The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti

Sekta ya utafiti Tanzania inakabiliwa na changamoto kadhaa, moja wapo ni uwekezaji mdogo.

subscribe to our newsletter!

Utafiti ni moja ya vichocheo vikubwa vinavyochochangia maendeleo ya dunia kutokana na mchango wake katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, afya, kilimo, uchumi, teknolojia nakadhalika.

Utafiti umetumika katika kubaini matatizo na kupendekeza suluhu ya matatizo hayo. Pia, umetumika kutabiri matokeo mbalimbali yanayoweza kujitokeza kwa wakati ujao.

Nchi nyingi zilizoendelea zimewekeza katika utafiti na matokeo yake yamekuwa chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizo. Nchi hizo ziliweza kuwekeza sehemu kubwa ya pato lao la taifa wa ajili ya maendeleo.

Ripoti zinaonesha kwamba nchi za Switzerland, Korea Kusini na Israel kama nchi zinazoongoza kwa kutenga zaidi ya asilimia moja ya pato lake kwa ajili ya utafiti na maendeleo.

Nchi hizo zimeweza kupiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na uwekezaji wake mkubwa katika utafiti. Wakati nchi mbalimbali barani Ulaya na Asia zikionekana kuwekeza katika utafiti kwa kiasi kikubwa, nchi za bara la Afrika bado uwekezaji wake ni wa kiwango cha chini.

Pamoja na makubaliano ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2006 yaliyofanyika Khartoum, Sudan ya nchi wanachama kutenga asilimia moja ya pato la taifa kwa ajili ya utafiti na maendeleo, ni nchi chache tu ambazo zimeweza kuwekeza kwa zaidi ya nusu ya makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa ripoti ya UNESCO ya mwaka 2021, nchi hizo ni Kenya iliyowekeza kwa asilimia 0.8, Afrika Kusini kwa asilimia 0.75 na Misri kwa asilimia 0.6 na nchi nyingine zilizobaki bado ziko chini.

Tanzania hali tete

Tanzania kama nchi nyingine duniani ilitambua umuhimu wa utafiti katika sera yake ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996. Katika sera hiyo, moja ya malengo ni kuwekeza kwenye utafiti kwa asilimia moja ya pato la taifa.

Ili kuweza kufikia malengo yake, Tanzania iliweza kuanzisha taasisi mbalimbali za utafiti katika sekta mbalimbali.

Uwepo wa taasisi hizo umekuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi kwa kutatua matatizo mbalimbali kupitia tafiti ambazo zimekuwa zikifanyika na kutoa mwongozo au ushauri kwa masuala mbalimbali nchini.

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu

Kwa mfano, Taasisi ya Utafiti ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ni baadhi ya taasisi zilizoanzishwa na Serikali na taasisi hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya afya na kilimo.

Pamoja na jitihada hizo za Serikali, bado uwekezaji katika sekta ya utafiti ni mdogo ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika ambazo zimeweza kuvuka nusu ya asilimia moja.

Kwa mujibu wa UNESCO, Tanzania imewekeza asilimia 0.5 ya makubaliano ya Umoja wa Afrika ambayo ni kuwekeza asilimia moja ya pato la taifa. Mbali na changamoto hiyo, sekta ya utafiti bado inakabiliwa na changamoto nyengine kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti ya SRIA-Programme ya mwaka 2019 iliyofanya tathmini juu ya mahitaji ya mfumo wa utafiti Tanzania, changamoto mbalimbali zilibainishwa.

Changamoto moja wapo ni kutokuwepo kwa mfumo kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ndani wa utafiti, kwamba bado Serikali haijaweka mazingira wezeshi kwa ajili ya mfumo wa ndani wa shughuli za utafiti na badala yake shughuli hizo zimekuwa zikifanywa na wafadhili kutoka nje.

Pia, kutokuwepo kwa miundombinu inayotosheleza kwa ajili ya shughuli za utafiti ambapo mazingira ya kufanyia utafiti yameelezwa kuwa siyo rafiki kwa sababu ya uhaba wa miundombinu mbalimbali ambayo ni muhimu katika kufanya shughuli hizo.

Changamoto nyingine ni uwezo mdogo wa kufadhili shughuli za utafiti hali inayotokana na Serikali kutenga kiwango kidogo cha fedha kwa ajili ya utafiti.

Wakati mwingine taasisi za utafiti zinashindwa kutekeleza majukumu yake, au kutegemea ufadhili kutoka nje. Ripoti hiyo inaonesha kwamba Tanzania imekuwa ikifadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweden (SIDA) na Benki ya Dunia.

Bado uwezo wa kuwajengea uwezo watafiti pia ni mdogo, huku watafiti wakielezwa kutokupata mafunzo mbalimbali ya kutosha ya kujengewa uwezo ili kuimarisha uwezo wao katika kufanya shughuli zao za kila siku.

Kuna changamoto ya uhaba wa watafiti pia. Ripoti hiyo ya SRIA- Programme inaonesha kwamba Tanzania ina watafiti 18.3 kwa watu milioni moja.

Kwa mujibu wa viwango vya UNESCO, hiki ni kiwango kidogo kwa nchi kwani kwa Afrika inatakiwa kuwa na wastani wa watafiti 95.1 kwa watu milioni moja.

Pia, tafiti zinazofanyika bado hazifanyiwi kazi. Inaonekana pamoja na taasisi nyingi kujitahidi kufanya tafiti katika sekta mbalimbali, matokeo ya tafiti hizo yamekuwa hayafanyiwi kazi kwa kiasi kikubwa.

Utafiti na maendeleo

Kwa hiyo, Serikali inalo jukumu la kuhahikisha inafanyia kazi changamoto hizo zilizoibuliwa kwenye ripoti mbalimbali. Hii ni kwa sababu upo ushahidi wa wazi kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya  utafiti na maendeleo.

Tafiti zinaonesha kwamba baadhi ya nchi za bara la Asia (Asian Tiger Countries) maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii yalitokana na uwekezaji wao mkubwa waliofanya kwenye eneo la utafiti.

Vilevile, katika sayansi ya sera za umma upo ushahidi kwamba utafiti ni nguzo muhimu katika kutunga sera ambazo zinaweza kuwa na matokeo chanya kwa taifa.

Kwa ushahidi huu, basi Serikali haina budi kulichukulia suala hili kwa uzito zaidi ili kuweza kupiga hatua kwenye sekta mbalimbali.

Chagulani Shabiru ni mhitimu wa Shahada ya Uzamili katika Utafiti na Sera za Umma, Chuo Kikuu Mzumbe. Unaweza kumpata kupitia au Twitter kama @Chagulanishabie. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *