Dar es Salaam. Jumla ya Watanzania milioni 10 wanaripotiwa kuugua magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji, huku watu 33,000 wakiripotiwa kufa kila mwaka kutokana na magonjwa hayo ambayo wataalamu wanaamini huchangiwa, pamoja na sababu nyengine, na matumizi ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Taarifa hizi ziliwasilishwa wakati wa mkutano wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini hapa tangu Novemba 1, 2022, na kutegemewa kuhitimishwa leo, Novemba 2.
Akizungumza wakati wa mjadala mkutanoni hapo, Dk Pauline Chale, daktari bingwa wa mapafu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alisema matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya nishati chafu ya kupikia ni mengi na kupelekea mzigo mkubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.
“Nishati chafu ya kupikia ni tatizo katika afya na ni mzigo mkubwa [kwa familia],” Dk Chale aliwaeleza washiriki wa mkutano huo. “Kwa sababu siyo wote wanaweza kumudu hii gharama [ya matibabu]. Kwa mfano, kama huna bima [ya afya], mara ya kwanza ile dozi ya kivuta pumzi, pamoja na kile kifaa cha kutumia, ni karibu na Sh120,000.”
Ni asilimia tano tu ya Watanzania, ambao kwa sasa wanakadiriwa kufikia milioni 61.7, ndiyo wanaripotiwa kutumia nishati safi ya kupikia kama vile gesi na umeme. Asilimia 96 ya Watanzania inaripotiwa kutumia nishati chafu, kama vile kuni na mkaa.
Hali hii siyo tu imethibitika kuwa na athari kubwa za kimazingira, bali pia imegundulika kuathiri afya za Watanzania waliowengi, na kuzisababishia familia kadhaa, pamoja na taifa, gharama kubwa, ikiwemo za kimatibabu pamoja na kuondokewa na nguvukazi ya taifa.
“Kumbuka katika ule moshi unaotolewa katika ile nishati kuna sumu nyingi ambazo kitaalamu tunaita, kuna vumbi vumbi ambazo tunaita ‘particulate matter’ kitaalamu ambazo zile, kwa ukubwa, yaani ukubwa wa zile vumbi vumbi huwa ni ‘diameter’ kama 2.5 ambazo tunasema [ni] ‘micro diameter’ kwa kitaalamu, ambazo hizo zinaingia moja kwa moja katika mapafu yetu na kuleta athari kubwa katika upumuaji,” Dk Chale alisema wakati wa mkutano huo.
“Pia, kuna sumu nyingi ambazo gesi kama ‘carbon monoxide’ ambazo hizo zina athari [za] moja kwa moja [kwenye] kupoteza ule uhalisia wa kinga ya mfumo wa njia ya hewa,” aliongeza daktari huyo bingwa wa mapafu.
Dk Chale alitolea mfano wa wagonjwa wawili wanawake, mmoja akiwa na umri wa miaka 60 na mwingine akiwa na miaka 66 ambao wote amewahudumia hapo MNH na ambao wote historia zao zinaonesha kuwa walikuwa wakitumia nishati chafu kupikia, hali iliyopelekea athari katika mifumo yao ya upumuaji.
Mtaalamu huyo alieleza kwamba tayari mmoja kati ya wagonjwa hao, ambaye ni mwenye umri wa miaka 66, alipoteza maisha mnamo Oktoba 10, 2022.
Dk Chale alieleza kwamba wagonjwa hao ni kati ya wagonjwa 480 ambao MNH iliwapokea na kuwahudumia kati ya kipindi cha Julai mkapa Septemba, 2022, ambao walikuwa na matatizo mablimbali ya mfumo wa kupumua.
“Ukiangalia hawa wagonjwa na idadi ya madaktari [waliopo], inakuwa ni mzigo [kwa hospitali], kwa sababu madaktari wabobezi kama mimi wa magonjwa ya mapafu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tupo watatu tu,” anasema Dk Chale.
“Kwa hiyo, inabidi upate madaktari wengine waweze kukusaidia kuendesha kliniki ambayo kila siku ya Alhamisi ina wagonjwa siyo chini ya 60, ukipunguza sana mahudhurio ni watu 40,” anaongeza mtaalamu huyo.
Dk Chale aliongeza kwamba kinachosikitisha zaidi ni kwamba Watanzania wengi hushindwa kumudu gharama za matibabu zinazohitajika katika hospitali zilizopo. Hivyo, mzigo huo hubaki kwa Serikali kuwalipia watu hao ili waweze kupata matibabu.
Mtaalamu huyo alitolea mfano wa gharama ya kumuweka mgonjwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ambayo ni Sh500,000 kwa siku na huwa inatokea mgonjwa kuwekwa chumbani hapo kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, gharama ambazo familia yake haiwezi kuzimudu.
“Hiki siyo kitu cha mzaha,” alitahadharisha Dk Chale kuhusiana na matumizi ya nishati chafu. “Ni kitu ambacho inabidi tukichukulie kwa umuhimu mkubwa. Ni muhimu tuanze kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu na tuanze kutumia nishati safi sasa.”
Hadija Said ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam anayepatikana kupitia hadijasaid826@gmail.com.