Dodoma. Aliposikia kwa mara ya kwanza, Hussein Hamad Hussein alikuwa mzito kuamini taarifa kwamba watoto wake wawili wakiume walikuwa ni wahanga wa vitendo vya ulawiti vilivyokuwa vinafanywa na mtoto wa kiume mwengine aliyekuwa akiishi katika mtaa huo wa Mathias, mkoani hapa.
“Kwanza, kwanza, sikuwa nimeamini,” Hussein, mwenye umri kati ya miaka 35 na 40, alisema wakati akisimulia mkasa huo kwa waandishi wa habari. “Kwanza, ilibidi kwanza niwachukue watoto, niwaonye kwa kuwapiga kwanza, maana niliwaita, nikawauliza, wakawa hawasemi.”
Ni baada ya kuwachapa watoto wake, wenye umri wa miaka sita na tano, wote wakiwa ni wanafunzi wa darasa la pili, ndipo Hussein alipoweza kubaini ukweli kwamba wamekuwa wakilawitiwa na mtoto wa kiume mwenzao mwenye umri wa miaka 14 baada ya kuwaonesha picha za ngono.
Watoto hawa ndiyo watoto pekee kwa Hussein kwa sasa na ukatili huo wa kingono waliofanyiwa ni kitu ambacho kimemuumiza sana Hussein, anayejishughulisha na ufundi wa kuchomelea vyuma kuendesha maisha yake, kitu unachoweza kukigundua kwenye sauti yake.
“Unajua,” alisema Hussein kwa sauti ya masikitiko, “unaweza kumpoteza mtoto wako wa kiume hivi hivi, akawa siyo mwanaume kabisa aliyekamilika. Ukawa na mtu ambaye ni jinsia mbili tofauti. Kwa hiyo, hapo unakuwa umeshapoteza nguvu kazi pia.”
Wakati ni vigumu kudai kwamba ulawiti ni jambo jipya, kasi ya kuongezeka kwa kesi za ukatili wa kijinsia wa aina hiyo umekuwa ukichukua vichwa vya mbele vya habari kwa siku za hivi karibuni na kuwa mada ya midahalo na makongamano mengi yanayofanyika nchini.
Kasi hii inaweza kuelezewa kuwa ni kasi ya kutisha, kwa mujibu wa takwimu zilizopo zinazoonesha kutamalaki kwa ukatili huo nchini, na kuiweka hatma ya mtoto wa kiume kwenye njia panda.
Kwa mfano, wakati takwimu kutoka Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba watoto 537 walilawitiwa nchini Tanzania kwa mwaka 2016, idadi hiyo imepanda hadi kufikia watoto 1,114 kwa mwaka 2021, idadi ambayo ni mara mbili ya ile iliyorikodiwa mwaka 2016.
Wadau wanahofia kwamba tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi ya linavyoonekana hivi sasa ukizingatia ukweli kwamba takwimu hizi zimechukuliwa kutoka kwenye zile kesi tu zilizoripotiwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Kufumbia macho
Gemma Akilimali ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambaye anahusisha kukithiri kwa matukio haya na tabia ya Watanzania ya “kufumbia macho” mambo yanayoonekana kuwa ni ya aibu kwenye macho ya walio wengi, hali anayosema inaanzia kwenye ngazi ya familia.
Kimsingi, huku “kufumbia macho” kumelalamikiwa hata na viongozi wa Serikali za Mitaa ambao wamekuwa wakibainisha kwamba hali hiyo imechochea matukio ya ukatili wa kingono – dhidi ya wanawake, mabinti na watoto wa kiume – uendelee kushamiri kwenye jamii.
Hii ilidhihirika hivi karibuni wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu ukatili dhidi ya watoto wa kiume uliofanyika wakati wa Wiki ya Asasi za Kiraia, hapo Oktoba 27, 2022, jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa mjadala huo, Mtafiti Mwandamizi kutoka LHRC, Fundikila Wazambi, alisema familia kutokuwa tayari kushirikiana na mamlaka za nchi kwenye kukabiliana na tatizo hilo sugu limekuwa ni lalamiko kubwa wao kama shirika wamekuwa wakipokea kutoka kwa mamlaka hizo.
“Usiri huu unashajihishwa na nia ya kutaka kuficha aibu ya familia,” alisema Wazambi wakati wa mjadala huo. “Kwa sababu, kama tunavyojua, wengi kati ya wanaofanya huu ukatili wanakuwa ni ndugu wa karibu – takriban asilimia 66, kwa mujibu wa tafiti zetu– kwa hiyo kunakuwa na ile tabia ya kutaka kufichiana aibu.”
Lakini kwenye mahojiano yake na The Chanzo, Akilimali wa TGNP alienda mbali na kuhusisha kushamiri kwa matukio haya pia na hali duni ya kimaisha inayozikabili kaya nyingi za Kitanzania, hali inayozifanya familia kushindwa kukidhi mahitaji ya kimalazi kwa wanachama wote wa kaya husika.
