The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Mjamaa Lula Atainusuru Demokrasia Brazil?

Mwanasiasa huyo wa mrengo wa kushoto anakabiliwa na mtihani mzito wa kurekebisha makosa ya mtangulizi wake, Jair Bolsonaro.

subscribe to our newsletter!

Mnamo mwaka 2019 niliandika makala kwenye gazeti moja la nchini Tanzania, punde tu baada ya kuingia madarakani kwa Rais Jair Bolsonaro, huko nchini Brazil, ambaye hadi Disemba 31, 2022, alikuwa kiongozi wa taifa hilo, nikimwita “Donald Trump wa Brazil.”

Nilimwita hivyo kutokana na aina yake ya uongozi iliyoandamana na maamuzi ya kibabe. Kimsingi, Bolsonaro mwenyewe alielezea hadharani kwamba yeye alikuwa ni mfuasi wa Trump, Rais wa 45 wa taifa la Marekani aliyeondoshwa madarakani na Joe Biden kwenye uchaguzi uliofanyika Novemba 3, 2020.

Akiwa madarakani, Bolsonaro, kapteni wa jeshi mstaafu aliyegeuka kuwa mwanasiasa, anaripotiwa kukandamiza haki za wakaazi asilia; aliendekeza ubaguzi dhidi ya Wabrazil waliochanganya damu; na aliyakumbatia makampuni makubwa yaliyokuwa mstari wa mbele kuifyeka misitu ya Amazon.

Kwa maneno mengine, Bolsonaro, 67, ambaye ni mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, alikuwa ni dikteta mkamilifu, asiyeamini kwenye sayansi na kwenda mbali zaidi hata kukanusha uwepo wa janga la UVIKO-19 nchini mwake na kupelekea maafa makubwa kwa wananchi wa Brazil.

Akiwa Rais wa Brazil, Bolsonaro aliwakumbatia majenerali wa kijeshi na kujinasabisha na Wabrazil wahafidhina weupe. Bolsonaro alimteuwa pia jenerali mstaafu kuwa mgombea wake mwenza. 

Katika kipindi cha miaka yake minne madarakani,  majenerali na maafisa wengine wa vyeo vya juu, walijitajirisha kupita kiasi na Bolsonaro alilipa jeshi  fursa ya kujipatia tija mbalimbali, akitumai litamsaidia aendelea kubaki madarakani. Kitu ambacho, hata hivyo, hakikutokea.

Kwa kuheshimu ule usemi usemao umma ndiyo wenye usemi na maamuzi ya mwisho, lazima yaheshimiwe, jeshi la Brazil lilikataa kuzuwia demokrasia isifuate mkondo wake. 

Lilikataa kuiona Brazil ikirudi katika enzi za kiza kinene, wakati ilipokuwa moja wapo ya nchi kadhaa za Amerika Kusini zilizokuwa na tawala za kidikteta za kijeshi, ikitumbukia kwenye janga hilo baada ya mapinduzi ya kijeshi ya 1964.

Jinamizi limekwisha

Ni katika muktadha huu ndipo mamilioni ya Wabrazil na wapenda demokrasia ulimwenguni kote walipopata fursa ya kuvuta hewa safi hapo Januari 1, 2023, baada ya utawala wa Bolsonaro kuhitimishwa kwa kuapishwa kwa Luiz Inácio “Lula” da Silva kama Rais mpya wa taifa la Brazil.

Lula, 77, amekuwa Rais kwa muhula wa tatu wa taifa hilo la Amerika Kusini baada ya kumuangusha Bolsonaro kwenye ngwe ya pili ya kinyang’anyiro cha urais hapo Oktoba 30, 2022. Mihula miwili ya kwanza ya urais wa mwanasiasa huyo wa mrengo wa kushoto ilikuwa ni kati ya 2003 na 2010.

Maelfu ya wafuasi wa Lula walijitokeza kwenye hafla ya uapisho wa mwanasiasa huyo iliyofanyika katika mji mkuu Brasilia, wakiipamba shughuli hiyo kwa nyimbo, shangwe na vifijo, wakiamini kwamba Lula atarekebisha makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake kwa kipindi cha miaka minne.

Sehemu ya furaha hiyo, bila shaka, ilichangiwa na kushindwa kwa jitihada za dola za Brazil za kutaka kumzuia Lula asigombee kwa kumfungulia mashtaka ya ufisadi alipokuwa madarakani. 

Licha ya kuhukumiwa kwenda jela miaka tisa na nusu, Lula aliachiwa huru 2019 baada ya hukumu kubatilishwa na Mahakama Kuu, alishiriki uchaguzi na sasa ni Rais wa nchi hiyo.

Wakati Lula akiapishwa kushika hatamu, Bolsonaro, ambaye pingamizi zake dhidi ya ushindi wa Lula zilikataliwa na Mahakama, hakuhudhuria hafla hiyo na kukimbilia nchini Marekani.

Lula, mjamaa na mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi (PT), alikielezea kipindi cha utawala wa Bolsonaro kama “zama za giza na mateso tele,” huku wakiwatoa hofu wafuasi wake kwa kuwaambia kwamba “hili jinamizi limekwisha.”

Kazi zinazomsubiri Lula

Machozi yaliyokuwa yanawatoka wafuasi wa Lula wakati mjamaa huyo akitoa hotuba yake punde baada ya kuapishwa, bila shaka yalikuwa ni machozi ya furaha. Hii, hata hivyo, haimaanishi kwamba mambo yanaenda kuwa rahisi kwa Lula.

Moja kati ya changamoto kubwa zinazomkabili Rais Lula hivi sasa ni kurudisha mshikamano katika jamii ya Wabrazil ambayo imegawanyika vibaya kutokana na miaka minne ya  mtangulizi wake, mgawanyiko mkubwa ukiwa ni wa kiitikadi/kisiasa.

Mengine makubwa ni kupambana na njaa na umasikini, uhalifu mkubwa wa makampuni makubwa katika mkoa wa Amazon na kuwalinda wakazi asilia wa eneo hilo. Amazon linautajiri mkubwa wa misitu ya mvua. Mafanikio katika hilo yataisaidia Brazil kupunguza  gesi zinazoharibu mazingira.

Vizingiti ambavyo Lula atapaswa kuvivuka ni vingi na kukabiliana navyo kutahitaji fedha, lakini umma umempa ridhaa kwa kumchagua na kuinusuru demokrasia ili akabiliane navyo.

Lula mwenyewe anasema mambo makuu matatu atayapa kipaumbele kwenye utawala wake: maridhiano ya kisiasa, utunzaji mazingira na haki jamii, au social justice kama haki hizo zinavyojulikana kwa kimombo.

“Siyo maslahi ya yoyote kati yetu kuiona nchi yetu ikiwa kwenye mivutano isiyokwisha,” Lula alisema kwenye hotuba yake punde tu baada ya kuapishwa, akiwataka wafuasi wake kujenga ushirikiano na urafiki miongoni mwao. “Hakuna Brazil mbili. Sisi sote ni wa moja.”

Hamasa nje ya Brazil

Sina shaka raia katika nchi nyengine za kanda hiyo ya Amerika Kusini watakuwa wameyafuatilia kwa karibu matokeo hayo, kwa maana kwamba kutakuwa na hisia za mchanganyiko, furaha na majonzi. 

Kati ya nchi 12 za Amerika Kusini,  saba zina tawala za mrengo wa kushoto, kuanzia Venezuela, Mexico, Argentina, Bolivia, Chile, Colombia, Honduras na sasa Brazil.  

Nchi hizo zote zinazungumza Kihispanol (Spanish)  kutokana na kutawaliwa na Hispania isipokuwa Brazil inayzungumza Kireno kwa sababu ya kutawaliwa na  Ureno.

Nchi zote, hata hivyo, miongo mingi iliyopita zilikuwa  na tawala za kidikteta na nyingi za kijeshi, zikiiga mtindo uliokuwa umeenea katika nchi zilizowatawala. Hispania ilikuwa na dikteta Fransisco V na Ureno,  Antonio Salazar na Marcelo Caetano.

Hispania na Ureno pia zilitawala Afrika. Hispania katika Guinea ya Ikweta (Equtorial Guinea) na pia Sahara Magharibi na Ureno katika yale mataifa matano yaliyojikomboa kwa mtutu wa bunduki: Angola, Msumbiji, Guinea Bissau, Cape Verde na Sao Tome na Principe. 

Kuanguka kwa udikteta katika mataifa hayo mawili ya Ulaya kulifungua pia enzi mpya ya demokrasia katika mataifa hayo.

Bila shaka macho na masikio yote yataelekezwa nchini Brazil kwa siku zijazo, kuona kama kweli Lula ataweza kurekebisha makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake na hivyo kuwapatia Wabrazil na wapenda demokrasia duniani kote tumaini jipya.

Kazi, bila shaka, haitakuwa rahisi, lakini, kama tusemavyo Waswahili, penye nia, pana njia. Kila la kheri Lula, kila la kheri Brazil!

Mohammed AbdulRahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mammkufunzi@outlook.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com  kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts