Dennis Phombeah mmoja kati ya wanachama wa mwanzo wa chama cha kupigania uhuru cha Tanganyika African National Union (TANU) jijini Dar es salaam Julai 7, 1954 anatajwa na mashirika makubwa ya kijasusi wakati wa vita baridi kama jasusi wa kipekee au kwa kimombo Spy muhimu sana katika ukanda wa Afrika Mashariki wakati huo.
Aliibuka katika kipindi cha vita baridi ambapo upande mmoja kulikua na mataifa ya magharibi yaani Marekani, Uingereza na washirika wao na upande wa pili kulikua na Shirikisho la Sovieti, China na nchi zingine.
Kwa kuweza kufanya kazi na mashirika ya kijasusi ya kambi mbili tofauti za vita baridi na wakati huo huo akijidhatiti katika mapambano ya uhuru kunamfanya Dennis Phombeah kuwa mmoja wa mashushu wa kiwango cha juu kuwahi kutokea katika karne ya ishirini wakati wa vita baridi.
Kuibuka katika siasa
Maisha yake ya kisiasa yanatajwa kuanzia Tanganyika akifanya kazi na vijana waliofanya mapinduzi ya uongozi wa Tanganyika African Association (TAA) mwanzoni mwa 1950, Abduwahid Sykes na Vedastus Kyaruzi waliopindua uongozi wa TAA uliosheheni wazee ili vijana waweze kuchukua hatamu na kuleta ari mpya kwenye chama hiko.
Hata hivyo, Phombeah badae alifanya kazi na TANU na baada ya uhuru aliteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Biashara na Ushirika kabla ya kwenda uhamishoni Uingereza kumfuata Oscar Kambona mwaka 1967.
Dennis Phombeah alizaliwa nchini Nyassa Land ambayo sasa ni Malawi miaka ya 1920s, ambako huko alipata elimu yake ya msingi na sekondari. Haifahamiki lini hasa alikuja Tanganyika, lakini inaelezwa alianza kuonekana katika mitaa ya Karikaoo na viunga vya jiji la Dar es salaam kwa ujumla miaka ya mwanzoni mwa 1950s akijivinjari na pikipiki yake aliyopewa na Serikali ya Kikoloni akiwa kama mfanyakazi kwenye ukumbi wa Anatouglou pale Mnazi mmoja.
Ni katika kipindi hicho wakati akifanya kazi katika ukumbi wa Anatouglou ndipo Dennis Phombeah aliweza kujenga urafiki na watoto wa mjini kama vile kina Abdulwahid Sykes, Dossa Azizi na baadhi ya Waafrika wasomi waliokuwa wakifanya kazi Serikalini kama Daktari Vedasto Kyaruzi, Daktari Wilbard Mwanjisi, Hamza Mwapachu, Ally Sykes na Joseph Mutahangarwa.
Ukaribu huu ulimfanya Phombeah kushiriki kikamilifu ndani ya siasa za TAA, kwani Aprili 1953 alishiriki katika kuandaa mkutano wa TAA uliofanyika ukumbi wa Anatouglou ambapo katika mkutano huu Mwalimu Julius Nyerere wa St. Francis College, Pugu aliweza kumbwaga Abdulwahid Sykes katika kinyang’anyiro cha Urais wa TAA.
Mkutano huu wa TAA wa mwaka 1953 una historia kubwa kwani ndio mkutano uliomfukuzisha kazi kijana Alexander Thobias kwa kudaiwa kuiba nyaraka za TAA na kuwakabidhi Special Branch. Thobias aliajiriwa kuwa katibu wa Ofisi ya TAA, Mtaa wa New Street sasa Lumumba na nyaraka alizodaiwa kuziwasilisha Special Branch ni zile zilizohusu mapendekezo ya Kamati ya Kisiasa ya TAA zilizokuwa na mkakati wa kuhamasisha vuguvugu la kisiasa Tanganyika.
Kuingia katika ujasusi
Moja ya sifa kubwa inayotajwa kwa mashushu thabiti ni wale wanaoweza kujichanganya na jamii fulani na hata kuwa nguzo muhimu ya jamii husika bila kujulikana huku akitimiza malengo ya mwajiri wake au malengo yake ya ujasusi.
Phombeah alifanikiwa kuwa shushushu aliyeweza kupenya katika sehemu nyeti zaidi bila kujulikana, na hii ilitokana na sifa alizokuwa nazo Phombeah.
Machoni mwa Waafrika wengi Phombeah alionekana kama Mwana-Afrika kweli kweli au kwa kimombo tungesema a true Pan-Africanist kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la ukombozi la Waafrika.
Mfano mwaka 1959 Pombeah alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya kupinga manunuzi ya bidhaa za Afrika Kusini kutokana na ubaguzi wa Makaburu.
Pegine umbele wake katika kujihusisha na mavuguvugu hayo ndiko kulikovutia mashirika ya Kijasusi kufanya naye kazi kama vile MI5 la Uingereza, StB la iliyokuwa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Czechslovakia, PIDE la Ureno na Tawi Maalum la Serikali ya Kikoloni Tanganyika lilofahamika kama Special Branch.
Hakuwa tu mtoa-taarifa ama kijumbe (informat), ama kificho (undercover) bali alikuwa pia mchambuzi (analyst) wa taarifa za kiintelejensia alizokuwa akizikusanya na kuzituma kwa waajiri wake [mashirika ya kijasusi] kwa miaka takribani ishirini.
Haya yote yamekuja kudhihirika kupitia nyaraka mbalimbali zilizowekwa wazi za operesheni za mashirika hayo ya kijasusi wakati wa mpambano ya uhuru. James Bennan, Mwanahistoria kutoka Chuo Kikuu cha Illinois ambaye amejikita katika kutafiti historia ya Afrika Mashariki hususani Tanzania ameweza kubainisha mengi kuhusu Dennis Phombeah.
Tafiti zinaonesha Phombeah alianza kufanya kazi na kitengo cha Special Branch cha wakoloni kuanzia 1953 hadi mwaka 1955 baada ya kuasisiwa kwa TANU na baada ya hapo Phombeah alitoweka katika mazingira ya kutatanisha katika macho ya umma.
Imekuja kubainika kuwa kitengo cha Special Branch kilimuajiri na kumtuma Yugoslavia kwenda kusomea ushushushu. Yawezekana kwa maksudi Special Branch ilimtuma kwenye nchi zenye siasa za mrengo wa Kikomunisti ili kuwapoteza wanaharakati wenzake wasije kufikiri kuwa Phombeah anatumika na nchi vinara wa vita baridi zikiongozwa na Marekani na Uingereza.
Special Branch ya Tanganyika ndio mwajiri wa kwanza wa Dennis Phombeah akifanya kazi ya kutoa taarifa za maendeleo ya TANU na wasifu wa viongozi mmoja mmoja wa TANU.
Lakini miaka ya mwishoni mwa 1950 Phombeah alienda London huku akifanya kazi na shirika la kijasusi la MI5. Kazi kubwa ya Phombeah ilikuwa ni kutoa taarifa za vyama mbalimbali vya wanafunzi waliotoka Afrika kwenda kusoma nchini Uingereza.
Jukumu hili lilimfaa sana Phombeah na alilitekeleza kwa ufanisi mkubwa kwani wakati akiwa hapo London aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Vyama Vya Wanafunzi wa Afrika waliopo jijini London. Hebu fikiria ni kwa kiasi gani ilikuwa rahisi kwake kupata taarifa za mtu mmoja mmoja na vyama hivyo vya wanafunzi wa Afrika?
Katika miaka ya mwishoni ya 1950s ndio kipindi ambacho pia Katibu Mkuu wa TANU Oscar Kambona alikuwa masomoni Uingereza. Hivyo Phombeah alijenga urafiki mkubwa sana na Kambona na hata waliporudi Tanganyika na baada ya uhuru aliendelea kuwa mtu wa karibu zaidi wa Kambona.
Jasusi mwenye sura mbili
Haikuishia hapo tu, kipindi cha mwaka 1961 na 1962 nchi ya Jamhuri ya Kisoshalisti ya Czechslovakia iliyokuwa upande mmoja wa vita baridi ulioongozwa na Shirikisho la Sovieti, ulikuja na mpango maalumu wa kusaidia vuguvugu la kupambana na ukoloni barani Afrika wakati huo huo kutengeneza nchi washirika wa Warsaw Pact kwenye ukanda wa Afrika.
Katika mpango huo wa Czechoslovakia, ilifungua ubalozi wake jijini Dar es salaam mwaka 1962 na walilipa kazi shirika lao la Ujasusi lilofahamika kama Státní bezpečnost (StB) kufanya hizo kazi kutokea Dar es salaam kwenye ubalozi wao.
Hivi ndivyo StB lilivyoweza kumnasa Phombeah kwani licha ya kufahamu kuwa Phombeah alikuwa na mtandao mkubwa na wapigania uhuru, pia alikuwa ni mtu mwenye mweleko wa kisiasa za kushoto yaani Kisoshalisti au Kikomunisti.
Ndio maana imekuja nadharia kwamba Phombeah alifanya kazi na StB kwa sababu za kimtazamo wake wa kifikra za Usoshalisti au Ukomunisti kuwa ndio mtizamo sahihi wa kisiasa, tofauti na alivyofanya kazi na MI5, Special Branch au PIDE ya Wareno ambako alifanya kazi kwa lengo la kupata fedha na kupata marupurupu kama ya kusafirishwa bure kwenda mapumziko kwenye hoteli za miji mikubwa na kadhalika.
Pamoja na kuanza kufanya kazi na StB, Phombeah hakuacha kazi na MI5. Kwani katika miaka ya 1962 hadi 1963 inatajwa kwamba alifanya kazi za ushushushu na MI5 na StB kwa pamoja bila ya wao kujua kama anafanya kazi na shirika jingine la kijasusi. Hadi baadaye miaka ya 1965 ambapo StB walivyoanza kumhisi kuwa akifanya kazi na CIA ya Marekani kitu ambacho bado hakijathibitshwa.
Haikuwahi kuthibitika kuwa aliwahi kufanya kazi na shirika la kijasusi la Sovieti maarufu kama KGB licha ya MI5 kumtilia mashaka kutokana na safari zake za kwenda Moscow miaka hiyo. Pengine labda siku Urusi itakapoziachia nyaraka kama hizo zilizoachiliwa na MI5 ndio ukweli utafahamika.
Nyaraka za StB ambazo kwa sasa zipo wazi kwa watafiti na wanahistoria zinaonesha kuwa Phombeah alitumia jina kificho la ‘Victor’ ili kumlinda asijekukamatwa na Serikali ya Tanzania na mashirika mengine ya kijasusi.
Nyaraka moja ya Serikali ya Tanzania ambayo Phombeah ama Victor aliifanyia kazi ya uchambuzi ni nyaraka ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Tanzania wa mwaka 1964-1969 mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mdogo wa Biashara na Ushirika mwaka 1965.
Kuna zaidi ya nyaraka 500 za StB kuhusu ripoti za Phombeah ama Victor zilizohusu maendeleo ya siasa na uchumi Tanzania pamoja na taarifa kuhusu shughuli mbalimbali za vyama vya ukombozi vilivyokuwa vimejikita Dar es salaam.
Udhaifu wa Phombeah mpaka kupoteza mwelekeo
Pamoja na umahiri wake, Phombeah alikuwa na udhaifu mkubwa ambao mashirika ya kijasusi kama StB aliyofanya nayo kazi yalimtilia mashaka. Tabia ya kulewa kupita kiasi na kupenda wanawake ilitajwa na StB kama changamoto kubwa kwa kificho wao.
Hata hivyo Phombeah alikimbia Tanzania mwaka 1967 baada ya rafiki yake na msiri wake Oscar Kambona kuondoka Tanzania kwenda uhamishoni Uingereza. Akiwa Uingereza kwa mara nyingine alifanya kazi karibu na Kambona akiwa kama mwandishi binafsi wa hotuba za Kambona alizokuwa anazitoa dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Akiwa Uingereza MI5 walimbwaga kwani walishamtilia mashaka tangu akiwa Tanzania kuwa anafanya kazi na nchi za Kikomunisti. Kitendo hiki cha kubwaga kilipelekea maisha kuwa magumu sana kwa Phombeah hadi kupelekea kufanya kazi na majasusi wa Ureno dhidi ya wapigania uhuru wa Msumbiji na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kupata pesa.
Phombeah aliunganishwa na Shirika la Ujasusi la Ureno yaani PIDE kupitia Jorge Jardim, aliyekuwa mwekezaji katika Koloni la Ureno la Msumbiji ambaye pia anatajwa kuhusika na kifo cha Edwardo Mondlane kilichotokea mwaka 1969 jijini Dar es salaam alipokuwa akijaribu kufungua kifurushi kilichotumwa kwa njia ya Posta nyumbani kwake Masaki.
Jorge Jardim alikutana na Phombeah mwanzoni mwa miaka 1970 ambapo Phombeah alipewa kazi ya kuandika habari za propaganda ambazo zilikuwa zinarushwa na stesheni ya redio ya Ureno iliyokuwa kaskazini mwa Msumbiji na kusikika mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Lengo la propaganda hizo ikiwa ni kuwavunja moyo wapigania uhuru wa FRELIMO na wananchi wa Tanzania wa mikoa ya kusini katika mapambano dhidi ya Ureno.
Hata hivyo nyaraka za Ureno pia zinamtaja Phombeah kuhusika kwenye mkakati wao na Oscar Kambona wa kutaka kuvamia mikoa ya kusini ili kujenga ngome ya kijeshi ya Kambona itakayokuwa inatoa ukizani kwa Serikali ya Nyerere. Mpango ambao haukufanikiwa kwa sababu ya kujidhatiti kwa Serikali ya kimaendeleo ya Nyerere iliyoungwa mkono na wananchi.
Katika kujaribu kutekeleza mpango huo pia majasusi wa Ureno walijaribu kushirikiana na Serikali ya Idd Amin aliyeingia madarakani kwa njia ya kijeshi mwaka 1971. Phombeah alitumwa na PIDE Uganda na alikaa kwa kipindi kirefu kidogo haikufahamika alikuwa akitekeleza majukumu gani nchini Uganda wakati ambao kulizuka mgogoro mkubwa wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda mwaka 1972.
Haya ndio maisha ya Phombeah, kutoka kuwa mwanaharakati wa kupigania uhuru hadi kuwa shushushu wa kiwango cha juu wa nchi zilizokuwa kwenye vita baridi. Shushushu anayetajwa kuwa taarifa zake alizozituma kwa waajiri wake zilitumika kwenye maamuzi ngazi za uongozi wa juu wa nchi husika dhidi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Moja ya jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanaendelea kulishangaa kwa Phombeah ni namna alivyoweza kutimiza majukumu yake hayo kwa ufanisi. Ni jambo moja kuwa na sura mbili tofauti, ni jambo jingine kuweza kuhimili kufanya ujasusi kwa mashirika manne yenye malengo kinzani, na kufanya hivyo kwa miongo kadhaa.
Phombeah alifariki mwaka 1974 nchini Uingereza wiki tatu baada ya kuhitimu Shahada ya Falsafa aliyokuwa anaisoma alipokuwa Uingereza. Mazishi yake yalifanyika Uingereza huko huko na kuhudhuliwa na Waafrika wachache pamoja na mkewe Ilona Halberstadt, mwanamama mwenye asili ya Poland na Kiyahudi aliyekuwa akifundisha Sosholojia katika Chuo cha Enfield Uingereza.
Phombeah alimuoa Ilona alivyokwenda nchini Uingereza, lakini kabla ya hapo pia inasemekana alikuwa na mke raia wa Kenya aliyezaa naye watoto wanne.
Joel Ntile ni Mwanamajumuhi wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @NtileJoel. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
3 responses
Alikuwa mwamba
Huyu alihangaika kwa vihela vya bis na vinyama baa. Kuwa ‘double agent’ ni shughuli hatarishi katika idara za ujasusi ‘espionage’!
Ukisoma chapisho hili utagundua kuwa alikuwa ‘kipandikizi’ ( Pigion hole) kazi kubwa ikiwa ni kuiba nyaraka, hasa miniti za mikutano, na maazimio hasa ya kisiasa.
Vinginevyo alijitahidi kupata kula yake kuwasili waafrika wenzake! Bure kabisa
Safi sana kwa kipindi chake aliihujumu Afrika,nimekaa Msumbiji na Afrika ya Kusini wazee waliokaa Tanzania wanakiri nchi yetu ilipitia Misukosuko na Wazungu kwa sababu ya wao kutaka kujikomboa na Tanzania kuwapokea na kuwasaidia.