“Mfumo wa maisha tulio nao [Watanzania] unachangia matukio haya kuongezeka,” mwanaharakati huyo wa siku nyingi wa haki za binadamu anaeleza. “Unakuta baba ana chumba kimoja, ameoa, anazaa mtoto wa kwanza, chumba kimoja, wa pili, wa tatu.
“Yule wa nne anakuja kuona kwamba kwa jirani kuna nyumba yenye wavulana, anaenda kulala huko.
“Wakati mwingine [watoto] wanaambiwa kalaleni na wavulana wenzenu bila kuangalia kule wanakoenda kulala wana maadili gani. Kwa hiyo, watoto wamekuwa wakifunzana kule,” alisema Akilimali kwenye mahojiano na The Chanzo.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) ni moja kati ya wadau wengi waliomstari wa mbele katika kuhakikisha janga hili linatokomezwa nchini Tanzania.
Sera ya familia
Mkurugenzi wake, Dk Rose Reuben, aliieleza The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba mbali na jitihada nyengine ambazo wadau wamekuwa wakizipendekeza ili kutokomeza janga hili, Serikali haiwezi kukwepa umuhimu wa kuja na Sera ya Familia.
Dk Reuben anaamini kwamba kama Sera ya Familia ingekuwepo ingetoa muongozo wa namna gani bora familia inaweza kukabiliana na matukio kama haya na hivyo kuchukua juhudi za makusudi za kumlinda mtoto – yule wa kike na wa kiume – dhidi ya ukatili.
“Nguvu ni lazima ielekezwe kwenye ngazi ya familia kwa sababu tumeshaona huko ndiko matatizo yanakotokea,” anasema Reuben kwenye mahojiano na The Chanzo. “Huko ndiko ukatili unakotokea na huko huko ndiko juhudi za kuulinda huu ukatili usifichuke ndiko zinakofanyika.”
The Chanzo ilimtafuta Dk Dorothy Gwajima, waziri mwenye dhamana ya watoto, ili kufahamu kama Serikali inaweza kutekeza pendekezo la Dk Reuben. Hata hivyo, juhudi zetu zilishindwa kufua dafu baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Lakini Serikali inaonekana kutambua ni wapi tatizo lipo na imekuwa ikichukua jitihada kadhaa zinazolenga kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Kwa sehemu kubwa, juhudi hizi zimekuwa zikihusu elimu kwa umma.
Mnamo Juni 6, 2022, kwa mfano, Dk Gwajima, akiwa katika Shule ya Msingi Mnadani mkoani Dodoma, aliwataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyotokea, hususan katika maeneo ya shule na nyumbani.
“Wanangu, baba akikukatili mwambie mama na kama ni mama basi mwambie baba,” Dk Gwajima aliwaasa watoto kote nchini. “Au kama unaona huwezi kumwambia baba, au mama, basi mwambie mtu unayemwamini.”
Serikali ifanye zaidi
Akilimali wa TGNP pia anadhani ni muhimu kwa polisi, pindi wanapopelekewa kesi za ukatili, wasiwarudishe watu nyumbani na kuwaambia wakamalizane kifamilia, akisema hili ni jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na baadhi ya wadau.
The Chanzo ilipofika nyumbani kwa Hussein, ikiwa ni sehemu ya vyombo vya habari vilivyofika hapo kumuhoji kuhusu kadhia hiyo iliyowapata watoto wake, alikuwa yupo katika hamkani ya kutengeneza mizani ya kupimia bidhaa kama vile mchele.
Ilikuwa ni ngumu kumshawishi Hussein azungumzie kadhia hii.
Hata hivyo, baada ya kushawishiwa sana, akielezwa kwa nini sauti yake inahitajika katika juhudi za kukomesha vitendo hivi, Hussein alikubali kuongea na kuwa mzazi pekee aliyekuwa tayari kufanya hivyo kati ya wazazi ambao watoto wao wa kiume wamelawitiwa na mtoto wa kiume huyo wa miaka 14.
Kwa mujibu wa ripoti, mtoto huyo anayedaiwa kulawiti watoto wenzake wapatao nane tayari amefikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya haki kuchukua mkondo wake.
“Serikali iangalie namna ya kuwalinda watoto kwenye jamii, itusaidie sisi ambao tuko huku mitaani, ili haya mambo yasiweze kutokea,” ndiyo wito wa Hussein.
“Serikali itupe hata uongozi ambao unaweza kusimamia haya mambo kwa nguvu,” anaongeza mzazi huyo.
“Kwa sababu sisi uongozi wetu huku chini unakuwa hauna nguvu,” Hussein aliendelea kufafanua. “Unaweza kumfuata balozi, anakuambia hivi na baadaye asitekeleze. Unaeleza hili suala baadaye lisichukuliwe kwa uzito.”
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.