The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Matukio ya Ulawiti, Ubakaji Yalivyoendelea Kutikisa Tanzania 2022

Ni hofu ya kila mzazi kuona mtoto wake anakuwa takwimu nyengine ya tatizo hilo linalozidi kukua nchini.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Serikali, wadau wa ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla wanaendelea kukuna vichwa kuona ni njia gani zinaweza kutumika kumuepusha mtoto wa Kitanzania na ukatili, hususan ubakaji na ulawiti, aina mbili za ukatili dhidi ya mtoto zilizoendelea kuitikisa Tanzania mwaka huu wa 2022.

Ripoti za matukio ya ulawiti na ubakaji zilitawala vichwa vya habari mwaka huu, hali inayoendelea kuwajaza hofu wazazi juu ya hatma za watoto wao wa kike na wa wale wa kiume.

Nchini Tanzania kwa mwaka huu wa 2022 ilikuwa ni nadra kwa siku kupita bila kusikia ripoti ya mtoto kubakwa au kulawitiwa, hali inayowatia hamkani Serikali na wadau wengine kutafuta tiba ya janga hilo linalolitafuna taifa.

Ingawaje matukio haya yameripotiwa sana mwaka huu, takwimu zinaonesha kwamba matukio haya yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kwa siku za hivi karibuni na kuufanya mwaka 2022 kama mwaka mwengine tu ulioshuhudia kuongezeka kwa matukio hayo ya aibu.

Wakati The Chanzo imeshindwa kupata takwimu za mwaka 2022, takwimu zilizopo kutoka Jeshi la Polisi zinaonesha kwamba watoto 537 walilawitiwa nchini Tanzania kwa mwaka 2016, idadi ambayo imepanda hadi kufikia watoto 1,114 kwa mwaka 2021, ikiwa ni mara mbili ya ile iliyorikodiwa mwaka 2016.

Kuporomoka kwa maadili

Uchambuzi wa sababu zinazotajwa kuchangia janga hili unaonesha kwamba sababu kubwa inayotajwa kuchochea matukio hayo ni kuporomoka kwa maadili katika jamii, ikifuatiwa na wazazi kukosa muda wa kutosha kukaa na watoto wao kwa ukaribu.

Ni sababu zilizojitokeza kwenye mazungumzo yetu na viongozi waandamizi wa Serikali, Asasi za Kiraia, viongozi wa kijamii, wakiwemo Masheikh na Mapadri. Hata hivyo, kwenye mazungumzo na watu wote hawa, kitu kimoja kikowazi: hawajui nini kinaendelea.

Dk Zainab Chaula ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambaye kwenye mahojiano na The Chanzo hivi karibuni alionesha kuchanganywa na hali hiyo ambayo Serikali imeendelea kubuni mikakati ya kukabiliana nayo.

Dk Chaula alimweleza mwandishi wa makala haya kwamba kasi ya matukio hayo ni ya kustaajabisha, akitoa wito kwa wadau kwamba wanapoyakemea ni vizuri wakaenda mbali zaidi na kupendekeza namna ya kukomesha janga hilo.

“Maana ukipinga tu bila kuonesha unaondoaje, yenyewe si ni changamoto, au unasemaje?” Dk Chaula alimuuliza mwandishi katika hali iliyoonesha masikitiko. “Mimi ninachoweza kusema ni vizuri tukafikiria namna tunavyoweza kuzuia mporomoko wa maadili kwenye jamii zetu. Tuhimize elimu, uwajibikaji na matunzo kwa watoto.”

Gemma Akilimali ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambaye kwenye mazungumzo na The Chanzo hivi karibuni alihusisha kukithiri kwa matukio haya na tabia ya Watanzania ya “kufumbia macho” mambo yanayoonekana kuwa ni ya aibu kwenye macho ya walio wengi, hali anayosema inaanzia kwenye ngazi ya familia.

Tabia ya “kufumbia macho” imelalamikiwa pia na viongozi wa Serikali za Mitaa ambao wamekuwa wakibainisha kwamba hali hiyo imechochea matukio ya ukatili wa kingono – dhidi ya wanawake, mabinti na watoto wa kiume – uendelee kushamiri kwenye jamii.

Hii ilidhihirika hivi karibuni wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kuhusu ukatili dhidi ya watoto wa kiume uliofanyika wakati wa Wiki ya Asasi za Kiraia, hapo Oktoba 27, 2022, jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa mjadala huo, Mtafiti Mwandamizi kutoka LHRC, Fundikila Wazambi, alisema familia kutokuwa tayari kushirikiana na mamlaka za nchi kwenye kukabiliana na tatizo hilo sugu limekuwa ni lalamiko kubwa wao kama shirika wamekuwa wakipokea kutoka kwa mamlaka hizo.

“Usiri huu unashajihishwa na nia ya kutaka kuficha aibu ya familia,” alisema Wazambi wakati wa mjadala huo. “Kwa sababu, kama tunavyojua, wengi kati ya wanaofanya huu ukatili wanakuwa ni ndugu wa karibu – takriban asilimia 66, kwa mujibu wa tafiti zetu– kwa hiyo kunakuwa na ile tabia ya kutaka kufichiana aibu.”

Kinachowaumiza vichwa watu zaidi ni kwamba matukio haya yameendelea kuongezeka licha ya ukweli kwamba Tanzania ina sheria kali za kukabiliana na matukio hayo na adhabu kali kwa wanaothibitika kuyatenda hutolewa kila kukicha.

Nguvu ielekezwe kwenye jamii

Kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali, ilibainika kwamba licha ya adhabu kali zinapaswa kuendelea kutolewa, nguvu zaidi zinapaswa kuelekezwa kwenye jamii ambako matukio haya hutokea ili yazuiwe kabla ya kutokea.

Kalebi Muhawi ni Mchungaji wa Kanisa la TAG ambaye aliiambia The Chanzo hivi karibuni kwamba sheria kali tu peke yake haiwezi kutosha kukabiliana na janga hili linaloiandama Tanzania.

“Tunaona kwamba sheria za kuzuia vitendo hivi zipo lakini vitendo hivyo vinazidi kuongezeka kila kukicha,” Mchungaji Muhawi alisema. “Hebu jamii yetu ijirekebishe, imrudie Mungu, watu wawe na ile hofu ya Mungu, na mwisho wa siku itasaidia wakaachana na vitendo kama hivi.”

Suala la kuongeza nguvu kwenye jamii limejitokeza miongoni mwa wadau wengi ambao The Chanzo imeongea nao kuhusiana na suala hili.

Rabia Saad ni Mkurugenzi Mtendaji wa Action Girls Foundation, shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na utetezi wa watoto ambaye anaamini kwamba ili jamii iweze kutoa mchango stahiki kwenye kukomesha janga hili wazazi ni lazima wawe mstari wa mbele.

Kwa mujibu wa mdau huyo, wazazi wameonekana kuwa na muda mchache sana wa kuzungumza na kuwadadisi watoto wao, hali inayowapelekea kugundua tatizo kwa kuchelewa sana.

“Juzi nilisikia kuna tukio limetokea, mzazi alikuwa anasema mpaka mtoto alikuwa ameoza,” Saad aliiambia The Chanzo hivi karibuni. “Mtoto anamuambia mama yake natoa funza huku nyuma, nashindwa kutembea. Na huyu mama alikiri kwamba ni kweli mtoto yuko hivyo lakini hajui sababu ni nini.”

“Wazazi na walezi inaonekana wana nafasi ndogo ya kuzungumza na watoto wao mpaka kuweza kutambua mtoto amepata changamoto kama hiyo,” aliongeza Saad. “Wazazi wawaambie watoto wasiguswe kwenye viungo vyao vya siri. Hiki ni kitu cha muhimu sana, waongee nao mara kwa mara wanapotoka shule.”

Dk Chaula mwenyewe anakiri kwamba sheria na kanuni kali tu peke yake hazitatosha katika kukabiliana na wimbi hili la ubakaji na ulawiti wa watoto. 

Afisa huyo mwandamizi wa Serikali anasema anakubaliana na maoni ya wadau kwamba ni muhimu pia uwekezaji ufanyike kwenye kuielimisha jamii.

“Tuongee mambo mema ya kuwatengeneza watoto,” Dk Chaula anashauri. “Turudi kwenye uwajibikaji wa matokeo. Tuachane na ulevi uliopitiliza. Watoto wahamasishwe kwenda kwenye madrasa, wahamasishwe kwenda kwenye kanisa, tuwatunze.”

Jackline Kuwanda ni Mwandishi wa Habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts