Dar es Salaam. Waziri Kivuli wa ACT-Wazalendo anayesimamia Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi Filberth Macheyeki amesema kwamba hali ya sasa ya vyombo vingi vya habari kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo wa kuwapasha habari wananchi inatokana na mazingira kandamizi ya kisheria na kikanuni yaliyopo nchini.
Macheyeki alitoa tathmini yake hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika hapo Oktoba 4, 2022, kufuatia ziara yake na viongozi wengine waandamizi wa chama chake katika ofisi za The Chanzo zilizopo Msasani, Dar es Salaam.
Macheyeki anadhani ni muhimu Serikali ikazifanyia mapitio sheria na kanuni zote zinazoongoza vyombo vya habari Tanzania kwa lengo za kuziboresha na hivyo kujenga mazingira rafiki kwa vyombo hivyo kuweza kufanya kazi zao.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya The Chanzo na Macheyeki:
The Chanzo: Ndugu Macheyeki, nilikuwa nataka kukuuliza unadhani vyombo vya habari vimetimiza wajibu wao kiasi gani kwenye kuwapasha habari wananchi kuhusiana na masuala, kwa mfano, ya kupanda kwa gharama za maisha na nini ambacho kinaweza kuwa kipo nyuma ya kupanda kwa gharama hizo za maisha? Wewe kama Waziri Kivuli unayehusika na mambo ya habari, unatathmini vipi wajibu wa vyombo vya habari kwenye kuwapasha habari wananchi kuhusiana na maswala haya?
Filberth Macheyeki: Asante sana. Kimsingi vyombo vya habari vinajitahidi kwa kiwango kikubwa kuweza kufikisha taarifa japo kuwa sasa kwa sababu walio na mawazo kinzani ni kutoka vyama pinzani mara nyingi wanashindwa kuwafikia, au kuweza kuchukua, yale mawazo kwa hofu fulani ya kuweza kudukuliwa au kuweza kuonekana kwamba wanapinga kile ambacho kimepelekwa bungeni.
Lakini vyombo vya habari vinafanya kazi kubwa sana kwa ajili ya kuhabarisha. Na huu muswada [wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote] umepigiwa kelele sana ukiachilia mbali namna ambavyo bungeni umeonesha kwamba kuna changamoto kadhaa lakini bado wananchi wameona ni kama inakwenda kufanyika biashara kwa wananchi, kama ambavyo ilivyo kwenye magari, gari likipata ajali basi lile ambalo lenye bima litarejeshwa na lile ambalo halina bima basi ndiyo hivyo.
Kwa hiyo, wananchi wamezungumza lakini pia vyombo vya habari vimejitahidi kwa kiwango kikubwa sana, mitandao ya jamii, kuona namna gani imefikisha taarifa na wananchi wanaweza kuwa na uelewa na pengine kutoa maoni yao kwa vyombo vikubwa.
The Chanzo: Unadhani labda, kwa mfano, kama mazingira ya uhuru wa habari, kama ingekuwa hakuna sheria na kanuni kandamizi, vyombo vya habari vingekuwa vipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutimiza wajibu wao kuliko ilivyo sasa kwenye kuwapasha wananchi habari kuhusiana na mambo yanayowahusu?
Filberth Macheyeki: Kimsingi tumepitia wakati mgumu kidogo kipindi cha nyuma, hilo kila mmoja anafahamu. Lakini ni lazima tukiri tumepiga hatua kidogo, japo kuwa bado kuna watu bado wanatushika miguu turudi Misri tulikotoka. Sasa hatua hii ambayo tunaiona ipo japo bado kuna changamoto kubwa ya uhuru wa vyombo vya habari nchini nchini.
Uhuru wa habari bado ukiangalia kuna muswada [wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari] ambao ulipelekwa bungeni, muswada wa huduma za habari unavyo vizuizi vingi ambavyo vina wafunga mikono na midomo waandishi wa habari kuweza kufanya kazi zao kwa uhuru.
Na ukiangalia zaidi inakwenda kukandamiza, bado inaendelea na kuminya uhuru wa vyombo vya habari, bado kuna taasisi kama TCRA na BASATA na zingine ambazo zinaendelea kutumika kuminya uhuru wa vyombo vya habari.
Waandishi wa habari kupitia Baraza la Habari Tanzani (MCT) walitoa maoni yao na mapendekezo kwa asilimia kubwa kuna mambo ambayo walikuwa hawakubaliani nayo kwa sababu yalikuwa yanakwenda kuminya uhuru wa vyombo vya habari, yanakwenda kuzuia watu kupata habari na kadhalika.
Sasa masuala kama haya ambayo wadau wa habari wamejaribu kuyaeleza kama vikwazo ni lazima Serikali iangalie kuweza kuyaondoa ili wananchi waweze kupata habari kwa uhuru. Na ukiangalia kwa kiwango kikubwa kwa sasa mbali na hizi habari ambazo tunazipata kwenye vyombo vya habari vya kawaida kama TV, habari sasa hivi zimehamia kwenye mitandao, kwa maana watu wanapata habari mitandaoni.
Sasa hizi sheria za maudhui mtandaoni zimewekwa kuwanyima na kuwashika mikono waandishi wa habari kuweza kufanya kazi zao kwa uhuru.
Tumeshuhudia juzi kuna chombo kilifungiwa ukiangalia sheria iliyotumika ni kandamizi, hawezi kufanya kosa mwandishi mmoja ukafungia taasisi nzima. Ina maana unakwenda kupoteza ajira za watu wengi. Lakini pia unakwenda kuumiza, kuminya uhuru wa watu kupata habari.
Ilipaswa sheria hiyo iondolewe na mhusika aliyefanya hilo kosa aadhibiwe, japo ni hatua kubwa kuweza kuondoa kabisa sheria za vyombo vya habari nchini tuwe na mfumo ambao ni huru, ambao tunaweza kusema ni mfumo usiokuwa na udhibiti, yaani vyombo vya habari vijiongoze vyenyewe kwa kanuni zake kupitia kwa Baraza la Habari la Taifa.
Sasa hatua hii tukifikia hivi vyombo vya habari vitakuwa huru pengine kama ilivyo kwa [Chama cha Wanasheria Tanganyika] TLS. Hii ni Jumuiya ya Wanasheria wa Tanganyika. Kwa hiyo, tukiwepo na baraza la habari kutakuwa na maamuzi ya wao wanahabari ya kuweza kuona namna gani wanaweza kuwajibishana lakini pia wanaweza kuona namna gani wanaweza kuondoa hivi vizuizi na vikwazo ambavyo vipo.
Lakini bado uhuru wa vyombo vya habari upo kwenye mashaka makubwa kutokana na sheria zilizowekwa. Waziri [wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari] kupewa mamlaka makubwa. TCRA kupewa mamlaka makubwa ya kuweza kuviminya na kuvidhibiti hivi vyombo vya habari na uhuru wa habari kwa ujumla nchini.
Kwa hiyo, bado kuna mashaka makubwa, na hatuwezi kusema kwamba wananchi wanapata habari zilizo kamili. Bado habari zinachujwa na kuonesha kwamba zile ambazo Serikali haizitaki ndizo ambazo zinazuiliwa na ambazo zinatakiwa ndizo zinazotoka. Kwa hiyo, bado uhuru upo kwenye mashaka na hasa tunapoona wanahabari hawako huru kuelezea kile halisi ambacho wananchi wanapaswa wakipate.
The Chanzo: Nyinyi ACT-Wazalendo msimamo wenu kuhusiana na suala zima la uhuru wa vyombo vya habari ni upi? Yaani, mapendekezo yenu ni yapi? Sera gani mbadala mnaweka mezani?
Filberth Macheyeki: Msimamo wetu upo wazi. Moja ya vitu vikubwa na kipaumbele cha kwanza ambacho tumeeleza kwenye ilani baada ya kutathmini yale mambo magumu ambayo tumeyapitia kwa miaka sita iliyopita, kipaumbeke kikubwa cha kwanza ambacho tumekielezea ni kuhakikisha kwamba tunaondoa sheria kandamizi zote ambazo zinaminya na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutoa maoni na uhuru wa mawasiliano.
Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo wetu na tumetoa mapendekezo yetu kwa uwazi kwamba ni lazima tuondoe sheria kandamizi ambazo zinakandamiza uhuru wa habari, uhuru wa kutoa maoni na namna ya kuwasiliana.
Na ukiangalia kwa asilimia kubwa kwa sasa kama uchumi wa wananchi umehamia katika mtandao, wanasema uchumi wa kidijiti, sasa unapominya uhuru wa habari ina maana kuna watu ambao wanashindwa kuwasiliana kupitia mitandao, wanashindwa kupashana habari. Sasa haya yote msimamo wetu ni kuhakikisha kwamba tunaondoa sheria kandamizi ambazo zinaminya uhuru wa habari nchini.
Na moja ya jambo kubwa wadau wa habari walieleza namna gani ya kuweza kushughulikia hii, sisi pia ACT-Wazalendo tumeeleza ni kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinakuwa huru kwa kuondoa sheria kandamizi lakini pia kuondoa mamlaka makubwa aliyonayo Waziri wa Habari dhidi ya vyombo vya habari nchini.
The Chanzo: Tungependa sana kuendeleza mjadala huu hapa lakini kama nilivyotangulia kusema muda siyo rafiki sana na tunakwenda kuhitimisha mazungumzo haya kwa kukupa mgeni wetu nafasi ya mwisho ya kutoa neno lolote lililopo moyoni mwako ambalo mimi hapa nimesahau au nimeghafilika kukuuliza.
Filberth Macheyeki: Kimsingi nami niwashukuru sana The Chanzo. Lakini katika kumalizia naweza kusema kwamba tumeelekea kwenye uchumi wa kidigitali na katika uchumi huu wa kidigitali ni lazima tuone ni namna gani Serikali inafanya jitihada za makusudi kabisa katika kukuza TEHAMA, [ikiwemo] kushusha gharama za intaneti.
Lakini pia kuhakikisha kasi ya intaneti lakini pia kuhakikisha kwamba mtandao unapatikana maeneo yote nchini ili kuhakikisha kwamba watu wanahabarika kwa sababu teknolojia hii ya habari imehamia zaidi kwenye mtandao kama ambavyo sisi tuko mubashara hapa.
Sasa bila kuwa na vifurushi ambavyo ni nafuu kwa kila mtu, mfano, wanavyopeleka tozo za vifurushi vya intaneti kitu ambacho ni hatari sana kinaenda kuua uchumi wa kidigitali. Lakini pia unapokwenda kuongeza gharama ya vifurushi ni kwenda kuua uchumi wa kidigitali kwa sababu watu wako mtandaoni saizi, biashara zinafanyika mtandaoni, kila kitu kipo mtandaoni.
Kwa hiyo, badala ya kupambana kuinua uchumi wa kidigitali, Serikali inapambana kuhakikisha inapandisha gharama ili watu washindwe kumudu gharama. Sasa ni hatua gani zichukuliwe?
Ni lazima Serikali ione namna nzuri sasa ya kuhakikisha kwamba gharama za intaneti zinashuka. Lakini pia inaondoa tozo kwenye mawasiliano, simu, lakini pia na bidhaa zingine za mawasiliano [kama vile] ving’amuzi, siyo simu pekee yake, ving’amuzi na kadhalika.
Lakini pia ihakikishe kwamba usalama wa watumiaji upo. Lakini pia uchumi wa watumiaji ni mkubwa ili kuhakikisha kwamba tunatoka kwenye hatua tuliyokuwepo, tunakwenda hatua kubwa zaidi kiuchumi.
Tumeona juzi Tanzania imetoka kushinda kuwa mjumbe wa Baraza la Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU). Sasa hatua hiyo ni lazima iendane na kasi ya intaneti ya kidigitali.
Ni lazima iendane na wananchi kuweza kupata mtandao uliobora lakini pia kuona namna gani tunahamia kwenye uchumi wa kidigitali kuhakikisha kwamba hizi gharama za mtandao, mawasiliano na upatikanaji wa habari unakuwa ni wa kila mtu.
Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na mwandishi wa The Chanzo Asifiwe Mbembela na kuhaririwa na Lukelo Francis. Shafii Hamisi amesimamia na kuzalisha mahojiano haya. Kwa maoni yoyote kuhusiana na mahojiano haya, wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.