The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ajali za Barabarani Zilivyoteketeza Maisha ya Watanzania 2022

Watanzania 886 wamepoteza maisha kati ya Januari na Novemba 2022 kutokana na ajali za barabarani.

subscribe to our newsletter!

Mbeya. Jumla ya Watanzania 886 wamepoteza maisha kati ya Januari na Novemba mwaka huu wa 2022 kutokana na ajali za barabarani. 

Wengine 573 wameachwa na majeraha kwenye ajali hizo 1,422 zilizorekodiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi.

Ajali hizi 1,422 ni ongezeko la ajali 11 ya zile zilizotokea katika kipindi kama hicho mwaka 2021 ambapo kulikuwa na ajali 1,411 zilizoua watu 1,008 na kujeruhi 1496.

Ingawaje maafa yaliyotokana na ajali za barabarani mwaka huu yalikuwa pungufu ya yale yaliyotokea 2021 kama takwimu zinavyoonesha, bado Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Ramadhani Ng’anzi anaamini idadi hiyo ni kubwa sana.

Kwa mtazamo wa kipolisi, ajali hizi zinatokana na kutokuwepo kwa weledi ndani ya chombo hicho cha usimamizi wa sheria nchini, tatizo ambalo Ng’anzi ameiambia The Chanzo kwamba ndilo ofisi yake inapanga kupambana nalo.

Ng’anzi anaamini kwamba endapo kama Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, litajitazama upya na kufanya kazi kwa bidii zaidi na kwa weledi, uaminifu na kwa kutenda haki, maafa yatokanayo na ajali za barabarani yanaweza kupungua Tanzania. 

“Sisi wajibu wetu kama chombo cha usimamizi wa sheria tumeona kwamba tuongeze nidhamu katika kufanya kazi, tusimamie maadili ya kazi yetu, tutende haki,” Ng’anzi aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye. 

“Vyote hivyo tukivifanya, bila shaka, kila mtu ataona kwamba kwenye usimamizi wa sheria tunamfaa na hiyo itatusaidia kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa sana,” aliongeza afisa huyo mwandamizi wa Jeshi la Polisi.

Ni ngumu kuorodhesha ajali zote za barabarani zilizotokea mwaka huu wa 2022 kwenye makala moja. 

Hata hivyo, tunakuwekea hapa baadhi ya ajali ambazo tunadhani ni kubwa kutokana na maafa zilizoyababisha:

Watu 19 wauwa kwenye ajali Mbeya

Ajali hii ilitokea mnamo Agosti 16, 2022, katika eneo la Inyala, kijiji cha Shamwengo, mkoani Mbeya, ikihusisha magari manne na kupelekea vifo vya watu 19 na majeruhi mmoja.

Ni kwamba lori lenye namba za usajili T 387 DFJ, tela namba T 918 DFE, mali ya kampuni ya Evarest French Ltd, likiwa na kontena la mchanga, liligonga kwa nyuma gari namba T 966 DUQ ambalo ni basi aina ya Fuso, mali ya kampuni ya Super Dogas likitoka Mbeya kwenda Njombe. 

Basi hilo baada ya kugongwa kwa nyuma nalo lilienda kugonga gari lenye usajili wa namba T 836 DRE Mitsubish Benz na kisha kwenda kugonga gari jingine lililokuwa na namba T 342 CHG/T 989 CGS Scania.

Basi la ‘Hakuna Kulala’ laua 19 Iringa

Kwenye ajali hiyo iliyotokea Juni 10, 2022, watu 19 walifariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya basi dogo aina ya Coaster, yenye namba za usajili T 542 DQV kugongana uso kwa uso na lori la mizigo lililokuwa na usajili namba T 736 AAE karibu na neo la Changarawe, Mafinga, mkoani Iringa.

Polisi walitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi wa Coaster iliyokuwa inatokea Mbeya kwenda Dar es Salaam ambayo ilienda kugonga kwa nyuma lori lililokuwa limeharibika katika eneo hilo.

Kati ya waliofariki, 14 walikuwa ni wanaume, wanne ni wanawake na mtoto mmoja wa kike.

Ajali yaua 14 Simiyu, wakiwemo waandishi wa habari

Mnamo Januari 11, 2022, katika eneo la Nyamikoma, kijiji cha Kalomela, mkoani Simiyu, ajali mbaya ilitokea ikihusisha gari la waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel na gari dogo la abiria Toyota Hiace, na kupelekea vifo vya watu 14. 

Polisi walitaja mwendo kasi wa gari la waandishi wa habari kama sababu ya ajali hiyo iliyochukua uhai wa waandishi wa habari wanne, dereva mmoja na watu sita kutoka kwenye Toyota Hiace.

Waandishi wa habari waliofariki kutokana na ajali hiyo mbaya ni Husna Mlanzi wa ITV, Anthony Chuwa wa HabariLeo Digital, Abel Ngapemba ambaye ni Afisa Habari mkoa wa Mwanza, Steven Msengi Afisa Habari wa Ukerewe na Paul Silanga dereva wao.

Ajali yauwa 11 Mtwara, wakiwemo watoto

Wanafunzi tisa wa shule ya King David mkoani Mtwara, na watu wengine wawili, walipoteza maisha kufuatia ajali iliyohusisha gari ndogo aina ya Toyota Hiace yenye usajili namba T 207 CTS iliyobeba watoto takribani 30 iliyopoteza mwelekeo.

Ajali yaua 23 Morogoro

Watu 23 walipoteza maisha na wengine 34 kujeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha gari la abiria la kampuni ya Ahmeed, aina ya lori, katika eneo la Maleki, Kibaoni, njia ya kutoka Morogoro kwenda Dodoma, mnapo majira ya mchana ya hapo Machi 19, 2022.

Polisi walieleza chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa lori ambaye alijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki na kujikuta anaenda kumvaa kwa mbele dereva wa basi la Ahmeed lililokuwa linatoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Zaidi ya weledi

Wakati wadau wa usalama barabarani nchini wanakubaliana na hoja ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Ramadhani Ng’anzi ya kusimamia weledi ndani ya Jeshi la Polisi, wadau hao wanaamini kwamba juhudi zinapaswa ziende zaidi ya hapo.

Augustus Fungo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania aliyeiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum hivi karibuni kwamba sehemu ya jitihada za kupunguza maafa yatokanayo na ajali za barabarani ni mabadiliko ya kisheria.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani wa mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Juni 30, 2021, ikiwa ni baada ya miaka takriban sita ya ushawishi, uchechemuzi na vuguvugu kufanikisha hatua hiyo. 

Hata hivyo, tangu kusomwa kwake muswada huo ulipotolea kusikojulikana na hivyo hatma yake kutojulikana.

SOMA ZAIDI: Nini Kimekwamisha Mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani Tanzania?

Fungo, hata hivyo, anabainisha kwamba wakati tukisubiri mabadiliko hayo ya kisheria, ni muhimu hizo sheria zilizopo zikasimamiwa vizuri.

“Kwamba katika usimamizi wa sheria na wenyewe usiwe wa kulegalega, usimamizi legelege ni ule kumuona mtu gari lake lina kipara aandikiwe faini halafu aendelee na safari, sasa hapo unakuwa umefanya nini?” anahoji Fungo. 

“Kwa sababu huyu mtu mbele akipata ajali kutakuwa na madhara makubwa lakini ameshakulipa faini yako ya Sh30,000,” anaongeza. “Kwa hiyo, kuna uhitaji kwa Jeshi la Polisi kuwa wakali, yaani kutokuwa na muhali na watu ambao wanaokiuka sheria.”

Mbembela Asifiwe ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mikoa ya kanda za juu kusini. Anapatikana kupitia mbembelaasifiwe@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *