The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Kimekwamisha Mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani Tanzania?

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani wa mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Juni 30, 2021, ikiwa ni baada ya miaka takriban sita ya ushawishi, uchechemuzi na vuguvugu kufanikisha hatua hiyo. Hata hivyo, tangu kusomwa kwake muswada huo ulipotolea kusikojulikana na hivyo hatma yake kutojulikana.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Wadau wa usalama wa barabarani nchini wametaja kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa upande wa Serikali kama sababu kuu ya Tanzania kushindwa kuwa na sheria mpya na ya kisasa ya usalama barabarani ambayo wanaamini ingesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali za barabarani nchini.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani wa mwaka 2021 ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni mnamo Juni 30, 2021, ikiwa ni baada ya miaka takriban sita ya ushawishi, uchechemuzi na vuguvugu kufanikisha hatua hiyo. Hata hivyo, tangu kusomwa kwake muswada huo ulipotolea kusikojulikana na hivyo hatma yake kutojulikana.

“Unapotaka kupitisha sheria kwanza ni lazima kuwe na utayari wa kisiasa,” anasema Augustus Fungo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA-Tanzania). “Lazima Serikali, au wanao fanya maamuzi, wawe na utayari wa kisiasa. Waone kwamba hilo jambo ni moja kati ya vipaumbele.”

Isabella Nchimbi ni Mratibu Miradi kutoka Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA)  ambao kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakipigania kubadilishwa kwa  Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 (Sura ya 168 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002), anasema hajui ni nini kimekwamisha mabadiliko hayo lakini anaamini mchakato unaendelea.

“Mimi najiaminisha kwamba [huu mkwamo] ni sehemu tu ya mchakato wa marekebisho ya sheria husika,” anasema Nchimbi wakati akiongea na The Chanzo. “Wao kama Serikali lazima wajiridhishe kabla ya mchakato hauja endelea mbele.”

Sheria mpya ingeleta mabadiliko gani?

Kwa mujibu wa uchambuzi uliofanywa na TAWLA mwaka 2015, ajali nyingi za barabarani zinazoripotiwa nchini Tanzania huhusisha vitu vifuatavyo: mwendokasi; uvaaji wa kofia ngumu; ufungaji wa mkanda; matumizi ya kilevi; na vizuizi vya watoto. TAWLA na wadau wengine wamekuwa wakihusisha ajali hizi na mapungufu makubwa katika maeneo haya kwenye sheria iliyopo na hivyo kuhitaji yaboreshwe.

Kwa mfano, sheria ya sasa ya usalama barabarani inamtaka dereva wa vyombo vya moto vya magurudumu mawili au matatu kuvaa kofia ngumu lakini haisemi chochote juu ya abiria. Muswada wa mabadiliko ya sheria unatamka kwamba dereva na abiria wanapaswa kuvaa kofia ngumu.

Kwenye eneo la mwendokasi, sheria mpya ingetambua maeneo yote katika kutambua mwendokasi badala ya maeneo ya makazi yanayotambuliwa na sheria ya sasa. Pia, sheria mpya ingezingatia aina zote za magari na sio magari ya biashara, yenye uzito mkubwa na yale yatumikayo kwa usafiri wa umma pekee kama inavyotakiwa na sheria ya sasa.

Sheria mpya pia ingetambua ufungaji wa mikanda kwa abiria wote wa kiti cha mbele na kiti cha nyuma muda wote wa safari, tofauti na sheria ya sasa isiyoweka sharti lolote kwa kwa abiria anayekaa kiti cha nyuma pamoja na watoto.

Kwenye eneo la ulevi, sheria mpya ingeweka kiwango cha kimataifa cha ulevi anaoruhusiwa dereva ambacho ni 0.05g/dl kwa dereva mzoefu na kiwango cha 0.02g/dl kwa dereva asiye mzoefu tofauti na sheria ya sasa ambacho ni 0. 08g/dl.

Kuhusu vizuizi vya watoto, sheria mpya ingetambua umuhimu wa matumizi ya mikanda maalum ya watoto tofauti na sheria ya sasa ambayo ipo kimya kabisa kuhusiana na jambo hilo.

The Chanzo ilimuuliza Waziri wa Katiba na Sheria George Simbachawene ni nini kimezuia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani kuwa sheria kamili ambapo alisema kwamba hawezi kuongea chochote juu ya muswada huo kwani tayari uko mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Alipoulizwa kama ni kweli muswada huo uko mbele ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Joseph Mhagama hakuweza kutoa majibu mpaka wakati wa kuchapisha habari hii.

Sababu za kiuchumi

Mbali na kukosekana kwa utashi wa kisiasa, Fungo, ambaye shirika lake la RSA-Tanzania limekuwa likijihusisha kwa kiasi kikubwa na uhamishaji wa usalama wa barabari kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, anaamini kwamba zipo sababu za kiuchumi pia zinazo fanya marekebisho hayo ya sheria kusuasua.

“Unapotaka kuongeza faini, kwa mfano, ya makosa ya usalama barabarani siyo kitu ambacho kinaweza kikapokelewa kwa urahisi,” anasema, akimaanisha kupandishwa kwa faini kutoka Sh30,000 mpaka Sh200,000. “[Serikali] hapo inafikiria hali ya wananchi. Mwanasiasa anafikiria wapiga kura wake.”

Wakati akiwa na uelewa wa sababu zote hizi, Nchimbi kutoka TAWLA anaamini kwamba juhudi zaidi zinahitajika kufanyika kuishawishi Serikali na wabunge juu ya umuhimu wa kuifanyia marekebisho sheria husika kwani ajali za barabarani zimeendelea kukatisha maisha ya maelfu ya Watanzania huku zikiwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.

Ni katika muktadha huu ndipo mnamo Februari 6, 2022, TAWLA ilifanya kikao na baadhi ya wabunge wa kwa lengo la kuwapitisha kwenye mchakato mzima wa mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani kama sehemu ya kuendeleza jitahada za kupigania mabadiliko hayo.

“[Wabunge] inabidi wajue mapungufu yako wapi, wafahamu mapendekezo ni nini ili na wao waweze kujengea hoja katika hilo eneo pale muswada utakapopelekwa bungeni,” anasema Nchimbi. “Kwa hiyo, hiyo ni moja ya sehemu ya shughuli ambazo tumekuwa tukizifanya kwa muda mrefu.”

Mbunge wa Mlalo (Chama cha Mapinduzi – CCM) Rashid Shangazi alikuwa mmoja kati ya wabunge walioshiriki kwenye warsha hiyo iliyoandaliwa na TAWLA mjini Dodoma ambapo wakati wa kuchangia alikiri kwamba sheria inayotumika sasa ya usalama wa barabarani imepitwa na wakati na hivyo ni lazima ibadilishwe.

“Tusidhani kwamba kuna viongozi wengine wa kufanya wajibu huu; jukumu hili lipo mikononi mwetu,” anasema Shangazi. “Tutapeana namna ya kupaza sauti  jambo hili lirudi [bungeni]. Lakini kwa kuwa kuna mabadiliko ya uongozi katika bunge tutakwenda kuwatambulisha wenzetu hawa wa TAWLA waweze kuwafahamu na waweze kuwaeleza nia njema.”

Jackline Kuwanda mwandishi wa habari wa The Chanzo jijini Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *