Dare es Salaam. Umeshawahi kudhani kwamba kadiri tatizo linavyoripotiwa na, tuseme, Jeshi la Polisi au vyombo vya habari, ndivyo linavyoweza kuzidi kukua na kutamalaki zaidi katika jamii husika?
Angalau hivyo ndivyo Spika wa Bunge Tulia Ackson anaamini kuhusiana na wimbi la mauaji holela yaliyoikumba na kuitikisa Tanzania mwaka 2022.
Licha ya kwamba baadhi ya watu walimshangaa Dk Ackson, kauli yake hiyo ilidhihirisha ni kwa kiwango gani matukio hayo yamewachanganya watu wengi nchini.
Ukweli ni kwamba, kauli ya kiongozi huyo wa mhimili wa kutunga sheria ilikuja miezi kadhaa baada ya Makamu wa Rais Dk Philip Mpango kuzungumza hadharani kwamba yeye binafsi na Rais Samia Suluhu Hassan wamechoka kusikia ripoti za mauaji kila siku.
Mpango alitoa kauli hiyo hapo Januari 26, 2022, baada ya kutembelea kijiji cha Zanka, mkoani Dodoma ambapo iliripotiwa kwamba watu watano waliuawa na watu wasiojulikana.
Tatizo hili ni kubwa sana kiasi cha kuipelekea Serikali kuunda tume maalum kuchunguza nini kipo nyuma ya wimbi hilo la mauaji na kupendekeza namna bora za kukabiliana na janga hilo.
Tume hiyo iliyowasilisha ripoti yake bungeni hapo Septemba 14, 2022, ilitaja sababu zilezile ambazo zimekuwa zikihusishwa na mauaji hayo, kubwa yao ikiwa ni watu kujichukua sheria mikononi, kunakosababishwa na wivu wa mapenzi na ushirikina.
Ripoti ya tume hiyo, hata hivyo, haikutolewa kwa umma, huku Serikali ikiahidi kutekeleza mapendekezo yake, na kwamba itaitoa ripoti hiyo kwa umma ikiona kama inafaa kufanya hivyo.
The Chanzo ilishindwa kupata takwimu sahihi za idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na wimbi hili la mauaji holela linaloendelea kuikumba nchi.
Lakini kwa mujibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), haki ya kuishi ndiyo haki iliyoongoza kukiukwa nchini Tanzania kwa mwaka 2022.
Akizungumza wakati wa hafla iliyoandaliwa na LHRC ya kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu 2022, Mkurugenzi wa LHRC Anna Henga alisema kwamba tathmini hiyo imetokana na ufuatiliaji wa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu yaliyokuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari.
“Kwa mwaka huu tukitathmini kwa haraka haraka, haki za binadamu zilizovunjwa sana ni haki ya kuishi,” alisema Henga wakati wa hafla hiyo.
“Mauaji ya wenza yamekuwa mengi. Mauaji ya kujiua watu wenyewe yamekuwa mengi. Lakini pia, mauaji yanayotokana tu na imani za kishirikina pia yamekuwa mengi,” aliongeza Henga.
Yafuatayo ni baadhi tu ya matukio ya mauaji yaliyoishtusha nchi kwa mwaka 2022:
- Mauaji ya watu watano wa familia moja Dodoma
Mnamo Januari 23, 2022, watu watano wa familia moja, wakazi wa kijiji cha Zanka, wilayani Bahi, mkoani Dodoma walikutwa wameuawa ndani ya nyumba yao, huku miili yao ikikutwa tayari imeharibika.
Haikujulikana mara moja ni nani aliyetekeleza mauaji hayo na kwa nini, hali iliyopelekea Serikali mkoani Dodoma, pamoja na Jeshi la Polisi, kuanza uchunguzi juu ya tukio hilo ambalo Makamu wa Rais Philip Mpango alilieleza kama la “kinyama.”
Ni wakati akizungumzia tukio hili ndipo Dk Mpango aliposema yeye na Rais Samia wamechoka kusikia ripoti za muaji, akilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi usiku na mchana kuwatia mbaroni waliohusika na tukio hilo la kutisha.
