

Nataka Tanzania yenye amani, Tanzania ambapo  zamani raia hata ukipotea njia unamuuliza polisi, umenielewa? Leo unaenda kuuliza polisi kuna mahali mimi nakumbuka wakati tunasoma usafiri ulikuwa unasumbua tulishawahi kuomba msaada wa usafiri kwenye gari ya polisi yenye king’ora. [Hiyo] ndiyo Tanzania ninayoitaka. Siyo sasa nikimuona polisi naanza kukunja uso, kisaikolojia nasema huyu jamaa hata sitaki kuongea naye. 

Hapana na nje ya mambo haya ndiyo unapaswa kujua kwamba hapa hata hivyo vifaa na dhana wanazotumia magari ya ulinzi, bunduki, tunalipa kodi ndiyo zinanunua. Yaani kati ya mimi na wale polisi sidhani kama kuna kodi yao inaendesha maisha yangu. Mimi lakini, mimi kama mwanamuziki ninayelipa kodi katika nchi hii, inakwenda kununua vifaa wanavyotumia wao. 

Sasa haiyumkinini vitu ambavyo vinanunuliwa kwa mimi ikiwa sehemu ya mchanganyo wa kodi sasa leo vije vinitese mimi. Ndiyo wakati wao kujitathimini. Mimi nataka Tanzania yenye amani ambapo tutaishi kwa kuheshimiana. Lakini kila mtu atimize wajibu wake kama mwananchi wa Tanzania.

Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Omar Mikoma. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts