Tumbatu/Zanzibar. Kisiwa cha Tumbatu, chenye watu wapatao 25,000, 13,659 wakiwa ni wanawake, hakina kituo kinachotoa huduma ya kujifungua na hivyo kuwalazimisha wajawazito kisiwani hapa kujifungulia nyumbani au kufunga safari ndefu na isiyo salama kwenda kujifungulia nje ya kisiwa hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, akina mama wajawazito wa Tumbatu, moja kati ya visiwa vikubwa vinavyounda kisiwa cha Unguja, walikuwa wanahudumiwa na vituo viwili vikubwa vya afya, kile cha Gomani na kile cha Jongowe.
Hata hivyo, vituo vyote viwili kwa sasa vimeacha kutoa huduma ya mama na mtoto kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kukosekana kwa wahudumu.
Dk Yusuph Machano ni Afisa Tabibu Mkuu wa Kituo cha Afya cha Gomani ambaye ameithibitishia The Chanzo kusitishwa kwa huduma za kujifungua katika kituo hicho kutokana na uhaba wa wataalamu.
“Tupo wawili tu [hapa kituoni] kwa sasa,” Dk Machano alieleza. “Hali hii ya hiki kituo inaumiza zaidi wanawake wajawazito maana wapo hatarini.”
Kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya ya Zanzibar, Kituo cha Afya kama cha Gomani kinahitaji wauguzi nane na madaktari watatu ili kiwe katika nafasi nzuri ya kuhudumia watu. Kwa sasa, hata hivyo, kituo hicho kina muuguzi mmoja na daktari mmoja tu!
Hali hii ya kukosekana kwa wahudumu kwenye vituo vya afya kumewarudushia wakunga wa jadi umuhimu wao uliokuwa unapotea kwa kasi kwani sasa wamekuwa wakiitwa mara kwa mara kusaidia mama mjamzito kujifungua nyumbani.
Moja kati ya wakunga hawa wa jadi ni Khalida Mfaume, mkunga wa jadi wa siku nyingi, ambaye huduma yake imekuwa ikihitajika mara kwa mara. Ingawaje Khalida, 52, anajiamini kwenye kazi yake, si kitu anachokifanya kwa kujivunia.
“Mimi ni mzoefu wa kazi hii lakini siyo kitu ambacho nakifanya kwa kujivuna,” Khalida aliiambia The Chanzo ilipomtembelea nyumbani kwake. “Tunalazimika kuifanya kwa sababu huduma hakuna, hospitalini hakuna wahudumu. Vituo vya afya vipo lakini havifanyi kazi.”
Kwa baadhi ya akina mama waliolazimika kujifungulia nyumbani kutokana na changamoto hiyo, huo si uzoefu ambao wanatamani kuurudia tena, wakiiangukia Serikali kuviwezesha vituo vya afya vilivyopo kisiwani hapa ili waweze kujifungulia sehemu salama.
Miza Hassan ni mama wa mtoto mmoja wa kiume mwenye wiki mbili sasa ni miongoni mwa wanawake waliowahi kujifungulia nyumbani.
The Chanzo ilimkuta Miza, 20, akiwa amelala kwenye mkeka huku mtoto wake akiwa amelala chumbani. Wiki mbili zilizopita zilikuwa ni kama usiku wenye kutisha kwa Miza baada ya kulazimika kujifungulia nyumbani.
Roho mkononi
“Ilikuwa asubuhi, hali yangu ilibadilika kidogo ndiyo nikaambiwa kuwa safari ya kujifungua ikaanza,” anakumbuka Miza. “Mama yangu alikuwepo na bibi mmoja wakanisaidaia kujifungua. Ila roho ilikuwa mkononi. Si haba sote wazima.”
Shufaa Said Kombo ni mama wa watoto sita anayetarajia wa saba ifikapo hapo Februari 2023, mzazi mwengine aliyelazimika kujifungulia nyumbani watoto wake wawili kutokana na kukosekana kwa huduma ya kujifungulia kwenye kituo cha afya kilicho karibu naye.
“Nilipoteza mpangalio wangu wa tarehe, hivyo nikajifungulia nyumbani,” Shufaa, 30, anasimulia. “Ni hatari maana mimba ya pili nusra nife. Mtoto alikwama, bahati nzuri mkunga [wa jadi] akanisaidia.”
Hali hii ya kuwa na hofu ya kujifungulia nyumbani imewafanya baadhi ya akina mama wajawazito hapa Tumbatu kusema kwamba iwe itakavyokuwa ni lazima wakajifungulie nje ya kisiwa ili kuepuka kujifungulia nyumbani.
Moja kati ya wajawazito hao ni Mwajuma Ismail ambaye baada ya miaka mitano ya ndoa yake mwaka huu wa 2022 ndiyo kabahatika kupata ujauzito. The Chanzo ilimkuta Mwajuma, 32, akiwa kwenye foleni ya kuonana na mhudumu katika Kituo cha Afya cha Gomani.
Naogopa sana
“Mimi siwezi kuzalia nyumbani, naogopa sana,” Mwajuma aliiambia The Chanzo akiwa amebaki kwenye foleni yake. “Nitaondoka wiki mbili kabla, niende mjini, ili nizalie sehemu salama. Nina hofu ya kumpoteza mtoto wangu.”
Mwajuma hatakuwa mjamzito peke yake kuikimbia Tumbatu kwa ajili ya kutafuta sehemu salama zaidi ya kujifungulia.
Uchunguzi wa The Chanzo umebaini kwamba wajawazito wengi hulazimika kuvuka maji wakiwa kwenye siku za mwisho za ujauzito wao ili kwenda kutafuta sehemu salama ya kujifungulia.
Wengi wanaotoka nje ya Tumbatu huenda Mkokotoni, safari inayochukua wastani wa dakika 30 kwa kutumia boti za abiria.
Kwa kawaida, mashua hizi ili zianze safari ni lazima ziwe na abira wasiopungua 15 lakini huweza kukodiwa kusafirisha mama mjamzito kwa Sh20,000.
Baada ya kufika bandarini Mkokotoni, familia hulazimika kukodi gari ili iwafikishe kwenye kituo cha afya, ambayo hugharimu Sh15,000.
Hassan Kassimu ni nahodha wa mashua hapa Mkokotoni. Akiwa na miaka mitano ya kufanya kazi hii, Kassimu anaiambia The Chanzo kwamba wakati mwengine huamshwa usiku kuwapeleka wanawake wajawazito mjini ili waweze kujifungua.
“Tunambeba [mama mjamzito] na kumpandisha kwenye mashua na kuanza safari,” anaeleza nahodha huyo.
“Hata wakati mwengine usiku nakuwa nafanya hivyo,” anaongeza. “Ni hatari kwa mama na mtoto na ikatokea bahati mbaya maanake hakuna mtu wa kumsaidia humu kwenye mashua hii.”
The Chanzo ilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud kama analifahamu tatizo hili na kama kuna mkakati wowote Serikali imepanga kuchukua kulitatua ambapo alikiri kulifahamu.
“Ni kweli Kituo [cha Afya cha Gomani] kimefungwa kwa sababu hakuna wahudumu wa afya,” Mahmoud alisema kwenye mahojiano na mwandishi wa habari hii. “Ila suala hili tumeshalipeleka wizarani na mchakato wa ajira kwa wahudumu wa afya unaendelea.”
Mahmoud anaamini kwamba kwenye mchakato wa ajira wa wahudumu wa afya unaoendelea hivi sasa Zanzibar na wao Mkoa wa Kaskazini Unguja watapata ili wawapeleke Tumbatu “ili kuokoa maisha ya mama na mtoto,” anasema.
Juhudi zetu za kumpata Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui hazikufua dafu baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
The Chanzo ilitaka kufahamu tatizo la upungufu wa wahudumu wa afya ni kubwa kiasi gani Zanzibar na ni mikakati gani ipo inayolenga kutatua tatizo hilo.
Sehemu ya tatizo kubwa
Hata hivyo, Katibu wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Muhidini Ussi Haji aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano naye kwamba Zanzibar kwa sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wauguzi, hali inayoathiri utoaji mzuri wa huduma za afya visiwani humo.
Kwa mujibu wa Juma, idadi ya wahudumu wa afya waliopo Zanzibar kwa sasa hawafiki 2,500, huku akibainisha kwamba wahudumu wanaohitajika ili huduma za afya zitolewe vizuri ni wahudumu 5,000.
“Uhaba huu unasababisha madhara makubwa kwenye sekta ya afya maana wakati mwengine unakuta muuguzi mmoja anafanya kazi ya kushughulikia wodi tatu mpaka nne,” alisema Haji.
“Tumeshalifikisha suala hii katika ngazi mbalimbali na Serikali inaendelea kuajiri [wahudumu] lakini bado kuna upungufu mkubwa,” aliongeza.
Najjat Omar ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com.