- Mama adaiwa kuwaua watoto wake wawili Mbeya
Mnamo Novemba 23, 2022, Shani Yohana, mkazi wa Mbeya, alishikiliwa na polisi kwa madai ya kuwaua watoto wake wawili kwa kuwacharanga na mapanga mpaka kufa. Haikujulikana mara moja chanzo cha mauaji hayo sasa kilikuwa ni kipi.
- Aua mke, watoto wawili kabla ya kujiua mwenyewe Mbeya
Mnamo Septemba 14, 2022, ziliibuka taarifa kutoka kitongoji cha Kibumbe, kata ya Kiwira, wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya zilizodai kwamba mke, mume na watoto wawili wakutwa wamefariki ndani ya nyumba na miili yao ikiwa imeharibika.
- Amuua mkewe kwa risasi saba, ajiua pia
Mnamo Mei 28, 2022, majira ya usiku, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Said Oswayo anadaiwa kumuua mkewe Swalha Salum, 28, kwa kumpiga risasi kadhaa katika tukio lililotokea nyumbani kwao eneo la Mbogamboga, Buswelu wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Siku moja baada ya kutekeleza uhalifu huo, Oswayo, aliyekuwa akijishughulisha na biashara, alikutwa pia ameuawa kwa kile polisi walieleza kwamba ni kuchukua uhai wake mwenyewe.
Kabla ya mauaji hayo, iliripotiwa kwamba wanandoa hao waliofunga pingu za maisha Desemba 31, 2021, walikuwa na ugomvi unahusishwa na wivu wa kimapenzi.
- Mabinti watatu wachinjwa Mwanza
Mnamo Novemba 23, 2022, iliripotiwa taarifa iliyohusisha mauaji ya kinyama ya mabinti watatu kutoka mkoani Mwanza ambao baada ya kuuwawa walitupwa kando ya mto wakiwa wamevuliwa nguo zao zote.
Polisi hawakusema nini kilipelekea ukatili huo, wakisema watachunguza zaidi na kuwafikisha wote waliohusika mbele ya vyombo vya sheria.
Ni ngumu kwa sisi kuweka orodha ya matukio yote ya mauaji yaliyoripotiwa nchini Tanzania kwa mwaka 2022. Vilevile, haya ni yale mauaji yaliyohusisha raia na raia tu, bila kuorodhesha yale matukio yaliyohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Wakati wadau wakiendelea kuumiza vichwa wakitafakari ni namna gani bora ya kukabiliana na janga hili, utafiti mdogo wa The Chanzo umebaini uwepo wa uhusiano kati ya matukio haya na masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo husika.
SOMA ZAIDI: Nini Kinachochea Mauaji Holela Yanayoendelea Kuitesa Tanzania?
Kwa mfano, tafiti za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinabainisha kwamba ukatili wa kijinsia uko juu mkoani Shinyanga, ambapo asilimia 78 ya wanawake walio katika ndoa mkoani humo wanapitia ukatili wa kijinsia.
Shinyanga inafuatiwa na Tabora (asilimia 71), Kagera (asilimia 67) na Simiyu (asilimia 62). Kwa mujibu wa uchambuzi wa The Chanzo, maeneo yote haya yamerekodi kisa cha mume kuua mke, pengine na watoto kati ya matukio 37 yaliyoripotiwa.
Kwa mfano, huko mkoani Simiyu, Golani Nh’umbu, 35, alimuua mke wake, Pili Masonga kwa kumkata mapanga wivu wa mapenzi ukitajwa.
Mkoani Shinyanga, Lima Kulwa, 30, aliuliwa na mume wake kwa kushukiwa kuwa ni mchawi. Mkoani Kagera nako, Odilia Rukasi, 47, aliuwawa na mume wake Clemence Mdende, 51, sababu ikiwa ni wivu wa mapenzi.
Wito umetolewa kwa wananchi kurudi kwenye msingi wa jamii inayojali utu, huku vyombo vinavyohusika na ulinzi na usalama wa wananchi vikitakiwa viwajibike, na kukataa kasumba ya ukatili na kutokujali.
Hadija Said ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam anayepatikana kupitia hadijasaid826@gmail.com.