The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mheshimiwa Rais Samia, Unaiona Lakini Hali ya Elimu ya Sekondari Tanzania?

Kuongeza idadi ya wanaoenda shule bila kuboresha mazingira yaliyopo, tunaendelea kulitumbukiza taifa letu kwenye umaskini.

subscribe to our newsletter!

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, niruhusu niungane na Watanzania walio wengi kukupa salamu za siku kuu za mwisho wa mwaka na kukutakia afya tele katika utendaji wako wa kazi.

Siku za hivi karibuni nimeona watu kwenye mitandao ya kijamii wakiziimba sifa zako kwa wingi, huku wakikupongeza kwa “kuifungua nchi” kiuchumi na wengine wakisema kwamba unaonesha tumaini katika masuala ya demokrasia. 

Hata hivyo, kundi ambalo limenigusa ni lile linaloziimba sifa zako katika masuala ya elimu, huku wakitaja mambo kama vile kuongeza kiasi kikubwa cha fedha za mikopo ya elimu ya juu; kujenga vyumba vipya 15,000 vya madarasa; kuongeza udahili mara dufu; pamoja na kufungua ajira za walimu. 

Kama mdau wa elimu, niliguswa na sifa hizi nami nikatamani kukupongeza, lakini kabla ya kufanya hivyo, niliamua kupitia takwimu ili kujiridhisha na kile kinachoongelewa. Hata hivyo, Mheshimiwa Rais, nachelea kusema takwimu nilizoziona zinanipa wasiwasi kuhusu maendeleo ya elimu yetu badala ya kunifurahisha.

Mheshimiwa Rais, wasiwasi wangu mkubwa unaanzia kwenye uwiano kati ya wanafunzi na walimu katika shule za sekondari. Mwaka 2017, shule za sekondari za Serikali na binafsi Tanzania zilikuwa na wanafunzi 1,908,857 waliokuwa wanahudumiwa na walimu 110,163 (BEST, 2017, p. 85). 

Kati yao, wanafunzi 1,565,201 walikuwa katika shule za Serikali wakihudumiwa na walimu 89,475, huku shule binafsi zikiwa na wanafunzi 343,656 waliohudumiwa na walimu 20,688 (BEST, 2017, p. 124).

Ilipofika mwaka 2020, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 1,908,857 hadi 2,473,506, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 564,649 ndani ya miaka mitatu (BEST, 2020, p. 214). 

Ongezeko hili la wanafunzi lilizihusisha shule za sekondari za Serikali pekee ambazo idadi yake ya wanafunzi ilipanda kutoka wanafunzi 1,565,201 mwaka 2017 mpaka kufikia wanafunzi 2,172,257 mwaka 2020, huku wanafunzi katika shule za binafsi wakipungua kutoka wanafunzi 343,656 mwaka 2017 mpaka wanafunzi 301,249 mwaka 2020. 

Cha ajabu, walimu katika shule za sekondari za Serikali walipungua kutoka walimu 89,475 mwaka 2017 mpaka kufikia walimu 84,614 mwaka 2020, huku walimu wa shule binafsi wakiongezeka kutoka walimu 20,688 mwaka 2017 na kupanda kufikia walimu 21,392 mwaka 2020 (BEST, 2020, p. 282, 286). 

Mheshimiwa Rais, katika kipindi cha miaka mitatu, yaani 2017-2020, wanafunzi 564,649 waliongezeka katika shule za sekondari za Serikali, huku walimu 4,861 wakipungua, achilia mbali upungufu ambao tayari ulikuwepo.

Mheshimiwa Rais, kutoka mwaka 2020 mpaka 2022/23, Serikali yako imeongeza udahili mara dufu. Mwaka 2022 pekee, Serikali imedahili wanafunzi kidato cha kwanza 907,802 (waliopo shuleni kwa sasa ni 784,061), huku idadi hii ikiongezeka mwaka 2023 kufikia wanafunzi 1,073,941

Hii inamaanisha Januari 2023, kidato cha kwanza na cha pili pekee kutakuwa na wanafunzi 1,858,001, au zaidi ya wanafunzi 1,700,000, endapo baadhi ya waliochaguliwa 2023 hawatafika. 

Hii idadi ya haya madarasa mawili pekee ni kubwa kuliko wanafunzi wote waliokuwepo shule za sekondari za Serikali mwaka 2017 ambao walikuwa 1,565,857

Tukiongeza wanafunzi 1,148,413 watakaokuwa kidato cha tatu na cha nne, pamoja na wanafunzi 142,174 waliopo kidato cha tano na sita, jumla kuu ya wanafunzi watakaokuwepo shule za sekondari za Serikali Tanzania mwaka 2023 ni zaidi ya 3,000,000. 

Mheshimiwa Rais, kama wanafunzi 1,565,201 walifundishwa na walimu 89,475 mwaka 2017, tulitegemea ongezeko la wanafunzi 1,500,000 mwaka 2023 lije na walimu wapya zaidi ya 90,000.

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kwenye website ya TAMISEMI, Serikali imeajiri walimu wa sekondari 3,000 tu mwaka 2021, na wengine 4,800 tu mwaka 2022. 

Tukijumlisha walimu 7,800 walioajiriwa mwaka 2021-22 na wale 84,614 waliokuwepo mwaka 2020, tunapata jumla ya walimu 92,414 kwenye shule za sekondari za Serikali mwaka 2023. 

Tukichukua idadi hii ya sasa ya walimu 92,414 tukatoa walimu 89,475 (BEST, 2017, p. 124) waliokuwepo kwenye shule za secondari za Serikali mwaka 2017, tutaona kuwa idadi ya walimu walioongezeka ni 2,939 tu kwa miaka mitano iliyopita. 

Je, idadi hii inatosha kuwahudumia wanafunzi zaidi ya 1,500,000 walioongezeka kwa kipindi cha miaka hii mitano iliyopita? Mheshimiwa Rais, tunategemea hawa watoto wa Watanzania maskini walioipigia kura Serikali yako watafundishwa na nani?

Hali ya vitabu nayo tete

Mheshimiwa Rais, ongezeko hili kubwa la wanafunzi lililokuja bila kuangalia idadi ya walimu lilinisukuma pia kuangalia suala la vitabu. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya vitabu haijaongezeka tangu mwaka 2017, achilia mbali idadi ya wanafunzi iliyoongezeka. 

Masomo ya Kiingereza na Hisabati ndiyo yenye vitabu vingi zaidi kwa hiyo nitayaongelea kama mfano. 

Kwa mujibu wa BEST (2017, p. 104), mwaka 2017 kulikuwa na wastani wa vitabu vya Kiingereza 303,056 kwa kila kidato kuanzia kidato cha 1-4 (jumla ya vitabu vya Kiingereza kwa madarasa yote ilikuwa 1,245,716). 

Somo la Hisabati lilikuwa na vitabu 1,551,680, sawa na wastani wa vitabu 387,920 kwa kila darasa. Badala ya idadi hii ya vitabu kuongezeka kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyoongezeka kwa miaka hii mitano, takwimu za Serikali za mwaka 2022 zinaonesha kupungua. 

Vitabu vya Kiingereza kwa kidato cha kwanza mwaka 2022 vilikuwa 268,402 na kidato cha pili vitabu 241,183. Kwa upande wa Hisabati, kidato cha kwanza kuna vitabu 314,882 na kidato cha pili kuna vitabu 314,430

Hata hivyo, kama nilivyoonesha awali, mwaka 2023 haya madarasa mawili yanategemewa kuwa na wanafunzi 1,858,001. 

Mheshimiwa Rais, wakati idadi ya wanafunzi imeongezeka zaidi ya mara mbili ya wale waliokuwepo mwaka 2017, idadi ya vitabu imepungua kuliko ile ya 2017. Je, hawa watoto zaidi ya 1,500,000 walioongezeka watasoma kwa kutumia vitabu gani?

Madarasa, madawati hayatoshi

Idadi ya madarasa na madawati haiendani pia na ongezeko hili kubwa la wanafunzi. Mwaka 2017, shule za sekondari za Serikali zilizokuwa na wanafunzi 1,565,201 zilikuwa na madarasa 39,490 yenye madawati 1,469,904 (BEST, 2017, p. 127, 129). 

Takwimu za mwaka 2020 zinaonesha idadi ya madarasa kufikia 46,928 (BEST, 2020, p. 311) na idadi ya madawati ikiwa ni 1,833,476 (BEST, 2020. p. 336) huku idadi ya wanafunzi ikiongeza kufikia 2,172,257. 

Ingawa zaidi ya wanafunzi 607,056 waliongezeka kutoka idadi ile ya mwaka 2017, ni madawati 363,572 tu yalioongezeka. Hii inamaanisha nusu ya wanafunzi walioongezeka mwaka 2020 hawakuwa na sehemu ya kukaa na kwa ujumla kulikuwa na upungufu wa madawati 34,1324

Ingawa sina data kamili zinazoonesha idadi ya madawati kwa sasa, mwenendo niliouonesha awali unashawishi kuamini kwamba ongezo la wanafunzi haliendani na ongezeko la madawati.

Kwa upande wa madarasa, tukiongeza idadi ya madarasa 1,500 (kwa mujibu wa maelezo ya Serikali) yaliyojengwa hivi karibuni, na madara 39,490 yaliyokuwepo mwaka 2020, tutapata jumla ya madarasa 61,928. 

Mheshimiwa Rais, hii inaonesha kwamba japo idadi ya wanafunzi zaidi ya 1,500,000 walioongezeka katika miaka mitano iliyopita ni kubwa kuliko wale waliokuwepo mwaka 2017, wanafunzi hawa wameandaliwa madarasa 22,438 tu, ambayo ni pungufu ya 17,052. 

Kwa hali hii, tunategemea hawa watoto watasomea wapi? Hatuoni kama hali hii inalazimisha hawa watoto wakaendelee kujazana kwenye yale madarasa machache yaliyokuwepo ambayo tayari nayo yalikuwa yameshaelemewa kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi?

Lugha ya kufundishia mtihani

Mheshimiwa Rais, wasiwasi wangu mwingine upo katika uwezo wa lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi tunaowadahili, haswa ukizingatia kwamba lugha hiyo ndiyo lugha ya kufundishia kwa shule za sekondari. 

Ufaulu wa somo la lugha ya Kiingereza katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba unaonesha wazi kwamba watoto wengi hawamudu lugha ya Kiingereza, lakini cha ajabu watoto hao hao wamedahiliwa na kulazimishwa kusoma kwa Kiingereza hicho hicho wasichokiweza. 

Katika matokeo ya mtihani wa taifa wa Kiingereza kwa darasa la saba mwaka 2021, ni wanafunzi 531,640 (NECTA BRN, 2021, p. 1) tu waliofaulu kwa kupata madaraja A, B, na C kati ya wanafunzi 1,107,778. 

Hata hivyo, waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 ni wanafunzi 907,802. Idadi hii inamaanisha kwamba wanafunzi 376,162 waliokuwa kidato cha kwanza mwaka 2022 walifeli somo la Kiingereza.

Katika matokeo ya mtihani wa taifa wa Kiingereza darasa la saba mwaka 2022, ni wanafunzi 396,139 tu waliofaulu kwa madaraja A, B, na C kati ya wanafunzi 1,350,881. 

Hii inamaanisha kuwa kati ya wanafunzi 1,073,941 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023, wanafunzi 677,802 walifeli mtihani wao wa Kiingereza wa darasa la saba.

Kwa maana hiyo, kati ya wanafunzi 1,858,001 watakaokuwa kidato cha kwanza na cha pili mwaka 2023 wakitumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, wanafunzi 1,053,964 walifeli somo la Kiingereza kwenye mtihani wao wa taifa wa kumaliza sarasa la saba. 

Mheshimiwa Rais, tunategemea hawa watoto watasomaje kwa kutumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia ikiwa wameshaonesha kutokumudu lugha hiyo?

Mheshimiwa Rais, sina mashaka na nia yako ya dhati ya kuliletea taifa letu maendeleo makubwa katika elimu. 

Matamko ambayo umekuwa ukiyatoa mara kwa mara kuhusu elimu na jitihada ambazo umekuwa ukizichukua, ikiwemo ujenzi wa madarasa na kuajiri walimu, vimekuwa vikilishuhudia hili. 

Wingi kuliko ubora?

Hata hivyo, njia unayoitumia inayoonekana kujikita zaidi katika wingi badala ya ubora inayaweka hatarini maisha ya watoto wengi wanaoongezeka kwenye udahili kila mwaka. 

Kuwadahili wanafunzi kwa maelfu bila kuwaandalia walimu, vitabu, mazingira rafiki ya kujifunzia, tena pasipo kuwapa nafasi ya kujifunza kwa lugha wanayoielewa ni sawa na kuwapotezea hawa watoto muda wao muhimu ambao wangeweza kuutumia kujifunza mambo mengine yenye tija kupitia kujishughulisha kwenye jamii zao. 

Nafahamu kwamba maendeleo ya elimu ni mchakato wa muda mrefu lakini mchakato huo unapaswa kuwa wa mipango endelevu na inayotekelezeka. 

Ingekuwa na tija zaidi endapo fedha tunazozitumia kuongeza hii idadi ya wanafunzi zingetumika kuboresha mapungufu mengi yaliyopo sasa ili kuhakikisha wale wanaopata nafasi ya kwenda shule wanaandaliwa vilivyo na kuwa rasilimali watu wenye tija katika taifa letu.

Mheshimiwa Rais, hali ya elimu yetu kwa sasa ni mbaya sana, karibu asilimia 70 ya wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanafanya vibaya kwa kupata sifuri na daraja la nne kwenye mtihani wao wa mwisho karibu kila mwaka (BEST, 2020, p. 271) na hata wale wachache wanaofaulu mtihani wa taifa hawapati ujuzi wenye tija kwa taifa letu. 

Tunapoendelea kufanya udahili ili kuongeza idadi ya wanaoenda shule bila kuboresha mazingira yaliyopo, tunaendelea kulitumbukiza taifa letu kwenye umaskini na kuwaumiza wananchi maskini kwa kuwapotezea muda watoto wao.

Nakutakia afya njema na heri ya mwaka mpya, 2023!

Onesmo Mushi ni mwanafunzi wa elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Rochester, kilichopo New York, nchini Marekani na mchambuzi wa masuala ya elimu. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia onesmofrenk@yahoo.com au Twitter kama @EduTalkTz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

4 Responses

  1. Na bado Kuna kipindi walichukua walimu wa sekondari wakawapeleka msingi eti wamezidi,yaaaani hii nchi ngumu sana kitenndo kile kilipelekea baadhi ya walimu kujinyonga na wengine kupata msongo wa mawazo kutokana na poor decisions.

    1. Si madarasa tu hakuna hata ofisi za walimu. Walimu wanashare madawati na wanafunzi. Idadi ya vyoo hailingani kabisa na idadi ya wanafunzi. Wanafunzi 2,000 wanatumia matundu kumi wastani wa wanafunzi 200 kwa tundu.
      Katika kuboresha elimu haya yapaswa kuzingatiwa.

  2. Si madarasa tu hakuna hata ofisi za walimu. Walimu wanashare madawati na wanafunzi. Idadi ya vyoo hailingani kabisa na idadi ya wanafunzi. Wanafunzi 2,000 wanatumia matundu kumi wastani wa wanafunzi 200 kwa tundu.
    Katika kuboresha elimu haya yapaswa kuzingatiwa.

  3. Ni kweli ila changamoto ninkuwa ajira ni chache walimu ni wengi.hivyo ajira zitolewe nyingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *