The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Miaka 61 ya Uhuru Kweli?

Watu ambao hawaonekani juu ya majukwaa ya kisiasa ndio kipimo halisi cha uhuru wa taifa. Kama kundi hilo kubwa la watu linaigopa Serikali basi taifa limehama tokea miaka kadhaa ya uhuru limeingia kwenye miaka kadhaa tangia siku ya uhuru.

subscribe to our newsletter!

Kila inapofika Disemba 9, kila mwaka tunasherekea uhuru, lakini swali la msingi Je, tunasherehekea kuwa wananchi huru ama tunaadhimisha tu miaka 61 tokea ile tarehe ambayo bendera ya mkoloni ilishushwa na kutangaziwa kuwa sasa tu taifa huru?

Tunaouhakika mioyoni mwetu kuwa tumekuwa taifa huru kwa miaka 61? Yaani ni kwa ukweli na uhakika kwamba kwa kipindi chote cha miaka 61 tumeuishi uhuru kwa vitendo?

Katika kijitabu cha Uhuru na Maendeleo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kusema, ‘Uhuru na maendeleo ni kama kuku na yai; bila yai hupati kuku na bila kuku hutopata mayai. Vivyo hivyo bila uhuru hupati maendeleo na bila maendeleo unapoteza uhuru’

Kwa nukuu hiii itoshe kusema kwamba kiongozi huyu wa mbio za uhuru wa Tanganyika katika fikra zake alizifungamanisha dhana hizi mbili, yaani Uhuru na Maendeleo.

Dhana ya  uhuru na maendeleo

Si vibaya kuamini kuwa waliomwelewa Mwalimu Nyerere kinagaubaga walielewa pia kuwa sherehe za kusherekea Uhuru ni sherehe za kusherekea maendeleo.  Iwapo watu wenye sherehe ya uhuru hawana hakika na maendeleo yao basi uhuru wao ulikwisha kupotea kabla ya wao kupata mashaka ya maendeleo yao.

Mwalimu Nyerere pia alipata kusema  ‘maendeleo ni maendeleo ya watu na watu ni Watanzania wote’. Sasa hebu tutazame kwa upana kilichojiri kile kipindi Watanganyika wametangaziwa kujitawala kutoka kwa Mkoloni.

Siku moja baada ya uhuru, Watanganyika waliokuwa wameajiriwa kwenye kiwanda kilichokuwa kikimilikiwa na mwekezaji toka nchi za kikoloni, waliamka na kwenda kufanya kazi kwa bosi yuleyule.Uhuru ulimaanisha nini kwao?

Uhuru ulimaanisha kuwa mahusiano yao na bosi wao si mahusiano ya mkoloni na mtawaliwa bali ya mwajiri na mwajiriwa yanayolinda haki za mwajiriwa kwa mujibu wa sheria. Kwa mwajiriwa, kuhakikishiwa haki za msingi katika ajira yalikuwa Maendeleo.

Kwa mantiki hiyo basi uhuru haukumaanisha kumuondoa tu mzungu na kisha kuweka watawala wapya waafrika wenzetu.

Maendeleo nayo siku zote humaanisha katika nyanja zote muhimu za maisha yakiwemo masuala ya haki za kiraia.

Uhuru wa kutoa maoni

Maendeleo ya miundombinu hata ng’ombe au mbuzi anaweza kuwa nayo kwa kumtengenezea zizi lake. Lakini Maendeleo ya binadamu ni pamoja na kuwa huru kufikra, kutoa maoni yake, kukosoa na kuheshimiwa utu wake. Huwezi kuja kusikia kondoo anadai uhuru wa maoni.

Kwa Nyerere na wenzake waliowahi kushitakiwa kwa makosa ya uchochezi wakati wakieleza maoni yao; matarajio ya uhuru yalitafsiriwa kumaanisha serikali itokanayo na watu na inalinda uhuru wa watu kutoa maoni; yakiwemo maoni yasiyoifurahisha serikali.

Waliopigania uhuru waliishi wakiamini wakipata uhuru watapata maendeleo. Kielelezo cha maendeleo yao kingekekuwa uvumilivu wa kisiasa unaodhihirika kwa kuwalinda wenye maoni tofauti.

Dhana ya uhuru na maendeleo inaweza kujadiliwa asubuhi mpaka asubuhi nyingine. Mkoloni alijenga miundombinu kama viwanja vya ndege, reli, madaraja na barabara. Lakini hiyo, haikutosha, Watanganyika walidai uhuru.

Walipodai uhuru walidai maendeleo. Licha ya wao kutumia barabara na reli za mkoloni kutembea kila kona kuhubiri uhuru, hata mara moja hawakuona reli na barabara kama maendeleo. Walitaka uhuru kwa sababu hakuna maendeleo bila uhuru. Jambo pekee la maana linamtofautisha binadamu na wanyama wengine ni ule utu.

Hivyo hata kipimo cha maendeleo kwa binadamu ni lazima tuanze kuangalia mifumo inathamini vipi utu wa binadamu wake? Ukiwa huna uwezo wa kuuliza tunaenda wapi kwa mtu aliyekushika mkono. Huna utofauti na punda wa rafiki yangu Sokoine kule Berege. Maana Punda haulizi unanipeleka wapi?

Ni imani yangu kuwa waliopigania uhuru hawakupigania nafasi zao kisiasa wala huwakuwaza kuwalinda warithi wa viti vya uongozi baada yao. Walipigania uhuru kwa niaba ya umma wa Watanganyika.

Kwa kuliona hilo, ni dhahiri kuwa kipimo cha uhuru kinapimwa kwa kuuangalia Umma wa Watanzania uhuru kiasi gani. Ni kwa kiasi gani Watanzania hawa ambao sio majasiri kama walivyokuwa wengi waliowakilishwa na kizazi cha Nyerere wako huru.

Watu ambao hawaonekani juu ya majukwaa ya kisiasa ndio kipimo halisi cha uhuru wa taifa. Kama kundi hilo kubwa la watu linaigopa Serikali basi taifa limehama tokea miaka kadhaa ya uhuru limeingia kwenye miaka kadhaa tangia siku ya uhuru.

Vitu gani vinaashiria uhuru? 

Je mwenge? bendera? serikali iliyopo kupitia uchaguzi ndio viashiria vikuu vya uhuru wa nchi?

Je, vipi kuhusu uhuru wa watu kwenda mahakamani kupinga matokeo ambayo yakiachwa yatazalisha Serikali isiyotokana na watu? Na vipi kuhusu uhuru wa mahakama kusikiliza watu bila kuiogopa Serikali ili iwahakikishie watu kuwa Serikali lazima itokane na watu?

Uhuru uko wapi ikiwa watu hawawezi kuwashitaki viongozi waandamizi wa Serikali kwa sababu wanawaogopa? Ngoja, tuseme watu hawaogopi, uhuru uko wapi iwapo watu majasiri hawawezi kuwashitaki viongozi waandamizi wa Serikali kwa sababu viongozi waandamizi wana kinga ya kisheria inayowalinda wasishitakiwe kwenye mahakama yoyote?

Uhuru una maana gani iwapo bunge linailinda serikali kwa kutunga sheria ya kuizuia mahakama kusikiliza kesi dhidi ya viongozi wa serikali? Bunge lina uhuru gani iwapo wajibu wake ni kuisimamia serikali lakini lenyewe ndio linatunga sheria ya kuzuia viongozi wa serikali wasishitakiwe? Serikali itawajibishwa vipi kama watendaji wake hawagusiki kisheria?

Uhuru wa mtu mmoja mmoja na uhuru wa watu wote uko wapi iwapo mtu mmoja hawezi kwenda mahakamani kuomba amri ya mahakama kwa maslahi ya umma hata kama yeye hanufaiki na matokeo ya amri hiyo?

Pengine viashiria ni vingi zaidi, Je, uhuru unadhihirika iwapo raia wanaweza kuyapinga matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani? Ama uhuru upo wapi iwapo raia hawawezi kugombea nafasi za uongozi bila kulazimika kuwa wanachama wa vyama vya siasa?

Uhuru! Uhuru! Uhuru! Kuna wakati nadhani wafanyakazi waliounga mkono harakati za kudai uhuru walitaka uhakika wa kupandishiwa maslahi yao kadiri gharama za maisha zilivyopanda.

Wafanyakazi wa wakati ule hawakuweza kumgomea mwajiri wa kikoloni lakini walitamani uhuru wakiamini Serikali huru itatokana na watu na itawasikiliza watu, wakiwemo wafanyakazi, na itajibu ama kufanyia kazi madai yao.

Uhuru una maana gani kwa wanasiasa wa miaka 61 tangia uhuru? Je, unamaanisha uvumilivu wa kisiasa kwa maoni wasiyofurahishwa nayo?

Je, Uhuru ni tunu kwao wanasiasa hawa? ama unamaanisha wajibu wa viongozi kulinda haki za msingi za raia? Uhuru hautakuwa na maana yoyote kama utamaanisha mafanikio ya serikali kujenga shule, vituo vya afya, madaraja, barabara, reli na viwanja vya ndege kwa sababu vitu hivyo vilifanyika wakati wote wa madai ya uhuru.

Uhuru ulikuja baada ya ukoloni. Watawaliwa walichoka kutawaliwa na wakapata ujasiri wa kutowaogopa wakoloni, wakaanza kudai uhuru, wakapata Serikali iliyotokana na wao. Hawakuiogopa serikali tena.

Hali ikoje leo, watu wanaiogopa serikali ama serikali inawaogopa watu. Iwapo serikali inawaogopa watu basi watu wanasherekea miaka 61 ya uhuru na iwapo watu wanaiogopa serikali basi serikali inasherekea miaka 61 tangia siku ya uhuru bila kujali kama watu wameuishi uhuru kwa vitendo kwa miaka yote 61.

Nikiwa katika tafakari za sherehe hizi za maadhimisho ya miaka 61 toka Uhuru. Kuna rafiki mmoja akaniambia, unayowaza jibu lake ni KATIBA MPYA. Nikamwambia jibu sio KATIBA MPYA bali ni KATIBA MPYA itakayosadifu Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu.

Deogratias Cosmas Mahinyila ni Wakili na anapatikana kupitia namba za simu +255656872781 au baruapepe mahinyiladeogratius@gmail.com.Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Maoni yangu “Uhuru tunaousherehekea ni wa miaka tangu kutangazwa na kushushwa bendera ya mkoroni,ukoloni upo vilevile kifikra na utandawazi wote .Watu tunaogopa kuanzia kutoa maoni binafsi ,kufanya kazi kwa ubora ,kuziishi haki za kiraia na kuchagua viongozi wanaofaa.Mifumo ya ukoloni ilirekebishwa tuu kutoka kuwa wazi hadi kuwa ya mantiki ,tunatumika kwa kila jambo hivyo hii sio sikukuu kweli ya Uhuru maana watu wake hatuko kama neno Uhuru linavotaka
    Chaguzi ni za kujuana ,viongozi ni wakutengenezwa,tumeaminishwa maana isiyo sahihi kuitwa ndo Uhuru bali ni woga mtupu eti kutokupigana ndo Uhuru kumbe Uhuru ni neno pana sana.

  2. Hongera sana kwa makala nzuri ya kizalendo, inayotafakarisha juu ya uhuru wa kweli, kwa mujibu wa makala hiyo hatuko huru bado

  3. Hongeraaa sana Wakili kwa ufafanuzi mzuri na wenye mantiki,niseme wazi wewe ni Miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa sana wa kuchanganua mambo. Dhana ya neno Uhuru imekua ikipata tafsiri tofauti tofauti kulingana na uhitaji na maslahi ya watu wachache na kusahau walio wengi.Kiuhalisia dhana ya Uhuru katika mtazamo wa kisiasa,kiuchumi,kiutamaduni na kijamii haipo. Why are we putting ourselves in a Mental Jail (Ni lini usiku utakwisha?).
    Ikiwa dhana hii ya Uhuru tutaitekeleza kwa kufuata Sheria,Kanuni na Taratibu baasi Neno Maendeleo litaakisi uhalisia wa Watanzania. Naamini kwa kupitia Ufafanuzi wako umeokoa Vijana wengi sana kwa kuwapatia Chakula cha Ubongo.
    Ushauri wangu
    Kama Vijana inabidi tutafakari kwa makini na kuona nini kifanyike kuakisi hali ya Maisha ya Watanzania tukihusianisha na neno Uhuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *